Uhusiano wa Wakarmeli na Maria una uzito wa kipekee na ni wa ndani zaidi ukilinganisha na uhusiano tulionao kati yetu na Eliya. Tangia mwanzo kabisa mwa ukarmeli kama inavyoelezwa katika «Propositum» nia ya Wakarmeli ya kumtii au kujitoa wazima kwa Kristo ambaye ndiye Mtawala na «Bwana waeneo», yaani Nchi Takatifu, iliwasababisha wawe na uhusiano wa moja kwa moja na Maria Mama wa Yesu Kristo. Waliamini kuwa kwa kuwa Yesu alikuwa «Bwana wa eneo» basi hata mama yake alikuwa «Mama wa eneo». Maelezo hayo ya kiuhusiano na ya kiutawala, yaani: «Bwana wa eneo» na «Mama wa eneo» yalitokana na fikra za kiutawala za nyakati zile ambazo zilikuwa zikiukweza mfumo wa maisha ya nyarubanja –ukabaila. Eneo lilolengwa ilikuwa ni Nchi Takatifu. Wakarmeli waliamini kuwa, kazi kubwa ya Mama Bikira Maria “Mama wa eneo” ilikuwa ni kuwahudumia na kuwasaidia watumishi wa mwanae katika mahitaji yao. Suala hilo liliwafanya wamtambue Maria kama mlezi (Patroness) wa Shirika.