Mathayo 25:28-30
Neno la Bwana linaeleza vizuri mfano wa huu. Yule bwana anaamuru talanta ichukuliwe apewe yule aliyakuwa na talanta kumi. Aliye nacho ataongezewa na asiye kuwa nacho hata kile alichopewa atanyanganywa. Kwanza talanta ni za Bwana. Si zako. Vipaji ni vya Bwana si vyako. Wewe ni wa Bwana si wewe mwenyewe. Hivi vyote vinatakiwa vitumike kwa ajili ya ufalme wa Mungu. Vitu vya ufalme wa Mungu ni upendo, huduma na kushirikishana. Kila kitu kinachofaa kwa ajili ya kuishi pamoja na kukua pamoja inabidi kitumike. Mtu anayeogopa kushirikiana na wengine, anayeogopa kuchangia kwa hofu ya kupoteza alicho nacho huyu mwosho wake hupoteza hata hicho kidogo alicho nacho. Huyu ni mbinafsi. Wabinafsi mnajua hasara yao. Mtu ambaye huwa si mbinafsi huwa na marafiki. Huishi maisha ya pamoja. Katika kutoa kuna kupokea anasema Mtume Paulo. Ndiyo maana Bwana alisema mtu akitaka kuyaokoa maisha yake atayapoteza na mtu akiyatoa maisha yake atayapata Mt 10:39. Hakuna tofauti ya aliyepata tano, au mbili au moja. Wote wamepata kulingana na uwezo wao. Hivyo usiishi kwa kutazama mwingine ana nini. Wewe tazama una nini na unafanya nini. Kilicho cha msingi ni kujibidisha kwa ajili ya kueneza ufalme wa Mungu. Mfano huu unatufundisha jinsi ya kuwa katika uhusiano na Mungu kwa njia ambayo ni sahihi. Hawa wawili wa kwanza hawatafuti faida yao binafsi. Hawataki kitu kutoka kwa Bwana. Hawapigi mahesabu, o sijui nimechanga mara nyingi, o sijui misa imechelewa kuisha, o sijui nini. Wao wanafanya kazi na kuishi kwa ajili ya ufalme. Mtumishi wa pili yeye ni mwoga ana sababu kibao. Hataki kabisa kujihusisha na mambo ya Mungu. O mara kule kuna michango, o mara muda unakwenda sana. .. mara hili na lile. Yaani yeye hafanyi chochote. Kushughulika na mambo ya ufalme ni hatari. Kuna kuabika. Watu wanaogopa aibu. Nikijitahidi kuishi hivi halafu nikishindwa?