HISTORIA YA MAISHA YANGU HADI KUJIUNGA NA SHIRIKA LA BIKIRA MARIA WA MLIMA KARMELI.
Mungu ni mwema kila wakati.
Kwa majina naitwa Aidani Mutaleba Julius nimezaliwa 19.10.1998 Wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Natokea Parokia ya Bikira Maria wa Fatima, Rukindo Jimbo Katoliki la BUKOBA.Ninajihisi furaha kuwa mmoja wa waseminari wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli iliyo na nyumba ya Malezi hapa Morogoro.
Chini ninaelezea Historia fupi ya Maisha yangu juu ya Familia Yangu, Elimu, wito na jinsi nilivyopata kujiunga na Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli (O.CARM)
KUHUSU FAMILIA YANGU.
NINATOKEA KATIKA Familia ya Kikatoliki ya marehemu Bw.Julius Rwechubgura na Bi.Tryphina Kyabona waliofunga Ndoa mnamo mwaka 2000 katika Parokia ya Mt. YOSEFU Kirumba Jimbo Katoliki la mwanza. Familia yetu ina jumla ya watoto wawili (2) sote tukiwa wa jinsia ya kiume na mimi nikiwa mtoto wa kwanza. Kwasasa familia yetu iko chini ya uangalizi wa mama yetu mpendwa kufuatia na kutokwa kwa Baba yetu mpendwa aliyetangulia mbele za haki mwaka 2011. Mwenyezi Mungu ailaze Roho yake mahala pema peponi. AMINA.
ELIMU YANGU KIUFUPI.
Mwaka 2011 ndio mwaka ambao nilihitimu Elimu yangu ya Msingi katika shule ya msingi KAGONGO iliyopo wilaya ya Muleba mkoani Kagera. Mwaka huo ikiwa ni mwezi wa Septemba nilifanya Mtihani wa kujiunga na Seminari ya Mt. Maria-Rubya ya Jimbo Katoliki la Bukoba na kwa neema zake Mungu nilifaulu na hivyo kupata nafasi ya kuanza masomo yangu ya Sekondari Seminarini mwaka 2012.
Mwaka 2013 baada ya kumaliza Mitihani yangu ya kidato cha Pili, nilijiunga kidato cha Tatu na Seminari ya Shirika la Mitume wa Yesu ( Apostles of Jesus) iliyopo wilaya ya Moroto huko Kaskazini Mashariki mwa Uganda mwaka 2014. Mwaka uliofuata wa 2015 nilimaliza vyema Mitihani yangu ya Kidato cha Nne na kufuatia Ufaulu wa mitihani niliweza kuendelea na masomo yangu ya Kidato cha Tano hapohapo Seminarini mwaka 2016 nikichukua Masomo ya Historia, Elimu ya Biblia na Jiografia hadi mwaka 2017 nilipomaliza masomo yangu ya Sekondari. Shukrani za dhati kwa Mwenyezi Mungu aliyenisaidia kumaliza
JUU YA SAFARI YANGU YA WITO.
Nimekuwa na ndoto ya kumtumikia Mwenyezi Mungu na wanadamu wenzangu kama Padre tangu nilipokuwa mdogo na daima sichoki kumuomba Mwenyezi Mungu kunitimizia vyema ndoto hii na kuwa uhalisia. Nina Imani kabisa kwa hatua niliyopiga hadi sasa nikiwa katika Shirika hili pendwa la Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Mungu yuko name kunisaidia.
Niliposikia Tangazo la kuwataarifu vijana waliopenda kujiunga na kidato cha kwanza katika Seminari ya Mtakatifu Maria iliyopo Jimbo Katoliki la Bukoba kamwe sikusita nikiwa na Imani ndoto yangu ingeweza kufika mafanikio kupitia njia ile. Namshukuru Mungu nilijifunza mengi juu ya wito kwa miaka miwili niliyokuwa Rubya Seminary 2012-2013. Mwaka 2014 nilijiunga na Seminari ndogo ya Shirika la Mitume Wa Yesu huko Moroto, Uganda nikiwa kidato cha Tatu ambapo nilimalizia Elimu yangu ya Sekondari mwaka 2017. Baada ya kumaliza mitihani yetu ya Kidato cha Sita Seminarini nilituma maombi kupitia Baba Gambera ya kujiunga na Seminari Kuu ya Shirika la Mitume wa Yesu iliyopo Nairobi, Kenya kwaajili ya Falsafa na kwa Bahati nzuri mwezi MEI 2018 nilipokea Barua ikithibitisha maombi yangu yamekubaliwa na hivyo ilinipasa kuanza maandalizi.
Ilikuwa inatupasa kuripoti Seminari Kuu mwezi JULAI 2018 lakini kufuatana na misukosuko na matatizo yaliyolikumba Shirika la Mitume wa Yesu kwa Ujumla haikuwezekana na hivyo nilijikuta katika wakati mgumu. Kiukweli nilijihisi kuishiwa nguvu baadfa ya kupokea Taarifa hiyo ya kuwa tusingeweza tena kujiunga na Seminri Kuu lakini nilijitia nguvu na ujasiri nikimuomba Mungu anisaidie niweze kuendeleza wito wangu.
NILIVYOJIUNGA NA SHIRIKA LA BIKIRA MARIA WA MLIMA KARMELI.
Baada ya kuwa imeshindikana kuanza na masomo ya Falsafa Seminari Kuu ya Mitume wa Yesu nilizidi kumuomba Mungu anisaidie ili ndoto yangu isipotee. Namshukuru sana Mwenyezi Mungu ambaye amezidi kunionyesha mwanga katika safari yangu ya wito.
Mjomba wangu aliye muumini wa Parokia ya Bikira Maria wa Mlima wa Karmeli Bunju aliweza kuonana na FR.VICTOR BIRAMATA, Mkurugenzi wa Miito na Mkuu wa Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli Tanzania ambaye alimweleza juu yangu na hapo badaye Mkurugenzi aliweza kumpatia namba zake ili niweze kufanya mawasiliano naye. Ilikuwa ni mwezi wa OKTOBA 2018 nilipofanya mazungumzo na FR.VICTOR BIRAMATA ambaye nilimweleza kiufupi juu yangu. Alinipatia Anwani ya Barua pepe ambayo alinitaka nimtumie ujumbe au taarifa juu ya Familia yangu,Elimu, Historia ya wito wangu na nini kilichojiri hadi kushindwa kuingia Falsafa. Nilifanya kama alivyonielekeza na mwezi NOVEMBA alinitumia Ujumbe akinitaka nijiandae tarehe 16 mwezi huo kuripoti Nyumba ya Malezi Morogoro. Ilikuwa ni furaha kubwa sana kwangu, mzazi wangu na ndugu kiujumla na mnamo tarehe 16 niliianza safari kutokea Mwanza kuja Morogoro ambapo niliwasili saa TANO usiku na kumkuta FR. VICTOR akiwa tayari kunipokea kituo cha mabasi Msamvu.
Mwisho natoa shukrani zangu za dhati kwake Mwenyezi Mungu na daima nazidi kumuomba aniongoze katika safari yangu ya wito.