MADOAJUA NA MBINGU ZA JULAI HAPA TANZANIA

MADOAJUA NA MBINGU ZA JULAI NCHINI TANZANIA


Baada ya miaka mingi ya kuwa kimya tangu mwaka 2009, hivi sasa Jua limeamka, huku nishati nyingi ikitiririka usoni mwake, sasa yameanza kuonekana MADOAJUA katika sura ya Jua yanayoonekana kutoka hapa Duniani.

Kama ulibahatika kushudia tukio la karne, la mpito wa Zuhura tarehe 6 Juni, na kuona doa dogo la kivuli cha Zuhura likipita usoni mwa Jua, basi utaona kwa urahisi madoa katika sura Jua kwa vile yana ukubwa wa takribani mara sita ya doa la kivuli cha Zuhura.

Madoa ya jua yanaweza kuonekana mchana kwa kutumia miwani ya Jua au kwa kuangalia sura ya Jua kupitia darubini ya kawaida kama vile Galileoscope au kwa kupitisha mwanga wa Jua katika tundu dogo.   Picha zinaonesha mpangilio wa darubini wakati wa kuangalia sura ya Jua, na sura yenyewe ilivyoiona, ikilinganishwa na ile ya tovuti ya NASA ya www.spaceweather.com (utaona kwamba sura inavyoonekana kupitia Galileoscope imepinduliwa na lenzi za darubini). Tahadhari:  Utapofua macho yako mara moja ukiangalia Jua moja kwenye darubini.  

Kwa hiyo USIANGALIE JUA MOJA KWA MOJA KATIKA DARUBINI.


Madoa ya Jua ni  maeneo makubwa (yanayofika kipenyo cha km 100,000) kwenye sura ya Jua ambayo joto lake ni nyuzi 2,000 za sentigredi, ambayo imepoa ikilinganishwa na nyuzi 6,000 za sentigredi katika sehemu zilizobaki za sura ya Jua zinazotoa mwanga tunaoweza kuona.  Lakini mwanga sehemu za madoajua ni wa aina ya “infrared” ambabo macho yetu hayawezi kuona. Kwa hiyo madoa hayo huonekana meusi kabisa ililinganishwa na sehemu nyingine yote ya Jua ambayo ni angavu sana.

Madoajua ni maeneo yanayopitisha na kutoa ugasumaku mkubwa na kuingia tena kwenye doajua lingine, kama vile inayotokea katika sumaku ya kawaida inayotoa ugasumaku kutoka ncha ya kaskazini kwenda ncha ya kusini. Ugasumaku katika Jua hutokana na  chembe za Haidrojeni na Heliamu za chanya electroni (inayofamika kama plasma) iliyo na kasi sana.

Nishati ya Jua huanza huzalishwa katika kiini chake ambapo huwa zaidi ya nyuzi milioni 10 za sentigredi na ina kanieneo kubwa sana.  Katika mazingira hayo, muunganiko wa viini vya Haidrojeni na Heliamu huzalisha mnnunurisho mkubwa wa nishati  ya gamma. Miali hii ya gamma huchukua maelfu ya miaka kupenya kwenye gimba nene la Jua na hivyo kufifia nguvu hadi kuwa mwanga wa kawaida tele unaotiririka nje ya Jua kutoka kwenye uso wa jua wenye nyuzi 6,000 za sentigredi.

Kwa kawaida nishati ya plasma yenye ksi kubwa hubaki ndani ya ugasumaku kati ya doajua moja hadi jingine.  Lakini ikiwa nishati inakuwa na kasi kubwa sana, mistari ya ugasumaku inakatika na chembechembe za mada ya Jua hutupwa angani kwa kasi kubwa inayokaribiana na kasi ya mwanga.  Milipuko hiyo hujulikana kama Utoaji wa Mada ya Korona ya Jua (yaani Coronal Mass Ejection au CME) kama inavyoonesha katika picha.
CME zina madhara makubwa kwa binadamu, lakini kwa bahati nzuri tunalindwa dhidi ya chembechembe hizi na ngome ya ugasumaku unaozunguka Dunia.  Ngome hii inakengeusha chembechembe zenye madhara kuelekea ncha ya kaskazini na kusini ya Dunia na kusababisha mng’aro wa usiku unaojulikana kama ‘aurora’.  Hata hivyo, endapo CME zinazoelekezwa moja kwa moja Duniani zinaweza kufanikwa kupenya ngome ya ugasumaku kwa kiasi fulani na kuathiri mifumo ya elektroniki ya vyombo vya angani pamoja na vya ardhini.

Ongezeko kubwa la sasa la idadi ya madoajua baada ya miaka mingi ya ukimya linatarajiwa kuzalisha CME zenye nishati kubwa zaidi zinazoweza kuwa na athari kubwa kwa idadi iliyoongezeka ya vyombo vya angani vya mawasiliano na vya utafiti pamoja na mitambo tunayotumia katika maisha yetu ya kisasa yanavyotegemea zaidi umeme na elektroniki.

Kukabili tishio hili, uwanja mpya wa fani ya hali ya hewa ya anga za juu umeundwa na unatumika kuelewa, kufatilia na kutabiri hali ya Jua.   Kwa kuwa Jua linazunguka mara moja kwa takriban siku 25, madoa yake pia yanahamia, na idadi na nafasi zao pia hubadilika.  Unaweza kufuatilia hali ya Jua kwenye tovuti ya NASA ya www.spaceweather.com, inayotoa taarifa halisi ya hali ya Jua kwa muda huo.

Mbingu za usiku nazo zina mwonekano wa kufuraisha sana kwa kuwa anga ni kavu zisizo na mvua tangu mwanzo wa mwaka, na zinaonesha nyota vizuri na waziwazi. Sayari mbili ya Zohali (Saturn) na Mirihi (Mars) zitaonekana usawa wa utosi karibu na kundi la Mashuke karibu na nyota yake angavu zaidi ya Spica. Zohali iko mbali kutoka Jua kwa hiyo mwendo wake hauonekani kwa urahisi.  Lakini Mirihi, kwa kuwa ipo karibu zaidi na Jua inakwenda haraka zaidi. Kwa hiyo Mirihi inabadili nafasi yake na kuonekana kila siku kuikaribia Zohali na Spica. Nyota tatu hizo zitakaribiana na kuwa mstari mmoja tarehe 14 Agosti. Katika darubini Zohali inaonekana kuwa na pete ya kupendeza ya miduara ya bapa inayozunguka sayari hiyo, na kwa vile ubapa wa pete umeinamia kuelekea upande wetu.

Anga za asubuhi nazo zinaonesha nyota za kusisimua.  Hasa ni sayari za Sambula (Jupiter) na Zuhura (Venus), jozi inayong’aa kuwa kivutio cha ajabu.

Ishara ya Mwezi Mwandamo tarehe 19 Julai itawezesha kuandama kabisa kwa mwezi mtukufu wa Ramadhani jumamosi 21 Julai baada ya kuonekana waziwazi kwa juu kiasi cha kutosha kwenye anga angavu za upande wa magharibi mara baada ya jua kuchwa. Nusu Mwezi utakuwa tarehe 27 Julai ambapo utakuwa muafaka zaidi kuangalia mashimo na mabonde ya Mwezi kutokana na vivuli vyake virefu.  Mwezi mpevu itakuwa tarehe 3 Agosti wakati mwezi mwandamo unaofuatao utakaokuwa tarehe 17 Agosti utafikia kiwango cha kuonekana tarehe 18 Agosti itakayoashiria mwisho wa mwezi mtukufu wa Ramadhani.Mbingu za kusini zimejazwa na nyota angavu ambazo itakuwa vigumu kuficha!  Vielekezi vya upande wa kaskazini na kusini ambazo ni Kigai Kikubwa (Big Dipper) na Msalaba wa Kusini (Southern Cross), ziko juu vya kutosha kwenye mbingu za usiku wa mapema, na zinaweza kutumika kuonyesha mwelekeo wa kaskazini-kusini waziwazi.  Nge (Scorpio) ni kundi linalotawala sana anga mwezi huu, na kuonekana utosini na nyota zake tatu zinaunda mdomo wake.  Nyota nyekundu ya Antres kwenye shingo lake na mkia mrefu unao ishia kwa jozi ya nyota.

Nge ni mkusanyiko pekee wa nyota unaotendea haki jina lake na haiwezi kukosewa hata na mtazamaji nyota wa kawaida. Tumia fursa hii kuanza (au kuendelea) ushabiki wako wa kutazama nyota kwa kubaini kwa uhuru mkusanyiko wa nyota.

Chini ya Nge jaribu kuainisha kundi la nyota la Mshale (Sagittarius, archer).  Mkusanyiko huu unaonyesha upande kilichopo kitovu cha galaksi yetu ya Mkondo wa Maziwa (Milky Way).  Kwa hiyo sehemu hii utaona mkusanyiko mkubwa wa nyota kuliko sehemu zingine za anga.

Miongoni mwa nyota angavu zaidi zinazoonekana kwenye mbingu za mwezi Julai ni Alpha na Beta, Centauri upande wa kusini.  Jozi hii inaunda mstari ambao kila mara unaelekea upande wa Msalaba wa Kusini.  Nyota ya nne angavu zaidi kuliko zote angani ni Arcturus ambayo iko usawa wa utosini upande wa kaskazini.  Nyota angavu zaidi ya tano iitwayo Vega inachomoza upande wa kaskazini mashariki.

Nyota nyingine angavu utakazoziona kwa urahisi ni Altair inavyochomoza upande wa mashariki na Spica, nyota angavu zaidi kwenye mkusanyiko wa Mashuke inaweza kuonekana takribani usawa wa utosi upande wa magharibi.

Miongoni mwa satelaiti zinazozunguka sayari, mwezi huu tutaona wazi kituo cha angani cha Kichina cha Tiangong tarehe 18 Agosti itakapokatisha katikati ya mbingu kuanzia kuchomoza upande wa kusini magharibi saa 12:39 jioni na kufikia mwinuko wa juu zaidi saa 12:42 jioni na kutua upande wa kaskazini – mashariki saa 12:45 kwa kutumia dakika 6 tu na kukatisha mbingu kutoka upeo mmoja hadi mwingine.  Ukitaka kuona Kituo cha Kimataifa cha Angani (International Space Station, ISS) inafaa kuifuatilia katika mtandao wa www.heavens-above.com, karibu zaidi ya tarehe 4 Agosti, wakati itakapokatisha mbingu kuanzia saa 1:06 usiku upande wa kusini magharibi na kutua dakika 7 baadaye mnamo saa 1:13 usiku upande wa kaskazini mashariki.  Angalia tovuti www.atrononyintanzania.or.tz kwa maelezo zaidi na taarifa kuhusu astronomia nchini Tanzania.

MWISHO

 

Comments