SIKU ZA KUPOTEA VIVULI HAPA TANZANIA

SIKU ZA KUPOTEA VIVULI HAPA TANZANIA

Iwapo mtu angekuuliza Je Jua linakuchwa upande gani? Utamjibu haraka haraka kuwa ni magharibi, bila hata kufikiria kwa sababu ndivyo tulivyo fundishwa tulipokkuwa shule za msingi. Hata hivyo tunapokuwa wakubwa, katika shule zetu za sekondari tunafundishwa kuwa Dunia inajizungusha kwenye mhimili wake uliyoinama katika pande ya nyuzi 23.5 kwenye uso bapa wa Mfumo wa Jua na sayari zake.

Mwinamo huo wa mhimili umeelezwa kuwa ndiyo sababu ya Jua kuhama kutoka kaskazini hadi kusini na kusababisha misimu minne, yaani msimu wa joto (summer), baridi (winter), kupukutika majani (autumn), na msimu wa mchupuko wa majani (spring). Misimu hii haikuwa na maana kamili kwa waTanzania wengi kwa sababu tumezoea misimu mikuu mitatu tu – kiangazi, masika, na kipupwe. Ingawa msimu wa joto na baridi unahusiano na majira ya kiangazi na kipupwe tuliyoyazoea na tumekuwa tunakariri majira ya kuputika majani na kuchipuka majani ili kutaka kufaulu mtihani tu.

Si kila mtu anaelewa kuwa Jua linapohama angani katika mwaka, kutoka kaskazini hadi kusini na kurudi huwa linangaa utosini kwa ukali au utulivu kwa kuinama kufuatana na latitudo tofauti na hivyo husababisha misimu. Tunaweza kuona tofauti ya joto kati ya Jua kali la mchana utosini linaloangaza mionzi mkusanyiko na Jua la baridi nyakati za jioni lenye mionzi iliyoinama na kusambaa ardhini.

Misimu inabainika zaidi katika maeneo ya nje tropiki, kaskazini au kusini zaidi ya Ikweta. Yana misimu ya baridi kali kwa sababu Jua haliwi utosini kabisa, kwa hiyo mionzi ya Jua daima hupiga ardhini kwenye pembe zilizoinama mwaka mzima na hasa majira ya baridi wakati mionzi inapokuwa imeinama mno. Karibu na ncha ya kaskazini au kusini ya Dunia, mionzi ya Jua inapiga sambamba na ardhi na kusababisha nishati kidogo tu kunyonywa na ardhi na kusababisha ardhi ya sehemu hizo kuwa baridi mno. Pia karibu na ncha za Dunia Jua hupita chini ya upeo kwa nusu mwaka ilimaanisha kuwapo kwa giza miezi sita ambayo huwezesha kuwa na barafu ya kudumu pale.

Sayari zote zinazozunguka Jua katika Mfumo wetu wa Jua zina mizizingo iliyo kwenye uso bapa, kwa hiyo Mfumo wa Jua na sayari ni bapa. Mihimili wa Dunia umeinama kwa nyuzi 23.5 kutoka kwaenye bapa ya Mfumo wa Jua kwa hiyo tarehe 21 Juni mduara wa Ikweta unakuwa chini ya Jua kwa nyuzi 23.5 (angalia mchoro). Hii inasababisha nusudunia ya kaskazini kupigwa mionzi moja kwa moja. Baada ya miezi sita, yaani tarehe 22 Desemba, wakati Dunia imeshazunguka nusu mduara katika mzingo wake, mduara wa Ikweta unakuwa umeinama juu ya Jua kwa hiyo nusudunia ya kusini kupigwa mionzi ya Jua moja kwa moja. Katikati ya tarehe 21 June na 22 Desemba, yaani tarehe 21 Marchi na 23 Septembe, mwinamo wa mduara wa Ikweta hauwi juu wala chini ya bapa ya Mfumo wa Jua kwa hiyo husababisha Jua kuwa utosini kwenye Ikweta. Kwa ujumla tunaweza kuelewa kuwa mabadiliko ya mwinamo wa mduara wa Ikweta husababisha Jua kuwa utosini katika latitudo tofauti katika Dunia nyakati mbali mbali za mwaka.

Tarehe 21 machi na septemba 23 Jua liko utosini katika Ikweta, yaani latitudo ya nyuzi sifuri. Baada ya septemba 23, sehemu za kusini mwa Ikweta zinapata Jua la utosini hadi Desemba 22 linapokuwa utosini kwenye Tropiki ya Kaprikoni. Baada ya Desemba 22, Jua linsogea kaskazini na kuwa utosini kwenye Ikweta tarehe 21 Machi. Baada ya hapo, linaendelea zaidi kusogea kaskazini hadi kuwa utosini katika Tropiki ya Kansa tarehe 21 Juni. Hadi tarehe 23 Septemba Jua linakuwa tena utosini katika Ikweta. Msogeo kama huu wa Jua hurudia mwaka hadi mwaka.

Tarehe 22 Desemba Jua huwa kusini zaidi ya Ikweta na siku hiyo hjulikana kama Solstasi ya Kusini, wakati tarehe 21 Juni Jua liko kaskazini zaidi ya Ikweta na hujulikana kama Solstasi ya Kaskazini. Tarehe 21 Machi na tarehe 23 Septemba hujulikana kama Sikusare kwa vile Duniani kote masaa ya mchana na usiku huwa muda sawa kabisa. Wakati Jua linapokuwa kaskazini zaidi ya Ikweta tarehe 21 juni, mchana huwa mrefu zaidi na usiku mfupi zaidi upande wa kaskazini mwa Ikweta, wakati Jua linapokuwa kusini zaidi ya Ikweta mchana huwa mrefu zaidi na usiku huwa mfupi zaidi kusini mwa Ikweta. Zingatia kuwa kwenye Ikweta mchana na usiku huwa sawa mwaka wote.

Utoana kwamba mwezi Juni, wakati Jua linapokuwa kaskazini zaidi, ncha ya kaskazini ya mhimili uliyoinama wa Dunia unaelekea Jua, na wakati huo huo, Jua linapokuwa kusini zaidi mwezi Desemba ncha ya kusini ya mhimili wa Dunia inaelekea mbali mbali na Jua. Vilie vile, uelewe kuwa wakati wa sikusare za Machi na Septemba, ncha ya kaskazini haiimanii upande wa Jua wala mbali na Jua ambayo ndiyo inawezesha siku na mchana kuwa muda sawa.

Mwendo wa Jua kaskazini na kusini hatuuzingatii kabisa kwenye nchi za tropiki kwa sababu tunadhani kwamba Jua daima linapambazuka mashariki na kuchwa magharibi na mchana hupita utosini kila siku. Lakini iwapo utafuatilia kwa karibu wakati Jua linapoangaza kupitia dirishani kwako, utakumbuka kuwa linaangaza kutoka pembe tofauti majira tofauti ya mwaka na kusababisha vivuli vihame kutoka sehemu moja ya chumba hadi nyinginge. Mwendo huu una maana kwamba nafasi ya Jua angani hubadilika mara kwa mara mwaka mzima kwa hivyo Jua halichwi upande wa magharibi mwaka wote na halipambazuki mashariki nyakati zote mwaka mzima - bali hubadilika.

Desemba 22 ukilianglia Jua wakati wa kuchwa katika upeo wa magharibi utaliona kuwa lipo upande wa kusini-magharibi nyuzi 23.5. Siku zinazofuata, nafasi ya Jua upeoni wakati wa kuchwa itahamia kaskazini siku hadi siku hadi ifikie magharibi kamili Sikusare ya Machi 21. Baada ya siku hiyo, itaendelea kusogea kaskazini na ifikapo tarehe 21 Juni nafasi yake upeoni wakati wa Jua kuchwa itakuwa kaskazini-magharibi nyuzi 23.5. Baada ya hapo nafasi ya kuchwa Jua litarudi kwenda kusini hadi Septemba 23 ambapo siku hiyo nafasi ya Jua upeoni wakati wa kuchwa itakuwa magharibi kamili. Baada ya hapo hadi tarehe 22 Desemba Jua litakuwa tena kusini-magharibi nyzi 23.5. Ukiangalia, kupambazuka kwa Jua kwa mwaka mzima nafasi ya Jua nayo itaonekana kuhama upeo wa mashariki na kuwa mashariki kamili tarehe 21 Machi na 23 Septemba.

Je Jua linakuwaje katikati mchana? Tuangalie litakuwaje kwenye Tropiki ya Kansa. Hapo, Jua litakuwa utosini kabisa katikati mchana siku ya tarehe 21 June. Kwa hiyo pale, vivuli vya vitu vilivyo wima vitakuwa chini kamili ya vitu hivyo na hatutaweza kuona kivuli chochote. Baada ya miezi mitatu tarehe 23 Septemba, Jua litakuwa utosini kwenye Ikweta. Kwa hiyo katika miezi mitatu kuanzia 21 Juni hadi 23 Septemba, sehemu za Duniani ambapo Jua linakuwa la utosini zinahama siku hadi siku kutoka nyuzi 23.5 latitudo kaskazini hadi latitudo sifuri ya Ikweta. Hivyo kuna siku mahususi kwa kila latutido ya Jua kuwa la utosini kamili.

Kuanzia 23 Septemba hadi 22 Desemba nafasi ya Jua la utosini husongea kusini kila siku kutoka Ikweta hadi Tropika ya Kaprikoni, nyuzi 23.5 latitudo kusini. Kwa hiyo, kwa sisi tuliopo Tanzania ambayo ipo kati ya nyuzi 1 latitudo kusini hadi nyuzi 11 latitudo kusini, Jua litakuwa utosini mchana kati kuanzia tarehe 26 Septemba kwa sehemu za kaskazini kabisa hadi tarehe 22 Oktoba kwa waliopo kusini kabisa ya nchi. Wakati nafasi ya Jua, linapoelekea kaskazini kutoka tropiki ya kaprikoni hadi Ikweta, litakuwa utosini tena mchana kuanzia tarehe 20 Februari hadi 17 Machi

Kwa hiyo tunawezekuona kuwa kwa mahali paliyopo ndani ya tropiki yaani kati ya nyuzi 23.5 latitudo kaskazini hadi nyuzi 23.5 kusini, kutakuwa na siku mbili tu katika kila mwaka ambapo Jua litakuwa utosini kamili. Na siyo siku zote ambavyo tulifikiria. Nje ya tropiki, Jua haliwi utosini mahali popote penye latitudo za juu kaskazini au kusini ya tropiki hadi kwenye ncha za Dunia.

Vivuli vintokea wakati mionzi ya Jua iliyoinama inapoangazia vitu kwa hiyo kama kuna mionzi iliyoinama zaidi, vivuli vya vitu vya wima ni virefu zaidi kama tunavyoona nyakati za jioni na asubuhi. Hata hivyo kama Jua la mchana lipo utosini kamili, vivuli vya vitu vilivyo wima vitakuwa moja kwa moja chini ya kitu hicho kwa hiyo huwezi kuona kivuli chochote- yaani vivuli vitapotea. Siku hizo zinaitwa siku zisizo na kivuli. Kwa maelezo yaliyoelezwa juu, kuna siku mbili tu kwa vivuli kupotea katika sehemu zilizopo ndani ya tropiki. Kwa vile Tanzania ipo ndani ya tropiki tunaweza kushudida siku za kupotea vivuli.

Baada ya Sikusare ya 23 Septemba, wakati Jua lilipokuwa utosini kamili wakati wa mchana katika Ikweta, nafasi ya Jua angani hivi sasa inasogea polepole kusini, katika siku zinazokuja, Jua litakuwa utosini kuelekea latitudo za kusini kwa Tanzania kuanzia tarehe 26 Septemba mpaka 22 Oktoba. Jua litakuwa utosini mchana kuanzia 26 Septemba kaitka miji ya Bukoba na Musoma(nyuzi 1 latitudo kusini) kaskazini kabisa ya Tanzania, hadi tarehe 22 Oktoba pale Newala na Tunduru (nyuzi 11 latitudo, kusini ) kusini mwa Tanzania.

Nyakati za mchana kati ni kwa saa za mahali zinazotegemea longitudo ya mahali. Sehemu zilizo upande wa mashariki ya nchi ya kama vile Zanzibar, Dar-es-salaam na Tanga kutakuwa na nyakati zao za mchana kati ni mapema zaidi kuliko zile za upande wa magharibi wa nchi kama vile Bukoba, Kigoma na Sumbawanga. Kwa kuwa sehemu ya magharibi zaidi na mashariki zaidi ya Tanzania huwa na tofauti ya nyuzi 10 za longitudo, kuna tofauti ya dakika 40 kati ya saa za Dar-es-salaam na Kigoma.

Toka nje siku zilizooneshwa hapa chini ukaangalie VIVULI VIKITOWEKA mchana kati ambapo Jua liko utosini kamili. Kwa miji usiyoorodheshwa hapa chini, kadiria tarehe na nyakati kwa kutumia za miji ya karibu yako zilizopewa hapa chini.

==xx==