SAFARI KUELEKEA IRINGA KWA SHEREHE ZA MISA ZA SHUKRANI ZA FR DICKSON MARIA SAMBALA.
Mnamo Tar 18. August.2023, siku ya Alhamisi, safari ya kuelekea Iringa ilianza ambapo waseminari kumi walio katika hatua mbalimbali za malezi pamoja na ndugu Cornelius kutoka Kenya walisafiri kutoka Dar-es salaam hadi Morogoro ili kuungana na baba mlezi, Padre Victor Biramata tayari kwa safari ya kuelekea mkoani Iringa ili kusheherekea pamoja na Pd. Dickson Sambala katika misa zake za shukrani kwa daraja ya upadre.
Safari rasmi ilifanyika siku ya jumamosi ya Tar 19. August. 2023 kuanzia majira ya saa tatu na robo asubuhi baada ya adhimisho la misa takatifu katika nyumba ya malezi, Kola, Morogoro. Safari ilikuwa nzuri sana kwani ilikua imesheheni mambo mengi ya kujengana kiroho, kimwili na kiakili. Tulifanikiwa kupita katika hifadhi ya taifa ya Mikumi na hivyo kufanya utalii wa ndani na kuona Wanyama mbalimbali kama swala, twiga, pundamilia, Nyati, simba jike, nyani na ngedere, nyumbu na tembo.
Pia, kwa mara ya kwanza baadhi yetu tuliweza kuona mandhari ya Mlima Kitonga, mlima korofi wenye kona nyingi na kali ulio na umbali wa kilometa 8 kwa mzunguko wa rami. Basi kutokana na sababu zilizokuwa njee ya uwezo wetu gari yetu ilipata hitilafu kidogo hapo na kufanyiwa marekebisho stahiki na hatimaye safari yetu iliendelea vizuri kabisa mpaka kufika Iringa mahali paitwapo Mafinga mjini.
Tulifika Mafinga majira ya saa tatu na nusu hivi usiku, huku wenyeji wetu, paroko wa parokia ya Mafinga pamoja na msaidizi wake na Pd. Dickson na Pd. Melchizedek Lalika ambao ni mapadre wapya walitupokea kwa upendo na ukarimu mkubwa sana, huko pia tuliungana na wageni wawakilishi wa wawata kutoka parokia ya BMMK Bunju, Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-salaam. Tulipokea maelezo machache kutoka kwa paroko kuhusu parokia ya Mafinga pamoja na kuhusu eneo la Mafinga kwa ujumla kama shughuli za kiuchumi,shughuli za kiuchungaji, hali ya hewa ya eneo la Mafinga na kadhalika, pia tulipata kwa mlo wa jioni na baada ya sala ya pamoja wote tulitawanyika katika maeneo yetu husika kwa ajili ya mapumziko ili kujiandaa kwa misa za shukrani kwa siku zilizofuatia.
2. MISA YA SHUKRANI PAROKIANI MAFINGA.
Siku ya Jumapili ya Tar 20. August. 2023 ilifanyika misa ya shukrani kwa Mungu kwa zawadi ya upadre kwa mapadre wapya wawili, Padre Dickson Maria Sambala na Padre Melchizedek Lalika, mapadre wazawa wa parokia ya Mafinga. Adhimisho la misa lilianza mnamo majira ya saa tatu kamili asubuhi kwa maandamano kutokea kanisa la parokia hadi viwanja maalum vilivyokuwa vimeandaliwa kwa ajili ya tukio hilo kubwa. Misa hii takatifu iliongozwa na Padre Melchizedek Lalika wa shirika la Bikira Maria wa Konsolata na Padre Dickson Sambala wa shirika la Bikira Maria wa Mlima Karmeli kama mwadhimishaji mwandamizi. Na hivyi misa hiyo ya shukrani ilifanywa kwa heshima ya Bikira Maria.
Katika mahubiri yake, padre mhubiri wa siku hiyo aliwasihi mapadre wapya kutangiliza kwanza na hasa huduma yao ya kikuhani kuliko kujitafutia manufaa binafsi, kuwafikiria kwanza kondoo waliokabidhiwa kuwachunga na kuwaongoza kuliko kujifikiria wao wenyewe, huku akitumia mfano wa msamaria mwema uliotolewa na Bwana na mkombozi wetu Yesu Kristo alipokuwa akijibu swali la mwanasheria mmoja kusema “na jirani yangu ni nani?” rejea injili ya Luka 10:25-37. Basi aliwasihi kuiga namna yule msamaria alivyomwangalia kwa huruma na upendo na kumhudumia yule aliyeanguka katika mikono ya wanyang’anyi kwani huyu msamaria alijiuliza kuwa nikimuacha hapa huyu ni nini kitakachompata? na kuacha mwenendo wa yule mlawi aliyejifikiria kwanza yeye kwamba ni nini kitampata endapo atamhudumia yule mjeruhiwa.
Basi baada ya hayo adhimisho la misa liliendelea kama ulivyo utaratibu wa liturujia.
Baada ya misa takatifu kuisha, wakuhani walirejea kanisani ili kubadili mavazi ya ibada na hivyo kuja kwa ajili ya kuendelea na sehemu ya pili ya sherehe ambayo iliambata na utambulisho wa makundi mbalimbali yaliyoshiriki, neno kutoka kwa mapadre wapya, keki na shampeni, zawadi, michezo na hatimaye chakula na vinywaji kabla ya kuhitimisha sherehe hizo kwa sala na kutawanyika kwa kusanyiko lote.
3.MISA YA SHUKRANI YA NYUMBANI KIJIJINI ISALAVANU.
Agusti 22, 2023 ilikuwa siku ya Jumanne, siku iliyokuwa nzuri kabisa na yenye hali ya hewa tulivu ambapo watu kutoka maeneo mbalimbali ya Mafinga mjini na vijiji vyake waliamka asubuhi na mapema na kukusanyika katika Kijiji cha Isalavanu, wenyeji wakipaita Nazareth ya Fr. Dickson Sambala wakimaanisha mahali alipozaliwa na kupata malezi ya awali ya familia na elimu ya awali Padre Dickson Sambala.
Safari yetu kama familia ya wakarmeli waliokwenda Iringa ilianzia parokiani Mafinga mnamo majira ya saa tatu na robo asubuhi kuelekea Isalavanu. Safari hii ilikuwa ni ya takribani dakika thelathini hadi kufika nyumbani kabisa kwa Padre. Dickson Sambala. Basi huko mara tu baada ya kufika kwa mapdre walioandamana naye katika misa hiyo ya shukrani, Padre Dickson alianza kwanza kubariki nyumba na maeneo ya hapo nyumbani kwao na kisha adhimisho la sadaka ya misa takatifu lilianza mnamo majira ya saa nne kamili asubuhi, likiongozwa na Padre Dickson mwenyewe.
Katika homilia yake kwa padre Dickson, padre Thomas maria mtey o.carm aliyekuwa mshenga wake, paroko wa parokia ya Mt Yakobo Mabwepande na dekano wa dekania ya Kibaha, alimsihi Padre Dickson kufuasa na kuchochea ndani yake na katika utume wake kwa karibu kabisa fadhira na karama za kimaria hasa unyenyekevu, uvumilivu katika magumu na masumbuko na moyo wa shukrani kwa mungu kwa makuu hayo aliyomtendea. Aidha Padre Thomas aliwaasa waamini walioshiriki katika misa hiyo,wanafamilia, wanakijiji wa Isalavanu na viunga vya jirani kumshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa aliyopenda kuwapa na hivyo kuwaasa wawaheshimu, wawapende, wawatunze na kuwaombea mapadre wao.
Na hivyo basi baada ya homilia, adhimisho la misa takatifu liliendelea kama ilivyo utaratibu wa liturujia. Na kuhitimishwa baadae kwa baraka kutoka kwa Padre Dickson na mapadre wapya wenzake alioambatana nao. Na kisha mapadre wote walikwenda kwa ajili ya kubadili mavazi ya ibada.
Baada ya adhimisho la misa takatifu, lilifuatiwa na sherehe ya kumpongeza Padre Dickson Sambala kwa kufungua kwa sala, utambulisho, keki na shampeini, zawadi, neno la shukrani kutoka kwa Pd. Dickson na mwisho chakula, burudani na michezo.
Baada ya hayo familia ya wakarmeli iliagana na Padre Dickson na wanafamilia wa Padre Sambala na kuanza safari ya kuelekea jijini Dar-es-salaam tayari kwa shughuli nyingine za kiutume. Na hivyo basi tulifika Iringa mjini na kutembelea maeneo kadhaa ya kikanisa kama Kanisa Kuu La Jimbo Katoliki La Iringa Na Chuo Kuu Cha Kanisa Katoliki Ruaha, RUCU na baadae kupata malazi hapo kwa usiku huo na asubuhi iliyoufuatia safari ya kurudi Morogoro ilianza majira ya saa tatu hivi na baada ya kufika Morogoro, siku iliyofuatia waseminari wote walirudi Dar-es-salaam kuendelea na utume wao mdogo mdogo wa parokiani.
Na Mpostulant: Ansbert
Frate