Utawa wa Tatu katika Karmeli
Utawa wa Tatu katika Karmeli, una historia inayotofautina kidogo na Utawa wa Tatu wa Mashirika mengine ya kitawa, kama vile Wafransiskani ambao tangu mwanzo waliandaliwa Kanuni na Mt. Fransisko wa Assis[1]. Kwa Wakarmeli haikuwa hivyo. Utawa wa Tatu umeingia Karmeli taratibu na hatua kwa hatua kutokana na mabadiliko yaliyokuwa yakitokea ndani ya Shirika.
Wakonverse na Wakonversi (Waliotubu)
Wakati Wakarmeli waliporudi Ulaya kutoka Mlima Karmeli, Palestina, walianza kuishi maisha ombaomba lakini wakati huo huo waliendelea kuwa na tabia ya maisha ya kimonaki kama walivyoishi Mlima Karmeli. Hii iliwezesha baadhi ya watu wanaume kwa wanawake kuendelea kuingia na kuwa sehemu ya Wanafamilia wa Shirika kwa mtindo wa “oblatio”. Baadhi yao walikuwa wakiweka nadhiri kama za kitawa na wengine walikuwa hawaweki nadhiri. Hawa wote kwa pamoja walijulikana kama Wakonverse”[2] au Wakonversi. Walikuwa wakitafuta manufaa ya kiroho na walipenda kuishi maisha kama ya watawa.
Wakonverse mabikira na wajane
Kundi mojawapo la Wakonverse[4] lilikuwa kundi la wanadada mabikira na wajane. Baadhi yao waliishi pamoja kama jumuiya kwenye nyumba zilizokuwa zimejitenga kidogo na konventi za kiume na wengine walikuwa wakiishi nyumbani kwao. Hawa walikuwa wakiahidi utii kwa mkuu wa nyumba na walikuwa wakiishi ufukara na useja kwa kiwango cha juu sana. Nadhiri zao zilikuwa za milele. Walikuwa wakisali pamoja na watawa wa kiume, yaani, mafrateri. Walioolewa hawakuruhusiwa kujiunga nao. Wale waliokuwa wanaweka nadhiri za milele wasingeweza kuolewa.
Wanandugu wa joho jeupe
Mbali ya kundi la Wakonverse na Wakonversi, yalikuwepo pia makundi mengine ya Wakonversi Walei wanaume kwa wanawake, ambao baadhi yao walikuwa wameolewa au kuoa na wengine walikuwa hawakuoa au kuolewa. Wao walikuwa wakitafuta kufaidika na maisha ya kiroho ya Wakarmeli. Kama vile kuombewa wakati wa shida na kuombea marehemu wao au wao wenyewe walipokuwa wakifariki dunia.Kwa kawaida walikuwa hawaweki nadhiri. Hata kama ilitokea wakaweka nadhiri, basi, nadhiri zao hazikuwa za milele, hivyo hawakutambulikana kama watawa. Walikuwa wakijulikana kama «wanandugu kaka na dada» wa joho jeupe. Walikubali kuishi undugu wa Shirika, wakijibidisha kuishi maisha ya kiroho ya Shirika kama inavyoelekeza Kanuni ya Shirika. Walikuwa wakivaa joho jeupe kama alama yao ya kuwatofautisha na wengine. Mbali ya kuwasaidia mapadri hata wao walikuwa wakisaidiana kwa kila hali. Walikuwa wakiwatembelea wagonjwa na kuwasaidia maskini.
Hati «Cum nulla» ya Nicolò V ya mwaka 1452
Utawa wa Pili
Kwenye Hati hii, Papa alitambua uwepo wa kundi la Wakonverse waliokuwa na nadhiri za daima. Hawa ndio wale waliokuwa wanaishi pamoja kama jumuiya. Akawaagiza wawe wanaishi kwenye jumuiya na kusali Sala ya Kanisa pamoja. Jumuiya zao zikapewa uhuru na mamlaka kamili ya kujiendesha. Wengi wao waliokuwa na nadhiri za daima wakawa wamonaki wa kike ambao ndio Utawa wa Pili.
Utawa wa Tatu
Wengine wote waliobaki ambao hawakuyakubali maisha ya faragha, ndio wale waliounda Utawa wa Tatu. Watu hawa walikuwa mchanganiko. Walikuwepo baadhi yao walioendelea kuweka nadhiri ambazo hata hivyo zilibaki za muda na wengine walikuwa hawaweki kabisa nadhiri.
Utawa wa Tatu wa wenye nadhiri za muda
Hati ya Cum nulla ilitambua uwepo wa wale waliokuwa wakiweka nadhiri za muda ambao walikuwa hawaishi maisha ya kijumuiya. Inaonekana hapa Papa aliongelea tu wale ambao hawakuwa na ndoa, yaani, wale wasioolewa. Maana Hati yake haikuongelea chochote juu ya wale waliokuwa wameolewa. Papa Sisto IV ndiye aliyewaruhusu hata wanawake walioolewa kujiunga na kundi hili mwaka 1476.
Utawa wa Tatu wa kilimwengu
Hawa ndio wale waliokataa kuishi maisha ya faragha, wala maisha ya kijumuiya ijapokuwa walikuwa na nadhiri za daima. Walikuwa wakijiita “Wa -Tatu” (Tertiary). Hata hivyo haikuwa sahihi kujiita Wa-Tatu (Utawa wa Tatu), kwa sababu walikuwa na nadhiri za daima. Kitendo chao cha kukataa kuishi maisha ya faragha kilisababisha nadhiri zao za milele kukataliwa na Kongresheni za Roma mwaka 1583. Papa Pio V na Papa Sisto V walisisitiza kwa nyakati tofauti kuwa wale waliokuwa na nadhiri za daima lakini wanakataa kuishi maisha ya faragha walikuwa si watawa tena. Baada ya Mapapa hao kueleza msimamo wao juu ya maisha ya kitawa, ilibidi kutafuta suluhisho la wale waliokuwa wameweka nadhiri na waliokuwa wakitaka kuweka nadhiri lakini wakawa hawataki kuishi maisha ya faragha, yaani, maisha ya klausura. Yakatolewa mapendekezo mawili. Pendekezo la kwanza lilikuwa la kuendelea kuishi na nadhiri zao lakini zisizo za daima na lingine likawa la kuachana na nadhiri ya ufukara na kuifanya nadhiri ya usafi wa moyo kuwa chaguo la mtu binafsi. Mtu angeweza kuchagua kuishi maisha ya usafi wa moyo, yaani, kuishi bila kuoa au kuolewa au kuoa au kuolewa hata mara baada ya kuweka nadhiri. Wengi wao walipenda pendekezo la kwanza. Matokeo yake kukaweko makundi mawili tena. Kundi la wasioolewa na kundi la walioolewa. Baadaye mwaka 1587 iliondolewa nadhiri ya ufukara kwa waliokuwa wanaweka nadhiri, hivyo wakawa wanaweka nadhiri mbili tu kulingana na hali zao. Nadhiri ya Utii na nadhiri ya Usafi wa moyo[5].
Wanandugu wa Skapulari
Kundi la tatu lilikuwa la “ndugu wa Madonna wa Karmeli” lilikuwa likitambulikana kwa kuvaa Skapulari. Watu wengi walijiunga na kundi hili ili kwa lengo la kufaidika na “Upendeleo wa Jumamosi”[6]. Ilifikia hatua ikawa ni vigumu kutofautisha wanandugu wa joho jeupe na wanandugu wa Skapulari. Makundi haya mawili yalikuwa yakihitirafiana mara kwa mara. Mwaka 1606, Papa Paulo V alitambua ulinganifu wa maisha na majukumu ya makundi haya mawili.
Juhudi za kuyaweka makundi mawili pamoja
Ili kumaliza msuguano uliokuwepo kati yao, mwaka 1637, Mkuu wa Shirika, Teodoro Straccio aliwaweka pamoja katika Utawa wa Tatu wale wote waliokuwa na nadhiri za muda za Utii na Usafi wa moyo kulingana na hali zao[7]. Wengine wote waliosalio aliwaweka katika kundi la wanandugu wa Skapulari mwaka 1640. Mwaka 1924 waliwaondolea nadhiri ya Utii na Useja wa Utawa wa Tatu kulingana na hali zao[8]. Lakini nadhiri hizo zikarudishwa mwaka 1948. Lakini wakazifanya kuwa chaguo la mtu. Hata Kanuni yao ya mwaka 1977 ilitoa uhuru wa kuweka nadhiri. Sasa walikuwa wanaweza kujiendesha wao wenyewe.
Mashirika ya Masista na Taasisi za kilimwengu
Mashirika ya Masista
Mashirika ya Masista yalitokana na makundi ya Utawa wa Tatu wa wale waliokataa kuishi maisha ya faragha (klausura). Hawa ndio wale waliokuwa wakiweka nadhiri za muda. Wengi wao walikuwa wanaishi kijumuiya. Lakini wasingeweza kujiita watawa kulingana na Sheria za Kanisa ambazo ziliwataka watawa wa kike wote kuishi maisha ya faragha wakiwa na nadhiri za daima.
Maisha yao yalikuwa ni ya kitume zaidi. Waliishi na watu wa kawaida wakiwasaidia wahitaji. Walikuwa wakiwahudumia wagonjwa, maskini, wazee na kuwafundisha watoto wadogo. Kidogo kidogo Vatikani ikaanza kuwachukulia kama watawa. ikawapatia miongozo na taratibu zilizotakiwa kufuatwa ili kutambuliwa rasmi. Mojawapo ya taratibu hizo ilikuwa ni kundi husika kujumuishwa kwenye Utawa wa Kwanza. Wengi wao iliwabidi wawe wanavaa mawazi yaliyokuwa na rangi na yaliyofanana na mavazi ya Shirika husika.