Dickson ni jina nililoitwa baada ya kuanza shule ya msingi mwaka 1992. Kabla ya hapo waliniita Majaliwa, jina ambalo lipo hata kwenye cheti changu cha klinic ya watoto wachanga. Inasemekana kwamba mara baada ya mimi kuzaliwa, sikupatiwa jina mapema, watu walipofika kuniona walimuuliza mama, umejaliwa mtoto gani? Alijibu wa kiume; waliuliza umempa jina gani? Alijibu bado sijampa jina; ndipo waliposema kwakuwa, umejaliwa kuzaa salama, basi mwanao ataitwa Majaliwa. Niliendelea kuitwa hivyo hadi ulipo fika wakati wa kuanza shule ya msingi ambapo waliniita Dickson, kama nilivyo jieleza hapo juu.
Mnamo tarehe 18/ 09/ 1981, nilizaliwa. Ilikuwa ni katika klinic iliyopo, kitongoji cha Ugute, kijiji cha Isalavanu, kata ya Isalavanu, tarafa ya Sadani, wilaya ya Mufindi, mkoa wa Iringa katika nchini ya Tanzania. Nilipo fikisha miaka tisa ilinipasa kuanza shule, lakini kwa bahati nzuri au mbaya mama yangu alijifungua na akajaliwa watoto mapacha, na mimi nilionekana kuwa ndie mtoto pekee ambae ningeweza kumsaidia mama yangu kulea wale watoto, hasa ikizingatiwa kwamba maisha yetu yalikuwa ni ya kijijini na yalitegemezwa na kilimo kwa asilimia mia moja. Popote alipo kusudia kwenda mama yangu, iwe shambani, iwe sokoni, iwe kisimani au kwenye klabu za pombe ya kienyeji nilipaswa kwenda nae, ili nimsaidie kubeba mtoto mmoja wapo.
Kama sehemu aliyo kusudia kwenda mama haikuwa mbali sana, basi aliweza kuniacha nyumbani na watoto wote wawili, wakilia nawabembeleza, mama akirudi anawanyonyesha na maisha yanaendelea.
Jina la baba ni Richard Sambala, na mama ni Dominica Mdapo. Kati ya wazazi wangu wawili, anae ishi hadi sasa (2016) ni mama, baba alifariki mnamo mwaka 2014/ mwezi wa 5 tarehe 15. Wazazi wangu hawakuwa na ndoa ya kanisa, bali ya kienyeji, hii ilitokana na baba kuwa na ndoa za mitala (polygamy), hata hivyo kabla ya ndoa yao, mama yangu alikuwa ni mkristo safi na mwanakwaya wa kanisa katoliki la wasa mkoani Iringa ambalo kwa sasa ni parokia. Alikuja kutengwa na kanisa baada ya kuolewa kwenye mitala, ingawa hakuacha kabisa kusali, kwani hata mimi/sisi kama watoto tulipokea chachu ya sala toka kwake, alisisitiza sana kwenda kanisani kila jumapili.Inasemekana kwamba mama yangu alibatizwa katika hatari ya kufa akiwa mtoto mchanga huko wasa.Katika ndoa yao walijaliwa kupata watoto kumi, ikiwemo mizao miwili ya mapacha wawili wawili, mzao mmoja wa mapacha motto mmoja alikufa wakati wa kujifungua.
Kati ya hao watoto kumi, mimi ni mtoto wa nne kuzaliwa. Na kati ya hao watoto kumi, wanao ishi hadi sasa (2016) ni sita. Walio tangulia mbele za haki ni mtoto wa 1,2, na mzao wa sita katika kuzaliwa, ambao walikuwa mapacha na walikufa kwa nyakati tofauti.
Kama nikiamua kulinganisha na kipindi cha nyuma, hali ya imani kwa sasa ina ridhisha, hasa baada ya mama yetu kuchukua uamuzi wa kurudi kundini. Hivyo sasa sisi ni familia ya kikristo, ingawa watoto karibu wote wanaishi katika miji yao na utaratibu wao wa maisha, ila mama yetu ameonesha mfano mzuri, kwa sisi watoto kwamba kuteleza sio kuanguka, waweza kusimama na kuendelea mbele.
Ikumbukwe kuwa familia yetu haikuwa na maisha halisi ya kikristo, kwahivyo, hakuna mtoto ambae alibatizwa akiwa mtoto. Ni mama yetu ambae katika kipindi chake cha usichana, alilelewa kikristo, na alikuwa na tabia ya kutukumbusha kwenda kanisani siku za jumapili. Tangu nilipokuwa mdogo, kaka yangu, ambae ni marehemu Robert Sambala, aliongozana na mimi kila jumapili kwenda kanisani; ndani ya kanisa niliposumbua, alinitishia msalaba wa kristo wenye sanamu ya msulibiwa, hapo niliweza kunyamaa na kumtazama padre hadi mwisho wa misa.
Kivutio changu kikubwa cha wito ni padre Sebastian, ambae alikuwa na asili ya weupe/mhindi; Vipengele vyake vya kuimba katika misa ndivyo vilivyo kuwa vinanifanya nitamani kuwa ndo kiongozi wa misa na kutamani kuwa padre.Nilipofika darasa la pili-tatu, nilifanywa mkatekumeni, nilihudhuria mafundisho ya ubatizo kwa mwaka mzima, hii ilikuwa ni kutokana na juhudi za katekista mmoja aitwae Emilyo Mbata, sitamsahau kwa hamasa yake kuu na Mungu ampe Baraka maridhawa zenye kumfaa kwa safari ya mbinguni. Wakati na baada ya ubatizo, nilijawa na furaha kubwa, iliyo nipa matumaini na tama ya kumtumikia Mungu kama Padre na sio kama katekista. Maana nakumbuka katika utoto wangu, sikuwaga tayari kwenda kanisani kama ni zamu ya katekista. Ni padre t undo angenifanya niende kanisani.
Naweza kusema kuwa, umaskini, kukosa malezi thabiti ya kiroho wakati wa utoto wangu, kukosa washauri makini na makandokando ya ibilisi, kilikuwa kikwazo kikubwa katika kufikia mapema wito wangu, na hii lazima niiweke wazi tena kwamba: mwanadamu katika ujinga wake na udhaifu wake, ana nafasi kubwa ya kuchelewesha mipango ya Mungu lakini sio kuzuia kabisa. Kikwazo cha umaskini kinajidhihirisha kama ifuatavyo;
Mara baada ya matokeo ya darasa la saba mwaka 1998, nilichaguliwa na kutumiwa barua ya kujiunga na masomo ya secondary katika shule ya MET (Mufindi Education Trust), iliyopo maeneo ya Sadani kule Mufindi Iringa. Kwa bahati mbaya, unaodaiwa kuwa ni umaskini, uliingilia kati, baada ya wazazi wangu kukiri kwamba hawana uwezo wa kunisomesha.
Dhana ya kukosa washauri wazuri, inajitokeza kupitia maamuzi niliyo yachukua baada ya kuambiwa kwamba, shule siendi kwasababu ya umaskini. Baada ya kuhangaika na kujipatia wafadhili, niliamua kuondoka Iringa na kuja Dar es Salaam kutafuta maisha, na hii hatua ilichukuliwa baada ya kukaa nyumbani mwaka mmoja baada ya kuhitimu darasa la saba.
Ilikuwa ni siku ya trh 23/09/1999, nilipoondoka rasmi iringa na kuja Dar es salaam kutafuta maisha. Nilipokelewa na kaka yangu ambae hakuwa na ajira rasmi, alinikabidhisha kwa mafundi wa kujenga, ambapo nilitumika kama msaidizi katika shughuli zao kwa mda wa mwaka mmoja. Ilipofika mwaka 2002 mwezi wa pili, nilianza kazi mpya ya ulinzi pamoja na kutunza bustani katika nyumba ya mtu binafsi kule mikocheni.Ikumbukwe kwamba kazi hii niliifanya kwa mda wa miaka nane(2002-2009), nikiwa na mshahara wa 45,000 na mwaka mmoja wa mwisho 70,000, kimsingi niliacha hii kazi kwakuwa mshahara ulikuwa hautoshi tena baada ya vyakula kupanda bei, hat hivyo naamini ulikuwa mpango wa Mungu, niache kwa mda ile kazi.
Hali ya kutamani upadre, ilikuwa ikipotezwa na shughuli nyingi za kutafuta pesa, lakini nikienda kanisani jumapili na kukutana na padre, wito ulirudi kwa kasi kubwa. Hali hii ilipelekea kuiheshimu sana jumapili. Kipindi chote nilicho kuwa Dar es Salaam nikifanya kazi niliiheshimu sana jumapili, wala sikuthubutu kufanya kazi siku hiyo bali nilienda kanisani kusali, ingawa nilikuwa mkristo wa jumapili nisie na jumuia, hata hivyo baadae nilianza kusali jumuia kule mikocheni Parokia ya Mt. Marta.
Baada ya kutamani sana kuwa padre kwa mda mrefu, mnamo mwaka 2006, nilimuuliza padre mmoja kule mikocheni, kwamba nifanyeje ili niweze kuwa padre? Kwa hakika jibu lake lilinikatisha tama, kwakuwa hata yeye hakuwa na namna ya kunitia moyo; aliniambia ukitaka kuwa padre lazima usome hadi fourm six ndipo utapokelewa, niliondoka kwa unyonge na elimu yangu ya darasa la saba, huku nikiamini kwamba Mungu anaupendeleo.
Kwakuwa niliyatamani sana madhabahu, niliend kwa mlei mmoja ambae alikuwa nimsomaji wa masomo kanisani, ili ni muulize japo nafasi ya kusoma somo kanisani… alicho nijibu ndicho kilinifanya nianze kusali jumuia, alisema hivi ‘jumuia yenye zamu ya kusimamia kanisani ndio huwa na jukumu la kutoa wasomaji wa masomo siki hiyo’ name sikuchelewa kuitafuta jumuia, na baada tu ya kujiunga zamu yetu ilipofika, nilijitokeza pia kama mtu mwenye uwezo wa kusoma na baadae nikawa msomaji rasmi.
Kwakuwa sikuwa na matumaini tena ya kuwa padre kutokana na elimu yangu ndogo, kumbe nilianza kuwa na mipango ya kufanya biashara ya kati. Hasa nilipanga kununua gari ndogo ili niifanye tax, na kwakuwa hela yangu niliyojikusanyia kazini haikutosha kununua gari, niliamua kujiunga na Saccos moja ya urafiki kule shekilango Dar es Salaam, ambao walikuwa na form inayo eleza kuwa baada ya kutimiza mashart ya uanachama, utakopa marambili ya kile ulicho nacho. Ilinichukua mda mrefu kidogo, kutimiza mashart ya uanachama na hapo akiba yangu yote ya bank nikawa nimeihamishia Saccos ya urafiki kwa matumaini kwamba baada ya mda mfupi nitakopa milioni sita, kwakuwa ya kuwekeza million tatu kama tunda na kazi ya mikono yangu. Hakika utayaona maajabu ya Mungu, kwani hiyo yote ilikuwa ni mipango yangu tu, na sio ya Mungu.
Ilipofika mwanzoni mwa mwezi wa tisa mwaka 2009, niliandika barua ya kuomba mkopo kulingana na maelekezo yao, chaajabu kishangae! Wakaniambia wanahitaji dhamana ya kati ya nyumba, kiwanja au gari… hapa nilishindwa kuwaelewa, kumbe walikuwa wamefilisika, maana hata nilipo waomba wanirudishie hela yangu milioni tatu walishindwa wakasema watanirudishia kidogokidogo. Sikuwa na namna zaidi ya kuumiza sana kichwa, kwasababu ya kuyumba kwa ndoto zangu na mipango yangu kwa ujumla wake.
Nikiwa kati ya moja ya mitaa ya pale mwenge opposite na ITV, nikitokea kule Saccos ya urafiki na majibu mabaya ya mkopo, nilisisimka na kukutana na kibao cha tangazo la shule kwa walio ikosa, kiliandikwa hivi ‘Tunatoa elimu ya sekondari kwa miaka miwili kupitia mfumo wa QT (Qualifying test), hapo nilijikuta moyo wangu umepata amani, hasira za kunyimwa mkopo zikaisha, nikakumbuka wito wangu, tangu mda ule nikagundua kwamba upadre bado unawezekana. Nilifuata kibao hadi hapo kwenye kituo cha mafunzo nikakutana na mkuu wa kituo ambae aliitwa pia Dickson, hakika alinitia moyo, akaniambia ada ya kila mwezi ni sh 20,000/. Nilianza rasmi kusoma trh 22/11/2009. Kwa kutumia pesa ambayo nilikuwa nalipwa kidogokidogo kule kwenye Saccos ya urafiki, huku nikiamini kwamba nilikosa mkopo wa kununua gare ili mpango wa Mungu upate kutimia.
Kiukweli mwanzoni shule ilionekana kuwa ngumu sana, kutokana na urefu wa mda niliokaa mtaani tangu kumaliza elimu ya msingi, ni miaka isiyo pungua kumi (1998-2009), lakini ashukuriwe Mungu kadiri siku zilivyo zidi kwenda ndivyo nilivyo zidi kupata wepesi, na mitihani nikawa sifeli. Baada ya mwaka mmoja na nusu hali yangu ya uchumi ilibadilika, na maendeleo ya shule yakaanza kulega, kwasababu nililazimika tena kurudia kazi ya ulinzi wakati wa usiku na mchana kuingia darasani, hata hivyo Mungu si athumani, ndani ya miaka mine, nilikuwa nimemaliza na nimefaulu, mtihani wa Taifa wa kidato cha sita. Ukawa ndio mwanzo wa safari yangu ya utume na kuitika wito.
Kutokana na ugumu wa fedha, wakati namalizia idato cha nne, nilishindwa kulipia huduma za msingi katika chumba nilicho kuwa naishi pale mwenge, hasa umeme na maji, hivyo nililazimika kuhamia pembezoni mwa mji kidogo (Bunju), kwakuwa huko kulikuwa na nyumba ambayo ningeishi bure, palikuwa mbali na shule pia na eneo langu la kazi ya ulinzi lakini sikuwa na namna zaidi ya kufanya. Baada ya kufika Bunju niliendelea kushirikiana na wkristo wa huko, nikajiunga na wasomaji, pamoja na jumuia, nikazoeleka na kuwazoea waamini wenzangu. Punde baada ya mtihani wa kidato cha sita, niliamua kwenda kwa paroko wa Bunju, Pd. Thomas Mtey, ili kumueleza hisia na nia yangu ya kutaka kuwa padre; alinielekeza kwa upole habari za shirika lao la Carmel na kwamba wataanza kupokea vjana walio maliza form six na kufaulu, mara tu baada ya matokeo. Niliyasubiri matokeo kwa hamu kubwa, na mara yakatoka nikawa namefaulu. Nilimtaarifu paroko, akaniita nikaanza malezi, mnamo trh 22/07/2014.
Tulipo anza kipindi cha malezi, tulikabidhiwa baba yetu na mlezi wetu wa maisha ya kiroho ambae ni padre Victor A. Bilamata. Ni baba wa ukweli, ajuae kuelekeza, kuonya kwa busara na hekima zote; kwa hakika ni Rafiki wa vijana. Nae kwa dhati ya Moyo wangu, namuomba Mungu ili amjalie Baraka maalum na zawadi ya ushindi katika mapambano ya haya maisha huku duniani. Na kazi yake ya ubaba idumu, ili iendelee kuwa furaha isiyo na kikomo, tangu duniani hadi mbinguni kwenye ukamilifu. Kwa ujumla maisha ya huku ni mazuri, na uzuri huu unapambwa na mfumo mzuri na endelevu wa kusali pamoja, pia kushiriki katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa kadiri ya mazingira yetu, hii ni njema na kwangu ina mvuto. Baada ya kumaliza mwaka wa malezi pale bunju, tulitumwa na wenzangu kwenda kule Morogoro kwaajili ya masomo ya falsafa, katika chuo cha Jordani.
Kwa upande wangu, masomo ya falsafa sio rahisi hata kidogo, kwanza nilipatwa na mashaka, ya kwamba iv ni Mungu kweli alie niita au nilijiita? Nilijiuliza swali hilo baada ya kujitafakari sana na kujiona kuwa sina uwezo wa kuyakabili yale masomo hata kidogo, lakini nilisema moyoni, ‘kwa mapito niliyopita hata kufika hapa, sio kwa nguvu zangu, wala za shetani bali ni mkono wa Mungu anaependa mema, basi na hapa atanisaidia!’ na kweli kadiri ya mwendo wa siku, masomo nayazoea na mtihani sifeli. Kwahiyo hadi sasa kwa haya masomo, bila Mungu mimi sina namna ya kushinda, ila kwakuwa yeye ni njia yangu, basi mimi nitashinda.
MWISHO……Napenda kumshukuru Mungu kwa mema yake yote anayo nikirimia, wazazi kwa kutimiza wajibu wao wa kunilea, shirika la Wakarmeli na wanajumuia wa jumuia ya Bunju Dar es Salaam Tanzania kwa kutupokea kama walelewa, ndugu, jamaa pamoja na marafiki wote hasa walelewa wenzangu!!! Nasema tusife moyo kwakuwa haki bado inaishi, mradi tumjue alie tuzaa. Amina.