SALA YA MWANZO
Ee Mungu, Baba yetu, amsha ndani mwetu,
dhamiri ya kwenda kukutana na Kristo wako
tukiwa na matendo mema anayekuja,
ili aweze kutukaribisha pembeni mwake
katika utukufu wa mbinguni.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Marko Mk 13:33-37
33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo.
34 Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameiacha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe.
35 Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi;
36 asije akawasili ghafula akawakuta mmelala.
37 Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.
Neno la msingi ni kesheni. Huu ni mwito wa Yesu kwa kila mmoja wetu, tukeshe. Kwa nini tukeshe, mwenye nyumba anaweza kurudi muda wowote. Inabidi tuwe makini. Hakuna kulala hapa. Katika Sura hii ya 13 tunasimuliwa habari za kuharibiwa kwa Hekalu la Yerusalemu na mji wa Yerusalemu kama ishara ya nyakati za mwisho. Lakini kwa nini Yesu anasema hivi? Kuna mwanafunzi wake mmoja akamwonesha uzuri wa Hekalu na mawe yaliyolipamba, "Mwalimu, tazama, yalivyo mawe na majengo haya!" Mk 13:1b. Ndipo hapo Yesu anamwambia kuwa hayo yote yatabomolewa Mk 13:2. Hekalu ni ishara ya uwepo wa Mungu. Yerusalemu ni mji wa Bwana. Hizi zilikuwa ishara za ahadi ya Mungu kwa Daudi. Halafu eti Yesu anasema zitabomolewa! Hii ni ishara tu ya yale yatakayo tokea mbeleni. Ndipo hapo wanafunzi wanakuwa na shauku ya kujua hayo yatatokea lini. Wanataka kujua kama kuna ishara yoyote itakayoashiria mwisho wa dunia au kuja kwake mara ya pili. Lakini Yesu anasema hiyo siku hakuna anayeijua. Hata malaika hawaijui. Halafu utasikia watu wanasema o mwisho wa dunia ni mwaka fulani, na watu wanaamini. Hii ni ajabu kweli. Hao ndio manabii wa uongo. Hata Mwana hajui ila Baba tu Mk 13:32. Kwa msemo huu unaweza kuona umuhimu wa kukeshe anaousema Yesu. Yaani malaika hawajui, na Mwana hajui, ila Baba tu. Sasa kwa nini usikeshe? Yesu anapotokea kila kitu kinakwisha. Ishara za Hekalu ni za muda, tu. Hakuna cha Hekalu wala nini. Sasa ni yeye uso kwa uso. Kama mnakumbuka mwito huu wa Yesu ameutoa mara nyingi. Alipokuwa na kwenye bustani ya Gethsemane, aliwaambia Petro, Yakobo na Yohana, "kaeni hapa mkeshe" Mk 14:34. Kukeshe kunasaidia kutoingia au kuanguka katika majaribu Mt 26:41. Wakati walipokuwa katika Gethsemane, tunaona kuwa Yesu anawaambia kuwa mwili ni dhaifu. Kuna wakati roho inataka, inakuwa tayari, lakini bwana! mwili unatuangusha Mk 14:38. Anayelala, anadondoka, anaanguka, anapotenza nguvu, ambazo ni zawadi ya Mungu. Anachotaka kusema Yesu leo ni kuwa kusali kunaepusha nafasi za vishawishi na hatari za mwovu kutupepeta kama ngano. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema " Amka, wewe usinziaye, ufufuke katika wafu, na Kristo atakuangaza" Efe 5:14