HUKUMU YA MWISHO YA MATAIFA
31 Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;
32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;
33 atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.
34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;
35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;
36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.
37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?
38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?
39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?
40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.
41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;
42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;
43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.
44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?
45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.
46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.
HUKUMU YA MATAIFA
Yesu hapa Mwana wa Adamu anafanya kazi ya Mungu ya kuhukumu. Anatimiza mapenzi ya Mungu. Yesu anajitambulisha kuwa alikuwa na
njaa,
kiu
mgeni
uchi
Mgonjwa
Mfungwa
Kama mtakumbuka zile heri 8 zilikuwa mlango wa kuingia katika ufalme wa Mungu.
Alitaja watu wa aina nane
Mafundisho ya leo yanatufundisha kitu gani ambacho tunatakiwa tufanye ili tuweze kuingia katika ufalme wa Mungu au kuumiliki. Kinachotakiwa na kuwapokea
wenye njaa,
wenye kiu,
wageni,
walio uchi,
wagonjwa, na
wafungwa.
Katika maisha yetu kuna watu ambao wamesahaulika.
Mt 25: 31-33 -Ufunguzi wa hukumu ya mwisho
Yesu atakuja -Mwana wa Adam anakuja pamoja na malaika wake wote katika utukufu na anazungukwa na mataifa toka pande zote za dunia. Kazi kuu anayoifanya ni kutenganisha watu kama mchungaji anavyotenganisha kondoo na mbuzi. Anajua jinsi ya kutenganisha. Hawezi kukosea hata kidogo. Yesu hafanyi kosa. Watajwa malaika kuonesha utukufu wake. Mtu anajitenganisha mwenyewe kwa matendo yake. Hii inategemea jinsi tunavyowatendea wadogo na wahitaji. Kondoo watakuwa upande wa kulia na mbuzi upande wa kushoto. Lakini ni kweli Yesu anahukumu? Jibu ni hapana Yn 3:17; 12:47 mtu anajihukumu mwenyewe. Yeye anachofanya ni kutenganisha. Anatenganisha kulingana na kile tulichoishi, tulichokuwa.
Mt 25:34-36 -Hukumu kwa wale walio mkono wa kulia
Walio mkono wa kulia wanaitwa waliobarikiwa na Baba yake. Wanaalikwa na kukaribishwa ili waweze kuingia katika ufalme wa Mungu. Ufalme huu umeandaliwa kwao tangu kuumbwa kwa kulimwengu. Mnakumbuka wale wana wa Zebedayo waliomba kuingia katika ufalme huo, Yesu akawaambia kuwa ni kwa ajili ya wale walioandaliwa tangu zamani..yaani watakao timiza vigezo Mt 20:23. Vigezo vyenyewe ndio hivi sasa. Hapa hakuna kujuana kwa sura tu au kwa majina. Jina lako ni matendo yako, sura yako ni matendo yako. Hawa wanakaribishwa katika ufalme sababu wanayopewa ni hii Yesu alikuwa na njaa,kiu, mgeni, uchi, Mgonjwa, Mfungwa wakamsaidia. Yesu anatambuliwa katika hao. Anasema hao ndio yeye. Hivyo tuwe makini sana. Tunakutana na Yesu kila siku huko mitaani.
Mt 25:37-40 -Wanaomba ufafanuzi
Yesu anatoa jibu: Ufalme wa Mungu hauji kwa kutunza au kutovunja amri tu, bali pamoja na hayo, unakuja kwa kuwapokea walio wa mwisho katika jamii. Lakini cha kushangaza hawa wabarikiwa, hawa wenye haki wanashikwa na mshangao, hawajui ni lini walikutana na Yesu na kumsaidia. Hawajui kabisa. Wanataka wawe na uhakika, wanauliza hivi ni lini Bwana au? Yesu anawaambia kila walipowasaidia wale wanyonge alikuwa yeye. Walimtendea Yeye. Kuna watu ambao ni vigumu kukubalika katika familia na katika jumuiya, tuwe makini, Yesu huyo. Leo umejua usije kusema padre hakusema. Hawa wabarikiwa wanatoka mataifa yote, makabila yote. Habari ndio hiyo.
Mt 25:41-43 - Hukumu kwa wale walio kushoto mwa hakimu
Hawa wanaitwa walio laaniwa. Yaani wamesemwa vibaya. Hatima yao ni ipi. Moto wa milele. Yaani hawataingia kamwe katika ufalme wa Mungu. Hata hapa sababu ni moja. Walikataa kumpokea Yesu alipokuwa na njaa, kiu, mgeni, uchi, mgonjwa, na mfungwa. Si kwamba Yesu anawazuia, la hasha, wamejizuia wenyewe. Hawakukidhi hadhi ya kuingia katika ufalme. Hapo waswahili wangesema watajiju.
Mt 25:44-46 -Wanaomba ufafanuzi maana wanashangaa
Kutokana na suali lao inaonekana hawa ni watu ambao waliishi vizuri, pengine kwa kufuata na kutovunja amri za Mungu. Kumbukeni yule kijana tajiri. Alizingatia amri zote. Lakini kikwazo kikawa kutowajali maskini Mt 19:21. Hata hawa inaonekana walifanya yale yale. Hapa kuna shida. Waliamini kuwa wametekeleza kile ambacho Mungu aliwataka wafanya kadiri ya amri na sheria. Yesu anawajibu...kwamba walimkataa katika wale waliokuwa na njaa, kiu, wageni, uchi, wagonjwa na wafungwa. Wanashangaa hata Yesu ulikuwa huko? Shida hawakuwajali maskini na wanyonge. Jamani tujitahidi tusijifungie nje ya ufalme. Tafute kwanza ufalme wa Mungu vitu vingine tutapewa kwa ziada. Tusianze kutuona macho kwa vitu ambavyo havitufikishi mbinguni.
Unaweza kuendelea kutafakari mwenyewe, ni kitu gani kimekugusa zaidi leo? Kaa chini jiulize kama leo hii, wewe na mimi tungeitwa tungekuwa upande gani? Wa kushoto au wa kulia?
.