Tarehe 19/07/2026 ni siku ya kipekee sana katika shirika la ndugu wa mama Bikira Maria wa mlima wa Karmeli, O.Carm. Kwani kwa kipindi kirefu kumekuwapo na matamanio ya uwepo wa utawa wa tatu wa wakarmeli walei. Na hivi leo wakarmeli walei 23 wameweka nadhiri zao za kwanza ndani ya shirika la wakarmeli. Misa iliongozwa na Padre Dominic Maria Somola O.Carm ambaye ni mwakilishi wa mkuu wa shirika na ndiye aliyepokea nadhiri zao.
Padre Dominic Maria aliwaasa wanadhiri wapya kuwa wanapaswa kuishi maisha ya kumfuasa Kristo, huku wakipaswa kujua ya kuwa wanakuwa utawa wa tatu sio kwasababu ya kujiweka karibu na mapadre bali wanapwaswa kujua kuwa wao ni wafuasi wa Kristo na ndiye mfano bora wa maisha yao ambayo kila siku wanapaswa kumfuata kama mfano bora wa maisha ya kumtafuta Mungu kwa mfano wa mababa wakarmeli wa kwanza waliokuwa ni walei kule mlima karmeli. Na pia wanapaswa kuwa chachu ya maisha ya kikristo ili kwa mfano wa maisha yao wawavute wengi Zaidi kwa Kristo.
Nadhiri hizi zilishuhudiwa na baadhi ya mapadre wakarmeli ambao ni padre Victor Maria Bilamata O.Carm, Pd Paul Maria Kaigarula O.Carm, Pd Dickson Maria Sambala ambaye pia alishiriki kuwaandaa kwa kipindi chote cha unovisi wao na Pd Paul Maria Malewa O.Carm. katika misa hii ilitolewa hati maalumu ya kulitambua kundi hili kutoka makao makuu ya shirika kwa mkuu wa shirika duniani. Hivyo kwa hati hii, inawafanya kuwa kundi rasmi la utawa wa tatu wa wakarmeli walei.
Ni dhahiri kuwa kundi hili la utawa wa tatu lilichelewa kutambulika mpaka pale kanuni ya maisha ya utawa wa tatu ilipotafsiliwa kwa lugha ya Kiswahili na kupitishwa na askofu wa jimbo. Hii iliwapa utambulisho wa kina kama kundi linalofuata utaratibu wa kikarmeli katika kuutafuta uso wa Yesu. Kwa kujiweka wakfu kwa Bikira Maria mama wa Mungu na kumfuasa Nabii Eliya baba katika karmeli.
Nadhiri hizi zilifuatiwa na hafra fupi ya kuwapongeza wanadhiri hawa 23 wapya ambao wameweka historia ya kuwa wanadhiri wa kwanza kuweka nadhiri kwa kundi la utawa wa tatu hapa nchini Tanzania. Ikumbukwe kuwa mababa wa kwanza kule mlimani Karmeli walikuwa pia walei waliotoa maisha yao kumfuata nabii Eliya na kwa maongozi na kujiweka wakfu maisha yao kwa mama Bikira Maria, hivyo walei hawa wanafanyika mwendelezo wa Baraka na neema ndani ya bustani ya Karmeli.
Familia ya karmeli inaundwa na makundi matatu muhimu ambapo kundi la kwanza ni mapadre na ma-brother, na kundi la pili ni masister wa ndani na kundi la tatu ni utawa wa tatu walei ambao leo wameweka nasdhiri zao za muda. Shirika pia huwatambua masister, mabrother na mapadre ambao wanahusianishwa na wakarmeli na wote wanaovaa skapulari kuwa sehemu ya familia ya karmeli. Hii inaifanya Karmeli kuwa bustani iliyochanua mauwa ya kilanamna ambayo ni watu wa aina tofauti tofauti wanaoipamba bustani hii ya sala.
Bikira Maria wa Mlima Karmeli utuombee!