Lazima msalaba uwepo. Kuinuliwa juu. Kusulubishwa na kuingia juu katika utukufu. Yesu anafahamu upendo wa Mungu. Msalaba ni fumbo.
Historia ya Israeli jangwani -dhamira zao zinawauma, zinawasuta. Walipitia mazingira magumu. Walipogongwa na nyoka kwa sababu ya kumtukana na Mungu, Musa aliwaombea msamaha na Mungu akawaponya kwa kuwawekea nyoka wa shaba (Kut 21:8-9). Ikiwa mwanadamu atainua kichwa chake na kutazama juu, kuutumainia msamaha wa Mungu kwa hakika ataupata.
Mwana wa mtu yuko katika jangwa la dunia hii iliyojaa nyoka wengi wa sumu. Wapo binadamu ambao wana matendo kama ya nyoka wakali wa sumu. Wanagonga watu kwa kushirikiana na Ibilisi kwa kutekeleza matendo maovu. Hawa dawa yao na kiboko yao ni Yesu Kristo. Akiisha kuinuliwa nguvu inayotoka katika msalaba inaponya dhambi, inaponya makali ya sumu wa nyoka. Yesu anainuliwa msalaba ili kuponya hayo yote. Lakini hii ni nafasi ya wale wanaotaka kuishi tu. Kuna wengine hawataki kabisa.
Hata sisi kama ilivyokuwa kwa Israeli kwa namna moja kama nyingine tumegongwa na nyoka wa sumu. Maisha yetu yana sumu za ubinafsi, kutojali wengine, uongo, na kutosamehe. Tunahitaji kumtazama Kristo anayeinuliwa msalabani ili tuweze kuponywa na sumu ya mauti.
Kutoa ni upendo. Huruma na Upendo wa Mungu unamfanya amtoe mwanae kwa ajili ya kutukomboa. Hili ni fundisho kuwa si Mungu aliyetusukuma katika matatizo yetu, bali ni matokeo ya kuisikiliza sauti ya mwovu shetani. Mungu hayuko tayari kutuacha katika utumwa wa huyu kiumbe katili, anamtoa mwanae wa pekee Yesu Kristo ili akate mzizi wa nguvu za mauti yaliyoletwa na Ibilisi kwa mauti yake msalabani.
Yeyote atakaye mwamini Kristo ataokolewa kutoka katika nguvu za mwovu shetani.
Ujio wa Yesu si kwa ajili ya kutusuta, bali kutushika mkono na kutuokoa katika hatari. Yesu Kristo anafahamu hatari inayotukabili, peke yetu hatuwezi kumshinda shetani. Bali pamoja naye nguvu za mwovu zinaisha. Tunaachiliwa twende na Kristo. Hiki ndicho kipimo cha upendo wa Mungu. Ubinadamu wetu uliojeruhiwa unamwitaji Mkombozi mkuu Yesu Kristo. Mungu ametuumba hawezi kutuangamiza.
Imani ndio hukumu yenyewe kwa imani mtu anaamua kuwa mbali na Mungu wake. Mtu anajihukumu kwa kusema hapana. Ndio maana Yesu Kristo anasema kuwa Mungu hamhukumu mtu. Kulikataa jina la Yesu Kristo moja kwa moja ndio hukumu yenyewe kitendo hicho kinamfanya mtu ajitenge na upendo wa Mungu. Mtu ameisha hukumiwa na tendo lake la kumkataa Mwokozi wa ulimwengu.
Wale wanaomkataa Yesu Kristo ndio wale ambao hawataki kuongozwa na mafundisho na maisha yake. Wanataka kufanya mambo yao wenyewe. Mungu kwao ni kikwazo. Ni kikwazo kwa sababu hataki matendo ya giza. Kwake hayana nafasi. Matendo maovu hufanyika kwa siri. Matendo mazuri hufanyika mchana na mbele ya watu. Yesu ndio mchana. Uhusiano wetu naye unayamulika matendo yetu. Kama hayafai anataka kuyarekebisha. Lakini watu hawataki kurekebishwa naye. Wanaona njia bora ni kutoambatana naye. Kila anayemkiri na kumsadiki Kristo hujitakasa mwenyewe.