Mapadre waitaliano wa Komisarieti ya “Santa Maria La Bruna” walipata wazo la kuanzisha misheni hapa Tanzania tangu mwaka 1988, baada ya kupokea barua kutoka kwa Masista Wakarmeli ambao ndiyo kwanza walikuwa wamefika hapa Tanzania mwaka 1984 kwa ajili ya kuanzisha misheni yao. Katika barua hiyo, Masista waliwashauri mapadre wa Napoli waanzishe misheni Tanzania. Mapadre walilipokea wazo hilo kwa utayari, lakini wakati huo huo walikuwa wakikabiliwa na uhaba wa mapadre. Ijapokuwa wazo lilikuwa zuri, walishindwa kulitekeleza upesi kutokana na uhaba wa mapadre waliokuwa nao. Kutokana na sababu hiyo, waliamua kuwa, ili kutekeleza nia yao hiyo, malezi ya vijana waliokuwa wakitaka kujiunga na Shirika, yafanyike kule kule Napoli, Italia. Vijana wa kitanzania walikwenda kusoma na kufanya malezi Italia. Jukumu la kuwasiliana na kuwakusanya vijana liliwekwa mikononi mwa Masista wakiongozwa na Sista Emmerensiana. Vijana waliopiga hodi walielezwa lengo la mapadre na mpango mzima waliokuwa nao wa kutaka kufungua misheni hapa Tanzania. Wale waliokuwa tayari walikwenda Italia kwa ajili ya malezi na masomo ya falsafa na teolojia. Mapadre wakarmeli waitaliano walitaka Watanzania wawe wamisionari katika nchi yao wenyewe. Mtanzania wa kwanza Mkarmeli kupewa Daraja ya Upadre ni Paulo Innocent Kaigarula, O.Carm. Mkarmeli wa pili Mtanzania kupewa Daraja Takatifu ya Upadre ni Pd. Thomas M. Mtey, O.Carm. ambaye alipadrishwa tarehe 19.11.2006 huko huko Napoli, Italia. Padre wa tatu ni Pd. Dominic M. Somola, O.Carm. aliyepadrishwa tarehe 24.08.2012 hapa hapa katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Vile vile kuna mapadre wengine watatu Pd. Paulo M. Malewa, O.Carm, Pd. Paschal M. Shirima, O.Carm. na Pd. Victor M. Biramata, O.Carm. Hawa watatu waliweka nadhiri za muda tarehe 13.09.2009 na wakaweka nadhiri za daima tarehe 05.12.2012 huko Napoli Italia. Walipewa Daraja Takatifu ya Ushemasi tarehe 4.1.2013 na Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo na kupewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 5.7.2013 na Mhashamu Askofu Titus Mdoe askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Baada ya kipindi cha masomo walisafiri toka Napoli Italia usiku wa tarehe 30.09.2009 na kuwasili Tanzania 1.10.2009 na hivyo ukawa mwanzo wa uwepo wa Wakarmeli bunju "A". Konventi ilibarikiwa tarehe 8.10.2009 na Mhashamu Askofu Methodius Kilaini, aliyekuwa askofu msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam. Mapadre wakarmeli wanafanya kazi katika Jimbo Kuu la Dar es Salaam katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli iliyotangazwa parokia tarehe 24.8.2012 wakati wa upadrisho wa Padre Dominic John Somola.
Baada ya kukamilisha malezi na maandalizi yaliyostahili, na kupokea baraka kutoka kwa Mkuu wa Komisarieti Pd. Alfredo M. Di Cerbo, tulianza safari ya kurejea tena Tanzania tukiwa tayari kwa ajili ya kufungua nyumba. Safari yetu ya kurejea Tanzania ilianza jioni ya tarehe 30.09.2009. Aliyekabidhiwa jukumu la kuongoza kundi letu la wamisionari wa “nyumbani” alikuwa ni Pd. Thomas M. Mtey, O.Carm. Siku yetu ya kwanza kuwa hapa Tanzania kama wamisionari ilikuwa ni tarehe 01.10.2009, siku ambayo ni sherehe ya Mt. Teresia wa Mtoto Yesu msimamizi wa misioni zote duniani. Mt. Teresia wa Mtoto Yesu ni Mkarmeli. Konventi yetu ilibarikiwa tarehe 08.10.2009 na aliyekuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaama, Mhashamu Methodius Kilaini. Tulianza kuishi rasmi katika konventi yetu tarehe 10.10.2009 baada ya kukaa kwa Masista Wakarmeli walioko Boko kwa wiki moja. Tarehe 30.11.2009 tulienda kujitambulisha kwa Kardinali Polycarp Pengo ambaye alitupokea kwa furaha na akatupa baraka zake za kibaba.
Mwaka 2014 Julai vijana wanne walifika Bunju kuanza uzoefu wa maisha, ya Karmeli. Baada ya mwaka mmoja wa uzoefu, walipenda maisha ya Wakarmeli na kuteuliwa na Shirika kuendelea na malezi. Tarehe 2 Novemba, 2015 walifika Morogoro kuanza falsafa kwenye Chuo cha Jordan (Jordan University College). Majina yao ni Dicksoni Sambala, Athanas Ngasa, Pascal m. Dominic na Deogratias Peter. Kulingana na changamoto za malezi na wito kijana mmoja aliondoka na kurejea nyumbani mwaka 2016. Kwa sasa kuna wanafunzi tatu (3) (postulants) ambao wamemaliza mwaka wa kwanza wa falsafa. Baada ya masomo ya falsafa, kwa wanao chaguliwa kuendelea, hutumwa nchini Zimbabwe kwa ajili ya noviziato.
Wanafunzi waliobaki baada ya kuondoka kwa mwanafunzi mmoja. Mwaka huu wa 2016 wanaingia mwaka wa pili wa falsafa.
Kundi la kwanza la vijana watatu Wakarmeli waliolelewa Tanzania lilianza unovisi 21 Julai, 2018, mara baada ya kumaliza masomo ya falsafa pale Morogoro. Walienda Zimbabwe kwa ajili ya kipindi cha unovisi cha mwaka mmoja kulingana na katiba za Shirika. Vijana hao walikuwa Dickson Richard Sambala, Athanas Mhina Ngassa na Pascal Dominic Mkaka. Waliondoka tarehe 20 Julai, 2018. Walichelewa kwenda kwa sababu walichelewa kumaliza mitihani yao ya chuo. Kwani walitakiwa kuanza unovisi tarehe 6 Julai, 2018 lakini haikuwezekana. Mwalimu wao Fr. Victor Alphonce Biramata, O.Carm na Mkuu wa shirika alijaribu kuwaombea ruhusa chuo lakini ilishindikana. Ndipo alipomwandikia Mkuu wa Shirika Zimbabwe akimwomba waanze unovisi mwishoni mwa mwezi wa saba, ndipo alipokubali na kumwambia kuwa hamna shida. Hii ilikuwa ni mara yao ya kwanza kutoka nje ya Tanzania.
Toka kushoto frt. Victor Alphonce Biramata, frt. Paschal James Shirima, Askofu Methodius Kilaini, Padre Thomas Raphael Mtey, Frt. Dominic John Somola, frt. Paul Dominic Malewa na Mpostulanti Richard Munishi. Kundi la kwanza la wakarmeli watanzania waliofungua misheni bunju Dar es Salaam 2009 wakiwa na askofu Methodius Kilaini siku alipobariki nyumba yao tarehe 8.10.2009.