Mchungaji Mwema (Yohane 10:11-18)
11 Mimi ndimi mchungaji mwema. Mchungaji mwema huutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo.
12 Mtu wa mshahara, wala si mchungaji, ambaye kondoo si mali yake, humwona mbwa-mwitu anakuja, akawaacha kondoo na kukimbia; na mbwa-mwitu huwakamata na kuwatawanya.
13 Yule hukimbia kwa kuwa ni mtu wa mshahara; wala mambo ya kondoo si kitu kwake.
14 Mimi ndimi mchungaji mwema; nao walio wangu nawajua; nao walio wangu wanijua mimi;
15 kama vile Baba anijuavyo, nami nimjuavyo Baba. Nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
16 Na kondoo wengine ninao, ambao si wa zizi hili; na hao nao imenipasa kuwaleta; na sauti yangu wataisikia; kisha kutakuwako kundi moja na mchungaji mmoja.
17 Ndiposa Baba anipenda, kwa sababu nautoa uhai wangu ili niutwae tena.
18 Hakuna mtu aniondoleaye, bali mimi nautoa mwenyewe. Nami ninao uweza wa kuutoa, ninao na uweza wa kuutwaa tena. Agizo hilo nalilipokea kwa Baba yangu.
Hapo awali tumesikia Yesu akijitofautisha na mwizi (Yoh 10:1-5). Halafu akasema kuwa yeye ni mlango wa kondoo (Yoh 10:6-10). Yeyote anayewafikia wanadamu kwa njia isiyo ya Kristo huyu ni mwizi.
Yeyote asiyepitia langoni huyo ni mwizi
Hapo zamani wachungaji walikuwa wakiwachunga kondoo mchana kutwa. Na jua lilipokuwa linakuchwa waliwaongoza kurudi zizini. Mazizi hayo yalijengwa imara kwa lengo la kuwazuia wezi. Mlinzi wa lango alikesha kuhakikisha kondoo wako salama. Asubuhi mwenye kuchunga kondoo alikwenda kwenye lango na kugonga na mlinda lango alimfungulia. Mchungali akiingia huwaita kondoo kwa majina. Kondoo waliijua sauti ya mchungaji na pindi alipokuwa akiwaita walisimama na kumfuata nje na yeye aliwapeleka malishoni. Wale kondoo ambao si wake hawakumfuata kwa sababu hawakuijua sauti yake. Lakini kulikuwa na hatari ya kushambuliwa. Wezi mara kwa mara walitoboa sehemu nyingine na kuingia kwa ajili ya kuiba. Hawakupitia langoni kwa sababu kulikuwa na mlinzi daima.
Yesu ni mlango -Msalaba
Kukubali kutumikia. Kufanywa mhudumu wa Injili kwa njia ya Sakramenti ya Daraja Takatifu. Hakuna mlango mwingine wa kuingia katika utumishi isipokuwa Yesu Kristo.
Wote waliomtangulia ni wezi na wanyang'anyi. Ni akina nani hawa? Pengine aliwaongelea viongozi wa dini waliomtangulia ambao walijitengezea wafuasi wao lakini wakashindwa kutimiza matarajio yao. Hawakujali shida za watu isipokuwa walijali fedha na shida zao. Walitafuta faida zao binafsi, walitafuta sifa na ukuu, na umaarufu. Kutafuta kufahamika. Watu wa namna ahiyo hawawezi kuwatumikia watu wa Mungu. Waliwahadaa watu na baadae kuwaacha katika hali mbaya zaidi. Ili uweze kujua yupi ni mchungaji wa kweli kipimo ni yule anayelinda kundi lake kwa maisha yake. Hatafuti faida binafsi bali hujishughulisha na kumtumikia KristoYesu. Yesu Kristo huyo huyo ni zizi la kondoo, ni lango la kondoo na ni Mchungaji Mkuu wa kondoo.
Sasa hapa anasema kuwa yeye ni mchungaji mwema (Yoh 10:11-18).
Hapa Yesu anaongelea mambo matatu
Kutoa uhai
Sakramenti ya upadre na maisha ya wakfu ni kujitoa kwa Mungu kwa ajili ya kuwatumikia watu. Mapenzi yetu yanatakiwa yaungane na ya kwake. Kuingia kupitia mlango ina maana kumjua na kumpenda. Anasema mtu akinipenda atanitumikia. Kutoa maisha anagusia fumbo la mateso ya msalaba. Kila mtu anayetaka kumtumikia lazima afumbue fumbo la msalaba linaloadhimishwa katika Ekaristi Takatifu. Kupitia Ekaristi hata sisi tunajifunza kujitoa kwa ajili ya wengine.
Anafahamu kondoo na wao wanafahamu sauti yake
Sauti ya Kristo ni sauti ya upendo, sauti ya msamaha, sauti ya huruma, sauti ya upole, sauti ya upatanisho. Kinyume cha hapo sauti nyingine ni ngeni kwetu. Kufahamu kunahitaji moyo.
Umoja
Na mwisho anaongelea umoja. Kuna kuna wengine wasio wa kundi hili. Utume wa Kristo ni wa dunia nzima, unamlenga kila mtu. Utume wa Yesu unahusu binadamu wote. Kanisa daima lisifurahie kuwa na kundi lilelile. Linatakiwa liendelee kutafuta kondoo wengine na kuwaleta katika zizi moja, katika Kanisa moja. Hapa anaongelea kanisa moja ambalo Kristo alikusudia kulijenga. Kanisa la upendo, haki na amani. Kupitia huduma zetu, za kuwahudumia watu maskini, wagonjwa na wengine wengi wanaohitaji msaada kupitia hayo matendo sauti ya Kristo huwafikia watu hao wasio wanakundi hivyo watatambua sauti hii ya Kristo na kumfuata. Sisi tutawafuta watu kwa Kristo ikiwa tutawatendea mambo mema. Tutawajali na kuwapenda.