HISTORIA YA MAISHA YANGU
Naitwa CHARLES MAKOYE MASIBUKA mzaliwa wa Jimbo Katoliki la Bunda Parokia ya Mtakatifu Paulo Bunda. Nilizaliwa tarehe 1/12/1996 katika kijiji cha GUTA wilaya ya BUNDA mkoa wa MARA. Nilipata Sakramenti ya Ubatizo 4/4/2010 Parokiani Bunda na Paroko Padre. Chrisogone Njau, pia nilipata Sakramenti ya Kipaimara tarehe 7/7/2010 Parokiani Bunda na Askofu. Michael Msonganzila. Mimi ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wawili, yaani mimi na dada yangu aitwae JANETH. Kabila langu ni MSUKUMA na baba yangu anaitwa MAKOYE ZACHARIA NGOSSO, mama anaitwa PRISCA JOYCE MASANJA. Japo nililelewa na mama wa kambo aitwae TEDDY VEDASTUS kwa mda mrefu sana. Mama huyu alinilea vizuri sana kama mtoto wake na ninaweza kusema ndio chanzo cha safari yangu ya wito maana alinipa malezi bora kwa kufuata maadili ya kikatoliki.
ELIMU
Nilianza elimu ya msingi mwaka 2004 hadi 2010 katika shule ya msingi iitwayo Guta “A” na baada ya hapo nilijiunga na masomo ya Pre-form one katika Seminari ndogo ya Mtakatifu Gregory Mkuu Sayusayu Maswa-Shinyanga, kwa muda wa mwaka mmoja. Ilipofika mwaka 2012 nilichaguliwa kujiunga na Seminari ya Mtakatifu Aloisius Gonzaga Shanwa-Maswa, hapo nilisoma kwa miezi kadhaa kisha Seminari ilifungwa kutokana na kutokukamilisha usajili serikalini maana ilikua ndio inaanzishwa. Baada ya hapo mwaka 2013-2016 niliendelea na masomo ya Secondari katika shule ya Sekondari Murutunguru iliyopo Nansio-Ukerewe, na mwaka 2017-2019 nilijiunga na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule iitwayo; Nyerere High school, iliyopo Migoli-Iringa kwa mchepuo wa masomo ya Historia, Gografia na Lugha ya kingeleza (HGL). Baada ya kuhitimu kidato cha sita mwaka 2019 nilijiunga na shirika la kitawa liitwalo Ardorini Missionaries, lililopo Morogoro na nilibahatika kuanza masomo ya falsafa mwaka huo huo katika chuo kikuu kishirikishi cha Mtakatifu Augastino (Jordan).
Mwaka 2022 nilihitimu digrii ya kwanza ya falsafa na niliomba ruhusa kwa mlezi wangu kwaajili ya kutafakari zaidi juu ya wito wangu. Aliniruhusu na nilikaa nyumbani mpka mwezi wa 8 mwaka 2023 ndiposa nilipojiunga na Shirika lingine la Bikira Maria wa mlima Karmeli na kuanza malezi katika nyumba ya malezi Bunju-Dar es Salaam.
SAFARI YA WITO WA UTAWA NA UPADRE
Nilianza kuwa na ndoto ya kuwa padre hasa nilipofika darasa la sita nikajiunga na chama cha watumikizi wa altare (chama cha wana wito) Parokiani Bunda. Nyumbani kwetu kilikua ni kigango (Guta) hivyo ilinibidi kila ijumaa jioni nisafiri kuelekea Parokiani (Bunda) kwaajili ya mahudhurio ya jumamosi na mafunzo ya utumukizi. Nilikua nafikia kwa shangazi yangu kisha kesho yake (Jumamosi) asubuhi niliwahi misa ya asubuhi baada ya misa tulikua tunafanya usafi wa mazingira ya kanisa na kufua kanzu zetu za watumikizi. Baada ya mwezi mmoja nilianza kutumikia altareni kama mtumikizi na hapo ndipo wito wangu ulivyozidi kuongezeka maana ilikua ni tamanio langu kuwa mtumikizi na nilikuwa navutiwa sana na Padre Chrisogone Njau (AJ) ambae alikua ni Paroko wa Parokia ya Bunda. Alinivutia kwa namna alivyokua anaadhimisha misa akiwa amevaa vazi la misa (Joho/Kasura), mafundisho yake na malezi aliyokua anatupa sisi kama wana wito. Mara nyingi kukiwa na adhimisho la misa kigangoni kwetu (Guta) nilikua natumikia na hivyo ikapelekea waumini wengi kuanza kuniita Padre mdogo. Ilikua ni furaha yangu sana kuitwa vile na nilipokua nyumbani mwenyewe nilikua natengeneza shuka na kulivaa kama Joho/Kasura kisha kuigiza kama naadhimisha Misa hasa kwa kuimba yale maneno ambayo Padre huwa anaimba wakati wa adhimisho la Misa Takatifu.
Baada ya kuhitimu darasa la saba nilifanya mtihani wa kujiunga na Seminari ndogo (St. Gregory the Great Seminary Sayusayu Maswa-Shinyanga) kwa masomo ya Pre-form one. Nilifurahi sana maana matokeo yalitoka nimechaguliwa kujiunga na Seminari hiyo. Nilisoma hapo kwa mwaka mmoja na baada ya hapo nilipelekwa Shanwa Seminari kwaajili ya masomo ya kidato cha kwanza mpka cha nne, lakini sikufanikiwa kumaliza mwaka maana Seminari hii ilifungwa kwa kutokamilisha usajili. Baada ya hapo nilijiunga na shule ya jimbo la Bunda iitwayo Shule ya Sekondari Murutunguru Nansio-Ukerewe, hapo nilisoma kidato cha kwanza mpka cha nne na matokeo ya kidato cha nne yalitoka vizuri nikachaguliwa kujiunga na kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Nyerere iliyopo Migoli-Iringa. Baada ya kuhitimu kidato cha sita, nilipita Dodoma kuwasalimu ndugu zangu hapo nikakutana na Padre Mosha Paroko wa Parokia ya Miyuji, ambae pia alichochea wito wangu wa kuwa padre kutokana na mafundisho yake. Nilipata wasaa wa kuzungumza nae kisha nikamuelezea nia yangu na ndoto yangu ya kutaka kuwa Padre hasa Padre Mtawa, ndiposa akanisaidia kutafuta Shirika la kitawa na Mungu ni mwema nikabahatika kupata Shirika liitwalo Ardorin Missionaries lililopo Morogoro. Nilijiunga na shirika hilo na kuanza malezi rasmi ya Utawa na Upadre, na baadae nilianza masomo ya falsafa katika Chuo Kikuu kiitwacho; Jordan University College kilichopo Mkoani Morogoro. Baada ya kuhitimu masomo yangu ya falsafa niliomba kwenda nyumbani kwaajili ya mapumziko na tafakari. Niliruhusiwa kisha nikaondoka kuelekea nyumbani, ambapo nilikaa kwa muda wa mwaka mmoja. Baada ya tafakari nilianza kuvutiwa na Shirika la Wakarmeli ndiposa nikaanza mawasiliano na Mkurugenzi wa Miito Padre Victor, kwaajili ya kuomba kujiunga na Shirika hilo.
Namshukuru Mungu baada ya kutuma maombi yangu nilikubaliwa kujiunga na Shirika la Wakarmeli na nikaanza malezi katika nyumba ya malezi Bunju - Dar Es Salaam. Kwa maombezi ya Mama Bikira Maria wa mlima Karmeli, Mungu anijalie kuifikia altare ya Bwana na niwe mtenda kazi katika shamba la Bwana. Amina