“Kwa Kuwa Mwenyezi Mungu Amenitendea Mambo Makuu, Jina Lake Ni Takatifu…”
Jioni tulivu ya tarehe 13 Februari 2026, shamrashamra za tukio la kihistoria la kuprofesi nadhiri za daima kwa ndugu wawili wakarmeli, Frt. Felix Damasi Malimi na Frt. Gabriel John Mtiti zilianza ambapo wanashirika wakarmeli pamoja na waamini wa Parokia Ya Bikira Maria Wa Mlima Karmeli-Bunju, walikusanyika katika kanisa la muda la parokia kwa ajili ya masifu ya taadhima ya kuwaombea wanadhiri wadaima wateule. Sala hii ya masifu ya jioni ilianza majira ya saa 11: 30 jioni, na iliongozwa na Padre Dominic Maria somola O.Carm akisindikiwa na Padre mlezi wa walelewa wakarmeli walio katika nyumba ya malezi Morogoro, Padre Victor Biramata O.Carm na Padre mkuu wa nyumba ya Bunju, Padre Paul Kaigalula, O. Carm.
Tukio hili liliambatana na picha za pamoja katika grotto-bustani ya mtoto yesu wa plague baada ya masifu hayo. Furaha ya siku iliyofuata ilianza kuonekana katika ukuu wake. Kisha kilifuata chakula cha jioni cha pamoja na ndugu wa Familia za wanadhiri.
Katika siku ya kimataifa ya wapendanao tarehe 14 Februari 2026, Mungu aliendelea kudhihirisha upendo wake mkuu kwa Kanisa na Shirika la Wakarmeli (O. Carm) nchini Tanzania, kwani wana wawili wa Maria walijiweka wakfu kabisa kwake kwa nadhiri za maisha. Ndugu Felix Maria Damas Malimi na Gabriel Maria walimwekea Mungu nadhiri zao za daima katika Parokia ya Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Bunju, na kuwa wanashirika rasmi ndani ya shirika hilo la kitawa.
Tukio hili kubwa la kiroho katika Maisha ya wanadhiri hao na kanisa, liliwakutanisha ndugu Wakarmeli kutoka pande kadhaa za Afrika, kwani Mwakilishi wa Mkuu wa Shirika la Wakarmeli kutoka Kenya, Padri Patrick msiimi O. Carm. alifika akiandamana na Mlezi wa Mapostulanti, Padri Emmanuel Shikoli O.Carm, lakini Udugu huo ulionekana bayana kwa uwepo wa ndugu wawili walio kuwa pamoja na wanadhiri hao katika kipindi cha Unovisi huko nchini Zimbabwe, ndugu hao ni Br. Caleb Maingi O. Carm na Br. Thomas Mwanzia O. Carm.
Uwakilishi kutoka Zimbabwe uliwahusisha Padri Shelton Zimondi O. Carm, ambaye ni Komisari Provinsio wa shirika nchini humo, akiandamana na Mlezi wa Wanovisi, Padri Wiseman Msemwa O. Carm. na hivyo basi wote kwa pamoja Uwepo wao ulikuwa kama daraja linalounganisha juhudi za kiroho za matawi mbalimbali ya shirika barani Afrika.
KILELE CHA SHEREHE: MISA TAKATIFU
Misa takatifu iliyokuwa ndiyo hasa kilele cha maadhimisho na sherehe hizo iliongozwa na Mwakilishi wa Padri Mkuu wa Shirika wa Komisari ya La Bruna, Padri Dominic Maria Somola O. Carm, ambaye ndiye aliyepokea nadhiri hizo za daima za kitawa za wanadhiri hao. Altareni, walihudumu Mafrateri wa shirika la Ndugu wa Mama Bikira Maria wa Mlima Karmeli, huku Mashemasi kutoka Shirika la Mt. Augustino (Order of St. Augustine) wakitoa huduma zao za kiliturujia, na kuleta mvuto maalum wa katika sherehe hizo.
Licha ya ndugu wa shirika, misa hiyo takatifu ilihudhuriwa na makuhani mbalimbali wa Jimbo katoliki la Bagamoyo na Bunda na mashirika mengine ya kitawa, wakiongozwa na Padre Saabath OSA, ambaye ni Makamu mkuu wa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo.
Kwa Upande wa masista-watawa wa kike walifika na kujumuika nao kwa wingi, wakiongozwa na Masista Wakarmeli Wamisionari wa Mtakatifu Theresia wa Mtoto Yesu, ambao walifika kwa wingi Zaidi kushuhudia “makuu ya Mungu,” kwa wanadhiri hao walioweka maisha yao kabisa mikononi mwa Bwana.
FURAHA, SHUKRANI NA MASHEHERESHO
Baada ya ibada ya Misa takatifu, washiriki wote walijiunga katika hafla fupi ya kuwapongeza wanadhiri hao wapya katika viwanja maalum vya parokia. Mafrateri wakarmeli kutoka nyumba ya malezi, Morogoro walionyesha furaha yao kwa kaka zao waliopiga hatua katika malezi kwa kuwatungia wimbo maalum wa kumshukuru Mungu pamoja nao kwa neema alizowajalia. Nyuso za wanadhiri hao ziling’aa kwa furaha na tabasamu zuri, wakipokea salamu za pongezi, zawadi na maombi mazuri kutoka kwa waamini, ndugu, jamaa na marafiki.
Nafsi za wazazi na ndugu zao zilijaa furaha isiyo na kifani walipopata nafasi ya kusimama mbele ya mkutano kucheza na kutoa shukrani zao kwa Mungu na kwa wote waliojumuika katika kulea na kukuza vipawa vya watoto wao.
HITIMISHO: BARAKA ZINAENDELEA KUMIMINIKA
Kwa nadhiri hizi za daima, jumla ya idadi ya wanadhiri wa daima ndani ya kanda ya Tanzania katika shirika la Wakarmeli imeongezeka na kufikia tisa. wakati idadi ya wanadhiri wa muda itakuwa watano na mapostulanti saba.
Kwa hakika, Bikira Maria wa Mlima Karmeli, Mama na Mlinzi wa shirika hili, anaendelea kulifunika kwa upendo wake. Na hii ni ishara wazi kuwa: Kila nadhiri inayotamkwa ni ishara ya wingu jingine la baraka linalomiminika kwa Kanisa na kwa shirika hili, likiwapa matumaini na hakika ya kuwa Mungu haachi kamwe kuitwa wafanyakazi kwenye shamba lake la mizabibu.
BIKIRA MARIA WA MLIMA KARMELI…. UTUOMBEE!!
Imetayarishwa na:
Timu ya Waandishi: Frt. Faustine Maria na Frt. Ansbert Maria
kwa niaba ya Shirika la Wakarmeli Tanzania
Tarehe: 22, Februari, 2026