USHEMASI WA FRT. DICKSON MARIA RICHARD SAMBALA O. CARM
Mnamo tarehe 6 Januari 2023, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam liliadhimisha ibada takatifu ya kutoa Daraja ya Ushemasi kwa Mafrateli watano ambao miongoni mwao wanne walikua wa jimbo kuu katoliki la Dar es Salaam ambao kwa majina ni Frt Paul Michael Mamboleo, Frt. Johannes Victor Kambadu, Frt.Amandi Pius Shirima, Frt. Daniel Richard Ntakwizile na mmoja wa Shirika la Wakarmeli (O. Carm) ambae si mwingine bali ni Frt. Dickson Maria Richard Sambala O.Carm. Ibada ya Misa Takatifu iliongozwa na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu, la Dar es Salaam Mhashamu Askofu Henry Mchamungu katika parokia ya Mtakatifu Yohane Bosco - Kibaha.
Misa hiyo takatifu ilihudhuriwa na waamini kutoka sehemu mbalimbali, Mhashamu Askofu Mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Askofu Mkuu Jude Thaddaeus Ruwa’ich, Askofu Msaidizi wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mhashamu Askofu Stephano Msomba, familia za wateule, mapadre,pamoja na watawa wa kiume na kike.
Katika homilia ya Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu, la Dar es Salaam Mhashamu Askofu Henry Mchamungu aliwasisitiza wanaotarajia kupata daraja la ushemasi kuwa wito ni zawadi kutoka kwa Mungu na Mungu anawatuma kwenda kuhubiri kwa watu mbalimbali wadogo, wanaolingana nao na wakubwa wanaowazidi umri na wakati mwingine watu wanaowazidi elimu hivyo wasiogope wala kuumizwa kichwa kwasababu Mungu aliyewaita atawaongoza.
Pia alisistiza kuwa utume wanao uwendea hautakuwa rahisi kuna milima na mabonde na baadhi ya watu watawapiga mawe wasiogope bali wasimame imara na kumuomba Mungu katika magumu watakayokutana nayo. Pia aliwakumbusha kuwa Ushemasi ni kazi ya huduma ya Neno la Mungu, huduma ya Altare na huduma kwa wahitaji hivyo basi wanahitajika kuchapa kazi kama mashemasi na badae kama mapadre. Kwa kufanya kazi ya ushemasi vizuri na kuishi maisha maandilifu watu watapendezwa na maisha yao na watu watamtukuza Mungu Baba mwenyezi kupitia maisha yeyo wanayoishi.
Baada ya homilia wateule waliopokea daraja la ushemasi walikiri nia yao ya kuitikia wito wa Kanisa kwa unyenyekevu na utiifu, wakiweka maisha yao wakfu kwa huduma ya Neno la Mungu na maskini.
Baada ya kutolewa daraja la ushemasi Ibada ya Misa Takatifu iliendelea kama kawaida na baada ya Misa ilifuatiwa na sherehe fupi ya kuwapongeza mashemasi wapya katika viwanja vya parokia ya Mtakatifu Yohane Bosco - Kibaha.