HISTORIA YA MAISHA YANGU
Naitwa Gabriel John Mtiti. Nilizaliwa tarehe 12 Novemba 1997, katika Wilaya ya Bunda, Mkoa wa Mara, katika familia ya Kikatoliki ya Baba John Mtiti na Mama Bernadetha Nabigambo. Mimi ni mtoto wa tatu kati ya watoto wanne-wavulana watatu na msichana mmoja. Nililelewa katika mazingira ya Imani Katoliki, maadili mema, upendo wa familia na heshima kwa Mungu, mambo ambayo yamekuwa msingi muhimu wa safari yangu ya maisha na wito.
SAFARI YANGU YA IMANI NA ELIMU
Safari yangu ya imani ilianza kwa namna ya pekee kupitia Sakramenti za Kanisa. Nilipokea Ubatizo tarehe 27 Desemba 1998, Ekaristi Takatifu tarehe 29 Juni 2007, na Kipaimara tarehe 26 Julai 2009, zote katika Parokia ya Mtakatifu Paulo, Bunda. Kwa sasa, baada ya kuanzishwa kwa Jimbo Katoliki la Bunda, ninatoka Jimbo Katoliki la Bunda, Parokia ya Mtakatifu Pastory-Nyasura.
Katika elimu, nilianza Shule ya Msingi Miembeni B (2004-2010), kisha nikasoma Shauritanga Secondary School, Rombo (2011-2014). Kuanzia mwaka 2015-2017, nilisoma Kidato cha Tano na Sita katika Chief Kidulile Secondary School, Ludewa, nikichukua CBG-Kemia, Biolojia na Jiografia. Baadaye, niliendelea na masomo ya Falsafa katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan, Morogoro (2018-2021), nikafanya Unovisi nchini Zimbabwe mwaka 2021-2022, na kuanzia Oktoba 2022 nikaendelea na masomo ya Theolojia katika Jordan, ambayo nilihitimu tarehe 25 Juni 2026.
SAFARI YA WITO WANGU WA UTAWA
Mbegu ya wito wangu ilianza kuchipua mwaka 2006, nilipoanza kuhudumu kama mtumishi wa altare katika Parokia ya Mtakatifu Paulo, Bunda. Huduma hiyo ilinipa nafasi ya kuwa karibu na mapadri na kuona kwa namna ya pekee maisha yao ya kujitoa kwa Mungu na kuwahudumia watu wake. Mwaka 2009 nilipata ushauri kutoka kwa Sr. Paschalina, mtawa wa Karmeli, aliyenisisitizia umuhimu wa sala, bidii katika masomo na utambuzi wa wito. Mwaka 2014 nilikutana na Paschal Dominic, ambaye alinisaidia kuifahamu zaidi karama na maisha ya Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Baadaye, mwaka 2016, nilipata nafasi ya kuwasiliana na Fr. Victor Biramata, O. Carm, na hatua hiyo ikawa sehemu muhimu ya safari yangu kuelekea Karmeli.
Tarehe 5 Julai 2017 niliingia rasmi katika malezi ya Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli. Nilipitia hatua za aspiranti, postulanti na novisi, kisha tarehe 15 Agosti 2022 nikaweka nadhiri za muda katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju. Baadaye nilipokea Huduma ya Usomaji tarehe 19 Mei 2024, Huduma ya Acolyte tarehe 1 Mei 2025, na hatimaye, kwa neema ya Mungu, nikaweka nadhiri za daima tarehe 14 Februari 2026 katika Parokia ya Bunju. Pia nilipata daraja ya Ushemasi tarehe 25 Juni 2025 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, kutoka kwa Mhashamu Askofu Stefano Lameck Musomba, OSA, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo.
Kwa moyo wa shukrani, namtukuza Mungu kwa yote aliyotenda katika maisha yangu yote na mpaka nilipofikia sasa na ninaendelea kumwomba anipe neema ya kuwa mwaminifu katika wito wangu, ili kazi njema aliyoianza ndani yangu aikamilishe kwa utukufu wake na kwa wokovu wa watu wake.
Bikira Maria, Mama yetu wa Mlima Karmeli- utuombee.