MUSA –MTUMISHI WA MUNGU
1. Maisha ya Musa: -Maana ya jina lake ni “mtolewa – okolewa kutoka majini [Kut2:10]”.
Historia fupi kabla ya kuzaliwa Musa: Yakobo –Israeli anaingia Misri pamoja na wanawe na familia zao [Mwa 46:1-28]. Walipokewa na Yusufu pale Gosheni ambapo waliishi. Walizaana sana na kuongezeka [Mwa 47:28]. Kuongezeka kwao kulionekana kama tishio kwa mfalme wa Misri [Kut 1:8-10].
2. Kifo cha Yusufu-hofu ya mfalme mpya [Kut 1:8-10] –utumwa wa wana wa Israeli
Baada ya kifo cha Yusufu na Farao Waisraeli walianza kuteswa na kufanyishwa kazi ngumu [Kut 1:11-14] kama ilivyotabiliwa [Mwa 15:13]. Lakini walizidi kuongezeka na wakaijaza nchi [Kut 1:7]. Maisha yao yalikuwa ya uchungu sana na magumu [Kut 1:13-14]. Pamoja na kufanyishwa kazi ngumu na uchungu wa maisha walizidi kuongezeka sana [Kut 1:12].
3. Mpango wa kuwaua watoto wa kiume wa kiebrania
Baada ya kuona hayo mfalme aliamuru watoto wote wa kiebrania wanaume wanapozaliwa wauawe [Kut 1:15-16] kwa kutupwa mtoni [Kut 1:22].
4. Kuzaliwa kwa Musa [Kut 2: 1-4] -Baba yake ni Amramu na mama yake ni
Yokebedi [Kut 6:20] -anaokotwa kwenye kingo za mto Naili
Musa alipozaliwa alifichwa kwa miezi mitatu [Kut 2:1-2], alipoona hawezi kumficha zaidi alimweka kwenye kikapu akamweka kwenye kingo za mto [Kut 2:3]. Binti Farao –alimchukua (alimwokota) Musa akamfanya kuwa mwanae [Kut 2:5-10]. Musa alilelewa na kufundishwa katika hekima yote ya kimisri [Mdo 7:22], akiwa katika nyumba ya kifalme. Wanasema kuwa alikuwa mtu hodari.
5. Musa anakimbilia Midiani [Kut 2:11-22; Mdo 7:24-29] -njia za kibinadamu za
kutetea haki: Musa anamuua Mmisri aliyekuwa akimpiga muebrania [Kut 2:12]. Musa anawaamua waebrania waliokuwa wakipigana, mmoja anafichua siri ya kumuua Mmisri. Farao anapata habari, anataka kumuua Musa, Musa anakimbilia Midiani [Kut 2:13-15]. Huko alikuwa akichunga mifugo ya Yethro ambaye alikuwa kuhani wa Midiani [Kut 3:1]. Alimuoa binti yake aitwaye Sipora [Kut 2:21].
6. Musa anaitwa na Mungu [Kut 3:1-6] -baada ya miaka 40 ya kuchunga mifugo.
Musa: akiwa Madiani alikuwa akichunga mifugo ya mkwe wake akaona kijiti kikiwaka moto lakini kilikuwa hakiteketei [Kut 3:1-2] -Ni Malaika aliyemtokea katika mwali wa moto [Kut 3,2].
Sehemu alipomtokea: katika mlima wa Mungu -Horebu [Kut 3:1]. Hali hii inamvutia sana Musa na anaamua kusogea kutazama. Katika wito wowote ule kuna kitu cha nje ambacho kwanza huwa kinamvutia mtu, kabla ya kuingia ndani zaidi.
7. Mungu Mtendaji Mkuu: –Mungu alipoona,.. akamwita,... -Musa akaitika,... Mungu
akasema....[Vua viatu vyako miguuni mwako...(Kut 3:4-5)]. Alitakiwa kuachana na kuwaza na kutenda kibinadamu, bali ilibidi amtegemee Mungu kwa kila kitu. Mungu anapokuita unaacha nyuma kila kitu, unaanza kutenda kile anachotaka yeye.
8. Mungu anajifunua kwa Musa [Kut 3:6] -Ni Mungu wa Ibrahimu, Isaka, Yakobo.
Musa: anaficha uso –hali ya ubinadamu dhaifu mbele ya Ukuu wa Mungu.
9. Kwa nini Mungu anamwita Musa? Anataka kumpa kazi ya kufanya-Misheni
Ameyaona mateso yao...amesikia kilio chao,....amejua maumivu yao,...ameshuka kwa ajili ya kuwaokoa. Ndiyo sababu anamtuma Musa (Kut 3:10)- [Kut 3:7-10].
10. Mungu analifunua jina lake [Kut 3:13-14]
Huwezi kumtumikia Mungu usiyemjua. Ili kumfahamu inabidi kujibidisha kulisoma na kulitafakari Neno lake, kulifanya liwe sehemu muhimu sana ya maisha yako.
11. Musa: anapewa kazi ya kuwakomboa kutoka utumwani [Kut 3:16-22]. Lakini
kiuhalisia ni Mungu mwenyewe anayewakomboa wana wa Israeli [Kut 19:3-4].
12. Musa anaogopa kazi hiyo na kutoa visingizio: -..anasema hawatasadiki,
hawataamini.....[Kut 4:1]...anasema kuwa yeye hana uwezo wa kusema, hana kipaji cha kuongea mbele ya watu [Kut 4:10]. Mungu anamwambia kuwa atatenda kazi naye [Kut 4:12]. Ni Mungu atakaye kuwa akitenda kazi kupitia mtumishi wake Musa. Ni Mungu anayemtuma na si vinginevyo “Basi sasa nenda” [Kut 4:12].
13. Huwezi kufanya kazi ya Mungu bila kutumwa [Rum 10:14-15]
MISHENI YA MUSA –alikuwa na miaka 80 [Kut 7:7] -miaka 40 ya jangwa.
14. Musa anasita: kufanya kazi hiyo [Kut 4:13]. Hatimaye anakubali na anarudi tena
Misri [Kut 4:18-20]. Inabidi awaongoze wana wa Israeli kutoka Misri mpaka kwenye nchi ya ahadi [Kut 6:6-8]. Inabidi wamtolee Mungu dhabihu, wamfanyia sikukuu [Kut 5:1].
15. Musa na Taifa la Israeli –[Matatizo aliyokumbana nayo, wanamlalamikia Musa].
Waliona njaa kiu [Kut 17:3-6; 16:3], na kumuasi Mungu kwa kutengeneza ndama wa dhahabu kama mungu wao [Kut 32:1-6]. Kazi ya kulitumikia taifa la Mungu, si kazi rahisi. Inahitaji uvumilivu mkubwa kama aliokuwa nao Musa.
16. Wito wa Musa katika maisha ya Kikristo –maisha ya utumishi
Musa anafahamika kuwa alikuwa mtu wa Mungu, mtumishi wake, aliyefanya kazi kwa unyenyekevu mkubwa, aliyekuwa na uvumilivu wa hali ya juu, na alikuwa na msimamo wa dhati. Aliongea uso kwa uso na Mungu [Kumb 34:10-12]. Jina la Musa linatajwa mara kwa mara katika Zaburi na katika vitabu vya manabii kama mkuu wa manabii. Maisha yetu inabidi yawe ya utumishi uliotukuka kama wa Musa. Kumtegemea Mungu kwa kila hatua. Tusikatishwe tamaa na udhaifu wetu, Mungu mwenyewe atatutegemeza ikiwa tutamwamini kwa imani kubwa.
17. Musa –alibidi ajifunze jinsi ya kumtegemea Mungu katika kazi zake-akiwa kama
Mtumishi na rafiki ya Mungu. Alikufa akiwa na miaka 120 [Kumb 34:7].
18. Musa katika Agano Jipya –kiongozi, mtoa sheria na mshenga
Musa: anatajwa mara kwa mara katika Agano Jipya- [Mt 17:3; Mk 9:4] Katika tukio hilo Yesu anageuka Sura mbele ya Petro, Yakobo na Yohane. Musa anasimama badala ya Sheria (Torati). Anapata fadhili ya kuuona utukufu wa Mwana wa Adamu. Musa amepokea Sheria na kuisimamia katika Agano la kale. Kristo ameleta neema. Musa alikuwa ni mshenga (mediator) kati ya Mungu na Taifa Teule.
19. Kristolojia – tipolojia -[Ushenga]-baadhi ya maeneo anayotajwa
Musa anatajwa katika Waraka kwa Waebrania akipambanishwa na Kristo [Ebr 3:1-6]. Anatajwa vile vile katika Injili ya Yohane, ambapo Kristo anaonekana kuwa utumilifu wa Maandiko yote [Yoh 1:17]; [Mt 19:8-9].
Kazi kubwa iliyofanywa na Musa inakamilishwa kwa kiwango cha juu sana na Yesu Kristo Mwana wa Mungu Aliye Hai.