Watu wenye mvuto na ushawishi kwa Wakarmeli
1. Maria Mama Mpole
Sisi Wakarmeli tuna uhusiano wa kipekee na Bikira Maria na nabii Eliya. Ninapoongelea uhusiano nina maana ya “nafasi yake katika maisha yetu” ambayo inatufanya tumtambue kwa dhamiri zetu kama, Dada, Mama na Mlezi wetu. Wakarmeli wa kwanza walikuwa na dhamiri hiyo tangu walipoanza kuishi katika mlima Karmeli. Bikira Maria na Eliya ni watu wenye mvuto na ushawishi mkubwa kwa Wakarmeli kutokana na maisha yao na uhusiano wa pekee waliokuwa nao na Mungu. Mfano mzuri na wa wazi ni jinsi Neno la Mungu lilivyopata nafasi katika maisha yao. Imani yao kwa Mungu ilikuwa ni dhabiti na haikuteteleka kamwe. Kutokana na sifa za kiimani, kimapendo, na kimatumaini walizokuwa nazo, Wakarmeli walipenda kumtukuza Mungu kwa kuwaiga wao yaani walitaka kuzifuata nyayo zao. Tamanio hilo walilokuwa nalo la kuwaiga, liliwasukuma kuzifuata nyayo zao si kiroho tu wakiwa mbali, bali hata kwa kwenda wenyewe mahali walipoishi watumishi hawa wa Mungu. Kutokana na heshima kubwa waliyokuwa nayo kwa Bikira Maria na kwa kuvutwa naye, basi Wakarmeli wa kwanza walijenga kikanisa cha kwanza kabisa pale mlima Karmeli na wakakiweka wakfu kwa heshima yake. Yeye alikuwa mama katikati yao.
2. Katika kumwiga Maria, waliishi maisha ya sala na taamuli
Uhusiano wa Wakarmeli na Maria una uzito wa kipekee na ni wa ndani zaidi ukilinganisha na uhusiano tulionao kati yetu na Eliya. Tangia mwanzo kabisa mwa ukarmeli kama inavyoelezwa katika «Propositum»[1], nia ya Wakarmeli ya kumtii au kujitoa wazima kwa Kristo ambaye ndiye Mtawala na «Bwana wa eneo», yaani Nchi Takatifu, iliwasababisha wawe na uhusiano wa moja kwa moja na Maria Mama wa Yesu Kristo. Waliamini kuwa kwa kuwa Yesu alikuwa «Bwana wa eneo» basi hata mama yake alikuwa «Mama wa eneo». Maelezo hayo ya kiuhusiano na ya kiutawala, yaani: «Bwana wa eneo» na «Mama wa eneo» yalitokana na fikra za kiutawala za nyakati zile ambazo zilikuwa zikiukweza mfumo wa maisha ya nyarubanja –ukabaila. Eneo lilolengwa ilikuwa ni Nchi Takatifu. Wakarmeli waliamini kuwa, kazi kubwa ya Mama Bikira Maria “Mama wa eneo” ilikuwa ni kuwahudumia na kuwasaidia watumishi wa mwanae katika mahitaji yao. Suala hilo liliwafanya wamtambue Maria kama mlezi (Patroness) wa Shirika.
3. Maria Mlezi na Kiongozi wa Shirika
Wakarmeli walipomchagua Maria kuwa Mlezi lakini zaidi kuwa Mlinzi wa Shirika walijua kuwa anao uwezo na nafasi ya kufanya hivyo kutokana na neema tele alizojaliwa na nafasi yake Utukufu wa mwanae. Katika imani yetu, sisi Wakatoliki tunaamini kuwa Mwenyezi Mungu ametupatia malaika walinzi ili watulinde na watuepushe na hatari zote za kiroho na za kimwili (Rej Zab 91:11-12)[2]. Lakini ulinzi wa Bikira Maria ni wa aina yake kwani yeye ni Malkia wa malaika na mama wa Kanisa zima. Ameshiriki kwa namna ya pekee katika kazi ya ukombozi. Kwetu sisi Wakarmeli ishara ya ulinzi wa Bikira Maria ni skapulari. Imani hiyo tumeipokea kutoka kwa Wakarmeli wa kwanza kabisa ambao walijenga kikanisa cha kwanza katikati ya makazi yao, yaani katika mlima Karmeli, na wakakiweka wakfu kwa heshima ya Bikira Maria. Ulinzi wake kwa wanashirika, kama ilivyo kwa wanakanisa wote, unatokana na nguvu za neema alizojaliwa na Mwenyezi Mungu ambazo zilimwezesha kushiriki kwa namna ya pekee kabisa katika kuufanikisha mpango wa Mungu wa kuwakomboa wanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi. Kwa kuwa Wakarmeli wa kwanza walimweka Kristo katikati ya maisha yao, kama Mwongozo wa Maisha ulivyowaelekeza, walitumia muda mwingi wa maisha yao kumtafakari Yesu mfufuka, wakiamini kuwa walikuwa wakisali pamoja na Maria. Kadiri walivyokuwa wakimtafakari Kristo kwa undani zaidi, ndivyo walivyopatiwa hekima ya kuifahamu hata nafasi ya Bikira Maria katika fumbo la Kristo na la Kanisa.
4. Usafi wa moyo kwa mfano wa Maria
Inafahamika katika mafundisho ya Kanisa kuwa usafi wa Maria ambao uliotokana na kujazwa neema nyingi ulimfanya akubali mpango wa Mungu bila kusita kwa kuitikia “Ndiyo” wakati alipopashwa habari na Malaika Gabrieli. Sisi Wakarmeli, kama ilivyo hata kwa Wakristo wengine, tunaalikwa kumwiga kikamilifu Bikira Maria, aliyekingiwa dhambi ya asili na aliyejaa neema, tukiamini kuwa tunaweza kufanya hivyo kwa njia ya sala, tafakari na kusikilizaji Neno la Bwana na kushiriki Sakramenti kwa unyenyekevu mkubwa. Usafi wa Maria ni uzuri uliomvutia Mungu ambaye kwa utayari wa Maria aliipatia dunia Mwokozi. Ndiyo maana maisha ya wakfu yanamtaka mtu kuwa tayari kumsikiliza na kumwamini Mungu wakati wote ili moyo uwe safi. Sikio la Bikira Maria lilimwelekea Mungu daima[3]. Maria alimsikiliza hata mwanae katika kazi yake ya ukombozi ndiyo maana anaitwa “mwanafunzi wa kwanza wa Yesu”. Hili lilirutubishwa na usafi wa moyo aliojaliwa na Mungu naye akautunza. Kwa mantiki hiyo basi, kila Mkarmeli anayetaka kumtumikia Kristo kwa uaminifu inabidi ajifunze kutoka kwa Maria. Ndiyo maana hata Maria anaitwa mwalimu na kiongozi. Kama walivyowahi kusema watakatifu na wenye heri Wakarmeli (Kwa mfano, Elisabetta wa Utatu Mtakatifu) kuwa Maria anaonyesha njia ya utakatifu uliyomshinda Eva. Njia hiyo ni kumwamini Mungu kabisa, kumtii na kumpenda.
5. Sala endelevu, umaskini, upweke na kufunga
Tunampomtafakari Maria tunaalikwa kumwiga katika tunu zifuatazo.
(a) Sala endelevu:
Sala katika maisha ya kikarmeli ni tunu ambayo hutokana na mwito wa kumweka Kristo katikati ya mambo yote. Sala ni maongezi yenye uhusiano binafsi kati ya mtu na Mungu na humwezesha anayesali kuwa na uwezo wa kulisikiliza na kulipokea Neno la Mungu kwa utayari wa kuliweka katika matendo kama alivyofanya Maria. Tunu hii ya ndani huongeza shauku ya kumtafuta Mungu katika maisha ya kila siku. Moyo uliozoea kusali hujazwa na nguvu za Roho Mtakatifu kwa ajili ya kusimama imara katika imani kwa lengo la kuyashinda majaribu ya yule mwovu. Tabia ya kupenda sala ni tunu ya ndani kabisa ya roho ambayo mtu anatakiwa aikuze. Sala kama tabia ya kudumu ya kuufungua moyo kwa ajili ya kuongea na Mungu, humuongoza mtu katika kujifahamu vizuri na hivyo huboresha uhusiano wa kimapendo kati yake na Mungu aliye Upendo wa ndani kabisa wa roho. Anayesali kwa imani huboresha uhusiano wake na watu wengine wanaomzunguka, katika jumuiya au katika jamii. Mkarmeli anatakiwa awe mwalimu wa sala. Sehemu muhimu katika sala ya jumuiya na ya binafsi ni kushiriki adhimisho la Misa Takatifu ambayo ni chemchemi na kilele cha maisha ya kijumuiya na ya kikristo. Ekaristi ni nguvu ya maisha ya kitawa na ya kikristo kwa ujumla wake. Sala ina nguvu ambazo huunganisha moyo wa anayesali na Mungu kwa ajili ya kuonja upendo usioelezeka kwa maneno bali hutambulika katika nafsi.
(b) Ukimya
Ukimya ni mojawapo ya vitu muhimu tunavyovikuta kwa Maria na Eliya. Maria alikuwa ni mama wa ukimya na tafakari (Lk 2:19,51). Lengo kuu la kusisitiza ukimya ni kumsaidia mtu kuwa tayari kuisikiliza sauti ya Roho Mtakatifu na kumpa nafasi nzuri ya kulitafakari Neno la Mungu kwa undani na mapana yake. Mafumbo yasiyoeleweka hutafakariwa katika ukimya. Fumbo la ukombozi linahitaji ukimya. Maandiko Matakatifu yanasema kuwa Mungu wetu ni Mungu wa ukimya na hunena Neno lake katika ukimya. Lakini kuwa kimya haina maana ya kuwa mpweke, yaani mwenye huzuni asiye na neno lolote la kuongea kwa wengine na asiye na watu wengine wa kuongea naye. Hiyo si maana ya ukimya, bali ukimya ni mojawapo ya kipawa cha kihekima ambacho ni uhalisia wa mpangilio kamili wa utendaji wa haki ndani ya roho. Ushuhuda huo unapatikana katika kitabu cha Hekima ya Sulemani mahali panapoongelea tukio la kuokolewa kwa wana wa Israeli kutoka utumwani Misri, mwandishi anasema: «Kwa maana majira mambo yote yalipokuwa kimya, na usiku ulikuwa katikati ya mwendo wake mwepesi, Neno lako Mwenyezi alishuka toka mbinguni, kutoka kiti chako cha kifalme....mwenye upanga mkali» (Rej. Hek 18:14-18; Yoh 1:1.14). Kuishi katika ukimya ni kutoa nafasi ya kutosha kwa Mungu ili aweze kunena Neno lake la wokovu ambalo hufanya kazi ndani mwetu. Kuwa kimya ni kuwa katika hali ya usikivu makini kwa lengo la kusikiliza kile anenacho Mungu. Ndiyo maana nyumba nyingi za kikarmeli huweka mazingira mazuri ya ukimya na upweke, kwa lengo la kumsaidia Mkarmeli aweze kuyaelekeza mawazo na fikra zake katika mambo ya kiroho. Watakatifu wengi Wakarmeli wanasema kuwa kuishi katika hali ya ukimya kwa lengo la kuyatafakari mafumbo ya wokovu, humfanya mtu aingie katika hali ya muungano na Mungu kwa kiwango cha juu kabisa.
(c) Kufunga na kujinyima.
Kitu kingine ambacho Wakarmeli wamekiendeleza katika hali ya kumwiga Maria ni na Eliya ni kufunga na kujinyima. Maisha ya sala hupata nguvu kwa kujinyima na kufunga. Kujinyima kwa watawa ni jambo la maana sana kwani huilainisha roho na huwapatia wanaojinyima nguvu za ziada za kuitiisha miili yao ili isiwe tegemezi katika anasa za kidunia. Tendo hili la kujinyima huisafisha roho na kuifanya iwe katika hali ya kupokea mwanga wa Kristo bila kuweka ukinzani wa ndani. Nguvu za kiroho huwa ndiyo silaha za kuvishinda vishawishi viletwavyo na vionjo vya kimwili. Mtu anayetaka kuupanda mlima Karmeli kwa ajili ya kukutana na Kristo na kulipokea Neno lake, inambidi awe tayari kujikatalia kwa ajili ya Mungu na wengine. Awe tayari kumtumikia Kristo kwa: «moyo safi na kwa dhamiri njema».
(d) Umaskini au ufukara
Ni hali ya kumtegemea Mungu kwa kila kitu na kwa kila hali. Maskini ni yule asiye na kitu. Hutegemea msaada tu ili aweze kuishi. Hali hiyo ndiyo inayosisitizwa katika maisha ya Wakarmeli. Kujua kumtegemea Mungu kila siku.