Kwa jina naitwa Ansbert Protace Mulaly, nilizaliwa tarehe 18/07/2000, Dar-es-salaam Tanzania. Mimi ni kijana wa kwanza katika familia ya watoto wa nne wa Bw. Protace Francis na Bi.Victoria Richard ,nao ni wanandoa . Sambamba na hilo nimepokea sakramenti za Ubatizo, Ekaristi Takatifu na Kipaimara katika Kanisa Katoliki.
Nilianza elimu ya msingi mnamo mwaka 2007 hadi mwaka 2013 katika shule ya msingi Bunju “A”, na ni kwa hakika kabisa kuwa ni katika kipindi hiko cha maisha yangu ya uanafunzi historia ya wito wangu inaweza kuanza kuhadithiwa kwani nilipokuwa darasa la tatu, mwaka 2009 nilipata kuwaona kwa mara ya kwanza mapadre wa shirika la Wakarmeli katika ibada ya misa ya tatu ambayo ni misa maalumu kwa watoto katika kigango cha Mt. Yosefu walipokuja kujitambulisha kwetu wakitokea nchini Italia. Kwa kweli nilitokea kuvutiwa sana na vazi lao safi na nadhifu la shirika walilokuwa wamevaa na hivyo kutamani kuwa siku moja niwe katika vazi la namna hiyo kwani walikuwa kama malaika mbele ya macho yangu, lakini kwa wakati ule sikuwa na maamuzi thabiti ya kuchagua ni namna gani ya maisha ninayopenda kuishi, kwani nilikuwa hata sijui mapadre wanapatikanaje. Hivyo basi niliendelea na masomo hadi nilipohitimu elimu ya msingi nikiwa na matamanio ya kuwa daktari wa binadamu.
Baada ya kuhitimu elimu ya msingi nilifanikiwa kufaulu mitihani yangu vizuri na hivyo kuchaguliwa kuendelea na masomo ya elimu ya sekondari ambapo nilijiunga na seminari ndogo ya Jimbo Kuu Katoliki la Dar-es-Salaam inayojulikana kwa jina la Seminari Ndogo ya Mt. Maria, maarufu kama Visiga Seminari. Hapo nilipokea elimu ya sekondari kuanzia kidato cha kwanza hadi kidato cha nne kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2017, na baadae nikarudi kumalizia elimu ya juu ya sekondari (kidato cha tano na sita) kuanzia mwaka 2018 hadi mwaka 2020.
Wakati wote tulipokuwa seminarini masomo yetu ya elimu ya sekondari yaliambatana na malezi makini ya kuwaandaa waseminari kwa hatua zinazofuata za malezi ya kipadre hivyo basi yalisaidia sana waseminari katika kujitathimini katika dhamiri zao juu ya wito wao wa maisha. Binafsi malezi haya yalinisaidia katika kujitathimini, na baadae kutambua dhumuni na mpango wa Mungu katika maisha yangu. Hii ilikuja baada ya kuruhusu ukimya na utulivu wa ndani kabisa wa moyo, uliotoa nafasi katika moyo ili kusikiliza sauti ya Mungu inayosema na watu kwa namna mbalimbali, jambo hili linisaidia kutambua wito wangu wa maisha ambao Mwenyezi anapenda nimtumikie kama kasisi katika kanisa lake katoliki. Na kwa hakika kabisa baada ya kutambua hili nilianza kuitikia na kuanza mapambano ya kujiimarisha kiroho wakati wote kwa kuomba neema ya Mungu katika safari hii ya matumaini.
Kadhalika, ni katika kipindi hiki cha maisha nilikuwa nikivutiwa sana nilipokuwa nahudhuria maadhimisho ya misa takatifu za kuwaweka mafrateli katika daraja ya ushemasi, na mashemasi katika daraja ya upadre na hivyo nilijitahidi sana kuhudhuria katika maadhimishi hayo, jambo lililochochea zaidi shauku na nia yangu ya kuwa padre. Nilivutiwa zaidi pale nilipoona mapadre watatu wakarmeli wakipewa daraja ya upadrisho katika parokia ya mbezi Louis.
Kama nilivoainisha hapo awali kuwa nilitokea kuvutiwa sana kuwa padre kwa namna ya mapadre wa shirika, hivyo basi baada ya kumaliza elimu ya juu ya sekondari nilifanya utaratibu wa kuanza kuulizia ni kwa namna gani ningeweza kutimiza kiu yangu ya ndani ya kutaka kufanya kazi na Mungu kama kasisi wa kanisa katoliki ndani ya shirika la wakarmeli. Kwa hakika kabisa jambo hili liliwachanganya na hata kushangaza wengi hasa walezi seminarini, kwani wengi walifikiri kwamba ningeendelea na safari ya altareni kwa kujiunga na nyumba ya malezi ya Jimbo Kuu la Da-es-salaam, jambo hili lilikuwa kinyume cha matazamio yao.
18/Julai/2020, Tarehe na mwezi sawa kabisa na siku yangu ya kuzaliwa, nilifanikiwa kukutana na Padre-Mkurugenzi wa miito wa shirika la mapadre wakarmeli Fr.Victor Biramata na kumueleza nia yangu ya kutamani kuwa Padre wa Kanisa katika shirika lao, kwa kweli aliibariki nia hii na kunipongeza kwa kufikia uamuzi wa namna ya kumtumikia Mungu katika maisha ya kitawa na hivyo kunipa maelekezo na namna ya kuendelea na maandalizi ili niweze kupokelewa rasmi katika Konventi ya Shirika iliyopo Bunju, Dar-es-salaam,Tanzania.
Mnamo tarehe 09/09/2020 nilipokelewa kama mkandidati tayari kwa kuanza mwaka wa malezi, mimi pamoja na wenzangu wawili Ndg. Faustine na Ndg. John. Nina furaha kuwa mahali hapa na wakati wote ninaomba neema na huruma ya Mungu katika kuitikia kiaminifu wito huu mtakatifu.
SAFARI ILIENDELEA…. MALEZI YA UPOSTULANTI
Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu, msaada wetu unaotuonekania wakati wote (Zab 46:1).
Hatua nyingine ya muhimu ya Malezi ya kitawa na kipadre niliikabili kwa tumaini kuu katika yeye aliyeniita nimtumikie. Mnamo Oktoba 2021, nilianza kipindi cha malezi ya upostulanti na masomo ya falsafa katika chuo kikuu kishiriki cha Jordan kwa muda wa miaka mitatu. Kilikuwa ni kipindi cha panda shuka nyingi sana katika jitihada za kushirikiana na neema ya Mungu katika kuitikia wito huu wa kumtumikia katika kanisa na familia ya wakarmeli.
Malezi ya kipostulanti yakilenga hasa kuniimarisha katika fadhila, karama na roho ya shirika ambayo niliyapata kupitia vipindi mbalimbali vya Karmeli jumuiyani na katika kujisomea vitabu mbalimbali vya kiroho vya maisha ya watakatifu wakarmeli.
Malezi ya kiakili kwa upande wa masomo ya falsafa niliyapata chuoni ambapo wakufunzi walijitahidi kwa hali na mali kutujaza maarifa ya elimu dunia na kuturuhusu kujifunza kupitia midahalo na majadiliano madarasani. Haya yote yalinisaidia kuimarika kiroho, kiakili, kifikra na kimaadili.
MWAKA WA UNOVISI
Mnamo mwezi Julai 2024 baada ya sala na maoni chanya kutoka kwa mlezi na kamati ya malezi basi Mama Kanisa alitupendekeza kwa hatua nyingine muhimu sana ya malezi ya kitawa, hatua ya unovisi. Hivyo baada ya kupata pasi ya kusafiria, vibali vya kuishi na taratibu za msingi za kisheria mimi pamoja na wenzangu wawili, ndugu John na Faustine tulienda nchini Zimbabwe mnamo Tar 5. Julai 2024. Tayari kwa malezi ya kinovisi.
Katika mwaka huo tukiwa katika nyumba ya kinovisi ya Mt. Nabii Eliya, Nyazura, Mutare. Tulikutana na ndugu wengine kutoka nchi za Afrika ikiwemo Kenya(3), Msumbiji (4), na Zimbabwe (3). Hivyo kufanya jumla ya jumuiya ya wanovisi 13 na walezi watatu. Akiwemo Padre Simplicio Manyika O.Carm (mkuu wa nyumba), Fr. Wiseman Msemwa (mlezi wa wanovisi), Padre Lefani Mwanza (mhazini wa jumuiya na msimamizi wa kituo cha mafungo) ambaye baadaye nafasi yake ilichukuliwa na Fr. Underson Msina.
Maisha katika nyumba ya unovisi yalijikita hasa katika kujikuza katika roho na Karama ya shirika. Daima nikisindikizwa na msaada wa neema ya Mungu na maombezi bora ya Maria Mtakatifu Mama wa Mungu na Mama yetu katika Karmeli Mungu alitupa neema na baraka tulizohitaji ili kuhakikisha tunavuka na kumaliza salama kipindi hiki cha malezi.
Hivyo baada ya kipindi cha mwaka mmoja na kwa kadiri ya katiba ya shirika la wakarmeli (O.Carm) mnamo tar 28. Juni. 2025 ambapo mama kanisa aliadhimisha sikuuu ya moyo safi wa Bikira Maria, Nilimwekea Mungu nadhiri zangu za kwanza katika shirika la wakarmeli (O.Carm) katika Parokia ya Kristo Mfalme (Kriste Mambo) huko nchini Zimbabwe katika mikono ya Padre Dominic Maria Somola ambaye alikuja pamoja na mkurugenzi wa miito na mlezi wa wanafunzi wa shirika la wakarmeli katika nyumba ya malezi ya Mt. Titus Brandsma Morogoro, Fr. Victor Alphonce Biramata. Na kisha baada ya siku chache za mapumziko na utulivu tulirudi nchini Tanzania, mnamo Tar 5. Julai. 2025. Na kufanya misa ya shukrani kwa Mungu katika Parokia ya Bikira Maria wa mlima Karmeli, Bunju, Dar es salaam mnamo Tar 28. Julai. 2025. Ikifuatiwa na tafrija fupi katika nyumba ya mapadre.
THEOLOJIA: SAFARI INAENDELEA....
……ndani Yake Yeye tunaishi, tunajimudu na kupata uhai. (mat 17:28)
Safari ya malezi na makuzi ya kiroho, kiakili, kifikra na kimaadili haijaisha, bado inaendelea. Kwani baada ya kurudi nyumbani, Tanzania tulifanya mitihani kadhaa ambayo tuliachia njiani kwa sababu ya kuwahi nchini Zimbabwe kwa hatua ya unovisi. Baada ya kupata matokeo mazuri tulihitimu rasmi masomo ya Falsafa kwa neema za Mwenyezi Mungu. Na hivyo tukaomba kuendelea na masomo ya Theolojia katika Chuo Kikuu Kishiriki cha Jordan. Na mnamo mwezi wa kumi na moja baada ya vurugu na purukushani za uchaguzi tulianza safari nyingine ya masomo ya Theolojia na kwa sasa nimemaliza muhula wa pili wa masomo kwa mwaka wa kwanza.
Katika yote na vyote Mungu apewe sifa, kupitia Kristo mwanae wa milele pamoja na Roho mtakatifu katika utatu usiogawanyika tangu sasa na hata Milele yote. Ee Maria mama na dada yetu mwema.... utulinde, utufunike na utusitiri kwa vazi lako zuri la skapulari mpaka tufikie Altare ya mwanao mpenzi, Yesu Kristo.
MAMA YETU BIKIRA MARIA WA MLIMA KARMELI, UTUOMBEE!