Sala ya ufunguzi
Tunafikia tamati ya kipengele cha ishara. kilichotawa katika sehemu hii ni mabishano makali kati ya Yesu Kristo na jamii ya watawala wa kidini.
Tunachokiona hapa ni kuwa watu wanamwihitaji Yesu. Wanakwenda wenyewe. Kunahitajika ushirikiano wa watu wengine na mazungumzo na Yesu ili kuweza kufika kwake Yesu Kristo. Wanamwendea yeye ambaye anagusia kifo chake kuwa ndicho kitakachowavuta watu wengi. Si hekima ya elimu ya falsafa au kitu kingine.
Tunamwona Yesu akiwa katika mateso, (kwa wainjili wengine ni Getsemani) kabla hata ya Mateso yake ya wazi. Roho iko katika mateso. Lakini anasisitiza kuwa kufa ni lazima ili uzima uweze kuchipuka.
Somo la Injili
20 Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.
21 Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.
22 Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.
23 Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.
24 Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.
25 Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.
26 Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.
27 Sasa roho yangu imefadhaika; nami nisemeje? Baba, uniokoe katika saa hii? Lakini ni kwa ajili ya hayo nilivyoifikia saa hii.
28 Baba, ulitukuze jina lako. Basi ikaja sauti kutoka mbinguni, Nimelitukuza, nami nitalitukuza tena.
29 Basi mkutano uliosimama karibu wakasikia, walisema ya kwamba kumekuwa ngurumo; wengine walisema, Malaika amesema naye.
30 Yesu akajibu, akasema, Sauti hiyo haikuwako kwa ajili yangu, bali kwa ajili yenu.
31 Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.
32 Nami nikiinuliwa juu ya nchi, nitawavuta wote kwangu.
33 Aliyanena hayo akionyesha ni mauti gani atakayokufa
Kimya kidogo
Soma tena na tena
"Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu"
Wayunani walikwenda kuabudu na baadae wanamwomba Filipo waonane na Yesu. Hawa ni watu ambao walikuwa wakiifuata dini ya kiyahudi ijapokuwa wao wenyewe hawakuwa wayahudi.
lakini kama tunavyoona ghafula Yesu anaanza kuongelea saa ya kutukuzwa kwa Mwana wa Adamu. Watu wawili wanawasaidia ili waweze kumwona Yesu. Katika maisha tuige kuwapokea wageni, na kuwasaidia kufika kwa Yesu. Mioyo yetu iwe wazi. Jiulize wewe umeisha wasaidia wangapi ili waweze kufika kwa Yesu? Taratibu zetu kwenye jumuiya zinawasaidia watu kumwona Yesu Kristo? Leo Filipo ni nani? Filipo wa leo ni jumuiya. Ni wanajumuiya. Mnakuja kwa paroko ikiwa kama Andrea mnamwomba hawa wanataka kumwona Yesu. Wanataka sakramenti. Hapo ndipo Yesu anasema anatukuzwa. Lakini tunafanya hayo yote?
Majibu ya Yesu ndiyo yanayoshangaza kidogo. Yesu hasemi neno lolote la ukaribisho kwao, bali anaanza kuongelea maisha yake na matunda yatokanayo na maisha yake. Anataka kuwaambia kuwa kinachowavutia zaidi ni kifo chake. Yesu ameisha kiona wazi wazi, amekitafakari na kuona matunda yatakayo tokea kupitia kifo chake. Anawaambia kuwa yeye ni maisha ambayo karibu yatanyamazishwa na kuharibiwa. Hivyo alikuwa anawaalika wasimtafute kama mwanadamu shujaa na hodari, bali watafute utukufu wake unaopatika kupitia mateso na kifo. Hili ndilo lilikuwa jibu la ukaribisho la Yesu Kristo kwao. Leo wewe ujumbe huu una maana yeyote? Unajisikia kumtafuta Yesu Kristo? Kwa nini unamtafuta, kwa nini unamtafuta?
Kuchukua msalaba na kumfuata Yesu. Kuwa tayari kuishi maisha ya kujitolea. Maisha ya kujisadaka kwa ajili ya Kristo. Anaongelea kuwa mfuasi wa kweli inabidi amtumikie Yesu.
Yesu anadhihirisha ubinadamu wake katika kusikia ukali wa mateso, mbele ya mateso makali na ya aibu Yesu anaogopa (Mk 14:). Yesu anakabiliana na hali hii kwa kujiaminisha kwa Mungu Baba.