Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo akiingia kwa maandamano kwa ajili ya kuadhimisha Ibada Takatifu ya Misa katika Misa ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kanisa la hija la Bikira Maria wa Mlima Karmeli bunju
Siku ya leo 25 Agosti, 2019 imekuwa siku ya kihistoria katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, bunju, baada ya Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, Askofu Mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, kuongoza ibada Takatifu ya Misa ya uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa Kanisa kubwa la hija. Katika adhimisho hilo la Ibada Takatifu ya Misa iliyoanza saa tatu asubuhi walikuwepo watu wengi na mapadre watano. Alikuwepo katibu wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Padre Frank Mtavangu, padre Thomas Maria Mtey O.Carm, paroko wa Parokia hiyo, Padre Dominic Maria Somola, O.Carm, paroko msaidizi, Padre Victor Maria Biramata, O.Carm, Mwakilishi wa Mkuu wa Shirika katika Commissarieti na Padre Njologe kutoka Consolata Mission Centre, bunju. Katika Homilia yake, Mwadhama amewahimiza waamini kujitoka kwa moyo wa sadaka kulijenga Kanisa la hija ambalo amesema itakuwa basilika. Basilika ni mlango wa mbingu mahali ibada na sala za namna ya pekee. Ndipo watu watakuja kukutana na Mungu. Matukio makubwa yalikuwa ni haya, ibada Takatifu ya Misa, Kufungua rasmi uchangiaji wa ujenzi kwa njia ya maandalizi ya chakula cha hisani kitakachofanyika mwezi wa kumi na mbili, alizindua uchangiaji huo kwa jina la kapu la Mwadhama, na uwekaji wa jiwe la msingi uliofanyika mara baada ya baraka ya mwisho. Watu wengi walihudhuria na kuonesha furaha yao na utayari wao wa kuchangia ujenzi wa Kanisa la Bwana. Bikira Maria atusimamie katika utume wetu. Inakusudiwa kukusanya kiasi cha zaidi ya milioni 650 kwa ajili ya kuweka sakafu.
Mwadhama akichangia ujenzi katika Kapu la Mwadhama