Misa Takatifu ya Sherehe ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli 16 Julai
IBADA YA MWANZO
Mwanzo
Padri au Askofu
Kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
Waamini wanaitikia:
Amina.
Halafu kuhani, hali amefumbua mikono, anawasalimu watu waliopo, akisema:
Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, na upendo wa Mungu Baba, na ushirika wa Roho Mtakatifu viwe nanyi nyote.
Waamini wanaitikia:
Na viwe rohoni mwako.
Au:
Neema na amani,
kutoka kwa Mungu, Baba yetu,
na kwa Bwana Yesu Kristo, viwe nanyi.
Waamini wanaitikia:
Na viwe rohoni mwako.
Au:
Bwana awe nanyi.
Waamini wanaitikia:
Na awe rohoni mwako.
Askofu, badala ya Bwana awe nanyi, katika salamu hii ya kwanza asema:
Amani iwe kwenu.
Waamini wanaitikia:
Na iwe rohoni mwako.
Tendo la Toba
Ndugu zangu, tukiri dhambi zetu,
ill tupate kustahili kuadhimisha mafumbo matakatifu.
Namwungamia Mungu Mwenyezi, nanyi ndugu zangu, kwani nimekosa mno
kwa mawazo, kwa maneno, kwa matendo, na kwa kutotimiza wajibu:
nimekosa mimi, nimekosa mimi, nimekosa mno. Ndiyo maana namwomba Maria mwenye heri, Bikira daima,
Malaika na Watakatifu wote,
nanyi, ndugu zangu, niombeeni
kwa Bwana Mungu wetu.
Mungu Mwenyezi atuhurumie
na, atusamehe dhambi zetu,
atufikishe kwenye uzima wa milele.
Amina.
K/.Bwana, Utuhurumie. W/.Bwana, utuhurumie.
K/. Kristo, utuhurumie. W/. Kristo, utuhurumie.
K/. Bwana, utuhurumie. W/. Bwana, utuhurumie.
Au:
K/. Kyrie, eleison. W/. Kyrie, eleison.
K/. Christe, eleison. W/.Christe, eleison.
K/. Kyrie, eleison. W/.Kyrie, eleison.
Utukufu (Gloria)
Utukufu kwa Mungu juu mbinguni
na duniani amani kwa watu wenye mapenzi mema.
Tunakusifu, tunakuheshimu, tunakuabudu, tunakutukuza,
tunakushukuru kwa ajili ya utukufu wako mkuu,
ee Bwana Mungu, Mfalme wa mbinguni,
Mungu Baba mwenyezi.
Ee Bwana, Yesu Kristo, Mwana pekee,
ee Bwana Mungu, Mwanakondoo wa Mungu, Mwana wa Baba,
mwenye kuondoa dhambi za dunia, utuhurumie;
mwenye kuondoa dhambi za dunia, pokea ombi letu.
Mwenye kuketi kuume kwa Baba, utuhurumie.
Kwa kuwa ndiwe uliye peke yako Mtakatifu, peke yako Bwana,
peke yako Uliye juu kabisa,
Yesu Kristo, pamoja na Roho Mtakatifu,
katika utukufu wa Mungu Baba.
Amina.
Sala ya mwanzo
Tuombe
Uwe na waamini wako, ee Bwana, katika safari ya maisha na kwa maombezi ya Mwenye heri Bikira Maria, Mama yetu na Malkia, utujalie tuweze kufika kwa furaha katika kilele cha mlima Mtakatifu, Yesu Kristo, Bwana wetu, aliye Mungu na anaishi na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina.
au
Ee Mungu, wewe umelipa hadhi Shirika la Karmeli kwa jina tukufu la Mwenye heri Bikira Maria, Mama wa Mwanao, utujalie sisi ambao leo tunaadhimisha Sherehe hii kuu, tuweze kwa nguvu ya msaada wake kufikia kilele cha mlima ambacho ni Kristo Bwana, Anayeishi na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele. Amina.
LITURUJIA YA NENO
Somo la kwanza 1Fal 18:42-45.
Somo la kitabu cha kwanza cha Wafalme
Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini. Akamwambia mtumishi wake, “Kwea sasa utazame upande wa bahari.” Akakwea, akatazama, na kusema, “Hakuna kitu.” Naye akanena , “Enenda tena mara saba.” Ikawa mara ya saba akasema, “Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu”. Akanena, “Enenda, umwambie Ahabu”, “Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.” Ikawa muda si muda mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi.
Neno la Bwana
Wimbo wa katikati Zaburi 14
Kiitikio: Tutakufuata popote utakapotuongoza, Bikira Maria.
1. Bwana, ni nani atakayekaa
katika hema yako?
Ni nani atakayefanya maskani yake
Katika kilima chako kitakatifu? (K)
2. Ni mtu aendaye kwa ukamilifu, na kutenda haki; asemaye kweli kwa moyo wake.
Asiyesingizia kwa ulimi wake,
wala hakumtenda mwenzie mabaya,
wala hakumsengenya jirani yake. (K)
3. Machononi pake mtu asiyefaa hudharauliwa,
bali huwaheshimu wamchao Bwana. (K)
Somo la pili Gal 4:4-7.
Somo la waraka wa Mtume Paulo kwa Wagalatia
Hata ulipowadia utimilifu wa nyakati, Mungu alimtuma Mwanae ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya Sheria, kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya Sheria, ili nasi tupate kupokea hali ya kuwa wana. Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana Mungu alimtuma Roho wa mwanawe mioyoni mwetu, aliaye “Abba!” yaani, “Baba!” Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.
Neno la Bwana
Sequenza
Ua la Karmeli,
Mzabibu stawi,
Mg'ao wa Mbingu
wewe peke yako
ni Bikira na Mama.
Mama mpole na mwadilifu
Uwe daima mpendevu
kwa wakarmeli wote,
Nyota ya Bahari.
Shangilio: Lc 11: 28.
Aleluya, aleluya
Heri wale wanaolisikiliza Neno la Mungu na kuliishi. Aleluya
Injili Yoh 19: 25-27.
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Yohane.
Penye msalaba wake Yesu walikua wamesimama mamaye na umbu la mamaye, Mariam wa Kleopa, na Mariam Magdalena. Basi Yesu alipomwona mama yake na yule mwanafunzi aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake “Mama tazama mwanao”. Kisha akamwambia yule mwanafunzi, “Tazama mama yako.” Na tangu saa ile, mwanafunzi yule, akamchukua nyumbani mwake.
Neno la Bwana.
Mahubiri
Nasadiki
Nasadiki kwa Mungu mmoja,
Baba mwenyezi, muumba wa mbingu na dunia na vitu vyote vinavyoonekana na visivyoonekana.
Nasadiki kwa Bwana mmoja Yesu Kristo, Mwana pekee wa Mungu,
aliyezaliwa kwa Baba tangu milele yote.
Mungu aliyetoka kwa Mungu, mwanga kwa mwanga, Mungu kweli kwa
Mungu kweli, aliyezaliwa, bila kuumbwa, mwenye umungu mmoja na Baba:
ambaye vitu vyote vimeumbwa naye.
Alishuka kutoka mbinguni,
kwa ajili yetu sisi wanadamu, na kwa ajili ya wokovu wetu.
Akatwaa mwili kwa uwezo wa Roho Mtakatifu kwake yeye Bikira Maria, akawa mwanadamu.
Akasulubiwa kwa ajili yetu sisi, kwa mamlaka ya Ponsyo Pilato;
akateswa, akafa, akazikwa,
siku ya tatu akafufuka, kadiri ya Maandiko,
akapaa mbinguni, amekaa kuume kwa Baba.
Atakuja tena kwa utukufu, kuwahukumu wazima na wafu, nao ufalme wake hautakuwa na mwisho.
Nasadiki kwa Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima: atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa, pamoja na Baba na Mwana:
aliyenena kwa vinywa vya manabii.
Nasadiki kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki, la Mitume. Naungama ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi.
Nangojea na ufufuko wa wafu,
na uzima wa milele ijayo. Amina.
Sala ya waamini
Ndugu zangu wapenzi, tunapoadhimisha Sherehe ya Bikira Mtakatifu, Mama wa Karmeli, tumwombe Mungu Baba yetu ili kwa maombezi ya Mama yetu awashushie wanadamu neema zake tele.
Tuitikie kwa kusema: Ee Bwana twakuomba utusikilize.
1. Kwa ajili ya Kanisa Takatifu la Mungu ambalo linamtafakari Maria aliye Mama yake na mfano wake ili kutoka kwake liweze kujifunza kulisikiliza Neno la Mungu na kulitangaza kwa watu wote. Tuombe.
2. Kwa ajili ya wale wanaomwomba Maria, Mama na Mlezi ili aweze kuwa kimbilio lao wakati wa shinda na kuwajalia moyo wa kikristo. Tuombe.
3. Kwa ajili ya familia ya Wakarmeli, ili katika Sherehe hii ya leo, itafakari kwa kina maana ya wito wake wa ushuhuda, sala na utakatifu wa maisha. Tuombe.
4. Kwa ajili ya wale wote wanaovaa skapulari kama ishara ya kujiweka wakfu na matumaini ili waweze kujifunza na kuiga fadhila za Bikira Maria na kutoa ushuhuda wa kiinjili kwa matendo yao. Tuombe.
5. Kwa ajili ya marehemu, ambao pamoja na Maria, walikuwa waaminifu kwa pendo lako, ili waweze kufurahi pamoja nawe milele mbinguni.
Ee Bwana, sikiliza sala za Kanisa lako, na kwa maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Karmeli, utujalie hayo tuliyokuomba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.
LITURUJIA YA EKARISTI
Kuombea dhabihu
Pokea, ee Baba, dhabihu tunazokuletea katika kumbukumbu ya Bikira Maria Mwenye heri; ili tunapoiga upendo wake katika kukutumikia, tuweze kushiriki kwa undani katika kazi ya ukombozi. Kwa Kristo Bwana wetu. Amina.
Utangulizi
Umama wa kiroho wa Bikira Maria.
P. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako
P. Inueni mioyo
W. Tumeinua kwa Bwana
P. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki
Kweli ni vema na haki, jambo la kufaa na kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, na kuimba vizuri utukufu wako,
ee Baba Mtakatifu, Mungu Mwenyezi wa milele,
sisi tunakusifu, tunakuheshimu, tunakutukuza,
Katika Sherehe ya Bikira Maria, Mama wa Karmeli.
Mtumishi mnyenyekevu, alipokea Neno lako na kulitunza katika moyo wake
akishiriki kwa namna ya ajabu katika fumbo la ukombozi,
alidumu pamoja na Mitume katika sala
wakimngojea Roho Mtakatifu;
Mama wa Kiroho wa waamini wote,
yupo macho akiwajali kwa upendo watu wengi na kuangaza,
safari yetu kuelekea mlima wa utukufu wako,
kama alama ya faraja na matumaini ya uhakika.
Katika yeye, kama picha kamili, sisi tunaona
kimekamilika kile tunachotamani na kutumaini tuwe katika Kanisa.
Kwa zawadi hii ya wema wako
tunaungana na Malaika na watakatifu
kuimba wimbo wa utukufu wako:
Mtakatifu, Mtakatifu...
SALA YA EKARISTI III
PC Ee Bwana, kweli u Mtakatifu,
na kiia kiumbe kilichoumbwa nawe kinakusifu kwa haki.
Maana, kwa njia ya Mwanao,
Bwana wetu Yesu Kristo,
na kwa uwezo tendaji wa Roho Mtakatifu,
unavitia uzima vitu vyote na kuvitakatifuza,
wala huachi kukusanya watu kwako,
ili, toka maawio ya jua hata machweo yake, dhabihu safi itolewe kwa jina lako.
CC Basi, ee Bwana, tunakusihi kwa
unyenyekevu, vipaji hivi, ambavyo tumekutolea ili uvitakase, upende kuvitakatifuza kwa Roho huyo huyo,
ili viwe Mwili na + Damu
ya Mwanao, Bwana wetu Yesu Kristo,
aliyetuamuru tuadhimishe mafumbo haya.
Maana, Yeye mwenyewe, usiku ule alipotolewa, alitwaa mkate na,
akikushukuru, aliubariki,
akaumega, na akawapa wafuasi wake, akisema:
TWAENI, MLE NYOTE:
HUU NDIO MWILI WANGU,
UTAKAOTOLEWA KWA AJILI YENU.
Vivyo hivyo, baada ya kula,
akitwaa kikombe,
na kukushukuru, alikibariki,
na akawapa wafuasi wake, akisema:
TWAENI, MNYWE NYOTE:
HIKI NDICHO KIKOMBE CHA DAMU YANGU,
DAMU YA AGANO JIPYA NA LA MILELE,
ITAKAYOMWAGIKA KWA AJILI YENU NA KWA
AJILI YA WENGI
KWA MAONDOLEO YA DHAMBI.
FANYENI HIVI KWA UKUMBUSHO WANGU.
PC Fumbo la imani.
Ee Bwana, tunatangaza kifo chako,
na kutukuza ufufuko wako, mpaka utakapokuja.
CC Kwa hiyo, ee Bwana,
tunapoadhimisha ukumbusho
wa mateso ya Mwanao yaletayo wokovu,
pamoja na ufufuko wake wa ajabu
na kupaa kwake mbinguni,
na tunapoutazamia ujio wake wa pili,
tunakutolea, kwa shukrani,
sadaka hii iliyo hai na takatifu.
Tunakuomba, uyaangalie matoleo ya Kanisa lako,
na kwa kumtambua Yeye, aliye kafara
ambaye ulitaka kutulizwa kwa sadaka ya kifo chake,
utujalie sisi tunaotiwa nguvu kwa Mwili na Damu ya Mwanao,
na kujazwa Roho wako Mtakatifu,
tupate kuwa mwili mmoja na roho moja katika Kristo.
C1 Yeye atufanye sisi tuwe kwako sadaka
timilifu ya milele,
ili tuweze kupata urithi pamoja na wateule wako:
kwanza kabisa pamoja na Bikira Maria, mwenye heri, Mama wa
Mungu, na Mitume wako wenye heri na Mashahidi wako watukufu,
na Watakatifu wote,
ambao tunategemea kupata daima msaada wa maombezi yao mbele zako.
C2 Tunakuomba, ee Bwana,
huyu aliye kafara na upatanisho wetu
alete amani na wokovu duniani kote.
Upende kuliimarisha katika imani na mapendo Kanisa lako, linalosafiri hapa duniani,
pamoja na mtumishi wako Baba Mtakatifu wetu J... na Askofu wetu J.... ,
pamoja na Maaskofu wote, Wakleri wote, na watu wote unaowafanya kuwa taifa lako.
C3 Usikilize kwa wema
sala za jamaa hii uliyoiita hapa mbele yako.
Ee Baba mwema, kwa huruma yako
uwakusanye kwako
wanao wote waliotawanyika popote duniani.
Uwapokee kwa wema katika ufalme wako ndugu zetu marehemu
na wote walioaga dunia wakiwa wamekupendeza.
Sisi nasi tunatumaini kufika katika ufalme huo ili pamoja tushibishwe milele kwa utukufu wako,
kwa njia ya Kristo Bwana wetu,
ambaye kwa njia yake unaujalia ulimwengu mema yote.
Kwa njia yake, na pamoja naye, na ndani yake, Wewe, Mungu Baba Mwenyezi,
katika umoja wa Roho Mtakatifu,
unapata heshima yote na utukufu
milele na milele.
IB ADA YA KOMUNYO
Tukionywa na amri ya Mwokozi,
na tukifuata mafundisho ya kimungu,
tunathubutu kusema:
Baba yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe;
ufalme wako ufike;
utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea.
Usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni.
Ee Bwana, tunakuomba utuopoe katika maovu yote, utujalie kwa wema amani maishani mwetu, kusudi, kwa
msaada wa huruma yako,
tuopolewe daima na dhambi
wala tusifadhaishwe na jambo lolote,
tunapotazamia tumaini lenye heri,
na ujio wa Mwokozi wetu Yesu Kristo.
Kwa kuwa ufalme ni wako,
na nguvu, na utukufu
hata milele.
Ee Bwana Yesu Kristo, uliyewaambia Mitume wako, "Amani nawaachieni, amani yangu nawapa", usizitazame dhambi zetu, ila tu imani ya Kanisa lako;
upende kulijalia amani na kulikusanya katika umoja, kama yalivyo
mapenzi yako.
Unayeishi na kutawala milele na milele.
Amina.
Amani ya Bwana iwe daima nanyi.
Na iwe rohoni mwako.
Mpeane amani.
Huku kuchanganya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo
kutupatie uzima wa milele sisi tunaopokea.
Mwanakondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi za dunia: utuhurumie.
Mwanakondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi za dunia: utuhurumie.
Mwanakondoo wa Mungu,
uondoaye dhambi za dunia: utujalie amani.
Ee Bwana Yesu Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, kadiri ya mapenzi ya Baba, na kwa kutenda kazi pamoja na Roho Mtakatifu, uliupatia ulimwengu uzima kwa njia ya kifo chako.
Uniokoe kwa Mwili huu mtakatifu sana na kwa Damu yako
katika maovu yangu yote na mabaya yote; unifanye niambatane daima na amri zako,
wala usiruhusu nitengane nawe kamwe.
Au:
Ee Bwana Yesu Kristo,
huku kupokea Mwili na Damu yako
kusiwe kwangu hukumu na adhabu,
bali, kwa huruma yako, kunifae mimi
kwa kunilinda akili na mwili
na kuwa dawa ya kuniponya.
Tazama, Mwanakondoo wa Mungu,
tazama anayeondoa dhambi za dunia.
Heri yao walioitwa kwenye karamu ya Mwanakondoo.
.
Ee Bwana, sistahili uingie kwangu,
lakimi sema neno tu,
na roho yangu itapona.
Mwili wa Kristo unilinde nipate uzima wa milele.
Damu ya Kristo inilinde nipate uzima wa milele.
Mwili wa Kristo.
Amina.
Ant. ya Komunyo Lk 2:19
Maria aliyaweka yote haya, akiyatafakari moyoni mwake.
Sala baada ya Komunyo
Tuombe.
Ee Mungu Baba yetu,
Kushiriki Mwili na Damu Azizi ya Mwanao, zawadi nzuri sana ya upendo wako, kuwaimarishe na kuwafanya wafuasi waaminifu wa fadhila za Mwenye heri Bikira Maria, wale waliojiweka wakfu katika utumishi wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu...
Baraka kuu
Mungu Mwenyezi, aliyeliweka Shirika la Karmeli na ninyi nyote chini ya ulinzi wa Maria awajaze furaha katika maadhimisho ya Sikukuu hii. Amina.
Awajalie neema ya kutafakari mioyoni mwenu Neno na kulitangaza kwa maisha yenu ili muwe mfano hai wa Maria ulimwenguni. Amina.
Awaongoze katika utakatifu ili baada ya kutakaswa kutoka katika udhalimu wote, kama watoto waaminifu wa Maria, baada ya kifo chenu, mfike mapema iwezekanavyo katika ushirika kamili wa watakatifu katika utukufu. Amina.
Na Baraka yake Mungu Mwenyezi, Baba, na Mwana ┼ na Roho Mtakatifu iwashukie na kukaa nanyi daima. Amina.
Nendeni na amani.
Wimbo wa Bikira Maria