TumsifuYesuKristu ………
Kwa jina naitwa Athanas Mhina Ngassa, mimi ni miongoni mwa vijana waliojiunga na Shirika la Wakarmeli, O.Carm mwaka 2014kwa lengo la kuwa mtawa na padre. Nilizaliwa tarehe 4 Julai mwaka 1992 katika mkoa wa zamani wa Shinyanga ambao kutokana na kugawanywa na serikali mahali nilipo zaliwa kwasasa ni kijiji cha lugunga wilaya mpya ya Mbogwe ya mkoa wa Geita. .
Kabla sijaeleza historia yangu fupi napenda kumshukuru Baba wa Mbinguni kwa zawadi njema ya wazazi na uhai anaotutunukia sote hadi sasa, pia ninawashukuru wazazi, walezi na wanajamii wote waliopo sehemu mbalimbali ambazo nimefanikiwa kuishi kabla ya kuitikia mwito huu wa kujiunga na maisha ya malezi ya upadre na utawa katika Shirika la Wakarmeli.
Kuhusu familia yangu ni kuwa baba yangu mzazi anaitwa Simon Ngassa Sitta na Mama anaitwa Maria Nyanzala Lazaro. Wazazi wangu kwa sasa wanaishi Ifakara. Mimi ni mtoto wa saba kati ya watoto nane wa familia yetu. Nilianza masomo yangu ya elimu ya msingi katika kijiji cha Lugunga mwaka 2001 na kumaliza darasa la saba mwka 2007. Nilifaulu na nilichaguliwa kujiunga na sekondari ya Lugunga ambapo nilisoma kati ya mwaka 2008 na 2011. Mwaka 2012 nikajiunga na kidato cha tano na sita katika shule ya Kigoma sekondari ambapo nilimaliza mwaka 2014.
Tangu nasoma nilitamani sana kuwa mapadre. Niliamini kuwa huu ndio wito wangu. Hivyo nilipomaliza masomo ya kidato cha sita, nikaanza juhudi za kuitikia sauti hii. Nilitafuta mashirika mbalimbali. Nilifanikiwa kufahamu Shirika la Wakarmeli baada ya kusoma kwenye mtandao. Nilivutiwa nalo na kuamua kuwatafuta. Nilifanya mawasiliano na mapadre, nikaondoka kwenda kujiunga na Shirika. Nilipoenda nikafikia kwa Wakarmeli wa OCD walioko kihondo. Lakini nikaona ni tofauti na jinsi nilivyokuwa nimesoma kwenye mtandao. Kutokana na kutoyamudu maisha ya kule, ilinibidi nilinde wito wangu kwa kutafuta sehemu nyingine. Nilipouliza vizuri ndo nikajua kuwa wapo pia Wakarmeli wa O.Carm ambao ndio wale niliokuwa nimewasoma kwenye mtandao. Basi Mwezi wa saba niliwasili kwenye konventi ya Mapadre watawa wa Shirika la Wakarmeli bunju. Baada ya kujiunga nilivutiwa zaidi na namna yao ya maisha, na hii ilikuwa mara baada ya kuelezwa taratibu za namna yao ya kuishi. Zaidi ni Shirika ambalo lipo chini ya mapadre wazawa wakitanzania hiyo pia ikawa ni sehemu ya kunitia moyo zaidi kuwa naweza kuungana na kaka zangu katika Karmeli na nikawa sehemu ya jumuiya yao na si hivyo tu bali nikawa sehemu ya uenezaji Injili.
Baada ya kujiunga rasmi nilifurahishwa zaidi na karama ya Shirika ambayo inamwaliko wa kuishi maisha ya Utii kwaYesu Kristu kupitia maisha ya Tafakari (contemplation), kindugu (fraternity) na huduma kwa watu (service in the midst of the people). Maisha ya tafakari ni namna ya kuishi kwa kuufuata uwepo wa Mungu na kujitahidi kuwa karibunae. Msingi wa maisha ya tafakari ni Neno la Mungu. Maisha ya tafakari ni namna ya kuuishi muungano na Mungu, na katika kuwa na muungano na Mungu wote hufanywa kuwa ndugu na hivyo kuishi kama ndugu na si bwana na mtumwa wake bali kama kaka na ndugu yake ambao wote huelekezana kwa utaratibu na kila mmoja husikiliza uhitaji wa mwingine. Jambo hili hufikisha jumuiya kwenye upeo wa kusaidiana kwa kumhusisha mwingine kutoa utumishi kwa wengine na kila mmoja kwa mwenzake pia na baadaye kutoa huduma kwa wengine nje ya jumuiya yao.
Kwangu kuishi katika jumuiya yenye upendo na namna ya kikristo kama hii inanitia changamoto zaidi katika kuuacha ubinafsi wangu na kuwa tayari kutoa huduma kwa wenzangu kwa upendo na ukarimu kama Kristu mwenyewe alivyofanya kwetu.
Tangu nilipowasili na kujiunga na maisha haya nimekaa miezi mitatu yakuchukua uzoefu na baadae nikajiunga na mwaka mmoja wa malezi baada ya muda huo niliandika barua ya kuomba kuendelea na hatua ya Upostulanti na masomo ya falsafa.
Baada ya mwaka wa malezi niliteuliwa kuwa mmoja wa vijana wane watakao anza masomo ya falsafa katika Chuo Kikuu kishiriki cha Jordan tawi la Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino.
Hivi sasa nimemaliza mwaka wa kwanza wa falsafa na nimeanza mwaka wa pili. Jumla huwa ni miaka mitatu hadi kumaliza falsafa kwa ngazi ya uzamili. Lakini ninachoweza kuwashirikisha kuhusu nini mchango wa masomo ya falsafa kwenye wito wangu ni kuwa.
Masomo ya falsafa yananisaidia kukua kiakili na kimsimamo juu ya wito nilionao nikiwa na hoja za msingi za kiimani, pia yananionyesha dhahili kuwa fikra za watu sio ukweli wa Mungu kwani Yeye hachunguziki ni imani tu ndio yenye kutupatia hakika juu yake. Kupitia kuyasoma Napata mitazamo mbalimbali juu ya namna mwanadamu anavyojaribu kufikiri na kuuleta uhalisia juu ya mambo mengi muhimu asiyo na majibu nayo lakini hata hivyo fikra hizi pasipo imani bado zinashindwa kwa kiwango kikumbwa kuufikia ukweli.
Mtakatifu Augustino katika falsafa yake aliongelea juu ya kuangaziwa (Illumination) katika utambuzi wa ukweli wa vitu na mambo mbalimbali yaliyo katika maisha yetu. Anaonyesha kuwa kama tusivyoweza kuona vitu mbalimbali bila mwanga wa jua, vivyo hivyo akili yetu haiwezi kujua ukweli wowote isipoangaziwa. Zaidi anajaribu kuainisha kuwa kuna namna ndani yetu,ambayo ni mwanga mwa mawazo ya kimungu ambao hutuangazia katika kuupata ukweli wa vitu vyote tuwezavyo kuvitambua
Mtakatifu Augustino anadhibitisha kuwa mwanga huo wa Kimungu ndani yetu ambao hutuwezesha kutambua ukweli wa mambo mbalimbali hutoka kwa Mungu mwenyewe. Hivyo akili yetu tu haiwezi kutupatia ukweli baina ya mambo yatuzungukayo ila inapoangaziwa na Mungu ndipo sisi huupata ukweli kwani Mungu ni ukweli wote .
Pamoja na mtakatifu Augustino yupo pia Mtakatifu Anselm ambaye aliongea kuwa Ninaamini ili nipatekuelewa (I believe in order I may Understand) hivyo pasipo kuamini hapana yeyote anayeweza kujua ukweli wowote. Imani ni jicho la kiroho ambalo hutufumbulia ukweli tusioweza kuuona na kuupata kupitia hisia zetu na vionjo vya kimwili.
Hivyo kwangu mtazamo wa masomo ya falsafa ni kusimika misingi dhabiti na Imara juu ya kile ninacho kiamini katika makuzi na ukomavu wa wito wangu.
Karibuni wote mjifunze katika maisha yetu ya kikarmeli tumwombe Mungu pamoja ili sote atufanikishie haja zetu katika maisha yetu. Lakini pia mtuombee sisi pamoja na wengine wote ambao wameamua kujiunga na maisha ya kitawa ili tufikie wito huo mwema na tujifunze kuwa wahudumu safi wa hadhi hiyo kubwa katika maisha yetu ya kikristo.
Karibuni sana katika familia ya wakarmeli tutafakari, tusali, tujifunze kuishi kindugu na kutoa huduma kwa watu wote kwa upendo usio na mipaka.
Mimi AthanasNgassa