EDITH STEIN –TERESA BENEDIKTA WA MSALABAUkweli wa msalaba –Kristo ni nguvu ya Mungu (Rum 1:16)
Hamu ya kutafuta ukweli -Alielewa maana ya mateso na thamani yake katika maisha
"We lock ourselves into the prison of our individuality when we take the self as the standard"
"Tunajifunga wenyewe kwenye gereza la ubinafsi wetu wakati tunapochukulia kuwa nafsi ni kiwango". Inabidi kuwa makini na self -nafsi. Kiwango chetu cha kuishi si sisi wenyewe.
Maisha yake
Edith Stein alizaliwa Oktoba 12, 1891 huko Breslau, Ujerumani,, katika familia ya kiebrania -kiyahudi. Baba yake aliitwa Siegried Stein na mama yake aliitwa Auguste Courant. Alikuwa mdogo kabisa kati ya watoto 11. Toka miaka yake ya kwanza ya alionesha hali kubwa ya kujifunza. Wakati Vita Kuu ya Dunia inazuka, yeye alikuwa tiyari amesoma Filolojia na falsafa katika vyuo vikuu vya Breslau na Goettingen. Baada ya vita, aliendela na masomo yake ya juu katika Chuo Kikuu cha Freiburg na kupata tuzo Suma Cum Laude ya udaktari katika nyanja ya falsafa. Baadaye akawa msaidizi na mshirika wa Profesa Husserl, mwanzilishi maarufu wa fenomenolojia, ambaye alimpenda sana kwa akili yake kipaji na kipaji chake.
Katikati ya masomo yake yote, Edith Stein alikuwa akitafuta si tu ukweli wa maisha bali Ukweli wenyewe (Yesu Kristo) na aliupata katika Kanisa Katoliki, baada ya kusoma maisha ya Mtakatifu Teresa wa Avila. Akabatizwa mwaka mpya, 1922.
Katika Karmeli
Baada ya kuongoka kwake, Edith alitumia siku zake akifundisha, akielekeza, akiandika na kutafsiri, na hivi ghafula akajulikana kamamwanafalsafa na mwandishi aliyesifika, lakini yeye alitamani sana maisha ya upweke na tafakari za Karmeli, ambapo angeweza kujitoa kwa Mungu na kwa watu wake. Kutokana na dhuluma za kinazi dhidi ya wayahudi shughuli zake zilizofahamika kwa umma na kupata ushawishi katika ulimwengu Katoliki zilikuwa zimekoma. Mshauri wake wa kiroho alimruhusu aingie monasteri ya Wakarmeli huko Cologne-Lindenthal tarehe 14 Oktoba 1933. Mwezi Aprili 1934, Edith alipokea vazi na kupewa jina la Teresia Benedikta wa msalaba. Aliweka nadhiri tarehe 21 mwezi wa nne mwaka 1935 Jumapili ya Pasaka.
Alipata ugumu wa kujifunza taratibu na sheria za shirika lakini alijifunza kwa furaha kwa sababu alichagua mwenyewe maisha yale. Japokuwa alikuwa msomi lakini aliishi kwa unyenyekevu. Chumba chake kilikuwa cha kimaskini lakini hakuwahi kujutia chaguo lake. Alipojiunga Karmeli mama yake alisikitika sana. Lakini yeye alisema atamwombea kwa Mungu ili alipokee chaguo lake. Kimsingi maisha yake mapya yalionesha kuwa si kwamba alikuwa amejikatilia bali alikuwa amekamilishwa -fulfilled. Aliwahi kumwambia mkuu wake kuwa katika maisha yake hakuwa kucheka kama anavyocheka wakati wa kukaa pamoja, recreaction. Furaha yake ya kiroho ilitokana na muungano wake Mungu. Pamoja na hayo inasemwa kuwa kila Ijumaa alikuwa akimwandikia mama yake lakini hakuwahi kumjibu hata mara moja. kitu hicho kilimuumiza.
Anahamia Uholanzi
Wakati mateso ya Wayahudi yalipoongezeka na vurugu za ushabiki, Sister Teresa Benedikta alitambua mapema hatari ya uwepo wake pale Karmeli ya Cologne, akaomba na kupata ruhusa ya kuhamia monasteri ya nje ya nchi. Usiku wa tarehe 31 Desemba mwaka 1938, alivuka mpka kwa siri na kuingia Uholanzi ambako alipokelewa kwa furaha na Wakarmeli wa Echt. Pale ndipo alipoandika kazi yake ya mwisho, Sayansi ya Msalaba.
Ushuhuda wake
Aliyatafsiri mateso ya wayahudi taifa lake katika mwanga wa mateso na msalaba wa Kristo. Aliandika hivi katika sala yake:
“Niliongea na Mwokozi kumwambia kwamba nimetambua kuwa ni msalaba wake ambao sasa umewekwa juu ya wayahudi, kwamba wachache waliolielewa hili walikuwa na jukumu la kuubeba kwa niaba ya wote na kwamba mimi mwenyewe nilikuwa tayari kufanya hivyo kama angeweza tu kunionesha jinsi ya kufanya. Niliondoka katika huduma nikiwa na imani ya ndani kwamba Mungu alikuwa amenisikiliza, lakini sikuwa na uhakika kamwe “kubeba Msalaba” kungekuwa na maana gani kwangu”.
Tena aliandika hivi:
“Nilielewa Msalaba kama hatima ya watu wa Mungu, ambao mwanzoni ulikuwa dhahiri (1933). Nilihisi kuwa wale ambao wanauelewa msalaba wa Kristoinawapasa kuuchukua juu yao wenyewe kwa niaba ya kila mtu .... Chini ya Msalaba nilielewa hatima ya watu wa Mungu.”
Kilichomfanya ateseke ni empathy -uwezo wa kuelewa na kushiriki hisia za mtu mwingine. Nikikutazama naona nini. Mwanadamu ameitwa kujishinda mwenyewe.Ndiyo maana anasema hivi: "ukitaka kuteseka kwa ajili ya wengine lazima uwe de-centering the self through a transcendent exercise of the free will". Sehemu hii inafanana na ile aliyosema Yesu Kristo -kujikana mwenyewe. Neno transcendenti lina maana hali ya kuwa mbali zaidi ya uzoefu wa kawaida wa kibinadamu na wa kimwili tu.
Kifo chake
Alikuwa tayari kukabiliana na yote kwa sababu ya imani yake. Alifanya hivyo kwa sababu ya taifa lake pia. Msalaba wake ulikuwa mbele yake. Wanazi walivamiaUholanzi, Maaskofu wa Uholanzi walitoa barua ya kichungaji ya kupinga kufukuzwa kwa wayahudi –waebrania na kufukuzwa kwa watoto Wayahudi kutoka katika mfumo wa shule za Katoliki. Wanazi waliwakama wakatoliki wote wa kiyahudi katika Uholanzi. Edith alichukuliwa kutoka Echt Karmeli tarehe 2 Agosti 1942, nakusafirishwa kwa treni ya ng'ombe kwenda kwenye kambi ya kifo ya Auschwitz. Hali ya chumba alichosafiria haikuwa ya kibinadamu kwamba watu wengi walikufa njiani maana safari ilikuwa ya siku nne. Alifariki tarehe 9 Agosti 1942 katika chumba cha gesi pale Auschwitz siku chache baada ya kuwasili.
Kumbuka alikuwa ameandika hivi:
“Kwa furaha nilikubali mapema kifo ambacho Mungu amenichagulia, kwa ukamilifu nikijiweka chini ya mapenzi yake matakatifu sana. Bwana akubali maishayangu, na kifo changu kwa heshima na utukufu wa jina lake, kwa mahitaji ya Kanisa lake takatifu - hasa kwa ajili ya kuhifadhi, utakaso, na mwisho kwa ajili ukamilifu wa shirika letu takatifu, na hasa kwa ajili ya Karmeli ya Cologne na Echt - kwa ajili ya wayahudi ya kwamba, Bwana aweze kupokelewa na watu wake mwenyewe na Ufalme wake uje katika utukufu, kwa ajili ya ukombozi wa Ujerumani na amani duniani kote, na hatimaye kwa ajili ya jamaa zangu wote walio hai na wafu na kila mtu ambaye Mungu amenipa; asipotee hata mmoja wao”.
Kutangazwa mwenye heri na Mtakatifu
Papa Yohane Paulo II alimtangaza mwenye heri tarehe 1 Mei 1987, na akamtangaza Mtakatifu tarehe 11 Oktoba 1998.