Nilizaliwa tarehe 09.06.2000 na kupokea sakramenti ya Ubatizo tarehe 01.12.2000 na padri Marcellus Kaberwa na kupokea sakramenti ya Ekaristi Takatifu tarehe 25.12.2008.Tarehe 09.08.2016 nilipokea sakramenti ya Kipaimara huko Rutabo na Mhsh. Askofu Methodius Kilaini. Familia yangu ina jumla ya watu tisa watoto saba na wazazi wasichana watatu na wavulana wane wote bado wapo hai.
ELIMU
Nilianza darasa la kwanza katika shule ya msingi Bumbire mwaka 2007 hadi 2010. Mwaka 2011 niliamia shule nyingine, shule ambayo ilisisitizia sana maadili ya kidini (Catholic school) ambayo ni St. Achileus Kiwanuka English Medium Primary School iliyopo mkoani Kagera wilayani Muleba hadi mwaka 2014. Mwaka 2015, nilijiunga na seminari ndogo ya Mt.Yohane Bosco, Rutabo nikiwa darasa la sita mpaka mwaka 2016, niliitimu masomo ya elimu ya msingi. Mwaka 2017 nilijiunga na seminari ya Mtakatifu Maria, seminari ya Rubya kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita, na kuitimu masomo yangu ya sekondari mwaka 2023, namshukuru Mungu niliweza kufauru masomo yangu vizuri.
WITO
Wito ni sauti kutoka kwa Mungu, hii sauti nilianza kuisikia tangu nilipo kuwa mdogo wa miaka tisa nilipokuwa nikitumikia misa na ibada mbalimbali huko parokiani Bumbire. Watu walipenda kunitania sana kwani walipokuwa wakiniona walisema
(Farther) tangu udogoni mwangu, nilihisi furaha kubwa moyoni mwangu kwa sababu nilitamani sana kuwa padri ili niweze kumtumikia Mungu pamoja na watu kama nilivyokuwa nikiwaona mapdre wengine wakiadhimisha misa na ibada mbalimbali altareni.
Siku moja niliwashirikisha wazazi swala hili na waliniunga mkono kwa kuhakikisha kwa kile ambacho kingehitajika katika safari yangu kipatikane ili kisije kikawa kikwazo katika safari yangu. Mwaka 2014 nilifanya mtihani wa kujiunga na seminari ndogo ya Mt.Yohane Bosco huko Rutabo, matokeo yalitoka vizuri kwani kati ya wanafunzi 150 nilikuwa wa 10, nilifurahi sana kwani niliona tamanio langu la kumtumikia Mungu pamoja na watu wake kama padre lingetimia .Niliendelea na masomo yangu katika seminari ya Mt.Maria Rubya. Nilipokea malezi lakini pia na kukua kiroho kwani licha ya taaluma, nidhamu ilisisitizwa zaidi seminarini hadi nikaitimu masomo yangu ya kidato cha sita mwaka 2023.
Kwa upande wa shirika hili la Bikira Maria wa Mlima Karmeli lilikuwa geni kwangu kwani nilipata kulifahamu kupitia kwa padre Albert ambaye kidogo alikuwa na ufahamu nalo, aliniambia kuhusu karama ya shirika na pia mahali linapopatikana Tanzania na akanisaidia kupata mawasiliano kutoka kwa mkurugenzi wa miito, padri Victor Biramata (O.Carm) ambaye niliweza kuongea nae kwa njia ya simu na baadae alinitumia fomu maalumu ya kujiunga shirikani ambayo iliitaji nijaze taarifa zangu.
Baada ya hapo nilitumiwa barua ya kupokelewa shirikani tarehe 26.06.2023 jioni. Mnamo tarehe 21.08.2023 saa sita nilipokelewa katika nyumba ya malezi Bunju, Dar es Saalam na Fr. Paul Malewa baadae Padri Dominic M. Somola (O. Carm) naye alinipokea kwa furaha katika nyumba ya malezi hapa Bunju. Nayafurahia maisha haya ya Utawa wa Upadri kwani ndilo tamanio langu la kumtumikia Mungu pamoja na watu wake ili wapate ukombozi kama Padri. Namshukuru Mungu kwa zawadi hii ya wito, namwomba kile alichokianzisha ndani mwangu akapate kukikamilisha. Amina
BIKIRA MARIA MAMA YETU WA MLIMA KARMELI, UNIOMBEE.