Utawa wa Tatu katika Karmeli, una historia inayotofautina kidogo na Utawa wa Tatu wa Mashirika mengine ya kitawa, kama vile Wafransiskani ambao tangu mwanzo waliandaliwa Kanuni na Mt. Fransisko wa Assis[1]. Kwa Wakarmeli haikuwa hivyo. Utawa wa Tatu umeingia Karmeli taratibu na hatua kwa hatua kutokana na mabadiliko yaliyokuwa yakitokea ndani ya Shirika.
Wakati Wakarmeli waliporudi Ulaya kutoka Mlima Karmeli, Palestina, walianza kuishi maisha ombaomba lakini wakati huo huo waliendelea kuwa na tabia ya maisha ya kimonaki kama walivyoishi Mlima Karmeli. Hii iliwezesha baadhi ya watu wanaume kwa wanawake kuendelea kuingia na kuwa sehemu ya Wanafamilia wa Shirika kwa mtindo wa “oblatio”. Baadhi yao walikuwa wakiweka nadhiri kama za kitawa na wengine walikuwa hawaweki nadhiri. Hawa wote kwa pamoja walijulikana kama Wakonverse”[2] au Wakonversi. Walikuwa wakitafuta manufaa ya kiroho na walipenda kuishi maisha kama ya watawa.
Wakonversi walikuwa wakiishi kwenye nyumba za watawa wa kiume. Hawa ndio wale waliokuwa wakitoa vitu vyao vyote kwa Shirika na walikuwa wanaishi maisha sawa na ya watawa. Wakawa wanaitwa «nusu mafrateri» “semifratres”[3]. Walikuwa wakipewa vazi la Shirika.
Kundi mojawapo la Wakonverse[4] lilikuwa kundi la wanadada mabikira na wajane. Baadhi yao waliishi pamoja kama jumuiya kwenye nyumba zilizokuwa zimejitenga kidogo na konventi za kiume na wengine walikuwa wakiishi nyumbani kwao. Hawa walikuwa wakiahidi utii kwa mkuu wa nyumba na walikuwa wakiishi ufukara na useja kwa kiwango cha juu sana. Nadhiri zao zilikuwa za milele. Walikuwa wakisali pamoja na watawa wa kiume, yaani, mafrateri. Walioolewa hawakuruhusiwa kujiunga nao. Wale waliokuwa wanaweka nadhiri za milele wasingeweza kuolewa.
Mbali ya kundi la Wakonverse na Wakonversi, yalikuwepo pia makundi mengine ya Wakonversi Walei wanaume kwa wanawake, ambao baadhi yao walikuwa wameolewa au kuoa na wengine walikuwa hawakuoa au kuolewa. Wao walikuwa wakitafuta kufaidika na maisha ya kiroho ya Wakarmeli. Kama vile kuombewa wakati wa shida na kuombea marehemu wao au wao wenyewe walipokuwa wakifariki dunia. Kwa kawaida walikuwa hawaweki nadhiri. Hata kama ilitokea wakaweka nadhiri, basi, nadhiri zao hazikuwa za milele, hivyo hawakutambulikana kama watawa. Walikuwa wakijulikana kama «wanandugu kaka na dada» wa joho jeupe. Walikubali kuishi undugu wa Shirika, wakijibidisha kuishi maisha ya kiroho ya Shirika kama inavyoelekeza Kanuni ya Shirika. Walikuwa wakivaa joho jeupe kama alama yao ya kuwatofautisha na wengine. Mbali ya kuwasaidia mapadri hata wao walikuwa wakisaidiana kwa kila hali. Walikuwa wakiwatembelea wagonjwa na kuwasaidia maskini.
Hati «Cum nulla» ya Nicolò V ya mwaka 1452
Kwenye Hati hii, Papa alitambua uwepo wa kundi la Wakonverse waliokuwa na nadhiri za daima. Hawa ndio wale waliokuwa wanaishi pamoja kama jumuiya. Akawaagiza wawe wanaishi kwenye jumuiya na kusali Sala ya Kanisa pamoja. Jumuiya zao zikapewa uhuru na mamlaka kamili ya kujiendesha. Wengi wao waliokuwa na nadhiri za daima wakawa wamonaki wa kike ambao ndio Utawa wa Pili.
Wengine wote waliobaki ambao hawakuyakubali maisha ya faragha, ndio wale waliounda Utawa wa Tatu. Watu hawa walikuwa mchanganiko. Walikuwepo baadhi yao walioendelea kuweka nadhiri ambazo hata hivyo zilibaki za muda na wengine walikuwa hawaweki kabisa nadhiri.
Hati ya Cum nulla ilitambua uwepo wa wale waliokuwa wakiweka nadhiri za muda ambao walikuwa hawaishi maisha ya kijumuiya. Inaonekana hapa Papa aliongelea tu wale ambao hawakuwa na ndoa, yaani, wale wasioolewa. Maana Hati yake haikuongelea chochote juu ya wale waliokuwa wameolewa. Papa Sisto IV ndiye aliyewaruhusu hata wanawake walioolewa kujiunga na kundi hili mwaka 1476.
Hawa ndio wale waliokataa kuishi maisha ya faragha, wala maisha ya kijumuiya ijapokuwa walikuwa na nadhiri za daima. Walikuwa wakijiita “Wa -Tatu” (Tertiary). Hata hivyo haikuwa sahihi kujiita Wa-Tatu (Utawa wa Tatu), kwa sababu walikuwa na nadhiri za daima. Kitendo chao cha kukataa kuishi maisha ya faragha kilisababisha nadhiri zao za milele kukataliwa na Kongresheni za Roma mwaka 1583. Papa Pio V na Papa Sisto V walisisitiza kwa nyakati tofauti kuwa wale waliokuwa na nadhiri za daima lakini wanakataa kuishi maisha ya faragha walikuwa si watawa tena. Baada ya Mapapa hao kueleza msimamo wao juu ya maisha ya kitawa, ilibidi kutafuta suluhisho la wale waliokuwa wameweka nadhiri na waliokuwa wakitaka kuweka nadhiri lakini wakawa hawataki kuishi maisha ya faragha, yaani, maisha ya klausura. Yakatolewa mapendekezo mawili. Pendekezo la kwanza lilikuwa la kuendelea kuishi na nadhiri zao lakini zisizo za daima na lingine likawa la kuachana na nadhiri ya ufukara na kuifanya nadhiri ya usafi wa moyo kuwa chaguo la mtu binafsi. Mtu angeweza kuchagua kuishi maisha ya usafi wa moyo, yaani, kuishi bila kuoa au kuolewa au kuoa au kuolewa hata mara baada ya kuweka nadhiri. Wengi wao walipenda pendekezo la kwanza. Matokeo yake kukaweko makundi mawili tena. Kundi la wasioolewa na kundi la walioolewa. Baadaye mwaka 1587 iliondolewa nadhiri ya ufukara kwa waliokuwa wanaweka nadhiri, hivyo wakawa wanaweka nadhiri mbili tu kulingana na hali zao. Nadhiri ya Utii na nadhiri ya Usafi wa moyo[5].
Kundi la tatu lilikuwa la “ndugu wa Madonna wa Karmeli” lilikuwa likitambulikana kwa kuvaa Skapulari. Watu wengi walijiunga na kundi hili ili kwa lengo la kufaidika na “Upendeleo wa Jumamosi”[6]. Ilifikia hatua ikawa ni vigumu kutofautisha wanandugu wa joho jeupe na wanandugu wa Skapulari. Makundi haya mawili yalikuwa yakihitirafiana mara kwa mara. Mwaka 1606, Papa Paulo V alitambua ulinganifu wa maisha na majukumu ya makundi haya mawili.
Ili kumaliza msuguano uliokuwepo kati yao, mwaka 1637, Mkuu wa Shirika, Teodoro Straccio aliwaweka pamoja katika Utawa wa Tatu wale wote waliokuwa na nadhiri za muda za Utii na Usafi wa moyo kulingana na hali zao[7]. Wengine wote waliosalio aliwaweka katika kundi la wanandugu wa Skapulari mwaka 1640. Mwaka 1924 waliwaondolea nadhiri ya Utii na Useja wa Utawa wa Tatu kulingana na hali zao[8]. Lakini nadhiri hizo zikarudishwa mwaka 1948. Lakini wakazifanya kuwa chaguo la mtu. Hata Kanuni yao ya mwaka 1977 ilitoa uhuru wa kuweka nadhiri. Sasa walikuwa wanaweza kujiendesha wao wenyewe.
Mashirika ya Masista yalitokana na makundi ya Utawa wa Tatu wa wale waliokataa kuishi maisha ya faragha (klausura). Hawa ndio wale waliokuwa wakiweka nadhiri za muda. Wengi wao walikuwa wanaishi kijumuiya. Lakini wasingeweza kujiita watawa kulingana na Sheria za Kanisa ambazo ziliwataka watawa wa kike wote kuishi maisha ya faragha wakiwa na nadhiri za daima. Maisha yao yalikuwa ni ya kitume zaidi. Waliishi na watu wa kawaida wakiwasaidia wahitaji. Walikuwa wakiwahudumia wagonjwa, maskini, wazee na kuwafundisha watoto wadogo. Kidogo kidogo Vatikani ikaanza kuwachukulia kama watawa. ikawapatia miongozo na taratibu zilizotakiwa kufuatwa ili kutambuliwa rasmi. Mojawapo ya taratibu hizo ilikuwa ni kundi husika kujumuishwa kwenye Utawa wa Kwanza. Wengi wao iliwabidi wawe wanavaa mawazi yaliyokuwa na rangi na yaliyofanana na mavazi ya Shirika husika.
Mfano mzuri wa Mashirika ya Masista yaliyotokana na Utawa wa Tatu, ni «Shirika la Wakarmeli Wamisionari wa Mt. Teresia wa Mtoto Yesu». Shirika hili lilianzishwa na Rosa Curcio ambaye kwa sasa anaitwa Mwenye Heri Maria Crucifissa Curcio. Rosa alizaliwa nchini Italia Sicilia tarehe 30.01.1877. Alipokuwa na umri wa miaka 13 alijiandikisha kwenye Utawa wa Tatu wa Shirika la Karmeli. Tarehe 15.07.1893 alipokea vazi la Karmel la Utawa wa Tatu na akaitwa Maria Crocifissa. Mwaka 1895 akaweka nadhiri za muda kama nilivyoeleza. Mwaka 1909 aliwakusanya wanawake wengine katika Taasisi ya kikarmeli ya kuwasaidia watoto waliokuwa wametelekezwa. Kazi hiyo alifanyikia nyumbani kwake. Akisaidiwa na Wakarmeli Alberto Grammatico na Lorenzo van den Eerenbeemt, mwaka 1925 akahamia Santa Marinella Roma akitokea Sicilia. Mwaka huo huo Taasisi aliyoianzisha akajumuishwa kwenye Shirika la Karmeli. Kardinali Tommaso Pio Boggiani aliitambua Taasisi yake kama Kongregesheni katika ngazi ya Jimbo tarehe 13.04.1930. Tarehe 10.07.1930 ziliidhinishwa Katiba zilizokuwa zimeandaliwa kwa msaada wa Pd. Lorenzo. Kwa kitendo hicho cha kuiidhinisha Katiba, Kongregesheni ikawa Shirika kamili la Kitawa lililojulikana kama. «Masista wa Utawa wa Tatu Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Teresia wa Mtoto Yesu». Tarehe 03.10.1963, Kongregesheni ya Mashirika ya kitawa Vatikani, ikalipatia Hati ya kutambuliwa katika hadhi ya kipapa. Papa Pio XI ndiye aliyependekeza jina linalotumika rasmi kwa sasa, yaani: «Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mt. Teresia wa Mtoto Yesu». Hapo mwanzo walikuwa wakiitwa «Masista wa Utawa wa Tatu Wakarmeli wamisionari wa Mt. Teresia wa Mtoto Yesu».
Kiambatanisho kwa ajili ya Skapulari ya Karmeli
Wanaskapulari ni kundi la waamini Walei wanaojibidisha kuishi maisha ya ukamilifu wa upendo huko duniani katika roho ya Shirika la Wakarmeli. Kujitoa kwao kwa uhuru kunawawezesha kushiriki maisha ya Shirika na kupata manufaa ya kiroho katika muungano wa ndani wa mawazo, mipango na wa kazi wakiwa pamoja na Maria. Mwenye Mamlaka ya kuwaweka kisheria katika Shirika ni Mkuu wa Shirika. Ruhusu inatolewa na Askofu ya kuweka nyumba ya kitawa katika jimbo lake inaambatana na ruhusa ya kuanzisha kikundi cha ndugu wa Skapulari ambacho kimsingi ni Utawa wa Tatu. Lakini mahali pengine pasipokuwa na nyumba au konventi, inahitajika barua maalum ya ruhusa kutoka kwa Askofu. Wanatakiwa kupokelewa katika Shirika na mtu mwenye mamlaka ya kufanya hivyo kwa jina la Shirika. Kupokelewa hufanyika kwa mujibu wa taratibu za ibada zilizowekwa na Vatikani. Lazima kujiandikisha kwenye kikundi na baadaye hupokelewa kwa kuvalishwa Skapulari. Jina la mpokelewa linatakiwa kuandikwa kwenye kitabu cha kumbukumbu likiwa na tarehe yake ya kupokelewa. Inawabidi kuvaa Skapulari muda wote kuonesha shirika wao katika Shirika la Wakarmeli. Lakini zaidi wanatakiwa washiriki sala, Ekaristi Takatifu na kusali kila siku Sala ya Kanisa na kusali rozari kila siku. Sikukuu yao huadhimishwa tarehe 16 Julai.
Linatokana na neno la kilatini Scapulae ambalo maana yake ni mabega. Ni vazi refu ambalo linavaliwa juu ya kanzu ya kitawa. linaangukia mbele na nyuma. Hili ni vazi la kimonaki. Mfano Wabenedikitini, Wadominikani wanavaa Skapulari. Inasemekana Wabenedikitini ndio walioanza kuitumia kwenye karne ya 7 kama eproni. Matumizi yake yalibadilika na kuwa sehemu ya vazi rasmi la Shirika mbalimbali. Waliichukulia kama ishara ya mzigo mwepesi wa Yesu.
Kuna aina mbalimbali za utengenezaji wa Skapulari. Kuna Skapulari yenye vipande viwili vya kitambaa cha brown chenye picha ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Skapulari hii inapovaliwa kipande kimoja huangukia upande wa mbele yaani kwenye kifuani na kingine kinaangukia nyuma ya shingo yaani mgongoni. Skapulari hii inavaliwa na wale tu wanaojiweka wakfu kwa Bikira Maria wa Mlima Karmeli katika Utawa wa Tatu. Skapulari ndogo zenye kitambaa upande mmoja tu huvaliwa na wale wote wenye ibada kwa Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Skapulari hii inaweza kuwa katika mfumo wa mwingine wa medali. Skapulari inavaliwa kwa ahadi maalum za kiroho.
Ibada kwa Skapulari –Historia, kukua na kusambaa kwa ibasa ya kiskapulari. Unapoongelea Ibada ya Skapulari unamaanisha Skapulari ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Katika utamaduni wa maisha ya Wakarmeli, tunaelezwa kuwa Bikira Maria alimtokea Mt. Simon Stock huko Uingereza akamwambia kuwa wale wote wanaovaa Skapulari kwa uchaji wataokolewa moja kwa moja. Kipindi kile Shirika lilikuwa likipita kwenye kipindi kigumu cha mabadiliko (1247). Simon Stock –ambaye inaaminika kuwa ndiye aliyekuwa Mkuu wa Shirika, akawa anaomba msaada wa Bikira Maria. Alitaka kuona alama yoyote ya ulinzi wake wa karibu kwa Shirika. Mwishowe alitokewa na Bikira Maria akiwa na Skapulari mkononi mwake na kumwambia “Yeyote anayekufa amevaa Skapulari ataokolewa katika moto wa milele”.
Baadaye ulisambaa waraka mmoja (wa uongo -pseudoprafi) uliodaiwa kuandikwa na Papa Yohane XXII 03.03.1322. Katika Waraka huo (Sacratissimo uti culmine), Papa anasema kuwa alitokewa na Bikira Maria na kumwambia kuwa, Yeye Bikira Maria angewatoa Wakarmeli wote wanaovaa Skapulari kutoka Purgatori siku ya Jumamosi ya kwanza toka kufariki kwao kama watakuwa wamezingatia masharti ya: kusali Sala ya Kanisa, kuishi maisha ya usafi wa moyo, maisha ya sala na kuvaa Skapulari kila siku, wale wasio jua kusoma inawabidi kufunga siku zilizoamriwa na Kanisa.
Mkutano Mkuu wa Shirika wa uliofanyika mwaka 1517 uliagiza kuwa, juhudi zifanyike ili Hati hii “ya Kipapa” itambuliwe na Papa. Walimwomba Papa Leo X aitambue lakini alifariki kabla hajasema chochote. Baadaye Nicholas Audet alipewa Hati na Papa Klementi VII. Hati hiyo Ex clement ya 12.08.1530 ilihusu Bull ya Papa Yohane XXII, ilidhibitisha maombezi ya Bikira Maria kwa Wakarmeli. Baada ya kupokea Hati hiyo Mkutano Mkuu ukatoa amri ya kuvaa Skapulari kwa ndugu wa Skapulari kwa manufaa ya kiroho. Yohane Mbatizaji Rossi alipata Hati Ut laudes kutoka kwa Papa Gregori XIII, 18.09.1577 iliyodhibitisha Rehema zilizotolewa na Mapapa waliomtangulia. Ilielezea upendeleo wa Bikira Maria kwa wale wanaovaa Skapulari. Hawa watapata ulinzi na msaada wake wa maombezi. Katiba za Shirika zilizochapishwa mwaka 1586 chini ya uongozi wa Yohane Mbatizaji Rossi ziliweka ibada ya kubariki Skapulari katika pontifikare ya kuvalishwa Skapulari. Mwaka 1604 Papa Klement VIII aliweka utaratibu wa kuwatambua ndugu wa Skapulari popote pale hata mahali ambapo Wakarmeli walikuwa hawajafika.
Papa Klementi VII, kwa Hati «Ex clementi Sedis Apostolicae» ya 12.08.1530 alidhibitisha Hati ya Upendeleo wa Jumamosi- Hati ya Jumamosi. Papa Paulo III, kwa Hati «Provisionis nostrae», alidhibitisha upendeleo wa Jumamosi. Papa Pio V, kwa Hati «Superna dispositione» alidhibitisha upendeleo wa Jumamosi, rehema na neema kwa Shirika la Wakarmeli. Papa Gregori XIII, Kwa Hati «Ut laudes» alidhibitisha rehema za upendeleo wa Jumamosi. Aliamuru Wakarmeli wavae Skapulare muda wote usiku na mchana kwa ajili ya rehema ambazo watazipata na kwa kuokolewa watakapo kufa. Papa Gregori XIV, alikuwa akivaa Skapulari kabla na baada ya kuwa Papa. Na alikuwa hali nyama siku ya Jumatano kulingana na utaratibu wa Shirika la Karmeli. Papa Leone XI, alikuwa akivaa Skapulari tangu mtoto. Alipochaguliwa kuwa Papa yule aliyekuwa akimvisha mavazi ya kipapa alitaka kuiondoa Skapulari. Lakini Papa alimkataza akisema kuwa huo uliokuwa ulinzi wa Bikira Maria. Alisema kuacha kuivaa Skapulari ni sawa sawa kumwacha Bikira Maria. Alisema “Niachie Maria ili Maria asiniache”. Papa Paulo V, aliwahi kusema hivi: “Mapadri Wakarmeli waruhusiwe kuhubiri kwamba, taifa la Wakristo linaweza kwa uchaji kuamini juu ya msaada wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli kwa roho za kaka na dada walioishi naye: yaani, Bikira Maria atawasaidia kaka na dada wanaokufa katika upendo, ambao maishani walikuwa wakivaa Skapulari yake..., kwa maombezi yake ya daima, kwa sala zake za uchaji na mastahili yake, na kwa ulinzi maalum baada ya kufa na hasa siku ya Jumamosi. Kwa hiyo picha zinazotengenezwa au kuchorwa na wapenzi wa huyu Mama kwa njia yoyote ile hazimfanyi Bikira Maria ashuke kwenda toharani kwa ajili ya kuzifungulie roho, lakini roho hizi , kwa maombezi yake huchukuliwa mbinguni kutoka katika mateso yale kwa mkono wa malaika”. Papa Alexander VII, Mwaka 1655, siku hiyo hiyo aliyotakiwa kuingia kwenye Koklave, Alexander VII, Msiena aliyeitwa Fabio Chigi, alikwenda kwenye konventi ya Wakarmeli wa Mt. Maria wa Transpontina, hapo baada ya kusali, alipokea kutoka kwa Pd. Mario Venturino, Mkuu wa Shirika (ndugu yake), Skapulari ya Maria na akaandikishwa katika kikundi cha ndugu wa Skapulari. Akiwa na alama hii ya ulinzi wa Mama wa Mungu, alielekea Vatikani na alichaguliwa kuwa Papa kwa msaada wa Bikira Maria (kama inavyoweza kuaminika), siku ya Jumatano, siku iliyotengwa na Wakarmeli kwa ajili ya kumheshimu Bikira Maria Mama wa Mungu. Alikuwa na ibada maalum kwa Bikira Maria.
Anayepokea Skapulari huingizwa kiundani zaidi kwenye Shirika la Karmeli. Ni alama ya upendo na kujiweka wakfu kwa Bikira Maria ambaye ni Dada, Mama na mfano wa kila mfuasi wa Kristo. Anayeipokea hufanywa kuwa mwana familia ya Wakarmeli na hivyo hutakiwa kujibidisha kuishi maisha ya kiroho ya Wakarmeli. Kuishi katika urafiki wa ndani na Mungu kupitia undugu na maombi. Anayeivaa hukumbushwa kuishi maisha ya wakfu kwa Bikira Maria na hukumbushwa wajibu wa Shirika. Vile vile hupata ulinzi kutoka kwa Bikira Maria. Hutakiwa kuishi maisha ya sala, maombi, Alisema Papa Pio XII kuwa, Skapulari inaongea juu ya unyenyekevu, usafi wa moyo na fadhila zote za Maria ambazo inabidi tuzivae.
· kumfuata Yesu kama Maria, mfano kamili wa wafuasi wote wa Kristo. Chimbuko la wajibu huo uko katika Ubatizo unaotufanya watoto wa Mungu. Maria anatufundisha jambo hilo. · Kuishi maisha yanayojifungua kwa Mungu na kwa kufuata mapenzi yake yanayojionesha katika maisha. · Kusikiliza Neno la Mungu katika Biblia na katika maisha, kuliamini na kuweka katika matendo matakwa yake. · Kusali daima na kutambua uwepo wa Mungu katika matukio yote. · Kuwa karibu na ndugu zetu wanaoishi katika matatizo mbalimbali. · Kutuonesha mfano wa watakatifu Wakarmeli. · Imani ya kukutana na Mungu katika maisha ya milele kwa maombezi ya Bikira Maria. Mwaka 1606, Papa Paulo V aliwapa wanandugu wa Skapulari upendeleo wa kindugu wakati huo huo wanandugu wa joho jeupe walitakiwa kuishi maisha ya Utawa wa Tatu au kuchagua kuishi maisha ya kindugu na watu wengine. Mkuu wa Shirika Teodoro Stracci aliumaliza utata huo mwaka 1637 baada ya kuwaweka katika Utawa wa Tatu wale wote waliokuwa na nadhiri za utii na usafi wa moyo kulingana na hali zao. Wengine wote waliosalia aliwaambia wajiunge katika kundi la wanandugu wa Skapulari. Utawa wa Tatu ukawa ni kwa ajili ya wanawake waliokuwa wanaishi useja kwa nadhiri. Leo hii makundi yanayounda Utawa wa Tatu ni Mashirika ya kitawa, Taasisi za kilimwengu[9], Walei wa Utawa wa Tatu na vikundi vingine. Ijapokuwa makundi yote yanashiriki Karama moja ya Shirika na utajiri wote wa maisha ya kiroho, lakini kila kundi lina uhuru kamili wa maisha na wa kisheria. [1] Il Terz’Ordine Carmelitano, Roma 1979. (Maana yake: Utawa wa Tatu wa Karmel, Roma 1979). [2] Wakonverse ni wanawake na Wakonversi ni wanaume [3] Semifratres maana yake ni «nusu mafrateri». [4] Hili ndilo kundi la “Soreres”. [5] Joachim Smet, O.Carm, The Carmelites, A History of the brothers of Our Lady of Mount Carmel, Vol II,Darien, Illinois 1976, uk 222. [6] Soma maelezo ya maono ya Mt. Simon Stock. [7] Teodoro Straccio Alichapisha Kanuni na Katiba kwa ajili yao. «Opusculum regularum et Constitutionum». Sasa hawa ndio wakawa wanaitwa Utawa wa Tatu. [8] Walikuwa wanaweza kuishi maisha ya ndoa. [9] Mashirika ya Kitawa hujiweka wakfu kwa Mungu kwa Mashauri ya Injili ya nadhiri tatu za Utii, Ufukara na Useja na wanaishi kijumuiya. Taasisi za kilimwengu hujiweka wakfu kwa Mungu kwa Mashauri ya Injili ya nadhiri tatu za Utii, Useja na Ufukara, lakini huwa si lazima kwao kuishi maisha ya jumuiya. Wanaishi nyumbani kama watu wengine lakini wakati huo huo wakijibidisha kuieneza Injili ya Kristo. Mfumo wao wa maisha ulitambulika rasmi mwaka 1947 na kuingizwa kwenye Sheria za Kanisa Mwaka 1983.