HISTORIA YA MAISHA YANGU KUHUSU FAMILIA, ELIMU NA KUJIUNGA NA SHIRIKA LA BIKIRA MARIA WA MLIMA KARMELI.
KUHUSU FAMILIA.
Jina langu naitwa Samweli Jackson nimezaliwa tarehe 11 Septemba mwaka 1996, ni mtoto wa tatu katika familia ya marehemu mzee Machandi Jackson ambaye alitutoka mwaka 2012. Ni huzuni sana kwa familia kuwa Baba alikuwa Mkatoliki alifariki kabla ya kufunga Ndoa na mama ambaye pia ni Mkatoliki. Mama yangu anaitwa Lucia Damas na katika Familia yetu tumezaliwa watoto watano kama nilivyosema hapo awali amabao wote ni wa kiume.
Familia yangu ipo wilaya ya Bunda mkoa wa Mara nyumbani yupo mama pia na mdogo wetu wa mwisho anayeitwa Damas Jackson, wengine tupo nje ya familia lakini bado tuko pamoja kupitia mawasiliano. Namshukuru Mungu kwa Rehema zake maana baada ya kifo cha baba, mama yetu aliendelea kutulea na kukua katika kimo na maaarifa mpaka muda huu tunajitambua wenyewe kwa kushirikiana na mjomba Boniphace Damas ambaye sasa ni marehemu.
KUHUSU ELIMU.
Nilimaliza Elimu ya Msingi mwaka 2010 katika shule ya Msingi KIHUZU iliyopo wilaya ya Butiama na baadaye kujiunga na Elimu ya Sekondari katika shule ya Sekondari KYANYARI iliyopo wilaya ya Butiama mwaka 2011 na kuhitimu mwaka 2014. Kwa neema zake Mungu nilifanikiwa kuendelea na masomo ya kidato cha Tano na cha Sita katika Shule ya Sekondari IHUNGO iliyopo Manispaa ya Bukoba mkoa wa Kagera mwaka 2015 na kuhitimu mwaka 2017 katika Taasusi ya PCB na namshukuru Mungu kwa kuniongoza kwa kipindi chote cha masomo yangu.
KUHUSU WITO.
Wito wangu ulianza nilipokuwa mdogo nikiwa katika Shirika la Utoto Mtakatifu parokia ya Bunda Jimbo Katoliki la Bunda. Siku moja Padre January Lyimo alikuja katika Shirika na kutuuliza kuwa wangapi wanapenda kuwa Mapadre, nilinyoosha mkono nikiwa peke yangu na akanishauri nisome kwa Bidii na pia nisali sana ili ndoto zangu zitimie. Tangia hapo nilihamasikika sana Rohoni na kupenda kuwa Padre. Baadaye nilijiunga na vijana watumikizi anbapo Paroko aliyekuwepo FR.CHRISTOGONE NJAU MLINA alitufundisha sana juu ya kutambua miito yetu mitakatifu na kutuhimiza kuwa lengo la kuwa karibu na mapadre mojawapo ni kujiunga na malezi ya Upadre kutokana na mafundisho yake nilipata mwanga wa kutimiza ndoto zangu.
Pia nilipokuwa katika shule ya Ihungo kulikuwepo na mapadre shuleni hivyo mara nyingi walitufundisha mambo mengi yaliyo tukomaza kiimani nakutushauri kuona wito wa upadre kama sadaka .Nilifurahi sana kuwepo pale muda wote kutokana na mafundisho tuliyokuwa tunapata hivyo ndoto zangu za wito wa upadre zilikuwa zinafunuliwa siku baada ya siku .
Mapema mwezi juni mwaka 2017 nilipo hitimu kidato cha sita namshukuru Mungu nilifaulu vizuri kutokana na matokeo hayo nilianza kuandika barua za maombi kwa Mashirika mbalimbali nikitafuta kujiunga na malezi ya upadre. Mashirika kama Mitume wa yesu (Apostles of jesus) na Shirika la Wabenedictini (Benedictians) wakati nilipo kuwa chuoni Dodoma.
Nilipokuwa na ngojea majibu ya barua nilizo tuma niliendelea na masomo ya Shahada ya Biologia katika chuo kikuu cha Dodoma mwaka 2017. Nikiwa na nia moja kuwa kama nitapata majibu mapema kati ya moja ya Shirika niliyo omba naacha na masomo chuoni na kwenda kujiunga na malezi katika shirika husika. Ilichukua muda sana kusubili mjibu bila mafanikio sikukata tamaa. Nilianza kuwashirikisha rafiki zangu na wakanisaidia kutafuta kupitia mtandao (google ) kwa Baraka za Mungu nikafanikiwa kupata Shirika la Bikira Maria wa mlima Karmeli (O.Carm) na kupata mawasiliano ya mkurugenzi wa miito nakumueleza kuhusu historia na nia yangu kwa Neema ya mungu akanipokea tayari kuingia nyumba ya malezi Morogoro .
Namshukuru Mungu kwa kipindi chote alipo kuwa akiniongoza kwa kunitia nguvu bila kukata tama na pia namuomba anisimamie vyema katika safari yangu hii. Nawashauri vijana wote wenye miito mitakatifu kuwa na Imani katika Sala na utulivu wa moyo Mungu yupo kazini wakati wote anajifunua wasikate tama.