Eliya katika Shirika Nabii Eliya anatajwa katika kitabu cha kwanza na cha pili cha Wafalme (1Fal 17:1). Aliishi kwenye karne ya 9 K.K wakati wa utawala wa mfalme Ahabu. Aliteswa na mfalme Ahabu (1Fal 17:2-7). Alilishwa kwa miujiza na kunguru (1Fal 17:2-7). Alitetea kuabudu Mungu wa kweli. Alikaa siku arobaini bila kula (1Fal 19:8). .Hali ya maisha waliyoishi Wakarmeli wa kwanza ilikuwa ni ya kieliya kiasi kwamba walijisikia kuwa katika hali ya kuwasiliana naye moja kwa moja. Wamerithi kutoka kwa Eliya shauku ya Bwana na hamu ya kuliweka Neno katika mioyo yao, ili kutoa ushahuda wa uwepo wake duniani, kukubali kuwa yeye ni kweli Mungu wa maisha ya duniani. Hawakuwa Wakarmeli tu waliokuwa wakivutwa na nabii Eliya bali hata mahujaji wengine wengi wa kipindi kile ambao walikuwa wakiitembelea Nchi Takatifu, walikuwa wakiguswa na maisha yake. Wengi wao waliokuwa wakienda kuhiji Nchi Takatifu walikuwa wakienda kuhiji pia katika mlima Karmeli sehemu ambayo Eliya aliishi maisha ya kimonaki. Wakarmeli waliishi mlima Karmeli karibu na chemchemi ya Eliya wakitamani kuwa kama yeye. Walimchagua Eliya “mtu wa jangwa” kuwa kama baba yao na kiongozi wao wa kiroho.
Eliya alikuwa ni mtu wa sala na aliishi katika uwepo wa Mungu akimtumikia kwa uaminifu mkubwa. Hata pale wana wa Israeli walipokengeuka, yeye alisimama imara akiitetea imani halisi ya Israeli, imani kwa Mungu mmoja. Kwa maisha yake Eliya anamfundisha kila mmoja wetu jinsi ya kuishi kwa vitendo upendo na imani kwa Mungu. Alipochagua kuishi maisha ya kipweke, ni wazi alikuwa akimfundisha kila mtu njia sahihi ya kuzitawala tamaa za kimwili kwa ajili ya kuwa na moyo safi. Eliya aliishi maisha ya kifukara, maisha ya kijangwa, maisha ya kipweke kwa utakatifu za wazi ulioonekana kwa watu wote (Soma YsB 48:1-11). Kutokana na maisha yake ya kimonaki, anaheshimiwa sana na mababa wengi wa kimonaki ambao wanamwona kuwa yeye ndiye “mwanzilishi” wa maisha hayo. Kwa upande wetu Wakarmeli tunamheshimu kama baba yetu wa kiroho na anatajwa katika vitabu vya kiliturujia vya Shirika.