KWA NINI MAJI YANACHANGANYWA NA DIVAI WAKATI WA MISA TAKATIFU?
1. Utamaduni wake
Kitendo cha kuchanganya maji na divai ni cha kale sana katika Kanisa. Inaaminika kwa uhakika kuwa, katika Kalamu ya Mwisho Yesu alitumia divai iliyokuwa imechanganywa na maji kwa sababu ulikuwa ni utamaduni wa kawaida miongoni mwa Wayahudi. Utamaduni huu unatumika kwa Makanisa yote ya Magharini na Mashariki. Ijapokuwa maji siyo kitu muhimu sana kwa uhalali (validity of the Sacrament) wa Sakramenti lakini Kanisa linasisitiza kuwa ni ya muhimu sana hivyo hayatakiwi kuachwa.
2. Mtaguso wa Trento
Mtaguso wa Trent ulitishia kumtenga na Kanisa mtu yeyote ambaye angejaribu kukataa kuwa siyo ya muhimu (Canon 9, Session XXII). Mt. Justin Mfiadini alitetea matumizi yake mwaka 150. Hata Cyprian alifanya hivyo karne moja baadaye. Mafundisho yake yamekubalika katika Kanisa. Yanasema hivi: «Kwa kuwa Kristo anatubeba sisi sote, katika hilo anazibeba pia dhambi zetu, tunaliona hilo katika maji lakini katika divai inaoneshwa damu ya Kristo. Lakini maji yapochanganywa na divai kwenye kikombe, watu wanafanywa kuwa kitu kimoja na Kristo, na jumuiya nzima ya waamini huunganishwa naye na kuunganika naye wanayemwamini, wakishaunganishwa hakuna uwezekano tena wa kuwatenganisha». Kutenganisha kimojawapo wakati wa mageuzo na kuwatenganisha waamini toka kwa Kristo. Hivyo huwezi kubariki maji peke yake au divai peke yake.
3. Mt. Tomasso wa Aquino
Maana nyingine ya kitendo hicho inatolewa na Mt. Thomas wa Aquino –Summa Theologiae, III pars q 74, 6-8. Anasema: maji ni lazima yachanganywe na divai kwa sababu:
(i) kwanza kabisa: Bwana wetu Yesu Kristo alitumia divai iliyochanganywa na maji kulingana na utamaduni wa wakati ule wa nchi ile. Hilo utalipata katika kitabu cha Mithali 9:5.
(ii) Pili ni kwa sababu inaweka uwiano wa kuonesha mateso ya Bwana, kama Papa Alexander I anavyosema “Katika kikombe cha Bwana lazima kiwemo divai iliyochanganywa na maji, na kisipo kimojawapo tu, maana tunasoma kuwa ubavuni mwake vilitoka vyote viwili, (Maji na damu)”.
(iii) Tatu anasema kuwa hii inatumika kuonesha yatokanayo na Sakramenti hii kama alivyosema Papa Julius; “tunaona kuwa watu wanamaanishwa na maji lakini damu ya Yesu na divai, hivyo maji yanapochanganywa na maji watu na Kristo huunganika kuwa kitu kimoja”.
(iv) Nne ni kwa uhalisia wa matokeo ya Sakramenti ambayo ni kuingia katika maisha ya milele. Mt. Ambrosi anasema: “maji hutiririka kwenda kwenye kikombe na kububujika katika maisha ya milele”. Hizo ndizo sababu ambazo Kanisa linazingatia katika kuadhimisha utaratibu wa ibada hii. Hilo linaonekana wazi kwenye sala ambayo Padre huisali chini chini wakati anapochanganya maji na divai. Anasema:
“Kwa fumbo la maji haya na divai hii
tujaliwe kushiriki umungu wa Kristo,
aliyekubali kushiriki ubinadamu wetu”.
Sala hii inagusia fumbo la Umwilisho wa Kristo na maji ni alama yetu sisi tunaoshirikishwa Umungu wake kwa ubatizo.