Utangulizi wa mkesha wa Ekaristi –Alhamisi Kuu
Mara tunapoanza kutafakari juu ya kuwekwa kwa Ekaristia, tunaweza kujiuliza sisi wenyewe jinsi gani ya kulitafakari Fumbo hili kubwa? Wainjili Luka na Yohana wanatupatia jibu wakifunua siri ya moyo wa Yesu alipoanzisha Fumbo hili kubwa.
Luka anaandika maneno ya Yesu mwenyewe: “Nimetamani sana kuila Pasaka hii pamoja nanyi kabla ya kuteswa kwangu” (Luka 22:15). Bwana ameufikia wakati huu wa kuteswa kwake kwa kuutamani. Ametamani kukamilisha kazi hii kubwa na muhimu sana. Katika tukio hili Mitume kumi na wawili wanachukua nafasi muhimu kabisa.
Kile alichotamani ni kusherehekea mlo wa Pasaka pamoja nao. Alitamani awe nao katika tukio hili la kipekee. Alitamani awape maisha mapya. Yeye alifahamu kile ambacho kingetokea katika wakati wa chakula cha jioni - alijua kuwa angeyagusa na kuyabadili maisha yao moja kwa moja kwa njia ya Ekaristia Takatifu. Ekaristi inahusishwa na zawadi ya Mwenyewe kupitia Mateso, ambayo ndiyo ilikuwa tamanio la Yesu, kama anavyogusia mateso hayo katika maneno yake mwenyewe ya kuweka Ekaristi. Mwili unaotolewa kwa ajili yenu Damu inayomwagika kwa ajili ya maondoleo ya dhambi. Yesu ametamani kuondoa dhambi milele.
Yohane, kwa upande wake, anaposimulia kuwekwa kwa Ekaristia katika Karamu ya Mwisho anaelezea ubora na kiwango cha hali ya juu kabisa cha tamaa yaKristo: “Kabla ya sikukuu ya Pasaka, Yesu hali akijua kuwa saa yake imefika atakayotoka katika ulimwengu kwenda kwa Baba, naye ali amewapenda watu wake katika ulimwenguni, aliwapenda upeo” (Yohana 13: 1). Anaeleza upendo usio na kikomo. Upendo tu usio na kifani unaotoa maisha hadi mauti ya msalaba ndio unaoeleza kile kinachotokea katika Siku Tatu Kuu za Pasaka, alipopita katika Mateso, Kifo, na kuhitimishwa na Ufufuko.
Kabla ya kuyatoa maisha yake, Yesu alisalitiwa na mmoja wa watu wa karibu naye, Yuda Iskariote. Mt. Agostino anasema kuwa Mwinjili Yohane anaposema kuwa Yuda alitoka nje baada ya kupokea tonge na kulikuwa usiku (Yoh 13:30) alitaka kumaanisha undani wake, kwamba Yuda wakati anamsaliti Yesu alikuwa na giza moyoni mwake. Yuda mwenyewe alikuwa giza. Lakini ndani ya chumba walimokuwa Mitume na Yesu kulikuwa na mwanga wa Upendo. Ndipo hapo Upendo wa Yesu unapojionesha katika Ekaristia. Amejitoa mwenyewe kwa ajili yetu. Anajitoa hata kwa wale wanaomsaliti.
Yesu alipokuwa anaweka Ekaristia alitangulia kufanya tukio ambalo ilibidi litukie hapo mbeleni. Alianzia kwenye bustani ya Gethsemane. Fikiria yale ambayo Yesu alifanya na kusema katika kuanzisha Ekaristi: alitwaa mkate, akashukuru, akaumega na akawapa akisema: “Huu ni mwili wangu, unaotolewa kwa ajili yenu;fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”. Kikombe nacho vivyo hivyo baada ya kula akisema, “Kikombe hiki ni agano jipya katika damu yangu, inayomwagika kwa ajili yenu” (Lk 22: 19-20).
Yesu anasema kuwa mwili wake umetolewa kwa ajili yetu. Kutoa ni tendo la upendo. Anaonesha namna ya upendo uliomo ndani kabisa ya mwanadamu unavyotakiwa uwe zawadi ya Kimungu. Ndani ya moyo ni upendo. Yesu anatoa mwili wake na damu yake yaani maisha yake, yeye mwenyewe. Kwanza kabisa hii ni zawadi kwa Baba yake. Anamtolea Mungu Baba Mwili na Damu yake sadaka yenye maana katika zote. Zawadi yenye thamani kubwa, kwa sababu inatokana naupendo wake unaomfanya ayatiishe maisha yake mpaka msalabani, “Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo” (Yohane 14:31). “Ndiposa Baba ananipenda kwa sababu nautoa uhai wangu, ili niutwae tena” (Yohana 10:17). Upendo na utii wa Yesu kwa Baba umeharibu uadui na kiburi cha shetani.
Zawadi ya mwili na Damu yake inamhusu kila mmoja wetu. Alipenda akae nasi na Kanisa lake hadi mwisho wa nyakati. Hata sisi tunashiriki sadaka hii kila tunapoadhimisha Fumbo hili kubwa. Mtume Paulo anaongela ushirika na Mwili na Damu ya Kristo (1Kor 10:16). Yesu anaingia katika maisha ya kila mtu anayempokea na kushiriki naye katika meza ya agano la ukombozi na kutufanya sisi tulio wengi kuwa kitu mmoja katika Yeye. Hii ina maana kwa njia ya Ekaristi tunaingia kuwa wamoja katika Utatu Mtakatifu. Kwa hakika Roho Mtakatifu hutufanya tuwe mmoja. Yesu alisema anitazamaye mimi amtazama Yule aliyenipeleka ni sawa sawa na kusema anayenipokeaye mimi amempokea Yule aliyenipokea yaani Mungu Baba (Yoh 12:45). Roho Mtakatifu anahusiano mkubwa mno na Fumbo hili la Ekaristia tunaloendelea kulitafakari. Yeye ndiye aliyemleta Yesu duniani. Maria alipata mimba kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, wakati wa Mageuzo ni Roho Mtakatifu ndiye anayemshusha Yesu Kristo na kuyageuza maumbo ya mkate na divai kuwa Mwili na Damu ya Yesu Kristo. Yesu anapoingia kwetu tunapompokea hutupatia Roho Mtakatifu ili atufanye wamoja ndani ya Kanisa. Ndipo hapo tunapokuwa hekalu la Roho Mtakatifu (1Kor 3:16).
Kifo cha Yesu kimetukomboa kutoka katika enzi ya utumwa wa mauti na Yesu ameiikata minyororo ya makucha ya shetani. Fumbo la Ekaristi linaadhimishwa na watu tulio milki ya Mungu. Mt. Yohane Paul wa II aliwahi kuandika hivi: “Ekaristi, uwepo uokoao wa Kristo katika jumuiya ya waamini na chakula chake cha kiroho, ni wa thamani kubwa zaidi ambayo Kanisa linaweza kuwa nayo katika historia ya safari yake. Hii inaeleza uangalifu ambao daima Kanisa limeonyesha kwa Fumbo la Ekaristi, uangalifu ambao hupata kujieleza katika mamlaka ya Mitaguso na ya baba Mtakatifu”. (Ensiklika Ecclesia de Eucharistia –Kanisa la Ekaristia, namba 9)
Basi tumwombe sana Kristo wa Ekaristi akae nasi, atubariki, atuneemeshe na kutulinda.
Wimbo kaa nasi