Siku ya watakatifu wote 1 Novemba. Mt 5:1-12.
Naye alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;
2 akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema,
3 Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa
mbinguni ni wao.
4 Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika.
5 Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi.
6 Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao
watashibishwa.
7 Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.
8 Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona
Mungu.
9 Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa
Mungu.
10 Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme
wa mbinguni ni wao.
11 Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na
kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
12 Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni
kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi
manabii waliokuwa kabla yenu.
Wale ambao sisi tunawaona hawana bahati, wasio na furaha hao ndio Yesu anawaita kuwa ni wenye "Heri". Kwetu sisi tajiri, mwenye mamlaka na mwenye heshima huyo ndio mwenye heri. Mwenye nacho ndio mwenye kutazamwa. Lakini kwa Yesu ni kinyume kabisa, maskini, mpole na aliyedharauliwa ndiye mwenye heri. Yesu hapa anabadilisha mtazamo wetu juu ya maisha halisi ya Mungu. Unaweza kuwaza, au tunakosea sisi au anakosea yeye. Jiulize nani anakosea? Wale ambao tunawaona wamelaaniwa ndio wenye baraka na wale ambao tunawaongelea kuwa na baraka ndio wanaongeleka vibaya. Lakini sehemu hii ya Injili inatuonesha wazi ni watu gani ambao ni wenyeji na warithi wa ufalme wa Mungu. Huu ni ufupisho wa maisha ya kikristo. Kanuni ya maisha ya Mwana wa mtu. Hii si amri mpya, bali ni maisha mapya. Kile ambacho Yesu anakisema ndicho kile anachokiishi.
Maneno yake ni habari njema. Hii ni zawadi kubwa sana katika maisha. anataka atukomboe kutoka katika hofu, kutoka katika dhambi, kutoka katika ugonjwa, kutoka katika kifo, ili tuwe na uweze wa kuona na kutangaza ufalme wa Mungu.
Maneno yake ni dawa ya maovu yetu. Ukweli unaoponya uongo wa nafsi zetu. Anataka tuwe ndugu kweli kweli. Mwanadamu lazima awe kile alicho. Anataka tuujue uso wa Mungu Baba.
Maneno haya ni kwa ajili ya kila mtu atafutaye ukweli wa maisha. Yanamrudishie mtu utu wake na hadhi yake. Basi haya ni maneno ya wokovu.
Yesu msulubiwa na mfufuko ni utumilifu wa maneno haya. Msulubiwa ni mpole, maskini, mwenye njaa, mwenye kiu, mwenye kiu ya haki, mwenye moyo safi, mleta amani, mteswa, -anapofufuka anadhirisha sehemu ya pili, ufalme ni wake, mrithi wa kiti cha enzi cha utukufu, anamwona Mungu, mwenye huruma.
Kanisa limeundwa na watu ambao wanapozisikiliza hizi heri wanamfanya Yesu kuwa msingi wao wa maisha.
Historia ya mwanadamu inabidi ikamilishe haya.
Hizi heri zinaonesha ufalme wa Mungu. Uko kati yetu. Unafanya kazi.
Watu wanakwenda kumsikiliza Yesu. Wanahamu ya kulisikiliza neno la Mungu.
Mlima ni mahali karibu na Mungu. Yesu anakaa ishara ya Mwalimu. Mwalimu pekee. Mwanafunzi ni yule anayelisikiliza neno la Yesu.
Yesu anaona makutano, anaona kwa jicho la upendo, anajali, anajitoa.
Hili ni fumbo la Kristo. Yesu ni maskini, mleta amani. Haya ndio maisha ya Yesu. Huu ni ufupisho wa maisha kila Mkristo. Hapa tunaona uso wa Yesu. Mtu mpya ambaye Mungu anamtaka, mtu mpya Roho Mpya.
Heri imerudi,,,maana yake ni nini...ninakufurahia, ninafuraha. Jaribu kusema heri yako ni maskini...utaona. Wanaona ambiwa heri ni matajiri. Mtu akishinda kitu chenye fedha tunasema..heri. Tunafikiria wenye heri ambao ni tofauti na wale wa Mungu. Yesu anaongea kitu ambacho watu hawaelewi. Katika tamaduni zao mwenye mali, tajiri, ndiye aliyekuwa mwenye heri. Umaskini si kitu kizuri ndio maana hata kanisa linajitahidi kuwasaidia. Lakini hapa tuelewa, anaongeza maskini wa roho. Utajiri ni kuwa kwa ajili ya wengine. Uhusiano na wengine. Mungu ni maskini lakini ni tajiri wa mahusiano.