Bikira-Mtakatifu wa “Upendo usio pendeka”
Alizaliwa kwenye familia yenye heshima na yenye uwezo, tarehe 2 Aprili, 1566 huko Firenze Italia. Baba yake aliitwa Camillo di Geri de’ Pazzi na mama yake aliitwa Maria Maddalena Buondelmonti. Alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto wanne. Nyumbani walimpa jina la Lucrezia na alibatizwa kwa jina la Catarina. Alipata malezi na elimu bora kabisa ya kikristo toka katika familia yake. Alionesha hisia kubwa ya uwepo wa Mungu tangu akiwa mtoto. Alikuwa na upendo mkubwa kwa Ekaristi Takatifu na alipenda sana kuipokea. Pia alikuwa na hamu ya kuishi maisha ya toba. Alijifunza kutafakari akiwa na miaka tisa (miaka 9) toka kwa mwungamishaji wa familia –mjesuiti. Alikwenda shule ya kutwa ya (1574-1578) na ya kulala (1580-1581). Alipokea Komunyo ya kwanza 25 Machi, 1576, akiwa na umri wa miaka kumi. Tarehe 19 April, 1576 akaweka ahadi ya ubikira wa daima.
Alipata maongozi ya kiroho kutoka kwa mapadre wa Jesuiti.
Akiwa na hamu ya kupokea Komunyo kila siku, alijiunga na wamonaki Wakarmeli katika konveti ya Mtakatifu Maria wa malaika huko Firenze. Alipokelewa kama mpostulanti 1 Disemba 1582, akiwa na umri wa miaka 16 kinyume cha mapenzi ya wazazi wake hasa baba ambaye alitegemea kuwa angeolewa na familia ya heshima. Akiwa mnovisi, aliumwa sana kwa miezi miwili na alikaribia kufa. Alipokea vazi la shirika 30 Januari, 1583, mwanzo wa unovisi na akachukua jina la Maria Magdalena. Kutokana na kuumwa kwake walihofia kuwa ilikuwa vigumu kwake kupona, hivyo walimruhusu aweke nadhiri 29 Mei, 1584 akiwa kitandani kilicholetwa kwenye kikanisa cha monasteri. Mara tu baada ya kuweka nadhiri aliingia katika ekstasi kwa muda wa saa mbili. Ekstasi hii iliendelea kwa muda wa siku arobaini na ilikuwa ikitokea mara tu baada ya kupokea Komunyo Takatifu.
Baada ya kupona alikuwa mwalimu msaidizi wa wanavisi kwa miaka mitatu. Alikuwa mlezi wa wenye nadhiri za muda toka mwaka 1595 hadi 1598. Na mwalimu wa wanovisi kwa miaka sita toka mwaka 1598 hadi mwaka 1604 alipochaguliwa kuwa msaidizi wa mkuu wa nyumba. Aliendelea kupata mateso ya kimwili na majaribu ya kiroho vilikuwa msalaba mkubwa sana kwake lakini alivumilia na alitegemezwa na neema ya Mungu.
Aliishi maisha ya sala na kujikana. Alijawa na hamu kubwa ya kulipyaisha Kanisa. Alitamani kuona jambo hilo likienea na alijitoa mwenyewe ili “wapakwa mafuta” waweze kuwa mashahidi tena wa Neno na walioanguka waweze kurudi kanisani. Kiini cha maisha yake ya kiroho kilikuwa ni Upendo. Tumeumbwa na Mungu na Upendo na kwa Upendo na ni njia hiyo hiyo inabidi tumwelekee. Upendo ni kipimo cha jinsi roho inavyomwelekea Mungu. Jukumu muhimu zaidi la upendo ni kuunganisha roho na Mungu. Maisha ya kiroho ni kama duara, yanavutwa na upendo kiasi kwamba Mungu ndio chanzo na kikomo. Mtakatifu Maria Magdalena de Pazzi alikuwa pia na ibada kubwa kwa Bikira Maria. Bikira Maria ni msafi kabisa. Uzuri wake ulikuwa katika usafi wake. Hicho ndicho kilichomfanya awe kitu kimoja na Neno wa Milele.
“ecstasies”-Hali ya kuwa katika “ecstasy –Self –transcendence, an overwhelming feeling of great happiness or joyful excitement”. Hisia kali za furaha kubwa au msisimko wa furaha.
Aliwahi kujizidi –kupoteza milango ya fahamu (ekstasi) akiwa na umri wa miaka 12.
Papa Benedikto XVI alimwelezea Maria Magdalena hivi juu ya uzoefu wake wa maisha ya kiecstasi “katika umri wa miaka 19 tu, alifanywa mweza wa kuelewa mafumbo ya wokovu –toka umwilisho wa Neno ndani ya tumbo la Maria hadi kushuka kwa Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste”.
Alipata uzoefu fumbo mwaka 1583 wakati wamonaki wenzake walipomwona akilia mbele ya msalaba akisema: “Ee Upendo, hujulikani wala hupendwi”. Baada ya nadhiri zake 1584 aliingia katika ekstasi kwa siku arobaini (40) akiwa katika mateso. Kila siku mara baada ya misa aliingia katika ekstasi kwa muda wa saa mbili (saa 2). Ekstasi zake zilikuwa za muungano wa ajabu na Mungu na alikuwa akiongea Ukweli wa kimungu. Muungamishaji wake aliamuru masista wawe wanaandika alichokuwa akiongea ili kulinda ufunuo wake (ufunuo binafsi). Alikuwa akiongea akiwa katika ekstasi na wamonaki wenzake walikuwa wanaandika aliyokuwa akiongea. Katika muda wa siku arobaini (siku 40), kati ya Julai 25 na Septemba 4, 1586 aliweza kuimla barua 12. Kikubwa alichokuwa akikizungumzia kwa shauku kubwa ni upyaisho wa Kanisa na maisha ya wakfu. Alipenda kutumia neno upya-renewal kuliko mageuzi –reform. Alipoongela upyaisho wa Kanisa alilenga mabadiliko ya to baya moyo –conversion. Viliandikwa vitabu vitano.
Vitabu vitatu vya kwanza viliandikwamo –ekstasi iliyotokea kati ya Mei 1584 na wiki ya Pentekoste ya mwaka uliofuata. Kitabu cha nne kilihusu majaribu yake na cha tano kilihusu upyaisho wa Kanisa na maisha ya wakfu.
Kitabu cha kwanza: Siku arobaini (Julai –Agosto 1584).
Kitabu cha pili: Mahojiano/Mazungumzo (Disemba 1584 –Julai 1585).
Kitabu cha tatu: Ufunuo na uelewa (Wiki ya Pentekoste -8 Juni -16 Juni 1585. )
Kitabu cha nne: Majaribu (yalianza Dominika ya Utatu Mtakatifu 1585-1590).Baada ya
hapo ekstasi zilipungua.
Kitabu cha tano: Upyaisho wa Kanisa (ekstasi moja –lakini kina barua 12 mbili
zilizoandikwa Julai –Agosto 1586 kwenda kwa watu mbalimbali –viongozi wa Kanisa lakini hazikuwahi kuwafikia).
Kazi yake nyingine: Maonyo (Mkusanyiko wa maneno yake aliyokuwa akiyasema ndani ya
monasteri).
Furaha ya neema aliyopewa na Mungu ilichanganyika na mateso ya ugonjwa wake. Siku moja Yesu alichukua moyo wake na kuuficha kwenye moyo wake (Yesu) akamwambia kuwa hatarudi mpaka ametakaswa kabisa na kujazwa upendo wa Mungu. Alikuwa na uhusiano binafsi na Yesu. Mazungumzo yake na Yesu yaliwatisha wengi waliokuwa wanamwogopa Mungu. Yesu alimpatia taji la maua ya miiba. Kuna kipindi Yesu alimwambia “sitakuondolea neema bali nitakuondolea hisia yake”. Ijapokuwa itaonekana nimekuacha lakini nitakuwa karibu nawe. Baadaye akiwa na umri wa miaka 19 kilifuata kipindi cha miaka mitano (5) cha ukavu na majaribu ya kila aina. Alieleza kuwa roho yake ilikuwa kama chumba chenye giza nene na miali ya mbali. Alijaribiwa kwa kiasi kikubwa juu ya usafi wa moyo. Alitilia wasi wasi wito wake. Alipoteza hamu ya kuishi (depressed-huzuni) na alikaribia kutoroka konventi na kujiua mara mbili. Alichofanya kwa kipindi hicho ni kusali sana, kufanya toba na kuwatumikia wengine hata kama alikuwa haoni matunda yake. Alifikia tamati ya majaribu yake mwaka 1590. Tangu wakati huo ekstasi zilipungua kwa kiasi kikubwa. Ekstasi ilimletea karaha na alipenda maisha yaliyo ya faragha.
Kuna usiku mmoja 1 Mei, 1592 aliamka usiku baada ya kuhisi upendo mzito, akaanza kugonga kengele za monasteri akiwaamsha wamonaki wapende Upendo. “Kupenda Upendo”. Tukio hili lilikuwa la kushangaza. Alikuwa akikimbia kwenye kuta za monasteri na kuwaita watu kwenye upendo wa Mungu. Aliona Mungu hapendwi kama inavyostahili.
Mtakatifu Maria Magdalena wa Pazzi alikuwa mtakatifu si kwa sababu ya ekstasi yake, bali kwa sababu ya upendo aliokuwa nao na kuuishi. Alitimiza wajibu wake sawa sawa. Alipenda kuwahudumia dada zake hasa wazee na wagonjwa.
Alifariki dunia tarehe 25 mwezi tano mwaka 1607.
Alitangazwa Mwenye Heri mwaka tarehe 8 Mei, 1626 na Papa Urbano VIII.
Alitangazwa Mtakatifu tarehe 28 Aprili, 1669 na Papa Klementi