KILA MTU ANA WITO WAKE AMBAO INABIDI AUTEKELEZE
Kila mtu hupokea wito wakati wa Ubatizo na Kipaimara
Inabidi tusaidiane kugundua upendo wa Mungu kati yetu na kuuonja. Unaweza kufahamu na kuamini kuwa kuna upendo wa Mungu lakini ukashindwa kuuonja. Kuonja ni kuguswa, ni kuchomwa. Kwa hiyo unaamua kuwashirikisha wengine. Mtu anayeguswa lazima anajibu. Haidhuru jibu lako ni lipi, lakini ni lazima ujibu tu. Ili hilo lifanikiwe inabidi kujiachia mikononi mwa Mungu. Tumpe Roho Mtakatifu afanye kazi yake. Hayo yatafanikiwa ikiwa tunafanikiwa kujitenga na ulimwengu. Kama Mungu ametuita ina maana ana mpango na sisi.
Gharama za ufuasi -Luka 9:57-62 na 14:25-32.
Huwezi kumfuata Yesu kwa kutarajia kupata mambo ya kidunia. Yesu hana mambo ya kidunia. Yesu ni maskini hana hata sehemu ya kuweka kichwa chake. Hana lakini hata watu wamemkatalia. Hana mahali pa kupumzika. Kuna mtu anaitwa lakini anatoa udhuru. Sasa tuangalie aina tatu za watu
Wanaitwa na Yesu na kukubali Mt 4:19-20. Haraka haraka wanaacha vyote wanamfuata. Hawana kipingamizi Mt 9:9.
Wanaitwa wanakubali lakini wanakataa kumfuata Mt 8:21. Kuna watu wanaitikia wito lakini hawataki kuachia mambo ya kidunia. Niko tayari lakini nipe muda. Nitafanya kwanza ya kwangu halafu ndo nitafanya ya kwako. Mimi kwanza Yesu Kristo baadaye Luka 9:62.
Nitakufuata -Wengine wanataka kuamfuata lakini Yesu hawapi ruhusa ya kumfuata. Luka 9:58. Marko 5:18-20. Anachanganya ya Yesu na ya kidunia.
Tunapoitwa tusitafute kufaidika kidunia. Tusitafute makuu ya kidunia. Tukitarajia ya kibinadamu tutashindwa kumtumikia Yesu. Kristo awe wa kwanza. Tuwe tayari kujitoa kabisa. Wazazi, ndugu na wengine wanakuja baadae kabisa. huna mamlaka tena na maisha yako.
KUKUBALI MSALABA WA KRISTO -Msalaba ni chemchemi ya furaha na amani.
Msalaba ulikuwa ni njia pekee ambayo Yesu aliitumia ili kuufikia ufufuko na ushindi.
Msalaba ni njia ya kushiriki maisha ya Yesu leo na daima.
Kuteseka kwa ajili yako, watu wengine na kwa ajili ya Mungu ni jambo la msingi katika ufuasi wa mkristo. Msalaba unakuja wenyewe, wewe unaupokea tu. Katika wito Yesu habembelezi. Anasema moja kwa moja we njoo. Tukimweka Kristo wa kwanza tutapata mengine yote. Ndio maana anasema tafuteni kwanza ufalme wa Mungu mengine yote mtapewa kwa ziada Mt 6:33. Yesu anataka tumpende kupita vitu vyote maana yeye alitupenda kwanza. Yoh 3:16. Yesu aliupenda ulimwengu upeo. Msalaba ndio kipimo cha upendo upeo. Upendo ni kutoa uhai. Hivyo anatudai sisi tumpende wazima wazima. Hakuna mambo mseto mseto. Tunapenda kuwa masista lakini vile vile tunapenda kuishi kama walei. Ubishi, kiburi, kujidai, kutowajali wengine, pengine hata kupenda kushiriki ufuska. Kujitoa ni kudhubutu. Jaribu kidogo uone. Hayo yote yanategemea:
na imani. Una ujasiri kwa sababu unayo imani.
Jambo la maana kwetu ni kujitambua.
Wokovu ni suala la neema.
Huwezi kuongelea msalaba bila kuongelea aibu ambayo watu wanaweza kuihisi katika maisha yao. Hapo kuna mawili ama kujishusha au kushushwa. Kwa sababu neno la msalaba kwao wanaopotea ni upuuzi, bali kwetu sisi tunaookolewa ni nguvu ya Mungu. Hapa kuna mambo mawili ya msingi:
MAENEO YA MSALABA KATIKA UTAWA
Inabidi kujilinda na hekima tuliyonayo. Kuna uwezekano mkubwa inaudhalilisha msalaba wa Kristo.
Upuuzi -unyenyekevu na utii ni upuuzi
Kikwazo -mtawa kupata ukinzani ni kikwazo. Kikwazo ni nini? Mahali ambapo kuna kushindwa, maumivu, kupoteza, ndipo mahali ambapo kuna upendo wa Mungu.
Ujumbe wa Papa -Kufurahi katika maisha
Jambo la hatari siku hizi ni kuishi bila kujitambua. Kuna vitu ambavyo tunavitamani tukifikiri kuwa vitatuletea furaha lakini si kweli. Matokeo yake tunakuwa na dhamiri isiyopenda. Maisha yetu ya ndani yanapokamatwa na kutafuta faida binafsi na wasiwasi wa maisha binafsi, ndipo hapo sauti ya Mungu hukosa nafasi ndani mwetu na matokeo yake ni kuwasukumia mbali wengine tunaoishi nao, nyumba moja. Furaha ya kuishi huanza kupotea. Na tamaa ya kutenda mema huyeyuka. Wengi huanguka huko na matokeo yake ni kukata tamaa na kuwa na hasira. Hapo hatuwezi kuishi tena kadiri ya mapenzi ya Mungu, bali huishi kwa kutetea mambo yetu. Maisha hupoteza furaha na uzuri wake. Mambo hayo hayampendezi Mungu, si mapenzi ya Mungu. Wala si maisha ya roho tuliompokea kutoka kwa Yesu mfufuka. (Evangelii Gaudium 1).
Jitafakari wewe uko wapi? Tunatamani kuishi kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake?
Kazi kubwa ya Injili na maisha ya kitawa ni kutuweka huru kutoka katika dhambi, huzuni, utupu wa ndani na upweke. Mtu asijisikie anaishi peke yake, mwenyewe. Bado kama hili tunalisikia ndani mwetu basi tujue kuwa tumeshindwa katika wito wetu. Hayo si maisha ya watawa. Katika Kristo furaha huzaliwa upya na kila siku.
KWANGU KUISHI NI KRISTO GAL 2:20
Kwangu kuishi ni Kristo. Nimesulubiwa pamoja na Kristo. Maana yake ni kukubali msalaba, kufisha mambo ya kidunia. Mambo ya kidunia yamekufa ndani mwako, bali ya Kristo yako hai. Hivyo jitambua na ujitahidi kufikia hilo lengo lako la msingi.
Kuna swali ambalo tunaweza kujiuliza, Mtawa ni nani?
Mtu wa Mungu
Mtu wa watu
Mtu wa Kanisa
Mtawa mtu wa Mungu, maana yake Mtawa ni mali ya Mungu. Unasema mimi ni wa Mungu. Kuna uwapo wa Mungu ndani mwako, katika maisha yako. Alitupenda na kutuchagua. Mungu ameamua hivyo. Mungu anachagua kwa hiari na wewe unakubali kwa hiari. Ukisoma Marko 10:16-22. Utaona kuwa huyu kijana alikuwa anatama kupata kitu cha pekee katika maisha yake lakini kwa hiari anakataa mwenyewe kukipokea. Yesu alimwalika amfuate akakataa. Lakini kukataa kwake hakumpi furaha. Hakuna sista wa lazima. Utawa ni upendeleo, ni mapenzi yake Mungu. Kukubali kwetu tunawekwa wakfu, Kukubali kwetu kunaoneshwa kwa kuandika barua. Hivyo ni lazima kujitahidi kuunganika naye kabisa. Maana yake ni sisi milki yake Kwa sababu hakuna mtu miongoni mwetu aishiye kwa nafsi yake, wala hakuna afaye kwa nafsi yake. 8 Kwa maana kama tukiishi, twaishi kwa Bwana, au kama tukifa, twafa kwa Bwana. Basi kama tukiishi au kama tukifa, tu mali ya Bwana. 9 Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia (Rum 14:7-8). Tunatumiwa naye katika kazi ya ukombozi . Kazi yetu ni kuendeleza ukuhani wa Kristo. Huu ni mwendelezo wa wito wa msingi wa utakatifu.
MUNGU ANATUCHAGUA
Maandiko Matakatifu yanaeleza wazi kuwa Mungu anapomchagua mtu au watu ili wamtumikie hasa kwa namna ya pekee katika maisha ya wakfu, huwa haangalii utakatifu wa kuzaliwa wa mtu, bali yeye huchagua tu mtu.
IMANI YA KRISTO KWETU
Kristo anaimani kuwa sisi tutatekeleza kazi yake ya ukombozi. Ukweli huu unadai utambuzi wa hali ya juu kabisa. Hii ni kazi tunayopewa, sisi ni vyombo tu. Inabidi kulinda, kuhifadhi hii tunu, watu wamwonwe Kristo ndani yetu. Wasiwe na wasi wasi kama tu wa Kristo au hapana. Hatuwi watawa kwa ajili yetu sisi wenyewe, bali kwa ajili ya watu. Sisi tuwe tangazo la Kristo alama inayoonekana.
LENGO LA MAISHA YA KITAWA -ALAMA YA UFALME WA MUNGU
Kujiweka wakfu moja kwa moja kwa Mungu kwa ajili ya kuutumikia ufalme wake.
Madhumuni ya maisha ya kitawa ni kuwasaidia watawa kumfuata Kristo kwa karibu na kuwa na umoja na Mungu kwa njia nadhiri za mashauri ya kiinjili.
Kwa maana nyingine lengo la maisha ya wakfu ni kufanana na Bwana Yesu katika kujitoa jumla katika nafsi yake kwa Baba na kwa ajili ya ufalme wa Mungu.
Ili kufanikiwa katika hilo lazima kuwepo mlinganyo kati ya sala na kazi. Hasa kwetu wakarmeli maisha ya taamuli -contemplative life na kujali na kutumikia watu. Yesu hakusali tu, au hakufanya kazi tu au hakukaa na watu tu, bali katika maisha yake aligawanya hivyo vyote vizuri.
Haya mambo matatu
kuishi na watu
kusali -kuwa na Mungu
na kufanya kazi -kujipatia mahitaji.
Tunaalikwa kurudi kwenye moyo wa Mitume kuishi kwa moyo mmoja na roho moja (Mdo 4:32). Maisha ya kitawa yatakuwa zaidi ya kitume ikiwa tutakuwa karibu zaidi na Yesu na tutaishi maisha ya kindugu katika jumuiya na kwa kuyafuata malengo ya shirika -mwanzilishi. Hapo usiweke malengo binafsi juu ya malengo ya shirika.
MTU WA WATU
Unapokuwa mtawa unatwaliwa kutoka katika familia, unaacha wazazi ndugu, mila na tamaduni zako ili uwe wa wote. Unakuwa wa dunia nzima. Huwi mtawa kwa ajili ya ndugu au kwa ajili yako mwenyewe, bali kwa ajili ya watu. Hii ni kwa sababu unamfuata Kristo kwa karibu ambaye ni wa wote. Kazi kubwa ni kuleta upendo na huruma ya Mungu kwa watu wote. Ukiwa mtawa inabidi uutazame ulimwengu kutoka juu. Usiache ulimwengu ukutawale. Hili litakupa uwezo wa kuwahudumia watu kwa upole na unyenyekevu. Wewe hutakiwi kuhukumu. Wewe kazi yako ni kutumikia. Kazi ya kuhukumu mwachie mwenye mamlaka ya kuhukumu. Usianze kubagua watu. Kazi hiyo ni ngumu na huiwezi. Usihudumia watu wa kabila lako tu, au wale ambao ni marafiki zako. Ukifanya hivyo utakosea. Wewe unatakiwa kuleta umoja katika kundi. Ili uweze kufanya hivyo inabidi kutoa nafsi yako mwenyewe. Wajibu mkubwa ni kumshuhudia Kristo. Huruma yake n aupendo wake. Usiende kushuhudia jinsi ulivyo hodari. Kabla ya kuhudumia watu inabidi kuamini. Imani kwanza wewe tena fanya kwa wengine. Imani ni kuishi. Kuna faida gani kuwa mtawa kama maisha yetu hayana tofauti na ya watu wasioamini? Au pengine yanakuwa sawa na ya walei. Si kwamba ya walei hayafai hapana , mimi ninachoongelea na karama na tabia ya maisha ya kitawa yenyewe. Watu wakikutana nawe wawe na furaha na amani. Wamwone Kristo na wajikute ndani mwako. Wapate nafasi ndani mwako.