MT. Theresia wa Mtoto Yesu -Patron Saint of the missions
Mtawa mmonaki mkarmeli, Msimamizi wa misheni, Ua dogo la Upendo, Theresia wa Mtoto Yesu, Ua dogo la Yesu na mwalimu wa KanisaAlimpenda sana Yesu Bwana wetu
Mt. Teresia wa Mtoto Yesu anayejulikana kama Ua dogo la Upendo alizaliwa tarehe 2 Januari 1873 Alençon, Ufaransa. Baba yake aliitwa Louis Martin ambaye alikuwa fundi saa na sonara, mwana wa ofisa mmoja wa jeshi na mama yake aliitwa Zélie Guérin ambaye naye alikuwa mtengeneza lesi. Baba yake alitaka kuwa mmonaki na mama yake alitaka kuwa mtakatifu. Wote wawili walitaka kuishi maisha ya kutohusiana kimwili. Lakini Padre mmoja aliwashauri maana ya ndoa na mpango wa Mungu wa ndoa. Katika familia yake walizaliwa wakiwa watoto tisa. Watoto wanne walifariki dunia bado wakiwa wadogo, wavulana wawili na wasichana wawili. Wasichana wote watano (Marie, Pauline, Leonie, Celine na Theresia) walikuwa watawa katika shirika la Karmeli. Theresia alikuwa mtoto wa mwisho na jina lake lilikuwa Francoise-Marie Therese. Akiwa mtoto aliishi kwa furaha.
Mama yake alifariki tarehe 28.8. 1887 wakati Theresia akiwa na umri wa miaka minne na nusu. Alifariki kwa ugonjwa wa kansa ya ziwa. Baada ya kifo cha mama yake baba yake aliacha biashara yake na familia ikahamia Lisieux. Dada mkubwa Marie alichukua jukumu la kusimamia familia akiwa na umri wa miaka 13. Na dada wa pili Pauline aliwasaidia wadogo zake kupata mafundisho ya dini. Pauline alichukua nafasi ya mama yake ya kumlea Theresia.
Theresia alipata elimu yake katika konventi ya wabenediktini wa Notre- Dame-du-Pre. (Mama yetu wa Pre). Lakini hakuwa na furaha.Mwaka 1886 aliacha shule akaanza kusoma masomo binafsi.
Baadaye mwaka 1882 Pauline aliamua kuingia katika maisha ya utawa pale Lisieux kwenye konventi ya wakarmeli. Kitendo hicho kilimtia huzuni Theresia akawa kama mgonjwa. Akiwa katika maisha ya wakfu alichaguliwa kuwa mkuu wa nyumba ya wakarmeli wa Lisieux. Mwaka 1886 dada zake wawili waliondoka nyumbani kwenda kujiunga na maisha ya wakfu. Leonie alikwenda Visitandines na Marie alikwenda Lisieux Karmeli.
Mwishoni mwa mwaka 1882 Mt. Theresia alianza kupata kizunguzungu cha mara kwa mara. Mwaka wa 1883 akapatwa na ugonjwa wa ajabu. Akawa anamwomba Bikira Maria wa Malkia wa Mbingu, alimwomba amhurumie na kumwondolea maumivu. Siku ya sherehe ya Pentekoste mwaka 1883 aliponywa ugonjwa wake baada ya kuona sanamu ya Bikira Maria iliyokuwa chumbani mwake ikitabasamu. Baada ya hapo akarudi shule kuendela na masomo. Alifundishwa na wamonaki wa kibenediktini wa Lisieux na baada maandalizi ya kina yaliyofikia kilele chake katika uzoefu wa wazi wa kuwa karibu sana na Kristo, akapata Komunio ya kwanza tarehe 8 Mei 1884. Alipata Sakramenti ya kipaimara tarehe 14 juni mwaka huo huo wa 1884.
Theresia naye akiwa na miaka tisa alitamani naye kuingia katika maisha ya utawa. Baadaye hata dada yake Marie naye alijiunga na maisha ya utawa. Kitendo hicho kilizidisha hamu ya Theresia ya kutaka kuwa mtawa. Akiwa na umri wa miaka 14 aliamua kuwa hata yeye anataka kuwa mtawa katika konventi ya Karmeli Lisieux. Lakini askofu alikataa akasema asubiri mpaka atimize miaka 21.
Wakati wa kesha la Noeli siku chache kabla ya kufikisha miaka 14, alipata hali fulani ambayo yeye anaiita kuongoka kwake. Maisha yake ya ndani yalipata nguvu za ajabu. Baada ya hali hiyo alisema kuwa Usiku ule Mtoto Mtakatifu alikuwa amemponya hisia zake kali na kumviringishia silaha zake. Hii ndio maana anaitwa Theresia wa Mtoto Yesu. Mwaka uliofuata akamwambia baba yake kuwa anataka kuwa mkarmeli.
Mt. Theresia alimwambia baba yake kuwa anataka kuwa mkarmeli. Baba yake alikubali lakini Viongozi wa shirika na askofu Hugonin wa Bayeux walikataa kwa sababu ya umri wake. Theresia alitamani suala hilo lifike kwa Papa. Alipata nafasi ya kumtembelea Papa Leo XIII ikiwa ni sehemu ya hija yao Roma. Alipopata nafasi ya kupita mbele ya Papa alitaka kumwomba Papa ruhusa ili aingie karmeli akiwa na miaka 15 lakini Mons. Reverony alimuwahi na kumwambia Papa kuwa anataka kuingia utawa akiwa mdogo na Papa akamwambia kuwa Mungu akipenda atakuwa mtawa. Kitendo hicho kilimuumiza sana kiasi kwamba alikiita kishawishi ambacho ilibidi apate nguvu kutoka kwa Mungu ili aweze kuyavumilia hayo yote.
Mt. Theresia aliingia Karmeli ya Lisieux tarehe 9 Aprili mwaka 1888. Alipokea vazi tarehe 10 Januari mwaka 1889, na akaweka nadhiri zake Septemba 8, 1890 katika sherehe ya kuzaliwa kwa Bikira Maria. Imani yake ilijaribiwa kwa kifo cha baba yake kilichotokea tarehe 29 Julai mwaka 1894. Hata hivyo Thérèse alikua katika utakatifu, akiongozwa na mwanga wa Neno la Mungu na aliongozwa na Injili akiuweka upendo katikati ya kila kitu
Theresia alitamani sana kuwa mtume tangu mwanzo kabisa mwa maisha yake. Alitamani sana kuokoa roho za watu wengi wakiwemo mapadre. Ili kutimiza azima yake hiyo alitamani sana kutekeleza miito mbalimbali. Alitamani awe mhubiri, mtume, mmishonari, na shahidi. Hata hivyoilikuwa tu baada ya yeye kujitoa mwenyewe akimiminwa katika Mungu na alijikabidhi mwenyewe kwa huruma Upendo ndipo alipogundua witoambao Mungu alimwitia. Alisema hivi "Nimelewa kwamba upendo hushikilia miito yote. Natambua kwamba tamaa zangu zote zimetimilika.Nimepata wito wangu. Katika moyo wa Kanisa, mama yangu, mimi nitakuwa upendo."Mafundisho yake -njia ndogo ya utoto
Mafundisho yake yanafahamika kama "njia ndogo". Alijawa na upendo wa Mungu na akajitoa kabisa kwa upendo huo. Alijua jinsi ya kuuweka katika vitendo kwa majirani zake katika njia ya kawaida kabisa. Hamu yake kubwa ilikuwa kumwona kila mtu akiangazwa na mwanga wa imani. Katika kutafuta jinsi ya kuitekeleza hiyo sauti ndipo alipogundua kuwa "wito wake alikuwa awe upendo katika moyo wa Kanisa". Ndipo hapo alipotembea katika njia ndogo ya watoto ya kujiachilia mikononi mwa Mungu. Ujumbe wake mkuu ni kuwa na tabia ya kitoto mbele ya Mungu. Aliona neema ya Kristo katika maisha yake. Mt. Theresia anawaita watu kuwa na ukarimu usio na ukomo na kuwakaribisha katika moyo wa Kanisa kuwa mitume na mashahidi wakereketwa wa upendo wa Kristo.
Teresia wa Mtoto Yesu hakuwa msomi lakini aliandika mambo ya msingi sana na ya kawaida yanayogusa maisha ya watu wengi. Wakati anaandika kurasa zake juu ya Maandiko Matakatifu, ilikuwa kabla ya Mtaguso wa Pili wa Vatican uliosisitiza umuhimu wa Maandiko Matakatifu katika maisha ya wakristo. Aliandika yale ambayo baadae yalikuja kusisitizwa na Mtaguso wa Pili wa Vatican. Aliwahi kuandika hivi:
"Ndiyo, inaonekana kwangu kuwa sikuwahi kutafuta kitu kingine zaidi ya ukweli".
Ukweli ambao alikuja kuupata katika Injili. Aligundua kuwa Maandiko Matakatifu ni muhimu kwani yanatufunulia Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Ndiyo maana alisema:
"Sipati tena kitu chochote katika vitabu isipokuwa katika Injili. Injili zinatosha". Andika tena hivi
"Nioneshe siri zilizofichika kwenye Injili, Ah! kitabu cha dhahabu/mpenzi hazina yangu". Alieleza huruma ya Mungu na haki yake.
Kazi yake ilichapishwa baada ya kifo chake anajulikana kama "Historia ya roho" ambayo anaieleza kama njia ndogo.
Mt. Theresia alifariki dunia tarehe 30 mwezi wa tisa mwaka 1897 kwa ugongwa wa kifua kikuu. Alifariki akiwa na umri wa miaka 24 tu.
Alitangazwa mtakatifu na Papa Pius XI tarehe 17 Mei 1925. Papa huyo huyo akamtangaza kuwa mlinzi wa misheni zote duniani tarehe 14 Desemba 1927.
Mt. Theresia wa Lisieux, alitangazwa Mwalimu wa Kanisa na Papa Yohane Paul II Oktoba 19, 1997.