Kesho Wakarmeli tunaadhimisha kumbukumbu ya Mt. Elisha nabii. Hili kupata Misa yake bonyeza hapa ili kuPakua/Dowload file la misa ya nabii Elisha
14 Juni
Mtakatifu Elisha, nabii
Kumbukumbu:O.Carm
«Basi akaondoka huko, akamkuta Elisha, akatupa vazi lake juu yake. Naye akawaacha ng’ombe, akamfuata Eliya na akamhudumia» (1Fal 19:19,21)). Elisha alipokea roho ya Eliya na baadhi ya miujiza mingi inayojulikana, alimponya Naamani ukoma, alimfufua mtoto. Aliishi kati ya watoto wa manabii na mara nyingi alikuwepo, kwa jina la Mungu, katika matukio ya taifa la Israeli. Shirika la Wakarmeli, linakumbuka chimbuko lake, katika Mlima Karmeli kwa maadhimisho ya kiliturujia ya manabii wakubwa Eliya na Elisha, kwa kusudio la kumbukumbu ya kudumu ya uwepo wao na matendo yao. Kwa hiyo mwaka 1399 Mkutano Mkuu uliamuru maadhimisho ya kumbukumbu ya Mt. Elisha. Hadi leo nabii anashuhudia kwa ufanisi karama ya kinabii kwa njia ya uaminifu kwa Mungu kweli na huduma kwa taifa lake.
Antifona ya Mwanzo Rej. 2Fal 2:15;3:12
Roho ya Eliya ikakaa juu ya Elisha
Na Neno la Bwana analo huyu.
Sala
Ee Mungu mlinzi na mwokozi wa watu, uliyeonesha maajabu yako kwa njia ya manabii waliochaguliwa nawe na umempatia nabii Elisha roho ya Eliya, uwe radhi kwa wema kuongeza mapaji ya Roho Mtakatifu ndani mwetu, ili kwa kujazwa karama ya kinabii tuweze kutangaza kila mahali uwepo wako na wema wako.
Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana, wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala na nawe, katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina.
Somo la kwanza 2Fal 5:7a,8-15a,17b.
Aje kwangu na atajua kuwa yupo nabii katika Israeli
Somo la kitabu cha pili cha Wafalme
Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli. Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha. Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi. Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma. Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira. Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi? Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi. Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako. Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa.
Basi Naamani akasema; mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana.
Neon la Bwana
Au 2Fal 2:11-15b
Somo la kitabu cha pili cha Wafalme
Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli. Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili. Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani. Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka. Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha.
Neno la Bwana
Wimbo wa katikati Zab 104
Kiit....Peleka roho wako, Bwana, na ufanye upya uso wa dunia.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Kwa hekima umevifanya vyote pia.
Dunia imejaa mali zako.
Kiit...
Hao wote wanakungoja Wewe,
Uwape chakula chao kwa wakati wake.
Wewe huwapa, Wao wanakiokota;
Wewe waukunjua mkono wako,
Wao wanashiba mema;
Kiit.....
Wewe wauficha uso wako,
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Kiit…..
Shangilio Rej. 2Fal 5:8;13:14
Aleluya, aleluya
Wote watajue ya kuwa yuko nabii katika Israeli,
Baba na gari la Israeli na kiongozi wake!
Aleluya
Injili Lk 4:24-27
Somo la Injili ilivyoandikwa na Luka
Wakati ule Yesu aliwaambia wafuasi wake: Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe. Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima; wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni. Tena, palikuwa na wenye ukoma wengi katika Israeli zamani za nabii Elisha, wala hapana aliyetakaswa ila Naamani, mtu wa Shamu.
Neno la Bwana
Kuombea dhabihu
Ee Mungu, uliyeweka wazi ukweli wa sadaka hizi katika dhabihu za ishara za kale, utujalie kwamba kwa sadaka hii ya ekaristi katika kumbukumbu ya nabii wako Elisha, tuwe zawadi ya kukupendeza. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
Komunyo Rej. 2Fal 4:44
Mtu wa Mungu, aliweka mkate wa matunda ya kwanza mbele yao, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.
Sala baada ya komunyo
Ee Mungu, uliyetoa mkate kwa njia ya ajabu kupitia maajabu ya nabii wako Elisha, ni kwamba, jalia kwamba kwa kuimarishwa na chakula cha sadaka hii, tuweze kila siku kuishi karama ya unabii.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
Baraka
Mtakatifu Elisha, nabii utuombee.