1. Ekaristi ni nini?
Ekaristi ni Sakramenti ya Mwili na Damu ya Yesu Kristo, katika maumbo ya mkate na divai. Sakramenti hii iliwekwa na Yesu Mwenyewe kwenye karamu ya mwisho, siku ya Alhamisi jioni kabla ya mateso yake. (Yoh 6:1-71; Mt 26:26-28).
2. Maana ya jina Ekaristia –Tendo la shukrani na baraka.
Jina Ekaristia limetokana na neno la Kigiriki, εύχαριστείν, maana yake ni “tendo la shukrani”, “kutoa shukrani”, (Lk 22:19; 1Cor 11:24). Ni tendo ambalo Yesu analifanya kwa Mungu. Anamshukuru Mungu kwa kukamilisha kazi ya ukombozi. Tendo la baraka –εύλογείν. Kulingana na utamaduni wa Wayahudi baraka ilikuwa ikitolewa wakati wa mlo ikitukuza kazi za uumbaji za Mungu (Mt 26:26; Mk 14:22).
3. Injili zinazoongelea kuwekwa kwa Ekaristi
Injili tatu zinatueleza jinsi Yesu Kristo alivyoweka Ekaristi Takatifu:
Mt 26:26-28.
Mk 14: 22-24
Lk 22:19-20
Mwinjili Yohane anaeleza Yesu Kristo mkate wa uzima. Sura ya sita.
4. 1Kor 11:23-25
Mtume Paulo anatueleza jambo hilo katika Waraka wa kwanza kwa Wakorintho. 1Kor 11:23-25.
5. Tunajifunza kutoka kwa Yesu mambo yafuatayo Lk 22:
1. Saa ya Yesu (Lk 22:14). Hapa hamaanishi saa ya kula, hapana. Bali saa ile ile ya kutimiliza tendo la wokovu. Yohane anapenda kusema saa ya kumtukuza Mungu, saa ya kupita kutoka ulimwengu huu kwenda kwa Baba. Sisi tunaweza kusema, tuna saa maalum ya kuingia katika ulimwengu wa roho.Saa ya kukutana na Mungu, kutoka ulimwengu huu kwenda kwa Mungu. (Sala au kifo).
2. Shukrani na masifu kwa Baba (Lk 22:17).
3. Kugawana sisi kwa sisi kikombe cha kwanza (Lk 22:17).
4. Kumbukumbu ya sadaka yake ya wokovu (Lk 22:19).
5. Uwepo wake (Lk 22:19).
6. Damu yake imemwagika kwa ajili yetu, kikombe cha pili (Lk 22:20).
Ekaristi ni Baraka kuu: Yesu anabariki –kazi ya wokovu inabarikiwa na Yesu Mwenyewe. Hata vitu tunavyovitumia kila siku ni lazima kuviombea baraka. Kabla ya mageuzo mkate na divai vinaombewa baraka (Mt 26:26).
Yesu anajitoa mwenyewe kwa watu –Yesu anajitoa kwa kila mshiriki (Mt 26:26).
5. Matunda ya Ekaristi katika maisha ya mkristo.
1. Muungano na Kristo: Ekaristi inatuunganisha na Kristo kwa muungano wa ndani kabisa (Yoh 6:56).
2. Uzima wa milele: Ekaristi ni chanzo cha uzima, maisha yetu yote yanapata uzima kwa kushiriki Mwili na damu ya Kristo, (Yoh 6:57).
3. Umoja: Ekaristi inaleta umoja wa kweli. Tunafanywa kuwa mwili mmoja (1Kor 10:16-17).
4. Huondoa dhambi: Inatuondolea kwa kuzifuta dhambi ndogo au inatutenga na dhambi ndogo (Mt 26:28; Yoh 1:29). Sakramenti ya kitubio ndio hasa huondoa dhambi za mauti (1Yoh 1:7; Yoh 20:22-23).
5. Dawa ya kutuponya kutoka katika umauti: Ekaristi ni dawa ya kutokufa (Yoh 6:57-58).
6. Kufufuliwa siku ya mwisho: (Yoh 6:54).
6. Nguvu ya Ekaristi –Kuponywa kwa kuondolewa dhambi zetu.
Nguvu za Mungu zimo katika Ekaristi. Kabla ya kupokea Ekaristi tunasali Ee Bwana sistahili uingie kwangu lakini sema neno tu na roho yangu itapona. Bila shaka litakuwa kosa kubwa kwetu sisi kufikiri kwamba uponyaji unahusu masuala ya mwili tu. Si kila uponyaji ni uponyaji wa mwili. Mtume Paulo katika Waraka wa kwanza kwa Wathesalonike sura ya 5:23 kuwa sisi wanadamu tu mwili, roho na nafsi. Hivyo tunaweza kuponywa nafsi zetu na roho zetu. Hata kama uponyaji haujanja katika mwili. Lakini mara nyingi ukitokea uponyaji wa ndani basi matokeo yake utayaona hata kimwili. (anima sana in corpore sano) (Roho yenye afya katika mwili wenye afya)
1. Ekaristi Takatifu inayalinda maisha ya kimungu ya roho tuliyoyapokea wakati wa Ubatizo, kwa kumpatia anayekomunika nguvu za kimungu za kupambana na vishawishi, na kudhoofisha nguvu za tamaa. Inaimarisha uhuru wa mapenzi ya nafsi zetu wa kuhimili mashambulizi ya shetani.
2. Ekaristi Takatifu inaongeza maisha ya neema ambayo tayari tunayo. Hufanya hivyo kwa kuhuisha fadhila na vipaji vya Roho Mtakatifu tulivyonavyo.
3. Ekaristi Takatifu inayatibu magonjwa ya kiroho ya nafsi kwa kuziondoa dhambi ndogo na kumkinga mtu na adhabu ndogo ndogo za kidunia zitokanazo na dhambi. Ondoleo la dhambi ndogo na mateso ya muda yasababishwayo na dhambi hizi hufanyika mara moja kwa sababu ya upendo kamili kwa Mungu ambao huamshwa kwa kuipokea Ekaristi. Ondoleo la dhambi hizi hutegemea kiasi cha upendo unaoelekezwa kwenye Ekaristi (Lk 7:47).
4. Ekaristi Takatifu inatupa furaha ya kiroho tunapomtumikia Kristo, tunapotetea njia yake, tunapotekeleza majukumu yetu ya maisha, na kufanya sadaka zetu zinazotukabili ziwe ni katika kuiga maisha ya Mwokozi wetu.
Hitimisho.