Historia ya Wakarmeli
(Waeremiti) Wamonaki wa kilatini katika Mlima Karmeli Mwaka 1192 kundi la wamonaki wa kilatini (Wakarmeli) lilionekana katika mlima Karmeli. Waeremiti hao waliojulikana kama mahujaji walitokea Ulaya, walikusanyika pamoja karibu na "chemchem ya Elia", katika moja ya mabonde membamba ya Mlima Karmeli kwa ajili ya kufanya toba na kuishi maisha ya upweke na maombi. Walitaka kuishi ukristo wao waeremiti (hermits) wakiiga mfano wa nabii Elia mwanzilishi wa maisha ya kieremiti katika nchi ya Bwana wetu Yesu Kristo. Eliya anachukuliwa kama mwanzilishi na baba wa ueremiti na umonaki. Wakarmeli walibakia wafuasi waaminifu wa Eliya ambayeana uhusiano na Mlima Karmeli kupitia matukio ya Biblia. Katikati ya vyumba vyao kulijengwa kanisaambalo walijitolea kwa Bikira Maria walilijenga kwa heshima yake, Mama wa Yesu, hivyo kuendelezahisia ya kuwa Maria ni Mama yetu kama Bibi wa mahali na kama mlezi, na wao kujulikana kwa jinalake.
Kati ya mwaka 1206 na 1214 Baba Mkuu wa Yerusalemu, yaani, Patriarch wa Yerusalemu (Askofu) aliwapatia wamonaki wa kilatini (Wakarmeli) wa mlima Karmeli «Mwongozo wa Maisha». Maisha ya waeremiti katika mlima Karmeli yalikuwa ni maisha ya toba. Mlima Karmeli ulikuwa sehemu mahususi ya kutekeleza azma yao ya hija kutokana na usalama uliokuwepo mahali pale. Kiini cha safari yao katika Nchi Takatifu kilikuwa ni kufanya hija takatifu ya toba katika ardhi alipozaliwa Bwana Yesu Kristo na kumtumikia. Kwenda kuhiji kulitafsiriwa kama kitendo cha «kujiachilia» kwa ajili ya kuambatana na Bwana kama walivyofanya Mitume. Kipindi kile, mhujaji alichukuliwa daima kama mtu mdogo kabisa katika jamii, yaani mtu asiye na usalama katika maisha yake, hivyo aliishi kwa kumtegemea Mungu zaidi.
Kuidhinishwa kwa formula vitae kuwa Kanuni rasmi
Shirika la wakarmeli lilianzia katika mlima Karmeli ulioko kule Israele (Palestina). Ampapo Alberto Avogadro, Patriarka wa Yerusalemu kati ya mwaka 1206 na 1214 aliwapatia wamonaki wa kilatini waliokuwa wakiishi Mlima Karmeli kanuni ya maisha (formula vitae). Kanuni hii ilikubaliwa na Papa Onorio III tarehe 30.1.1226, halafu tena ikaidhinishwa na Papa Gregori IX tarehe 6.4.1229 na tena ikaidhinishwa na Papa Innocent IV tarehe 8.6.1245. Papa huyu wa mwisho hatimaye aliipitisha kanuni hiyo tarehe 1.10.1247 kwa sherehe kuwa kanuni ya kudumu ya shirika la kitawa la Wakarmeli. Kwa kupitishwa kanuni hiyo wamonaki walianza kutambulikana kuwa ni watawa rasmi. Baada ya hapo shirika limeendelea kukua na kusambaa sehemmu mbalimbali duniani
Kitendo cha kujikuta katika nchi ya kigeni kiliwafanya waishi maisha ya unyenyekevu na ya kujitoa sadaka huku wakimtegemea Mungu kwa kila jambo. Ilikuwa ni njia mojawapo ya kuachana na usalama wa kibinadamu. Imani hiyo iliwasukuma kuishi maisha ya «toba» na ya «kujitoa sadaka» muda wote wa maisha yao. Wakiwa katika mlima Karmeli wamonaki hao waliweza kuishi katika hali ya upweke, ukimya, sala huku wakilitafakari Neno la Mungu usiku na mchana. Sala walizokuwa wanamwinulia Mungu, zilikuwa ni matunda ya tafakari ya Neno la Mungu. Mzizi wa maisha yao uliwekwa katika tafakari (contemplation) na sala. Katika hali kama hiyo ni wazi walikuwa wakimwiga Yesu Kristo na Mitume ambao walikuwa ni watu wa sala na tafakari (Mdo 6:4). Kwa upande wake, Yesu alipenda kusali daima mahali palipotulia: «Lakini yeye alikuwa akijiepusha, akaenda mahali pasipokuwa na watu, akaomba» (Lk 5:16); vile vile «Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake» (Math 14:23).
“Propositum” ya Wakarmeli wa Kwanza
(Propositum maana yake mapendekezo)
1. Wakarmeli wanamwendea Mt. Albert
Wakarmeli walioishi mlima Karmeli walimwendea Mt. Albert –aliyekuwa Patriarka wa Yerusalemu wakimwomba awapatie Mwongozo wa maisha. Yeye aliwaambia wamempelekee mapendekezo ya jinsi wanavyotaka kuishi. Mapendekezo hayo ndiyo yanayoitwa “Propositum”
2. Lengo
Kuwa na maisha yenye utaratibu
Toka mwanzo walikuwa na nadhiri ya kutorudi nyumbani kwao.
Huduma kwa Kristo – kuishi katika kumfuasa Yesu Kristo, “In Obsequio Iesu Christi”. Katika Propositum, anatajwa mtu aliyekuwa kama kiongozi wao, “B”.
Hivyo “Kanuni ya Maisha”, aliyowapatia Mt. Albert, ilitokana na Propositum yao.
3. Norma di Vita, Kanuni ya maisha
Maisha yao yalikuwa ya kimonaki lakini yakiwa na chembechembe za kijumuiya.
Yesu aliwekwa katikati ya maisha yao –kwa neno “obsequio”. Kumtegemea Yesu kwa kila kitu: Sura-7 na 18. Kristo kama nguvu Sura 10. Kutenda kadiri ya Nafsi ya Yesu 14. Matunda ya mfufuka Sura ya 9-10. Yote hayo yanafanyika katika ufunguo wa kitovu cha maisha ya Utatu Mtakatifu Sura 8, 14,15.
4. Kanuni na kukua kwa nafasi ya mtu
Kanuni ya maisha imepangwa kwa kufuata mpango wa kumfanya mtu aweze kukua kiroho; kupitia sala, kusoma Biblia, kukesha, na kusali Zaburi, Sura 7 na 8. Kushirikisha zawadi Sura 9. Usawa wa ndugu Sura 1. Kushiriki Ekaristi Takatifu Sura 10. Kuwajibika kijumuiya kutunza mali kundi Sura 11. Huduma na mamlaka ya Kanisa Sura 1 na 17 na 18. Inalenga kumwimalisha mtu kwa kupitia kufunga na kujinyima, silaha za kiroho, kazi za mikono, ukimya, Sura 12 na 16.
5. Ekaristia
Inawataka wote kukutana ili kuweza kuadhimisha Ekaristi Takatifu. Inawaongoza katika umoja wa kishirika ili kuweza kuunda jumuiya. Hiyo ndiyo iliyokuwa jumuiya ya Yerusalemu.
Mabadiliko ya wakati ule
6. Migogoro na unabii katika Kanisa
Kipindi hicho mkazo uliwekwa hasa katika kuhubiri , Sakramenti, Uadhimishaji wa Misa, Maandamano, Indulgensia, na Katekesi kidogo. Na ushiriki kwa kiwango kikubwa katika Vyuo Vikuu. Lakini kilikuwa kipindi cha mganganyiko.
7. Mambo makuu mawili ya wakati ule yaliyokuwa yakisigana.
(a) Hali ilikuwa imechafuka kidogo: Watawala wa Kanisa walijihusisha katika mfumo wa maisha ya kipindi kile uliofahamika kama “”, yaani, (i) kumiliki sehemu kubwa ya ardhi kwa ajili ya kupata faida, uhusiano wa kisiasa, na kiuchumi, (ii) Kuuza vitu vya Kanisa na huduma za kiroho, (Mdo 8:18-24), (iii) uasherati wa makleri, na (iv) Wamonaki walikuwa wameanza kuwa matajiri.
(b) Wengine walikuwa wakijitahidi kuleta mabadiliko katika Kanisa. Mabadiliko ambayo Papa Gregorio aliyafanya kwa mafanikio makubwa. Lakini pamoja na hayo hali ya kimaadili ilibaki bado tete. Ndipo hapo ilipozaliwa roho mpya ya kufanya utume na kuhubiri.
8. Pentekoste mpya
Baada ya mambo hayo huyo roho wa pentekoste mpya aliwaongoza Wakristo kurudi kwenye uhalisia wa Ukristo: kwa kulipokea Neno la Injili, kwa kuanza kuishi maisha ya kubana sana na ya kawaida. Wakaanza kusisitiza juu ya umaskini na kujikataa/kujikana mwenyewe. Wakaanza kusisitiza juu ya ubinadamu wa Yesu Kristo na ufuasi wake. Ikaingia sana dhana ya umaskini wa Kiinjili na umaana wa kuishi maisha ya kijamii. Kwa kweli walichokigundua ni kuanza kulisoma Neno la Mungu. Hayo yote yalikuwa yakifanywa na vikundi mbalimbali vilivyoishi kifukara.
9. Mashirika Ombaomba
Kulingana na hitaji la Kikristo la wakati huo, yakazaliwa Mashirika ombaomba ya kitawa Wafransiskani na Wadominikani n.k. Walisema “Maisha ya Kitume” maana yake ni kuishi maisha ya pamoja na ya kimaskini au ya kifukara, na kuhubiri sehemu mbalimbali, kutembea kwa ajili ya kueneza Neno la Mungu. Maisha haya yalionekana kuwa jibu kwa mahitaji ya wakati ule. Kanisa ilibidi liwe Maskini Mchumba wake Kristo aliye Maskini.
10. Hivyo Mashirika Ombaomba yaliishi:
(a) Maisha ya kimaskini kwa kuombaomba. Kama njia sahihi ya kuwafunza watu kujua thamani ya maisha kuwa haiku katika wingi wa mali. Bali maisha ni kugawana kile kilichopo.
(b) Walianza kutembea huku wakihubiri.
(c) Walianza kuishi maisha ya kindugu. Wote walikuwa sawa, wakitoa huduma kwa wahitaji.
(d) Mashirika yao yalikabiliana na hali kulingana na mahitaji wa mahali.
(e) Kwenda mahali popote pale waliposikia kuna hitaji la kiroho. Hawakukaa Ofisini, bali walikwenda wenyewe kwa watu kuwapelekea huduma.
(f) Walianza kusoma katika Vyuo Vikuu.
11. Umonaki
Watu walijisikia hamu ndani ya mioyo yao ya kujitenga na mambo ya kidunia. Walitafuta maeneo yenye ukimya. Wamonaki wanaweza kuishi kila mtu peke yake au katika jumuiya. Haya yalionekana kuwa ndiyo maisha makamilifu. Waliweza kuishi katika monasteri mojawapo au la. Walioishi maisha haya, walilenga kuishi maisha ya toba na ya mabadiliko. Maisha yao yaliambatana na kufanya hija maeneo mbalimbali.
Wao katika maisha yao walifanya mambo yafuatayo: Upweke, Maombi yaliyoambatana na Lectio Divina, Kufunga na kujitesa kimwili, kufanya kazi, na kutoka kwenda kuuza mazao yao. Haya maisha hayakuzingatia kutembea kuombaomba na kuhubiri.
12. Vikundi vya Walei waliofanya toba
Wakati hayo yakitokea, hata Walei nao walikuwa na vikundi vya vya toba, kujitesa, kujisomea Neno la Mungu n.k.
13. Hija
Waliohiji walizingatia maisha yao ya kiroho kuwa wazi kwa Mungu. Hawana tena makazi. Hawana usalama, ilikuwa alama ya kujiachia kwa Mungu. Ni mtu asiyetegemea usalama wa kibinadamu. Ni ishara ya yule ayatafutayo ya juu. Ili kuepuka kwenda tu katika kundi wahujaji walikuwa wakipewa fimbo, vazi maalum na kupokea baraka, wakiahidi kuyabadili maisha yao. Hawa walienda maeneo mbalimbali ya Watakatifu.Hija kubwa ilikuwa ile ya kwenda Nchi Takatifu.
Ukimya –nyenzo ya kujifahamu
1. Ukimya na ukomavu wa kibinadamu
Katika utamaduni wa Kikarmeli, Ukimya ni kitu muhimu sana katika maisha, ni kuishi katika uwepo wa Mungu. Ni nyenzo inayomwezesha mtu kuwa makini kuisikiliza sauti ya Mungu inayoongea katika nafsi. Unaunganishwa na uzoefu wa jangwa na upweke. Vitu hivi havitegemea jiografia ya kweli. Bali ni uwezo wa roho kuzalisha hali kama hiyo. Ni kuishi ukweli wa kibinadamu, kuishi katika upendo wa kweli, katika uhusiano na wengine.
2. Ukomavu wa kibinadamu
Ukomavu wa kibinadamu ni uwezo wa mtu kuishi katika “mahusiano” mazuri na watu wengine. Uhusiano wa yeye mwenyewe, na asili na Mungu. Kufahamu uwezo wake na kuuweka katika vitendo.
3. Aina mbalimbali za ukimya
Ukimya wa nje wa maneno na matendo, ukimya wa ndani wa uwezo mkubwa wa kibinadamu, na ukimya wa kufikirika, wa akili, na wa kupenda, ni ukimya unaousikia na kufahamu (aware, conscious). Kuna ukimya usioufahamu (unconscious), unaotakasa, unaounganisha, na unaoleta amani ya ndani. Ukimya hufunua uhalisia wa roho na undani wake.
4. Hatari ya baadhi ya ukimya
Ukimya unaweza kuwa kitandawili, unaweza kumwongoza mtu kuelekea ukamilifu wa upendo na ushirika au unaweza kuzaa ubinafsi, kijifunga rohoni, na hatimaye kuwakimbia wengine na kujiwazia mwenyewe kwa faida binafsi. Ukimya wa kweli unatakiwa umweka mtu mbele ya Mungu na kumfanya amtamani zaidi.
5. Upweke ni asili ya ubinadamu
Mwanadamu anapokutana na matatizo ambayo hawezi kuyatatua kwa wakati njia pekee ni kuingia ndani mwake na kuishi hali hiyo kwa upweke wa ndani. Jambo hilo humsaidia akutane na Mungu. Upweke wa ukimya ni kujikubali kama ulivyo, na kuwakubali wengine kuwa ni tofauti na wewe. Kumbe basi, yule anayeishi upweke na ukimya wa kweli huwa na uwezo mkubwa wa kujifunua kwa wengine na kuongea nao. Ni uwezo wa kweli wa kupenda. Ili uweze kufikia ushirikiano wa kweli, na kushirikishana maisha, kama kipimo cha upendo wa kweli, mtu anatakiwa awe na asili ya upweke na ukimya. Kumbe basi, ukimya ni nyenzo ya ukomavu wa kibinadamu. Unajisikiliza, unajijua, unajipima, na kuamua njia ya kufuata kwa upendo kwa nia ya kuishi na wengine vizuri. Ukimya unakufanya ukifikia kina cha ubinadamu wako. Ukimya unayapanga maneno ili yawe ya kufaa zaidi katika maisha. Ukimya ni nyenzo ya uhusiano.
6. Mfano katika Biblia
Tunaambiwa kuwa Maria na Eliya, walikuwa watu wa ukimya. Mwingine anayetajwa ni Yesu. Hawa walifahamu kwenda kwenye kina cha ubinadamu na mahitajika yake ya kina.