SAFARI YA WITO WANGU WA KITAWA
UTANGULIZI WA MAISHA
Kwa jina naitwa Edger Joseph Beneth, nilizaliwa katika mkoa la Dar-es- Salaam, mnamo tarehe 14 Julai 2004, nikiwa mtoto wa pili kati ya watoto wanne katika familia ya Joseph Beneth (Mnyakyusa kutoka Mbeya) na Happiness Temu (Mchaga kutoka Kilimanjaro). Familia yetu imeshika imani thabiti ya Kikatoliki, na wazazi wetu wametulea katika misingi ya kumtegemea Mungu katika kila hatua ya maisha.
ELIMU NA MALEZI YA AWALI
Safari yangu ya kiroho ilianza mapema kupitia malezi ya Masista wa Canossa. Nilihudhuria Shule ya Awali ya Josephine Bakhita kuanzia mwaka 2006 mpaka mwaka 2010 na baadaye kupata elimu ya Shule ya Msingi hapo hapo Canossa Primary School kuanzia mwaka 2011 hadi mwaka 2017, shule hizi zote zikiwa chini ya usimamizi wa Masista wa Magdalena wa Canossa. Nilipokea Sakramenti ya Ubatizo tarehe 15 Agosti 2004, Komunyo ya Kwanza tarehe 2 Juni 2013 katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju A, na Kipaimara tarehe 15 Julai 2018 katika Parokia ya Mtakatifu Gasper.
Baada ya elimu ya msingi, nilipata elimu ya sekondari (O-Level), katika shule ya Shule ya sekondari ya Libermann Boys kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2021 chini ya malezi ya Mapadre wa Shirika la Roho Mtakatifu (Spiritan Fathers). Kasha nilijiunga na Seminari Ndogo ya Mtakatifu Fransisko wa Asizi, Maua (2022–2024), mkoani Kilimanjaro, iliyo chini ya usimamizi wa Mapdre-Watawa wa Mtakatifu Fransisko kapuchini (OFM Capuchin Fathers), ambapo nilianza kuishi na kuthamini nguzo tatu za maisha ya kitawa yaani; usafi wa moyo, ufukara, na utii.
MWANGA WA AWALI WA WITO
Nilianza kuhisi wito mtakatifu wa upadre, nikiwa darasa la tano, nilipoanza kutumikia katika Misa Takatifu shuleni Canossa. Nilipenda sana kutumikia hasa nafasi ya chetezo, na hata baada ya kujiunga na Karmeli kama Muaspiranti nilikuwa bado napenda kutumikia chetezo, hivyo hamu ya kumtumikia Mungu iliendelea kukua zaidi na zaidi.
Pale nilipojaribu kuwashirikisha wenzangu kuhusu nia yangu wengi walibaki wakinicheka, lakini hilo halikuzima moto na msukumo wa ndani uliokuwa unanifanya kuhisi kuwa nmeitwa kuwa padre. Wakati wa O-Level, nilivutiwa sana na maisha ya sala, hasa sala za kijumuiya na zile binafsi. Nilipenda sana sala ya novena, hasa novena ya Mtakatifu Rita wa Kashia, tuliyofundishwa na mapadre wa shirika la Roho Mtakatifu waliotulea. Hii ilinijengea misingi ya tafakari na kujitenga kwa ajili ya Mungu.
KUKUA KIROHO NA MSUKUMO WA KARMELI
Baada ya elimu ya kidato cha nne, Katika hatua za ukuaji wa kibailojia ( Adolescence), nilichangamka, nikahudhuria sherehe na matukio mengi ili “kula ujana” na kusikiliza muziki wa kidunia. Lakini kadiri muda ulivyopita, nilikumbuka lengo na nia ya ndani kabisa ya moyo na hivyo nilianza kubadilika na kumkaribia Mungu tena. Nilianza kama awali kusali tena novena, kumwomba Bikira Maria, na kutafakari kwa undani. Nilivutiwa sana na gloto ya Mama Yetu Bikira Maria, hasa nilipojiunga na Seminari ya Maua.
Niliteuliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha kitume cha Legio Maria kutokana na ibada yangu kwa Mama huyu, ingawa nilimchagua kijana mwingine niliyemuona kuwa mwenye bidii na moyo wa sala zaidi. Tulikuwa tukisali pamoja, tukijadili ukuaji wetu wa kiimani na ukaribu wetu kwa Mama Maria. Niliteuliwa tena kuwa msambazaji wa mahitaji ya chama, na mara hii sikukataa na nilijitahidi kuhudumu na kujitolea kwa moyo wote. Nilisali mara kwa mara binafsi katika gloto, hasa baada ya masomo, usiku na hata asubuhi. Niliona ni nafasi ya dhahabu kwangu kuimarika kiroho.
UZOEFU WA PEKEE JKT
Baada ya kumaliza elimu ya kidato cha sita, nilijiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) katika kambi ya Ruvu. Hata na hapo nilipata mwanga wa kipekee kuhusu wito wangu. Nilihudhuria ibada kila Jumapili na hata kuwahamasisha wenzangu kuhudhuria ibada hizo. Tulisali kwa pamoja yaani; Wakatoliki, Walutheri, waanglikana na wa madhehebu mengine mwngi ya kipentekoste.
Wakati wa kuimba nyimbo za Kikatoliki, zilivutiwa watu wengi. Na mimi mara kadhaa niliguswa sana na mahubiri ya ndugu wa Kipentekoste kuhusu upendo wa Mungu na kitabu cha Ufunuo. Nilihisi hofu na hamu ya kutubu, lakini haikuwezekana kwa sababu hakukuwa na mapadre kambini.
Siku moja, Br. Clinton alihubiri kuhusu upendo wa Mungu na toba na mara baada ya kumaliza ibada nilimfuata na tukazungumza sana kuhusu maisha yangu ya kiroho. Nilimwambia, “Bro, nimetenda dhambi nyingi, nataka kutubu” Aliniambia, “Br. Edger, umeitwa.” Tulianza kutubu kwa mtindo wa kilokole hadi tukamaliza. Nilirudi kambini kwa siri, sikugundulika, na nilihisi uhuru na faraja ya kiroho. Na kwa wakati wote huo Nilibadilika sana na kuwa mtu wa utulivu, nikijitenga kwa tafakari na ukimya. Nikipenda kusaidia na kujitolea katika majukumu mbalimbali hadi wenzangu walianza kuniita “Baba Mchungaji.”
MAAMUZI YA KUJIUNGA NA KARMELI
Baada ya kumaliza mafunzo ya JKT, nilibahatika kuhudhuria Kongamano la Ekaristi na kujiunga na Mapadre na mafrateli wa Karmeli. Nilianza kuhisi kama niko nyumbani, walinionyesha upendo na kuniambia kuhusu maisha ya Karmeli na fadhila zake tatu kuu. Ijapokuwa nilikuwa tayari nimewasiliana na Fr. Manda wa OFM Cap kuhusu kujiunga na Wakapuchini, haikuwezekana kwa sababu ya masharti ya kambi. Nilizungumza na mama yangu na paroko wangu, ambaye alitufariji na kusema, “Kanisa ni moja, mashirika ni mengi. Mwambie avumilie na aendelee na mafunzo.”
Nilisali sana sala ya Kanisa nikiomba kujiunga na O.Carm, ingawa walikuwa hawapokei kwa wakati huo. Nilijihisi kuwa ni mkarmeli kwa moyo. Nilizungumza na Fr. Dominick Somola, Fr. Victor Biramata, na Fr. Dickson Sambala mara kadhaa. Hao Wakanipa moyo na mwongozo hadi nilipokubaliwa kujiunga rasmi katika shirka la wakarmeli kama Muaspiranti na baadae mpostulanti huko Morogoro.
HITIMISHO
Safari yangu ya maisha na wito imekuwa ya mabadiliko, sala, na mwongozo wa Mungu. Namshukuru Mungu kwa neema ya kutambua wito wangu, na kwa watu waliokuwa nami katika safari hii. Naendelea kuishi kwa furaha na uhuru katika kumtumikia Mungu, nikiikumbatia njia ya Karmeli kwa upendo na uaminifu.
“Yeye aliyeanza kazi njema ndani yangu, ataiendeleza hadi siku ya Kristo Yesu.” Wafilipi 1:6
NA: EDGER J. BENETH, MPOSTULANTI.