DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU

DINI YA KWELI YA MWENYEZI MUNGU NI IPI?

Kila mtu huzaliwa katika mazingira au hali ambayo si chaguo lake mwenyewe. Hupachikwa dini ya familia yake au mtazamo wa taifa lake toka mwanzoni mwa kuwepo kwake katika dunia hii. Wakati anapofikia ujana wa (miaka 13 – 20), kwa kawaida hulazimika kuamini kwamba imani ya jamii yake ndiyo imani sahihi ambayo kila mtu anapaswa kuwa nayo. Ingawa wakati fulani baadhi ya watu wanapokuwa wakubwa na wakaona imani nyingine huanza kuuliza na kuhoji ukweli wa imani yao. Wale wanaotafuta ukweli mara kwa mara hufikia mahali wakachanganyikiwa wanapogundua kwamba kila dini, dhehebu, au falsafa hudai ndio njia pekee iliyo sahihi kwa mwanadamu, kwani makundi yote hayo yanahamasisha watu kufanya matendo mema. Sasa ni ipi imani sahihi? Zote haziwezi kuwa sahihi, kwani kila moja hudai kuwa nyingine zote si sahihi. Sasa katika hali hiyo, yule anayetafuta ukweli vipi ataweza kuchagua njia iliyosahihi?

Mwenyezi Mungu ametupa sote akili na uwezo wa kutuwezesha kufanya maamuzi sahihi na ya maana. Nayo ni maamuzi muhimu sana katika maisha ya mwanadamu. Mustakabali wake unautegemea uamuzi huo, kufuatana na hilo, kila mmoja wetu lazima achunguze ushahidi uliotolewa bila kupendelea ndipo achague kile kinachoonekana kuwa ni sahihi mpaka pale ushahidi mwingine utakapotokea.

Kama ilivyo kwa kila dini au falsafa, Uislamu nao unadai kuwa huo ndio njia ya pekee iliyo sahihi kuelekea kwa Mwenyezi Mungu. Katika hali hiyo ya Uislamu kudai kuwa ni njia sahihi si tofauti na mifumo mingine. Kijitabu hiki kinakusudia kukupa ushahidi juu ya ukweli wa dai hilo. Hata hivyo, mara zote ni lazima izingatiwe kwamba, mtu anaweza kuipata njia ya kweli kwa kuweka kando hisia na chuki, vitu ambavyo mara kwa mara hutupofua tusiuone ukweli. Kisha, baada ya kufanya hivyo tu, ndipo tutakapoweza kutumia akili zetu tulizopewa na Mwenyezi Mungu kufanya maamuzi ya kiakili na yaliyo sahihi?

Kuna hoja mbali mbali ambazo zinaweza kutolewa ili kulipa nguvu dai la Kiislamu kuwa ndio dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Zifuatazo ni hoja tatu zilizo wazi sana. Ya kwanza inaegemea juu ya ukweli wa asili ya majina ya dini na upana wa maana zake. Hoja ya pili inahusiana na mafundisho ya kipekee na yasiyotatanisha yanayoonyesha uhusiano kati ya Mwenyezi Mungu, mwanadamu na uumbaji. Hoja ya tatu inatokana na ukweli kwamba Uislamu ni dini ya dunia nzima kwa watu wote na kwa nyakati zote. Hizi ndizo hoja tatu za msingi ambazo kimantiki na kiakili zinalazimu ziwepo kwa dini yeyote ile ili izingatiwe kuwa ni dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu. Kurasa zifuatazo zitaufafanua ufahamu huo kikamilifu.

JINA LA DINI

Kitu cha kwanza kabisa ambacho mtu anapaswa kukijua na kukifahamu kwa kina kuhusu Uislamu ni juu ya maana ya neno lenyewe “Uislamu.” Neno hilo ni la asili ya Kiarabu lenye maana ya kutii au kusalimisha matakwa ya mtu kwa Mwenyezi Mungu wa kweli wa pekee, ajulikanaye kwa Kiarabu kama “Allah”. Mtu ambaye amesalimisha matakwa yake kwa Mwenyezi Mungu (Allah) huuitwa “Mwislamu”. Dini ya Kiislamu haikupewa jina kutokana na jina mtu au watu, wala halikuamuliwa na kizazi chochote cha wanadamu kama vile Ukristo ambao ulipewa jina kutokana na “Yesu Kristo”, Ubudha unatokana na jina la Gautama Buddha, Kunfushian, unatokana na Confucius, Umaksi ulipewa jina la Karl Marx; Uyahudi unatokana na jina la kabila la Yuda na Ubaniani (Uhindu) unatokana na jina la Hindu. Uislamu (kutii amri za Mwenyezi Mungu) ni dini aliyopewa Adam, mtu wa kwanza na mtume wa kwanza wa Mwenyezi Mungu, na Uislamu ndio dini ya mitume wote waliotumwa na Mwenyezi Mungu kwa wanadamu. Kwa kuongezea, jina la Uislamu lilichaguliwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe na limetajwa wazi wazi katika kitabu cha mwisho cha Allah (Quran). Allah alimfunulia mwanadamu katika kitabu cha mwisho alichomfunulia Mwanadamu. Katika ufunuo wa mwisho, uitwao kwa Kiarabu Al-Quran Allah ameeleza yafuatayo:-

“… Leo Nimekukamilishieni Dini yenu, na kukutimizieni neema Yangu, na Nimekupendeleeni Uislamu uwe Dini yenu…” [Quran 5:3]

“Na anayetaka dini isiyokuwa ya Kiislamu basi haitakubaliwa kwake…” [Quran 3:83]

Kwa hiyo, Uislamu haudai kuwa ni dini mpya iliyoletwa Arabuni na Mtume Muhammad katika karne ya saba, lakini Uislamu ni mwendelezo wa sehemu ya mwisho ya dini ya Allah, kama ilivyofunuliwa toka mwanzo kwa Adam na mitume waliomfuatia.

Hadi kufikia hapa tutatoa maoni kwa ufupi kuhusu dini nyingine mbili zinazodai kwamba ndizo njia sahihi. Hakuna sehemu yoyote katika Biblia ambayo utakuta kwamba Mwenyezi Mungu amewafunulia watu wa Mtume Musa au vizazi vyao kwamba dini yao inaitwa Uyahudi, au kwa wafuasi wa Kristo kuwa dini yao inaitwa Ukristo. Kwa maneno mengine, majina “Uyahudi" na "Ukristo” hayakutokana na asili ya Mwenyezi Mungu wala hayani idhini yake. Jina Ukristo halikuwepo hadi muda mrefu baada ya kuondoka Yesu ndipo jina hilo lilipotolewa kwa dini ya Yesu.

Sasa nini lililokuwa jina la kweli hasa, la dini ya Yesu, ambalo linajipambanua na jina lake? (Majina yote mawili Yesu na Kristo yanatokana na maneno ya Kiebrania, kupitia Kigiriki na Kilatini. Jesus ni Kingereza na kwa Kilatini cha Kigiriki ni Iesous, ambalo kwa Kiebrania ni Yeshua au Yehoshua' (Joshua). Neno la Kigiriki Christos ni tafsiri ya Kiebrania kwa neno “Messiah”, jina la heshima linalomaanisha “Mpakwa mafuta.” Dini yake inaakisi mafundisho yake, ambayo aliwaamrisha wafuasi wake kuyakubali kama misingi ya kuwaongoza katika uhusiano wao na Mwenyezi Mungu. Katika Uislamu, Yesu ni mtume aliyeletwa na Allah na jina lake la Kiarabu ni Issa. Kama ilivyo kwa mitume ya kabla yake, yeye naye aliwalingania watu wasalimishe matakwa yao kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu (jambo ambalo ndilo linalosimamiwa na Uislamu). Kwa mfano katika Agano Jipya inasemekana kwamba Yesu aliwafundisha wafuasi wake kusali kwa Mwenyezi Mungu kama ifuatavyo:-

“Baba [yetu uliye mbinguni], Jina lako litakaswe, Ufalme wako uje, [Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] (Luka 11:2/Mathayo 6:9).

Wazo hili lilisisitizwa sana na Yesu katika maelezo yake mengi yaliyoandikwa katika Biblia. Kwa mfano, amefundisha kuwa, waliojisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, hao peke yao ndio watakaopata uzima wa milele. (Peponi).

Yesu pia alifafanua kwamba yeye mwenyewe amejisalimisha kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu.

“Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.” (Mathayo 7:21).

“Mimi siwezi kufanya neno mwenyewe; kama nisikiavyo ndivyo nihukumuvyo; na hukumu yangu ni ya haki, kwa sababu siyatafuti mapenzi yangu mimi, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” (Yohana 5:30).

Kuna maelezo mengi katika Biblia yanayoonesha kwamba Yesu aliweka wazi kwa wafuasi wake kwamba yeye siye Mungu.

Kwa mfano, aliposema kuhusu saa ya mwisho alisema:

“Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba. (Marko 13:-32).

Kwa hiyo, Yesu kama walivyokuwa Mitume waliopita kabla yake na yule aliyekuja baada yake, alifundisha dini ya Kiislamu: kujisalimisha kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu mmoja aliye wa kweli.

MWENYEZI MUNGU NA UUMBAJI

Kwa vile jambo la mtu kujisalimisha kikamilifu kwa Mwenyezi Mungu linamaanisha kiini cha kuabudu, ujumbe wa msingi wa dini ya Mwenyezi Mungu, Uislamu ni kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake. Vilevile Uislamu unawataka watu waachane na kuabudu binadamu, eneo au kitu zaidi ya Mwenyezi Mungu. Kwa vile vitu vyote ukimtoa Mwenyezi Mungu muumbaji wa vitu vyote, ni uumbaji wa Mwenyezi Mungu; inawezekana kusemwa kwamba Uislamu kimsingi unamlingania mtu aache kuabudu viumbe na kumwita amwabudu muumbaji wake pekee. Yeye ndiye pekee anayestahiki kuabudiwa na watu, kwa sababu ni kwa matakwa yake yeye tu ndipo maombi yote hujibiwa.

Kutokana na hilo, endapo mwanadamu atauomba mti na maombi yake kujibiwa, basi akumbuke kwamba si mti uliojibu maombi yake bali ni Mwenyezi Mungu, ndiye aliyeruhusu maombi hayo yawe kama alivyoomba. Mtu anaweza kusema, “jambo hilo lipowazi”. Hata hivyo, kwa wale wanaoabudu miti, inawezekana isiwe hivyo. Vivyo hivyo, wale wanaomwabudu Yesu, Budha, au Krishna au mtakatifu Kristofa, au mtakatifu Jude au hata Muhammad, maombi yao hayajibiwi na hao, bali yanajibiwa na Mwenyezi Mungu. Yesu hakuwaambia wafuasi wake wamwabudu yeye bali aliwaambia wamwabudu Mwenyezi Mungu, kama inavyoeleza Quran:

"Na (kumbukeni) Mwenyezi Mungu atakaposema: "Ewe Isa bin Maryamu! Je, wewe uliwaambia watu: 'Nifanyeni mimi na mama yangu kuwa waungu badala ya Mwenyezi Mungu'?" Aseme (Nabii Isa): "Wewe umetakasika na kuwa na mshirika. Hainijuzii mimi kusema ambayo si haki yangu (kuyasema, kwa kuwa ni ya uwongo). (Quran 5:116)

Yesu hajajiabudu yeye mwenyewe alipokuwa anaabudu, lakini alimwabudu Mwenyezi Mungu. Yesu amenukuliwa ndani ya Biblia akisema,

“…Imeandikwa, Msujudie Bwana Mungu wako, umwabudu yeye peke yake.” (Luka 4:8).

Kanuni hii ya msingi ipo katika sura ya kwanza katika Quran ijulikanayo kama Suratul-Fatiha, aya ya nne

“Wewe tu ndiye tunayekuabudu, na Wewe tu ndiye tunayekuomba msaada.” (Quran 1:5)

Na katika sehemu nyingine ndani ya Kitabu cha ufunuo wa mwisho, ambacho ni Quran, pia Mwenyezi Mungu amesema:

“Na Mola wenu Anasema: “Niombeni Nitakujibuni.” (Quran 4:60)

Ni muhimu mno kusisitiza kwamba msingi wa ujumbe wa Uislamu (umetaja kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake) pia umetangaza kwamba Mwenyezi Mungu na viumbe vyake ni tofauti kabisa. Mwenyezi Mungu hayuko sawa na viumbe vyake wala si sehemu ya viumbe vyake, na wala viumbe vyake si sawa Naye na wala si sehemu ya Uungu.

Hili lawezekana kuonekana ni jambo lililowazi, lakini kitendo cha mwanadamu kuabudu viumbe, badala ya Muumba kwa kiasi kikubwa Kinatokana na ujinga au kupuuza, ufahamu huu. Ni imani ya baadhi ya watu kwamba kuwepo kwa Mwenyezi Mungu kupo kila mahala katika viumbe vyake au kuwepo kwa uungu wake kupo au kulikuwepo katika baadhi ya sehemu za viumbe vyake, jambo lilowahalalishia waabudu viumbe vya Mwenyezi Mungu na kusema kuwa wanamwabudu Mungu. Hata hivyo, ujumbe wa Uislamu kama ulivyoletwa na Mitume ya Mwenyezi Mungu, ni kumwabudu Mwenyezi Mungu peke yake na kuacha kuabudu viumbe vyake kwa moja kwa moja au kwa kutumia njia yoyote ile.

Katika Quran Mwenyezi Mungu amesema wazi wazi:

“Na bila shaka Tulimpeleka Mtume katika kila umma ya kwamba: “Muabuduni Mwenyezi Mungu na mwepukeni (Iblisi) muovu.” (Quran 16:36)

Wakati wale wanaoabudia masanamu wanapoulizwa; kwa nini wanaabudu masanamu yaliyotengeneza na Wanadamu? Jibu la siku zote ni kuwa; kwa hakika wao hawaiabudu ile picha ya jiwe bali wanaabudia Mwenyezi Mungu aliyopo katika masanamu hayo. Wanadai kwamba masanamu hayo ni sehemu za kumuelekea Mwenyezi Mungu tu na si Mwenyezi Mungu mwenyewe! Mtu aliyekubali wazo la kuwa Mwenyezi Mungu kwa namna yoyote ile yupo ndani ya viumbe vyake atalazimika kukubali hoja hii ya kuabudu masanamu. Wakati, mtu aliyeufahamu vizuri msingi wa ujumbe wa Uislamu na utekelezwaji wake kamwe hawezi kukubali kuabudia masanamu hata kama kutajengewa hoja za kimantiki.

Wale waliodai ungu tangu zamani mara kwa mara wameelekeza madai yao katika imani potofu ya kwamba Mwenyezi Mungu yu katika mwanadamu. Tukienda hatua moja mbele, wanadai kuwa Mwenyezi Mungu yu pamoja nao kuliko alivyo kwetu sisi tuliobakia, kwa hiyo, wanadamu wanapaswa kunyenyekea kwao na kuwaabudu wao kama vile Mwenyezi Mungu aliye katika mwanadamu au Mwenyezi Mungu aliejiingiza kwa wanadamu. Vilevile wale wanaotangaza uungu wa watu wengine baada ya kufa kwao wamepata ardhi yenye rutba miongoni mwa wale wanaoamini imani potofu ya kuwa Mwenyezi Mungu yupo ndani ya mwanadamu.

Hadi sasa hivi, lazima iwe wazi kabisa kwamba mtu aliyeelewa msingi wa ujumbe wa Uislamu na vidokezo vyake kamwe hawezi kukubali kumwabudu mwadamu mwenzake katika hali yoyote ile. Dini ya Mwenyezi Mungu, kwa asili, ni wito uliowazi wa kumwabudu Muumba na kukataa kuabudu viumbe kwa namna yoyote ile. Na hii ndio maana ya wito wa Uislamu.

"Laa Ilaha Ill Allah" (Hapana Mola apasae kuabudiwa kwa haki ila Allah).

Kutamka kwa dhati ibara hii na kumkubali Mtume, moja kwa moja kunampelekea mtu kuwa katika Uislamu, na imani ya dhati kwa tamko hilo humuhakikishia mtu kuingia Peponi. Kwa hiyo, Mtume wa mwisho wa Uislamu (S.A.W) amenukuliwa akisema kuwa, “Yeyote asemaye: Hakuna Mungu wa haki ispokuwa Allah, na akafa akiwa na imani hiyo ataingia Peponi.”

Imani juu ya tamko hili la kiitikadi inamtaka mtu kusalimisha matakwa yake kwa Mwenyezi Mungu kwa namna zilizofundishwa na Mitume ya Mwenyezi Mungu. Vilevile tamko hilo linamtaka muumini aache kuabudu miungu ya uongo.

UJUMBE WA DINI ZA UWONGO

Kuna madhehebu, makundi ya kidini, dini, falsafa, na harakati nyingi duniani, yote hayo yanadai kuwa ndio njia sahihi au ndio njia ya pekee ya Mwenyezi Mungu. Sasa vipi mtu ataweza kugundua ni kundi lipi lililosahihi au kama yote ni sahihi? Njia moja ya kupata jibu la swali hilo ni kuondoa tofauti za kijuu juu, katika mafundisho ya wadai mbali mbali ili kuufikia ukweli, na kutambua kitu kikuu kinachoabudiwa na kitu hicho ndicho hasa wanachokilingania, moja kwa moja au sio moja kwa moja. Dini za uongo zote, kikawaida, zina hoja moja maarufu iliyo ya msingi juu ya Mwenyezi Mungu, aidha wanadai wanaume wote ni miungu, au wanaume fulani tu ndiyo miungu au maumbile (nature) ndiyo Mwenyezi Mungu au Mwenyezi Mungu ni kitu kilichopo tu katika dhana za watu.

Kwa hiyo, kuna uwezekano wa kusema kwamba, msingi wa ujumbe wa dini za uongo ni kwamba Mwenyezi Mungu anaweza kuabudiwa kwa mfumo wa umbaji wake. Dini za uongo huwaita watu waabudu viumbe vya Mwenyezi Mungu kwa kuviita viumbe hivyo au sehemu ya viumbe hivyo ni Mwenyezi Mungu. Kwa mfano, Nabii Issa (Yesu) aliwaita, wafuasi wake wamwabudu Mwenyezi Mungu, lakini wale wanaodai kuwa wao ni wafuasi wa Yesu leo hii wanawalingania watu wamwabudu Issa (Yesu), wakidai kwamba yeye ni Mwenyezi Mungu.

Budha alikuwa mrekebishaji ambaye alianzisha kanuni mbali mbali za kibinadamu katika dini ya Kihindu. Hakudai kuwa yeye ndiye Mungu mwenyewe, wala hakupendekeza kwa wafuasi wake kwamba yeye awe wa kuabudiwa. Leo hii, Mabudha wengi mno walio nje ya India wanamfanya yeye (Budha) kuwa ni Mwenyezi Mungu na wanasujudia masanamu yaliyotengenezwa kwa sura yake.

Kwa kutumia msingi wa kutambua kitu kinachoabudiwa, tunaweza kuzigundua kwa urahisi dini za uongo na asili ya vyanzo vyake.

Kama Mwenyezi Mungu alivyosema katika Quran:

“Hamuabudu badala yake (Mwenyezi Mungu ila majina (matupu) mliyoyapanga nyinyi wenyewe na baba zenu (mkayaita hayo masanamu). Mwenyezi Mungu hakuteremsha dalili kwa hayo. Haikuwa hukumu ila hii ya Mwenyezi Mungu tu; Ameamrisha msimuabudu yoyote ispokuwa Yeye tu. Hiyo ni Dini madhubuti, lakini watu wengi hawajui”. (Quran 12:40)

Watu wanaweza kutoa hoja kwamba dini zote zinafundisha mema, kwa hiyo, kuna haja gani ya kujali kuifuata dini mojawapo? Jibu ni kwamba dini za uwongo zote zinafundisha dhambi kubwa sana ya kuabudu viumbe. Kuabudu viumbe ni dhambi kubwa kabisa awezayo kuifanya mwanadamu kwa sababu tendo hilo linapingana na lengo la kuumbwa kwake.

Mwanadamu ameumbwa ili kumwabudu Mwenyezi Mungu tu kama Allah alivyosema katika Quran:

“Sikuwaumba majini na watu ila wapate kuniabudu”. (Quran 51:56)

Matokeo yake, kuabudu viumbe; jambo ambalo ni asili ya kuabudu masanamu ni dhambi pekee isiyosameheka. Mtu atakayekufa katika hali hiyo ya kuabudu masanamu, ameshaangamiza majaaliwa yake ya ahera. Hii si rai ya mtu, bali ni ufunuo wa kweli ulioelezwa na Mwenyezi Mungu katika ufunuo wake wa mwisho kwa wanadamu:

“Hakika Mwenyezi Mungu hasamehe kushirikishwa; na Husamehe yasiyokuwa haya kwa amtakaye. (4:48 na 116)

DINI YA MWENYEZI MUNGU NI YA ULIMWENGU MZIMA

Kwa vile matokeo ya kufuata dini ya uwongo ni hatari sana, dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu ni lazima ifahamike dunia nzima, iwe imepatikana dunia nzima wakati uliopita na lazima idumu milele na iwe inafahamika milele na ipatikane dunia zima. Kwa maneno mengine, dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu haiwezi kuwa na mipaka kwa watu fulani tu, eneo, au kipindi fulani tu. Wala si jambo la kimantiki kwamba dini kama hiyo iamuru mazingira yasiyo na maana yoyote katika uhusiano kati ya mwanadamu na Mwenyezi Mungu kama vile, kubatiza, au imani kwamba mwanadamu ni mwokozi, au ni mpatanishi. Katika kanuni kuu ya Uislamu na ambayo maana yake ni (kusalimisha matakwa ya mtu kwa Mwenyezi Mungu) ndipo inapopatikana mizizi ya Uislamu kuwa wa dunia nzima. Wakati wowote mwanadamu anapotambua kuwa Mwenyezi Mungu ni mmoja na ametofautiana na viumbe vyake, na mtu huyo akajisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, Mtu huyo anakuwa Mwislamu kimwili na kiroho na anastahiki Pepo.

Kwa hiyo, mtu yoyote katika muda wowote hata yule aishiye maeneo ya mbali anaweza kuwa Mwislamu, mfuasi wa dini ya Mwenyezi Mungu, Uislamu, kwa kukataa moja kwa moja kuabudu viumbe na kuamua kumgeukia Mwenyezi Mungu peke yake.

Ni lazima ikumbukwe, hata hivyo, ili kujisalimisha kwa matakwa ya Mwenyezi Mungu kikweli kweli, mtu ni lazima achague baina ya haki na batili. Kwa hakika, binadamu amejaaliwa uwezo na Mwenyezi Mungu sio tu wa kutofautisha kati ya wema na uwovu bali vilevile kuchagua kati ya vitu viwili hivyo.

Huu uwezo wa kupewa na Mwenyezi Mungu unabeba majukumu muhimu sana, nayo ni kuwa, mwanadamu atajibu kwa Mwenyezi Mungu juu ya chaguo alilolichagua. Kinachofuata mwanadamu anapaswa ajaribu kwa kutumia uwezo wake wote afanye mema na aache maovu.

Ufahamu huu umeelezwa katika ufunuo wa mwisho kama ifuatavyo:

“Katika walioamini (Mitume ya zamani huko) na Mayahudi na Wakristo na Wasabai; yoyote (miongoni mwao) atakayemwamini Mwenyezi Mungu (sasa kama anavyosema Nabii Muhammad) na akaamini Siku ya Mwisho na akafanya vitendo vizuri, basi watapata thawabu zao kwa Mola wao, wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika. (Quran 2:62)

Ikiwa kwa sababu yoyote ile, wanadamu watashindwa kuukubali ujumbe wa mwisho baada ya kuelezwa bayana, watakuwa katika hatari kubwa mno. Mtume wa mwisho amesema:

"Yoyote miongoni mwa Wakristo na Wayahudi atakayesikia habari zangu na akaendelea na imani ya kukakanusha kile nilichokuja nacho na akafa katika hali hiyo atakuwa ni miongoni mwa wakazi wa Motoni."

(Sahih Muslim [English Translation], Vol.1 p.91 N0, 284)

KUMTAMBUA MWENYEZI MUNGU.

Swali linalojitokeza hapa ni: vipi itarajiwe kuwa watu wote watamwamini Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli, ukizingatia watu hao wana asili za jamii na tamaduni tofauti tofauti? Ili watu wawajibike kwa kumwabudu Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli, wanahitaji wapate elimu ya kumtambua Mwenyezi Mungu. Ufunuo wa mwisho unafundisha kwamba wanadamu wote wana athari ya kumtambua Mungu mmoja wa kweli athari ambayo iliwekwa katika nafsi zao ikiwa ni kama sehemu ya asili yao waliyoumbiwa nayo.

Katika sura ya saba ya Quran (Al-Aaraf, aya ya 172 – 173), Mwenyezi Mungu ameeleza kwamba wakati alipomuumba Adam alijaalia kizazi cha Adam kuwepo ulimwenguni na Mwenyezi Mungu akuchukua ahadi toka kwao na kuwaambia: “Je, Mimi siye Mola wenu?" Wakasema: “Ndiye; tunashuhudia (kuwa Wewe ndiye Mola wetu)."

Kisha Allah akaeleza sabababu za kuwalazimisha wanadamu wote wakiri kwamba yeye ndiyo muumba wao na ndiye Mwenyezi Mungu wa kweli wa pekee anayestahiki kuabudiwa. Amesema:

“Msije mkasema Siku ya Kiyama kuwa sisi tulikuwa tumeghafilika na hayo (hatuyajui). (Quran 7:172)

Hii inamaanisha kwamba, hatuwezi kudai katika siku hiyo kwamba tulikuwa hatujui kuwa Allah ndiye Mungu wetu na kwamba hakuna mtu aliyetwambia kwamba tulipaswa kumwabudu Allah peke yake. Allah akaendelea kuelezea kuwa:

“Au mkasema, Baba zetu ndio walioshirikisha zamani, nasi tulikuwa kizazi nyuma yao, basi Utatuangamiza kwa sababu ya yale waliyoyafanya waovu?” (Hamuwezi kusema haya kwani nyote Tumekufahamisheni, nyinyi na wao). (Quran 7:173).

Kwa hiyo, kila mtoto huzaliwa na imani ya kumtambua Mwenyezi Mungu na mwelekeo wa kumwabudu Mwenyezi Mungu pekee. Imani hii ya kuzaliwa nayo na mwelekeo huo huitwa kwa Kiarabu “Fitrah”.

Mtume Muhammad (S.A.W) ameeleza kwamba Allah amesema, “Niliwaumba waja wangu katika dini sahihi, lakini shetani aliwapoteza.” Vilevile Mtume amesema, “Kila mtoto huzaliwa katika Fitrah. Kisha wazazi wake wanamfanya aidha awe Myahudi, Mkristo au Mmajusi (waabudio moto).’’ Ikiwa mtoto ataachwa peke yake, atamwabudu Mwenyezi Mungu kwa namna yake mwenyewe, lakini watoto wote huathiriwa na mazingira. Kwa hiyo, ni kama vile mtoto anatii sheria za kimaumbile, ambazo Allah ameziamrisha kimaumbile, katika hali hiyo hiyo nafsi yake pia inatii maumbile ya kuwa Allah ni Mola na Muumba wake. Lakini, ikiwa wazazi wake watajaribu kumfanya afuate njia tofauti, mtoto anakuwa hana nguvu za kutosha, hasa hasa katika hatua zake za mwanzo za maisha yake, za kuzuia na kupinga matakwa ya wazazi wake.

Katka hali kama hizo, dini ambayo mtoto anaifuata, ni tamaduni na malezi, na Mwenyezi Mungu hamuhesabu wala hamuadhibu kwa dini hiyo mpaka atakapofikia umri fulani maishani mwake. (baleghe).

DALILI ZA MWENYEZI MUNGU.

Katika hatua zote za maisha ya wanadamu, kutoka utoto hadi kufikia kufariki, dalili za Mwenyezi Mungu mmoja wa kweli zinaonyeshwa kwao katika pande zote za dunia na katika nafsi zao mpaka inapowabainikia kwamba kuna Mwenyezi Mungu mmoja tu wa kweli (Allah). Mwenyezi Mungu amesema katika Quran:

“Tutawaonyesha (ukweli wa) Maneno Yetu haya katika nchi za mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba haya ni kweli…” (Quran: 41:53)

Ufuatao ni mfano wa ufunuo wa Mwenyezi Mungu kwa dalili ya kosa la mtu mmoja la kuabudu sanamu. Katika maeneo ya kusini mashariki mwa msitu wa Amazoni huko Brazili, Amerika ya Kusini watu wa kabila la wasiostaarabika walijenga kibanda kipya ili kuhifadhi sanamu la mtu liitwalo Skwatch, likiwa ni Mungu mkuu wa viumbe vyote.

Siku iliyofuatia kijana mmoja aliingia kibandani kutoa heshima kwa Mungu huyo, na alipokuwa ameinama (kukisujudia) kile alichofunzwa kuwa ndicho Muumba na Mpaji wake, ghafla mbwa mkondefu mwenye viroboto na mafunza aliingia pole pole mule kibandani. Yule kijana aliinua kichwa chake kwa kitambo kidogo akamtazama yule mbwa, akiinua mguu wake wa nyuma na kulikojolea lile sanamu.

Yule kijana alimfukuza yule mbwa nje ya kile kibanda kikatili, lakini mara tu ghadhabu zake zilipoisha alitambua kwamba lile sanamu kamwe haliwezi kuwa Mola wa Ulimwengu wote. Mwenyezi Mungu, lazima atakuwa yupo sehemu nyingine, alihitimisha. Ni jambo la kushangaza kama linavyoweza kuonekana, mbwa kulikojolea lile sanamu ilikuwa ni alama kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kijana huyo. Alama hii imebeba ujumbe mtakatifu kwa kuwa kile alichokuwa akikiabudu kilikuwa cha uwongo. Huo ni ukombozi kutoka utumwa wa kufuata mafundisho ya utamaduni wa kuabudu mungu wa uongo. Matokeo yake, mtu huyu amehiyarishwa: aidha amtafute Mwenyezi Mungu wa kweli au aendelee katika njia yake ya makosa.

Allah (S.W) anataja utafutaji wa kumtafuta Mwenyezi Mungu unaomuhusu Mtume Ibrahimu kuwa ni mfano wa jinsi ya wale wote wanaofuata dalili zake wataongozwa katika njia sahihi.

“Na namna hivi Tulimwonyesha Ibrahimu ufalme wa mbingu na ardhi (kuwa ni wa Mungu), na ili awe miongoni mwa wenye yakini. Na usiku ulipomwingilia (Ibrahimu na hali kakaa na makafiri), akaona nyota, alinena (makusudi kutaka kuwavuta watumie fikra zao): “(Nyota) hii ni Mola wangu.” Ilipotua (ikapotea), alisema (kuwaambia wale makafiri kama kwamba yu pamoja nao katika ibada ile): “Sipendi waola wanaopotea (hawawepo ila wakati makhsusi tu).” Na (usiku wa pili) alipouona mwezi unachomoza alisema (kuwaambia wale marafiki zake wa kikafiri): “Huu (mwezi) ndio Mola wangu.” Ulipotua alisema: “Asiponiongoza Mola wangu, bila shaka nitakuwa miongoni mwa watu wapotofu. (Na mola huyu hawezi kuniongoza kwani anakuwa hayupo wakati mwengine).” Na (siku ya tatu) alipoliona jua linachomoza alisema (kuwaambia): “Hili (jua) ndilo Mola wangu. Huyu (mola) mkubwa kabisa,” lilipotua alisema: “Enyi watu wangu! Mimi simo katika hayo mnayoyashirikisha (na Mungu) “Mimi nimeuelekeza uso wangu kwa Yule aliyeziumba mbingu na ardhi. Hali ya kuwa nimewacha dini za upotevu. Mimi (ni Mwislamu) wala si miongoni mwa washirikina.” (Quran 6:75-79)

Kama tulivyosema hapo mwanzoni, Mitume wametumwa kwa kila taifa na kila kabila ili kuiwezesha imani ya kimaumbile ya mwanadamu juu ya Mwenyezi Mungu na ule mwelekeo wa kumwabudu Yeye, pia kuutia nguvu ukweli mtatakatifu kwa dalili na alama za kila siku zinazooneshwa na Mwenyezi Mungu. Ingawa mafundisho mengi ya Mitume hao yamebadilishwa, baadhi ya sehemu zinazofunua ujumbe wa zimebakia bila kuvurugwa na zinahudumia katika kuwaongoza watu katika kuchagua kati ya haki na batili.

Athari za ujumbe uliofunuliwa na Mwenyezi Mungu kwa muda mrefu zinaweza kuonekana katika "Amri Kumi" za Torati ya Wayahudi ambazo baadaye ziligeuzwa na kuwa katika mafundisho ya Kikristo, vilevile, kuwepo kwa sheri dhidi ya uuaji, wizi na uzinzi katika jamii nyingi kote kote katika zama za kale na za sasa za ulimwengu.

Matokeo ya alama za Mwenyezi Mungu kwa wanadamu wa zama zote zikiwa na ufunuo wake kupitia Mitume yake, wanadamu wote wamepewa nafasi ya kumtambua mungu wa kweli wa pekee.

Matokeo yake, kila nafsi itahesabiwa kwa imani yake juu ya Mwenyezi Mungu na kwa kukubali kwake dini ya kweli ya Mwenyezi Mungu, iitwayo Uislamu, ambayo inamaanisha utiifu mkamilifu kwa matakwa ya Allah.

HITIMISHO

Maelezo yaliyotangulia yamefafanua kwamba jina la dini ya Kiislamu linaeleza wazo kuu na la msingi la Uislamu, ni kujisalimisha kwa Mwenyezi Mungu, na kwamba jina "Uislamu" halikuchaguliwa na mwanadamu, bali lilichaguliwa na Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa vitabu vitakatifu vya Uislamu. Vilevile imeoneshwa kwamba ni Uislamu pekee unaofundisha kwamba Mwenyezi Mungu ni mmoja na Sifa zake na unaamrisha kumwabudu Mwenyezi Mungu tu bila ya mshirika. Mwisho, kutokana na utakatifu wa mwelekeo ulioingizwa pole pole kwa mwanadamu ili amwabudu Mwenyezi Mungu na dalili zilizooneshwa na Mwenyezi Mungu kwa miaka mingi kwa kila mtu, Uislamu unaweza kufikiwa na watu wote kwa nyakati zote.

Kwa ufupi, maana ya neno Uislamu (kujisalimisha kwa Allah), Uislamu kikamilifu unakiri upweke wa Mwenyezi Mungu na ufikiwaji wa Uislamu kwa watu wote katika nyakati zote kukinaisha watu kuunga mkono dai la Uislamu la kwamba toka mwanzoni mwa Ulimwengu katika lugha zote imeelezwa kwamba, Uislamu pekee ndio uliokuwa na utakaoendelea kuwa dini pekee ya kweli ya Mwenyezi Mungu.

Tunahitimisha kwa kumuomba Allah, Mtukufu, atuweke katika njia iliyosahihi ambayo ametuongoza kwayo, na atupatie baraka na rehema zake, kwani yeye ni Mwingi wa msamaha. Shukrani ziende kwa Allah, Mola wa ulimwengu wote, na rehema na amani ziende kwa Mtume Muhammad (S.A.W) na kwa Mitume ya Allah yote na kwa wafuasi wao waliowema.

Ayman Abu Saleh

أيمن أبو صالح – معسكر دير البلح

قطاع غزة - فلسطين

Phone: +358 44 290 9535

E-Mail: absayman (at) gmail.com

Skype: absayman

Google Talk: absayman