LITURUJIA
Sacrosanctum Concilium, 4 December, 1963.
1. Maana ya Liturujia
Neno Liturujia linatokana na neno la kigiriki, «leitourgia». Neno hili limeundwa na maneno mawili. La kwanza ni Leitos, laos, likiwa na maana ya watu –taifa na la pili ni ergon, likiwa na maana ya kazi au huduma –kufanya tendo. Hivyo neno liturujia lilitumika kumaanisha kazi inayofanywa hadharani au tendo linalofanywa hadharani kwa manufaa ya umma au ya taifa. Tunaweza kusema kuwa Liturujia ni wajibu wa umma au huduma kwa taifa inayofanywa na raia. Ni kazi ya watu wote au huduma kwa niaba/ kwa manufaa ya taifa.
2. Katika Biblia –huduma ni Liturujia
a. Katika Agano la Kale
Tafsiri ya Biblia ya kigiriki iitwayo Septuaginta inatumia Liturujia kwa ajili ya utumishi wa umma wa hekalu. Soma kitabu cha Kutoka 39:1 utaona kuwa kutumika ni liturujia (Tafsiri ya kiswahili haitumii neno liturujia). Baadae inatumika kueleza kazi za dini za makuhani, kama vile kazi ya huduma ya hekaluni, soma Yoeli 1:9, 2:17.
b. Katika Agano Jipya
· Adhimisho la ibada ya kimungu Lk 1:23
· Tangazo la Injili Mdo 13:2; Rum 15:16
· Mapendo kwa matendo Rum 15:27.
Katika Luka 1:23, “Ikawa siku za huduma yake zilipokuwa zimetimia akaenda nyumbani kwake.” Katika Waebrania 8:6, “Lakini sasa amepata huduma iliyo bora zaidi, kwa kadiri alivyo mjumbe wa agano lililo bora, lililoamriwa juu ya ahadi zilizo bora”. Kuhani mkuu wa Sheria Mpya amepata Liturujia bora, kwamba ni ainabora ya utumishi kuliko ule wa Hekalu.
3. Liturujia katika Kanisa
Soma Sacrosanctum Concilium namba 7. Tunasoma hivi: “Kumbe, kwa haki Liturujia hutazamwa kama utekelezaji wa kazi ya kikuhani ya Yesu Kristo. Katika Litutrujia, kwa ishara zinazoonekana, huoneshwa na kutendeka kutakatifuzwa kwake binadamu, kila ishara ikiwa na namna ya pekee. Katika Liturujia, ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo. Hili ni tendo takatifu kupita yote” (SC 7).
Matumizi ya Liturujia katika Kanisa lina maana ya huduma au utumishi rasmi wa Kanisa wa hadhara. Hivyo basi:
· Liturujia ni kazi ya ukuhani wa Yesu Kristo.
· Kazi ya Kristo –Kwa njia ya Liturujia, Kristo, Mkombozi wetu na Kuhani Mkuu huendeleza katika Kanisa lake, pamoja nalo, na kwa njia yake, kazi ya ukombozi wetu.
· Kazi ya Kanisa. Katika Liturujia Kanisa huadhimisha hasa Fumbo la Pasaka ambalo kwalo Kristo aliikamilisha kazi ya wokovu wetu. Taifa la Mungu lashiriki katika «kazi ya Mungu».
· Katika hali zote Liturujia ni swala la huduma kwa Mungu na kwa watu.
4. Liturujia
Ni tendo la hadhara la Kristo mzima kabisa katika Kanisa lake ambapo waamini hufanya Ibada ya hadhara ya kumsifu na kumtukuza Mungu Baba wakiwa wameunganika na kichwa –Yesu Kristo.
5. Nia ya liturujia
Liturujia ni chanzo au chemchemi safi na ya milele ya maji yaliyo hai ambapo inabidi kuchota bure zawadi ya Mungu. Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatikan wanaeleza nia ya Liturujia inayowekwa katika kazi ya wokovu kuwa ni kwa ajili ya:
· Tendo la shukrani na Kumsifu Mungu/ masifu kwa Baba
· Kumbukumbu ya sadaka ya Kristo na ya Mwili wake
· Na utakaso wa mwanadamu –kwa uwepo wa Kristo wa Neno lake na Roho wake.
6. Yesu Kristo chanzo cha Liturujia
1. Mpatanishi kati ya Mungu na wanadamu
2. Ukuhani wa Kristo unaendelezwa kwa njia ya Liturujia. (SC 7).
3. Inafanya tendo lote la wokovu la Kristo lifanye kazi wakati wa adhimisho. Kwa hiyo kila adhimisho la kiliturujia, kwa kuwa ni tendo la Kristo Kuhani, na la Mwili wake, ndilo Kanisa, ni tendo takatifu kupita yote kwa namna ya hali ya juu kabisa, na hakuna tendo jingine la Kanisa linalofanana nalo kwa manufaa kwa kiwango kile kile na kwa daraja ile ile. (KKK 1069).
7. Maana ya Sakramenti katika adhimisho la Ekaristi Takatifu
Lugha ya zamani ya Kanisa ilikuwa ni Kigiriki. Walipokuwa wakiadhimisha ubatizo na kipaimara. Walikuwa wakisema kuwa ni Mysterion (Μυστηριον) yaani, fumbo, (kitu kilichofichika). Walipokuja kulitafsiri neno hilo la Kigiriki katika kilatini wakasema kuwa ni Mysterium. Lakini watu walipata shida kuelewa vizuri neno hilo kwa sababu halikuwa rahisi kwao, ndipo wakatafsiri kwa kutumia neno la pili la Sakramentum, ambalo linatumika katika Kiswahili kama Sakramenti-alama inayoonekana. Katika Kiswahili Mysterium inatafsiriwa kama fumbo na Sakramentum inatafsiriwa kama Sakramenti. Sakramenti ni ishara inayoonekana ambayo ndani mwake kuna fumbo la wokovu (Mysterium). Ndiyo maana tunapoadhimisha Sakramenti tunasema tunaadhimisha mafumbo ya wokovu.
8. Mambo muhimu katika kuadhimisha Sakramenti
Sakramenti huadhimishwa katika imani kwa Bwana wetu Yesu Kristo. Katika kuadhimisha Sakramenti kuna mambo muhimu yanayohitajika. Materia –ishara na Forma –maneno na mhudumu. Materia ni kitu kinachotakiwa kutumika ili kuadhimishia hiyo Sakramenti. Mfano maji kwa ajili ya ubatizo. Forma ni Maneno yanayotamkwa wakati wa kuadhimisha hiyo Sakramenti. Mfano J...nakubatiza kwa jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu. Mhudumu ni yule anayeadhimisha Sakramenti kwa jina la la Kanisa na kwa Mamlaka ya Kanisa.
9. Sakramenti ya Ekaristi
Sakramenti ya Ekaristi ni chemchemi na kilele cha maisha yote ya Kikristo (K.K.K 1324). Kushiriki Ekaristi ndicho kiwango cha juu sana cha kuungana na Kristo katika tendo la kumwabudu Mungu Baba. Sakramenti hii huitwa majina mbalimbali yaliyotokana na jinsi ilivyoadhimishwa katika mwendo wa karne. Neno Ekaristi lamaanisha “kutoa shukrani”. Hivyo Ekaristi ni tendo la shukrani kwa Mungu, Yesu anatoa shukrani kwa Mungu kwa kukamilisha kazi aliyopewa. Huitwa pia karamu ya Bwana, ambayo yajieleza kwa kuumega mkate. Yaitwa ukumbusho wa mateso ya Bwana. Vile vile yaitwa Komunyo. Kwa sababu katika kuupokea Mwili na Damu yake tunaungana naye na kuwa Mwili mmoja. Adhimisho lake linaitwa Misa Takatifu. Materia ni Mkate na Divai iliyochanganywa na maji.
10. Anayeadhimisha Liturujia –Misa Takatifu
Ni taifa lote la Mungu –Mwili wa fumbo wa Yesu Kristo –Mwadhimishaji wa kwanza ni waamini waliokusanyika pamoja na Kanisa zima. Kila mtu huchukua nafasi katika adhimisho hili kadiri ya hali yake. Mtendaji mkuu ni Kristo na Kanisa ambalo linaonekana kwa njia ya waamini. Hivyo adhimisho ni tendo la Liturujia la Kanisa zima. Adhimisho la Liturujia ni sherehe –(Celebration).
11. Maeneo muhimu katika adhimisho
· Fumbo –Utatu Mtakatifu katika historia ya wokovu
· Ibada –sababu ya kipasaka. Tukio la Pasaka. Katika adhimisho ibada ni kuishi tukio au tendo la Pasaka -Kumbukumbu.
· Uwepo wa Kristo –fumbo linaloadhimishwa katika ibada ni lazima liwe hai, liwe maisha halisi.
12. Tabia zake
· Tendo la kukutana katika kundi –ecclesia
· Kuitwa –taifa la Mungu limekusanywa kwa Jina la Baba, la Mwana, na la Roho Mtakatifu.
· Kufanya sherehe –adhimisho la Ekaristi ni sherehe. Ni tendo la shukrani linalofanywa kwa Mungu.
· Ishara na maneno
13. Mwenendo wa adhimisho la Ekaristi Takatifu
· Liturujia ya Neno (Masomo ya Agano la Kale na Agano Jipya)
Kusoma Neno –homilia, na maombi yake.
· Liturujia ya Ekaristi –kuleta mkate, na matoleo, kushukuru –konsekrasio na komunyo.
· Matayarisho ya vipaji -Kuviweka altareni
· Utangulizi (Prefatio)- shukrani za Kanisa kwa Mungu Baba –uumbaji –duniani -mbinguni.
· Anaphora (Sala ya Ekaristi) –sala ya shukrani na sala ya wakfu (Consecratio) –epiklesi –Kumwomba Roho Mtakatifu pamona na maneno ya Yesu –kilele cha mageuzo.
· Anamnesi – kumbukumbu ya Mateso, Ufufuko na kurudi kwake katika utukufu.
· Maombi –Umoja wa Kanisa zima –yanagusa sehemu mbalimbali –
· Komunyo -Baba yetu, sala ya Bwana na kumega mkate.
14. Fumbo la Pasaka
Kiini cha adhimisho la Liturujia ni Fumbo la Pasaka ya Kristo, kufa na kufufuka. Katika adhimisho la Liturujia Kristo ndiye anayetenda.
1. Kristo yupo katika Neno lake
2. Kristo yupo katika mhudumu – Kasisi -Padre , Askofu.
3. Kristo yupo katika hadhara ya waamini –katika Kanisa linalo Sali na kumba
4. Kristo yupo katika Ekaristi Takatifu (Sakramenti zote saba).
15. Vitabu vya Liturujia (Misa Takatifu)
· Kitabu cha Masomo ya Misa Takatifu –The Lectionary -(Lectionarium). Ni kitabu chenye masomo yanayosomwa wakati wa Misa Takatifu.
· Misale (Missale Romanum) –Ni kitabu chenye sala na kanuni mbalimbali (rublics) zinazotumika kwa adhimisho la Misa Takatifu.
· Pontificale –kitabu chenye maadhimisho yanayoongowa na Askofu. (Ushemasisho Upadrisho , uaskofisho, kutabaruku Kanisa).
· Rituale – Kitabu hiki ni cha sala na maelekezo muhimu kwa ajili ya kuadhimisha Sakramenti na visakramenti, mazishi, maandamano na maadhimisho mengine.
16. Mwaka wa Liturujia –Adhimisho La Fumbo La Kristo
Mwaka wa Liturujia ni mzunguko wa kila mwaka wa kalenda ya Liturujia ambapo Kanisa huadhimisha matukio makubwa ya historia ya wokovu, toka umwilisho na kuzaliwa kwa Bwana Yesu Kristo, Mateso, Kufa na Kufufuka kwake, mpaka siku ya zawadi ya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste, mwishoni mwa mwaka Liturujia hutafakari kwa matumaini kurudi kwake Bwana. Mwaka wa Liturujia umewekwa kwa mzunguko wa makundi ya mwaka A, B na C. Hivyo kuna masomo yanayosomwa mwaka A, na B na C. Kima masomo yakiwa na lengo fulani.
17. Injili zinasomwa kwa mtiririko huu:
1. Mwaka A –Injili kadiri ya Mathayo.
2. Mwaka B –Injili kadiri ya Marko
3. Mwaka C –Injili kadiri ya Luka.
4. Injili ya Yohane haina mwaka maalum isipokuwa husomwa katika miaka yote mitatu kwa matukio. Injili hii husomwa zaidi wakati wa Mateso ya Bwana.
18. Mpangilio wa mwaka wa Liturujia
· Majilio
· Kipindi cha Kuzaliwa Bwana
· Kipindi cha mwaka –baada ya tokeo la Bwana
· Kwaresima
· Siku Tatu Kuu za Pasaka (Triduo pasquale). Kitovu cha maadhimisho yote ya mwaka wa Liturujia kimeundwa na «Siku Tatu kuu za Pasaka fumbo», Mateso, Kufa na Kufufuka kwa Yesu Kristo ambalo li katikati ya mwaka wa kiliturujia. Siku Tatu Kuu za Pasaka za Mateso na Ufufuko wa Bwana zinang’aa kama utimilifu kwa mwaka wote wa Liturujia.
· Kipindi cha Pasaka –mpaka Pentekoste Kipindi cha mwaka –baada ya Pentekoste. Kipindi cha mwaka cha Liturujia kina majuma 33 au 34. Ni maadhimisho ya historia ya wokovu ambapo Dominika ni Pasaka ya wiki.
19. Sherehe
Sherehe zinatazamwa kama siku muhimu katika mwaka wa Kanisa. Maadhimisho yake huanzia na Masifu ya Kwanza ya jioni siku inayotangulia. Baadhi ya sherehe zina Misa yake ya Kesha ambayo inaadhimishwa jioni kabla ya siku ya sherehe. Masomo ni maalum ya sherehe.
20. Sikukuu
Huadhimishwa siku yenyewe, hazina Masifu ya Kwanza ya jiopni. Sikukuu za Bwana zinazoangukia siku ya Dominika ya Mwaka au kipindi cha Noeli nazo huchukua nafasi ya Dominika.
21. Kumbukumbuku
Ni za lazima au za hiari. Hizo huingizwa katika ashimisho la siku ya Juma kadiri ya Kanuni zilizowekwa katika Katiba Kuu ya Misale ya Kirumi na ya Liturujia ya vipindi. Kumbukumbu za lazima zinazotokea siku za Juma wakati wa Kwaresima zaweza kuadhimishwa tu kama kumbukumbu za hiari. Iwapo katika siku moja zinatokea kumbukumbu zaidi ya moja, moja tu yaweza kufanyika.
22. Jumamosi
Jumamosi za kawaida kama hakuna kumbukumbu ya lazima, inaruhusiwa kufanya kumbukumbu ya hiari ya Bikira Maria.
23. Siku za Juma
Siku za Juma zinazofuata baada ya Dominika zaitwa siku za juma. Zinaadhimishwa kwa namna mbalimbali kadiri ya umuhimu wao wa pekee.
24. Maadhimisho kadhaa yanapoingiliana
Iwapo maadhimisho kadhaa yanaangukia siku moja, adhimisho lenye cheo kikubwa kadiri ya jedwali la siku za Liturujia hufanyika.
Ikiwa mwaka huo sherehe inazuiwa kutokana na Dominika ya Majilio, ya Kwaresima au wakati wa Pasaka, sherehe ihamishiwe jumatatu inayofuata, au iwe siku ya karibu zaidi inayoruhusu. Kama sherehe inazuiwa na Dominika ya Matawi au Diminika ya Pasaka, itahamishiwa katika siku huru baada ya Dominika ya pili ya Pasaka. Maadhimisho yoyote mengine yanayozuilika yanaachwa kwa mwaka huo.
Ikiwa siku hiyo hiyo inatakiwa kuadhimisha Masifu ya jioni ya Ofisio ya siku hiyo na Masifu ya jioni ya Kwanza ya siku inayofuata, Masifu ya Jioni ya siku yenye cheo kikubwa zaidi huchukua nafasi ya kwanza. Cheo kinapokuwa cha namna moja Masifu ya jioni yatakuwa ya siku hiyo.