MISA YA SHEREHE YA NABII ELIYA
MWANZO Tazama 1Fal 17:1.
Nabii Eliya akasema:
«Bwana aishi, Mungu wa Israeli,
ambaye ninasimama mbele zake».
SALA
Ee Mungu Mwenyezi wa milele, uliyemjalia nabii Eliya kuishi katika uwepo wako, na kutumika kwa wivu wa utukufu wako, uwajalie watumishi wako, kuutafuta siku zote uso wako, ili wawe duniani mashahidi wa upendo wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu daima na milele. – Amina.
Liturujia ya neno
Somo la kwanza 1Fal 18:20-39
Nabii Eliya alifanya waone yupi ni Mungu wa kweli
Somo la kitabu cha kwanza cha wafalme
Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli. Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno. Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini. Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri. Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini. Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya. Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe. Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika. Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli. Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni. Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu. Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji. Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie. Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji. Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.
Neno la Bwana.
Au
Somo la kwanza 1Fal 19:1-14
Na tazama, alisikia sauti ya Bwana katika upepo mtulivu akamwambia, “unafanya nini wewe hapa, Eliya?”
Somo la kitabu cha kwanza cha wafalme
Basi, Ahabu akamwambia Yezebeli habari ya mambo yote aliyoyafanya Eliya, na jinsi alivyowaua manabii wote kwa upanga. Ndipo Yezebeli akampelekea Eliya mjumbe, kusema, Miungu wanifanyie hivyo na kuzidi, nisipokufanya roho yako kesho, panapo wakati huu, kama roho ya mmojawapo wa hao. Naye alipoona hayo, aliondoka, akaenda aihifadhi roho yake, akafika Beer-sheba, mji wa Yuda, akamwacha mtumishi wake huko. Lakini yeye mwenyewe akaendelea katika jangwa mwendo wa siku moja, akaenda akaketi chini ya mretemu. kajiombea roho yake afe, akasema, Yatosha; sasa, Ee Bwana, uiondoe roho yangu; kwa kuwa mimi si mwema kuliko baba zangu. Naye akajinyosha akalala chini ya mretemu; na tazama, malaika akamgusa, akamwambia, Inuka, ule. Akatazama, kumbe! Pana mkate umeokwa juu ya makaa, na gudulia la maji, kichwani pake. Akala, akanywa, akajinyosha tena. Malaika wa Bwana akamwendea mara ya pili, akamgusa, akasema, Inuka, ule; maana safari hii ni kubwa mno kwako. Akainuka, akala, akanywa, akaenda katika nguvu za chakula hicho siku arobaini mchana na usiku hata akafika Horebu, mlima wa Mungu. Akafika kunako pango, akalala ndani yake. Na tazama, neno la Bwana likamjia, naye akamwambia, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu, waiondoe. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe.
Neno la Bwana
WIMBO WA KATIKATI Zab 16:
1. Mungu, unihifadhi mimi, Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Sina wema ila utokao kwako.
(K) Ndiwe Bwana wangu; sina wema ila utakao kwako.
2. Huzuni zao zitaongezeka Wambadilio Mungu kwa mwingine;
Sitazimimina sadaka zao za damu,
Wala kuyataja majina yao midomoni mwangu.
3. Bwana ndiye fungu la posho langu,
Na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
4. Kamba zangu zimeniangukia mahali pema,
Naam, nimepata urithi mzuri.
5. Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yuko kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
6. Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume Mna mema ya milele.
Somo la pili 1Pet 1:8-12
Wokovu wa Kristo ilivyotabiriwa na manabii
Naye mwampenda, ijapokuwa hamkumwona; ambaye ijapokuwa hamwoni sasa, mnamwamini; na kufurahi sana, kwa furaha isiyoneneka, yenye utukufu, katika kuupokea mwisho wa imani yenu, yaani, wokovu wa roho zenu. Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi. Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo. Wakafunuliwa ya kuwa si kwa ajili yao wenyewe, bali kwa ajili yenu walihudumu katika mambo hayo, ambayo sasa yamehubiriwa kwenu na wale waliowahubiri ninyi Injili kwa Roho Mtakatifu aliyetumwa kutoka mbinguni. Mambo hayo malaika wanatamani kuyachungulia.
Neno la Bwana
SHANGILIO Lk 9:35
Aleluya, aleluya
Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye.
Aleluya
Somo la Injili Takatifu ilivyoandikwa na Mathayo Mt. 17: 1-3; 9-13
Nguvu ya Eliya imekwisha kuja katika Yohana Mbatizaji.
Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani; akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang'aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru. Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye. Na walipokuwa wakishuka mlimani, Yesu aliwaagiza, akasema, Msimwambie mtu ye yote habari ya maono hayo, hata Mwana wa Adamu atakapofufuka katika wafu. Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza? Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote, ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao. Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji.
Neno la Bwana
Au
Somo la Injili Takatifu ilivyondikwa na Luka Lk 9:28-36
Musa na Eliya, wakizungumza na Yesu.
Baada ya maneno hayo yapata siku nane, aliwatwaa Petro na Yohana na Yakobo, akapanda mlimani ili kuomba. Ikawa katika kusali kwake sura ya uso wake ikageuka, mavazi yake yakawa meupe, yakimeta-meta. Na tazama, watu wawili walikuwa wakizungumza naye, nao ni Musa na Eliya; walioonekana katika utukufu, wakanena habari za kufariki kwake atakakotimiza Yerusalemu. Petro na wale waliokuwa pamoja naye walikuwa wamelemewa na usingizi; lakini walipokwisha amka waliuona utukufu wake, na wale wawili waliosimama pamoja naye. Ikawa hao walipokuwa wakijitenga naye, Petro alimwambia Yesu, Bwana mkubwa, ni vizuri sisi kuwapo hapa; na tufanye vibanda vitatu; kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya; hali hajui asemalo. Alipokuwa akisema hayo, lilitokea wingu likawatia uvuli, wakaogopa walipoingia katika wingu hilo. Sauti ikatoka katika wingu, ikisema, Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye. Na sauti hiyo ilipokwisha, Yesu alionekana yu peke yake. Nao wakanyamaza, wasitangaze kwa mtu siku zile lo lote katika hayo waliyoyaona.
Neno la Bwana
KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, uliyekuwepo kwa njia ya ajabu katika sadaka ya Eliya, upokee kwa huruma na wema matoleo ya Kanisa lako. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. – amina.
Bwana awe nanyi.
Na awe rohoni mwako.
Inueni mioyo.
Tumeinua kwa Bwana.
Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
Ni vema na haki.
Utangulizi wa nabii Eliya
Kweli ni vema na haki, jambo la kufaa na kuleta wokovu, kutangaza matendo yako makuu, na kukushukuru Wewe, kwa niaba ya watu wote,
Baba mtakatifu, Mungu mmoja aliye hai na wa kweli, kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
Wewe uliwachagua na kuwainua manabii, ili watangaze kwamba wewe ni Mungu aliye hai na wa kweli, nakuwafundisha watu wako kutumaini wokovu. Miongoni mwao umemvika nabii Eliya heshima ya urafiki wako, ili kwa kuwaka bidii kwa ajili ya utukufu wako, atangaze huruma yako kuu.
Yeye daima ametembea katika uwepo wako, na ulitaka awe shahidi wa kubadilika Sura na kutafakari uso mtukufu wa Mwanao mlimani Tabor.
Kwa hiyo sisi, tunajiunga na malaika na watakatifu wote, kutangaza kwa furaha utenzi wa sifa yako:
KOMUNYO taz 1Fal 19:8
Eliya akala na kunywa. Na kwa nguvu alizopata kutokana
na chakula hicho alitembea hadi mlima wa Mungu.
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, tumetiwa nguvu katika meza ya Mwanao, tujalie tukutafute tukidumu katika imani ili tufurahi kukuona huko mbinguni. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu. – Amina.