MASOMO YA USIKU WA MWAKA MPYA
SOMO LA KITABU CHA KWANZA CHA MAMBO YA NYAKATI 1Nya 29:10-20C
Kwa hiyo Daudi akamhimidi Bwana, mbele ya mkutano wote; naye Daudi akasema, Uhimidiwe, Ee Bwana, Mungu wa Israeli baba yetu, milele na milele. Ee Bwana, ukuu ni wako, na uweza, na utukufu, na kushinda, na enzi; maana vitu vyote vilivyo mbinguni na duniani ni vyako; ufalme ni wako, Ee Bwana, nawe umetukuzwa, u mkuu juu ya vitu vyote. Utajiri na heshima hutoka kwako wewe, nawe watawala juu ya vyote; na mkononi mwako mna uweza na nguvu; tena mkononi mwako mna kuwatukuza na kuwawezesha wote. Basi sasa, Mungu wetu, twakushukuru na kulisifu jina lako tukufu. Lakini mimi ni nani, na watu wangu ni nani, hata tuweze kutoa kwa hiari hivi? Kwani vitu vyote vyatoka kwako na katika vitu vyako mwenyewe tumekutolea. Kwani sisi tu wageni mbele zako, na wasafiri, kama walivyokuwa baba zetu wote; ni kama kivuli siku zetu duniani, wala taraji ya kukaa hapana. Ee Bwana, Mungu wetu, akiba hii yote tuliyoiweka, ili tukujengee nyumba kwa ajili ya jina lako takatifu, yatoka yote mkononi mwako, na yote ni yako wewe. Nami najua, Mungu wangu, ya kuwa wewe wajaribu moyo, nawe wapendezwa na unyofu. Nami katika unyofu wa moyo wangu nimeyatoa haya yote kwa hiari yangu mwenyewe; nami sasa nimeona kwa furaha watu wako, waliopo hapa, wakikutolea kwa hiari yao. Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, baba zetu, ulilinde jambo hili milele katika fikira za mawazo ya mioyo ya watu wako, ukaiongoze mioyo yao kwako; naye Sulemani mwanangu, umpe moyo mkamilifu, ili azishike amri zako, na shuhuda zako, na maagizo yako, akayatende hayo yote na kuijenga nyumba hii ya enzi, niliyoiwekea akiba. Ndipo Daudi akawaambia kusanyiko lote, Haya, mhimidini Bwana, Mungu wenu. Basi kusanyiko lote wakamhimidi Bwana, Mungu wa baba zao, wakainama vichwa vyao, wakamsujudia Bwana.
NENO LA BWANA
SOMO LA WARAKA WA MTUME PAULO KWA WAEFESO Efe 3:14-21
Kwa hiyo nampigia Baba magoti, ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa,
awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani. Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo;
ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina; na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu. Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu; naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.
NENO LA BWANA
SOMO LA INJILI TAKATIFU ILIVYOANDIKWA NA LUKA Lk 17:11-19
Wakati ule ikawa walipokuwa njiani kwenda Yerusalemu, alikuwa akipita katikati ya Samaria na Galilaya.
Na alipoingia katika kijiji kimoja, alikutana na watu kumi wenye ukoma; wakasimama mbali,
wakapaza sauti wakisema, Ee Yesu, Bwana mkubwa, uturehemu!
Alipowaona aliwaambia, Enendeni, mkajionyeshe kwa makuhani. Ikawa walipokuwa wakienda walitakasika. Na mmoja wao alipoona kwamba amepona, alirudi, huku akimtukuza Mungu kwa sauti kuu; akaanguka kifudifudi miguuni pake, akamshukuru; naye alikuwa Msamaria.
Yesu akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi?
Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa Mungu utukufu ila mgeni huyu?
Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa.
NENO LA BWANA