NABII YEREMIA –NABII WA AGANO JIPYA
Maisha yake
1. Yeremia: Maana yake ni «yule aliyeinuliwa na Mungu –yule amwinuaye Mungu». Alizaliwa
mnamo mwaka 645 K.K. Katika familia ya makuhani ya jamaa wa Anathothi [Yer 1:1], walioishi katika nchi ya Benyamini, katika mji mdogo ulioko kaskazini mwa Yerusalemu ambao kwa sasa unaitwa Anatâ [Yer 1:1]. Anasema kuwa aliishi upweke baada ya aliambiwa na Bwana asioe [Yer 16:1-2] –maana yake nin nini? Ni mfano wa fumbo? (simbolic?). Kwa kipindi kifupi alifanya kazi yake ya kinabii mahali alipozaliwa na kwa kipindi kirefu cha maisha yake alikuwa Yerusalemu. Baada ya kuanguka kwa Yerusalemu 587, alikwenda kukaa Mizpa [Yer 40:6]. Nabii Yeremia alikwenda pia Misri ambako kulikuwa na koloni la Wayahudi [Yer 43:6-13].
2. Wito wake [Yer 1:4-19]
Mwaka 627, wakati wa utawala wa Yosia mfalme wa Yuda, Yeremia aliitwa na Bwana, katika umri wa ujana (utoto), kuwa nabii wa Yuda na wa mataifa [Yer 1:6]. Kazi ambayo aliifanya takribani kwa miaka 40 yaani toka mwaka 627 hadi mwaka 587.
3. Neno la Bwana linamjia Yeremia [Yer 1:4-5]
Yeremia anasema kuwa neno la Bwana lilimjia na kusema “ametakaswa kuwa nabii wa mataifa kabla hajatoka tumboni, Mungu alimfahamu kabla ya kuumbwa kwake tumboni. Yeremia anakili kuwa Bwana ananguvu sana, amemkalia Yeremia hivyo hawezi hata kupinga [Yer 20:7.9]. Pengine hii inatokana na habari ya mwanzo kuwa alipoitwa alianza kutoa visingizio.
4. Anajaribu kupinga [Yer 1:6]
«Ndipo niliposema “Aa, Bwana Mungu! Tazama, siwezi kusema, maana mimi ni mtoto”».
5. Anapokea maelekezo ya misheni yake [Yer 1:7-10]
Utakwenda kwa kila mtu, ...utasema kila neno,...usiogope...“niko nawe”...halafu Bwana anamgusa kinywa chake. Kazi yake kuu ni kung’oa, kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda [Yer 1:10].
6. Yeremia na mfalme Yosia
Yeremia alimsaidia Mfalme Yosia katika juhudi zake za mabadiliko ya kidini kwa kurejesha maadili ya kidini katika taifa, [Yer 11:1-14], [2Fal 23:1-25]. Yeremia alihubiri mabadiliko na kuwataka watawala na watu wao watubu. Alikuwa na tumaini kuwa Israeli na Yuda zingeungana na kuwa kitu kimoja jambo ambalo lingekuwa ishara ya kipindi cha Masiya.
7. Kifo cha Mfalme Yosia (640-609)-[2Nya 35:20-26]
Kifo cha Mfalme Yosia kiliondoa matumaini ya Yeremia [2Nya 35:25 ]. Manase (687-642) mfalme wa Yuda aliyekuwa kibaraka wa Ashura ndiye aliyechochea «ibada ya sanamu» na kuporomoka kwa maadili ya kiagano, kitu kinachofananishwa na ukahaba [Yer 2:20; 3:1-3]. Hali hiyo ilidumu mpaka kipindi cha mfalme Yosia. Walipogundua kitabu cha Sheria Hekaluni [1Fal 22:3-13] (622-621) mfalme Yosia alianza kufanya mabadiliko ya kidini toka Yuda mpaka Israeli. Jaribio la Yosia la kuwazuia Wamisri wasimshambulie mfalme wa Ashuru ndilo lililomgharimu maisha yake kwani aliuawa katika vita ya Megido [2Fal 23:29].
8. Mahubiri ya Yeremia mara baada ya kifo cha Mfalme Yosia
Wakati wa utawala wa Yehoyakimu (Eliakimu) (609-598) [2Fal 23:34], aliendelea kuwahubiria wakazi wa Yuda juu ya umuhimu wa kulisafisha Hekalu, kushikamana na dini ya kweli, kuabudu Mungu wa kweli, akiwaonya juu ya kosa la usaliti walilokuwa wakilifanya kuwa litaingamiza taifa. Yeremia aliwaonya juu ya jambo hilo [Yer 7:30-34], anatabiri kuwa watapelekwa uhamishoni [Yer 16:10-13]. Jambo lilitimia kweli, [Yer 52:12-13], [Yer 44:2-3]. Alisisitiza kwa nguvu zote Sheria, Torati. Alisema kuwa ili taifa liweze kudumu ilikuwa ni muhimu kuwa waaminifu kwa ahadi za Agano la Bwana [Yer 2-6]. Upendo wa Mungu kwa watu wake ni sawa na ule wa mme na mke. Wajibu wa Taifa Teule kwa Mungu ulikuwa ni kuheshimu makubaliano ya Agano. Agano ni ishara ya Upendo wa Mungu kwa watu wake. Alisema kuwa kama hawatabadilika, basi kutatokea uvamizi ambao ni adhabu ya Mungu. Alitangaza kuwa Yuda, Yerusalemu na Hekalu [Yer 11,1-7], vitateketezwa kama adhabu kwa kutolitii neno. Watu watapelekwa uhamishoni [Yer 36], [Yer 17,27], [Yer 37,8]. Alitaka taifa limrudie Mungu. Alihubiri kwa mifano [Yer 13,1-11]; [Yer 19,1-5].
9. Hali ya maisha ya Yuda –Yerusalemu na Hekalu vinaangamizwa
Mwishoni mwa karne ya saba na kwenye miongo kadhaa ya kwanza ya karne ya sita ni kipindi kilichoshuhudia mahangaiko mengi yaliyosababishwa na mfululizo wa majanga ya kisiasa ambayo yaliibadili kabisa hali ya maisha Asia ya Magharibi. Ni kipindi kilichoshuhudia tawala mpya za Babeli zikiuangusha ufalme wa Ashuru 614 na Ninive makao yake makuu mwaka 612. Neko II mfalme wa Misri ajaribu, kwa msaada wa jeshi kubwa, kushambulia ngome ya adui wake wa kale wa Frati. Palestina ilikuwa njia ya moja kwa moja ya mamlaka zilizokuwa na nguvu kubwa za enzi izo juu ya Frati na Nile, na Taifa la Wayahudi lililazimika kuchukua hatua dhidi ya jeshi la Misri lililokuwa likisonga mbele kupitia mipaka yake. Jaribio la Yosia mfalme wa Yuda la kupambana na jeshi la Wamisri lilimgharimu maisha yake katika vita ya Megido 609, maana aliuawa na Neko mfalme wa Misri [2Fal 23,29]. Yehoahazi mwana wa Yosia akawekwa kutawala katika Yuda [2Fal 23,30]. Lakini akaondolewa na Neko mfalme wa Misri na badala yake akamweka Yehoyakimu (Eliakimu) (609-598). Chini ya utawala wake Yuda iliendelea kufanya ibada ya sanamu na iliishi chini ya ushawishi wa Wamisri [2Fal 23,34]. Yeremia alikemea tabia hiyo na ile ya kutotilia maanani Agano. Lakini mfalme hakusikia. Yehoyakimu aliweka upingamizi kwa Babeli. Hatari ya vita ilikuwa wazi wazi. Miaka minne baadaye (605) Neko aliouawa na Nebukadreza mfalme wa Babeli katika Karkemishi juu ya Frati. Tangu wakati huo macho ya Nebukadreza yalikuwa daima juu ya Yerusalemu. Yehoyakimu alipokufa, mwanae Yekonia akawa mfalme wa Yuda [2Fal 24,6-8]. Yekonia Mfalme wa Yuda alichukuliwa mateka Babeli [2Fal 24, 10-16]. Baada ya Mfalme Yekonia kutekwa na kuchukuliwa mateka uhamishoni Babeli na Nebukadreza Mfalme wa Babeli, nafasi yake ilichukuliwa na Sedekia (597-587) ambaye alikuwa mfalme wa mwisho wa Yuda [2Fal 24, ]. Aliamua kujiunga na upande wa Misri. Lakini baadaye naye alichukuliwa mateka Babeli pamoja na watu wake. Alitekwa akatobolewa macho na kupelekwa uhamishoni Babeli hakuri tena Yuda. Mwaka 587 Yerusalemu ilivamiwa na watu wa Babeli na wakaiba vito vyake na wakawachukua watu mateka [2Fal 25, 1-12]. Nebukadreza alimteua Gedalia kuwa Gavana wa Yuda lakini akauwa baada ya miezi kadhaa. Watu wengi jimbo la Yuda wakakimbilia Misri kwa hofu ya Nebukadreza [2Fal 25,25-26].
10. Yeremia anasimama kinyume na watawala –manabii wa uongo
Yerusalemu ilipozingirwa na majeshi ya Babeli Yeremia aliwashauri wakubali kuwa chini ya Nebukadreza ili kuepusha hatari ya kuaharibu mji na Hekalu, lakini hawakumsikiliza [Yer 27,1-22]. Alisema kuwa Yuda inapigwa kwa sababu imemwacha Bwana na Sheria yake [Yer 8,8], [Yer 11]. Alikuwa kinyume cha wote, wafalme, makuhani na manabii kwa sababu waliifanya Torati idharauliwe. Aliwaonya dhidi ya manabii wa uongo [Yer 14,13-16]. Manabii hao wa uongo walikuwa wakisema kuwa hayo hayatatokea [Yer 23,16-18].
11. Yeremia anapata mateso [Yer 11,18-12,1-13].
Yeremia alikabiliana na vipingamizi na mateso. Alichukiwa sana na viongozi na manabii [Yer 26,8-9] na hata na jamaa zake [Yer 11,21]. Viongozi wengi hawakupenda msimamo na maaguzi yake walimuona kama msaliti. Aliwahi kupigwa na kuhani Pashuri na kutupwa gerezani [Yer 20,1-2], [Yer 33,1]. Walimpiga na kumfunga [Yer 37,11-17]. Walijaribu mara kadhaa kumuua kwa kumtupa shimoni [Yer 38,6]. Alikuja kuokolewa na Ebedmeleki Mwithiopia? aliyekuwa towashi mtumishi wa mfalme wa Babeli [Yer 38,12]. Vitendo hivyo vilimkwaza sana katika misheni yake, akapata mgogoro wa ndani wa mambo ya imani yake, wa misheni yake na juu ya uhusiano wake na Mungu. Mambo haya anayaeleza katika mashairi yake yaitwayo «Ushahidi» [Yer 11,18].
12. Mataabiko na malalamiko ya Yeremia au maungamo yake [Yer 15,10-21], [Yer 17,14-18],
[Yer 20,7-20] -Yeremia alilalamika kutokana na mateso yaliyompata kipindi cha unabii wake [Yer 15,10-21]. Analalamika katika hali ya kibinadamu kabisa [Yer 15,18]. Anamlalamikia Mungu kuwa hakumsaidia kama alivyokuwa amemwahidi [Yer 1,8.17.19].
13. Alitabiri Agano Jipya na kuja kwa Masiya [Yer 31,31-34] –ufalme mpya wa Mungu utakuja
Ni Mungu tu anayeweza kuwabadilisha wanadamu, kwa nguvu zao wenyewe hawawezi. Alitabiri kuja kwa Masiya wa Bwana ambaye atatoka katika shina la Daudi [Yer 23,5-6]. Alisema kuwa waliouhamishoni watarejea tena katika nchi yao [Yer 29,10-11].
14. Kifo chake
Wasomi wengi wamejenga utamaduni unaosema kuwa nabii Yeremia aliuawa huko Misri.