HISTORIA YANGU NA JOSEPH K. PETRO
Kwa majina naitwa Joseph Kunyonga Petro, nimezaliwa Jimbo katoliki la Bunda, Parokia ya Mt. Gregory Mkuu Kamkoko – Ukerewe, Baba yangu anaitwa Petro Mashauri na Mama yangu anaitwa Cecilia Mkwaya ambapo wote ni wakerewe. Nilizaliwa tarehe 25/01/1998 nikiwa ni mtoto wa tano kuzaliwa kati ya watoto kumi na mbili.
SAKRAMENTI
Nilipokea Sakramenti ya ubatizo tarehe 11/04/1998 chini ya Padri Mwalimu, Komunio ya kwanza tarehe 01/01/2009 chini ya Padri Msonge na sakramenti ya Kipaimara nilipokea tarehe 17/10/2010 chini ya Mhashamu Baba Askofu Renatus Kwande. Katika Parokia ya Mt. Yoseph Baba Mlishi wa Yesu Nansio Ukerewe.
ELIMU
Nilianza elimu yangu ya msingi mwaka 2005 katika shule ya msingi Chamatuli iliyopo Ukerewe na kuhitimu mwaka 2011. Nilijiunga na kidato cha kwanza katika shule ya sekondari Bukongo tangu mwaka 2012 hadi 2015 ambapo sikufanikiwa kuendelea na masomo. Mwaka 2016 nilichukua uamuzi wa kurudia masomo ambapo nilirudia darasa la saba katika shule ya msingi Kabujaja iliyopo Wilaya ya Busega Mkoani Simiyu. Ninamshukuru Mungu kwani nilifaulu na hatimae nikajiunga na elimu ya sekondari katika shule ya sekondari Kabita iliyopo Wilayani Busega Simiyu , tangu 2017-2020 ambapo nilifanikiwa kufaulu na kuchaguliwa kujiunga na kidato cha tano katika shule ya sekondari Bulunde iliyopo Nzega Tabora, tangu 2021-2023. Ninamshukuru Mungu kwani nilifaulu vizuri.
WITO
Safari yangu ya wito ilianza tangu nilipokuwa na miaka kumi na tatu (13) mwaka 2010. Jambo hili lilijidhihilisha katika maisha yangu mara kwa mara kutokana na kuvutiwa na Paroko msaidizi wa Parokia Mtakatifu Yosefu Baba Mlishi wa Yesu iliyopo Nansio Ukerewe. (Padri Simon Mesondole) ambaye kwa sasa ni Baba Askofu wa Jimbo katoliki la Bunda.
Kutokana na changamoto za kitaaluma sikuweza kutilia manani sana ile hamu ya kujiunga na malezi ya upadri kwa siku zijazo kwani niliamini kabisa kwamba nisingeliweza kutimiza matamanio yangu kutokana na uwezo wangu wa kitaaluma kutolidhisha.
Mwaka 2015 nilihitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari Bukongo iliyopo Wilayani Ukerewe na sikufanikiwa kufaulu.
Mwaka 2016 niliamua kurudia masomo yangu katika shule ya msingi Kabujaja iliyopo Busega – Simiyu na mwaka 2017 nilijiunga na shule ya sekondari Kabita na kuhitimu mwaka 2020, ninamshukuru Mungu kwani alijalia uwezo mmzuri wa kitaaluma na nilipata ufaulu mzuri, ambao ulizidi kuchochea shauku ya kujiunga na malezi ya Upadri.
Kutokana na udhaifu wa kibinadamu tangu mwaka 2018-2020 nilijaribu kuachana na sauti ya wito niliyokuwa nikiisikia moyoni mwangu jambo ambalo lilipelekea kudondoka kiimani kwa miaka mitatu na kwa kipindi chote hicho nilipitia changamoto kali hasa magonjwa, lakini ile hamu ya kujiunga na malezi ya upadri hakutoka moyoni mwangu licha ya kupungua.
Mwaka 2021 kwa neema ya Mungu ile hamu ya kujiunga na malezi ya upadri iliongezeka jambo ambalo lilinipelekea kuwaeleza ndugu zangu na kuwashirikisha baadhi ya watu, ninamshukuru Mungu kwani tangu hapo niliadhimia kusimama imara katika Imani hadi pale nilipojiunga na kidato cha tano (5) mwaka 2021 katika shule ya sekondari Bulende Nzega Tabora.
Ninamshukuru Mungu kwani alinijalia kuwa kiongozi wa TYCS kanda ya Nzega tangu mwaka 2021 hadi 2022, jambo ambalo lilinipa nafasi ya kumtumikia Mungu katika nafasi niliyokuwa nayo na kufanya tafakari ya kina kuhusu wito niliyokuwa nikiutamani.
KUHUSU KARMELI
Nililifahamu shirika la wakarmeli mwaka 2022mara baada ya kuwaona Masista wa karmeli waliopo Jimbo katoliki la Bunda, lakini kwa kipindi hicho nilikuwa nikitamani kujiunga na shirika la Holy spirit Fathers (OSS) lililopo Moshi, hivyo sikufuatilia Zaidi kuhusu shirika la wakarmeli licha ya kujua ya kwamba ni shirika la kipadri.
Mwaka 2023 mwezi wa sita niliamua kubadili nia yangu ya kujiunga na shirika la Holy spirit Fathers (OSS) kutokana na kutokukubaliwa, niliendelea kumuomba Mungu kwa maombezi ya Mama Bikira Maria, ninamshukuru Mungu kwani nilibahatika kupata taarifa kuhusu shirika la ndugu wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli (O. Carm) kwa kusaidiwa na Frt. John Gazigile (OSS) ambae alinisaidia kupata mawasiliano na Frt. John Madava (O. Carm) ambaye alinipokea vizuri na nikapata nafasi ya kujua taarifa kuhusu shirika la ndugu wa Bikira Maria wa Mlima Karmeli hasa kuhusu karama ambazo zilinivutia nilifanya mawasiliano na Mkurugenzi wa miito Fr. Victor Bilamata ninamshukuru Mungu kwani Mkurugenzi alinipokea vizuri na kunipatia mwongozo na hatimaye kwa neema ya Mungu na kwa maombezi ya Mama Bikira Maria nilipokea taarifa taarifa ya kukubaliwa kujiunga na malezi ya upadri katika nyumba mama iliyopo Bunju. Nililipoti tarehe 21/08/2023 majira ya saa tano na kupokelewa vizuri na Fr. Paul Malewa na baadaye kukutana na Mkuu wa nyumba Fr. Dominic Somola.
Kwa namna ya pekee ninamshukuru Mwenyezi Mungu, Mama Bikira Maria, wazazi wangu na wote walionisaidia kwa kipindi chote hicho mpaka sasa.