DICKSON MARIA RICHARD SAMBALA O. CARM. APEWA DARAJA YA UPADRE
Mnamo tarehe 15.08.2023 Kanisa Katoliki na Shirika la Wakarmeli (O.Carm) lilipata Padre mpya. Ilikua ni shangwe na furaha kubwa kwani ndiye Padre wa kwanza Mtanzania aliyefanyia majiundo yake ya ukasisi nchini Tanzania. Ikumbukwe kuwa safari ya majiundo ya Ukasisi ya Shemasi Dickson Sambala yalianza mwaka 2014 na baada ya mwaka mmoja wa ukandidati alianza masomo ya Falsafa katika chuo Kikuu kishiriki cha Jordan Morogoro kuanzia Octoba 2015 mpaka Julai 2018. Baada ya kuhitimu masomo yake ya Falsafa Shemasi Dickson Sambala alinza safari yake ya unovisi nchini Zimbabwe kuanzia Julai 2018 mpaka Augusti 2019 alipoweka nadhiri za muda 3.08.2019 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli Bunju- Dar- es- Salam.
Baada ya Kuweka nadhiri za muda Shemasi Dickson Sambala aliendelea na Masomo yake ya Teolojia katika chuo Kikuu kishiriki cha Jordan Morogoro kuanzia Octoba 2019 mpaka Julai 2023. Na mnamo 15.08.2022 aliweka nadhiri za Daima katika Shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli Bunju- Dar- es- Salam. Mnamo 6.01.2024 alipokea Daraja takatifu la Ushemasi katika Parokia Mtakatifu Yohane Bosco, Kibaha katika Jimbo kuu Katoliki la Dar- es- Salam. Na adhimisho la Misa Takatifu ya Daraja ya Ushemasi iliongozwa na Mhashamu Henry Mchamungu Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar- es- Salam.
Adhimisho la Misa Takatifu ya Daraja Takatifu ya Upadre wa Shemasi Dickson Sambala. Iliongozwa na Mhashamu Henry Mchamungu Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar- es- Salam. Katika homilia Baba Askofu alimsihi shemasi Dickson Sambala kuwa atapakwa mafuta na kwenda kuwahudumia watu na kazi ya mafuta hayo ni kuwahubiria habari njema watu na kuwatia moyo na kuwapatia matumaini watu hasa wale waliokata tamaa. Pia alimsihi Shemasi Dickson sambala awe tayari kupigwa mishale katika utume wake na alimsihi adumu katika Sala na kuvumilia katika changamoto atakazokutana nazo katika utume wake.
Baada ya Homilia yalifuatia madhehebu ya daraja takatifu la shemasi Dickson Sambala O.Carm na mnamo saa tano asubuhi Kanisa na Shirika liliongeza mtenda kazi katika shamba la Bwana. Baada ya hapo, Askofu alimpongeza Padre mpya akifuatiwa na Mapadre waliokuwepo katika adhimisho la Misa Takatifu.
Baada ya utoaji wa daraja Takatifu ya Upadre ibada ya Misa Takatifu iliendelea kama kawaida. Na mwishoni mwa ibada Padre mpya alitoa Baraka kwa Baba Askofu na baadaye akatoa Baraka kwa waamini wote.
Pongezi nyingi zilitolewa kwa ajili ya Kumshukuru Mungu kwa zawadi ya Padre mpya, pongezi kwa wazazi wa padre mpya kwa malezi walio mpa kijana wao, na pia pongezi kwa Shirika la wakarmeli kwa zawadi ya kumpokea na kumlea vizuri mpaka kufikia daraja ya upadre. Baada ya hapo ilifuatia hafla na sherehe fupi ya kumpogeza Padre mpya.
Matukio mbalimbali wakati wa upadrisho