MABADILIKO YA MANDHARI YA SAYARI, NYOTA NA MWEZI ANGANI

MABADILIKO YA MANDHARI YA SAYARI, NYOTA NA MWEZI ANGANI

Dr N T Jiwaji
Ukiangalia upande wa magharibi baada ya Jua kutua, kuanzia saa moja hivi karibu na upeo kiasi nyuzi 30, utaona nyota kali inan’gaa angani.  Nyota hiyo si nyingine ila ni Zuhura (Venus) ambayo inawaka mno kiasi cha kushangaza. 

 

Pamoja na hiyo kuna sayari nyngine ya Zohali (Saturn) ambayo pia inan’gaa kiasi na utaiona kama nyuzi tano hivi juu ya Zuhura. 

 

Katika wiki mbili zijazo, siku hadi siku, Zuhura inaendelea kupanda juu angani na kukaribia Zohali.  Ukilinganisha sayari mbili hizi na nyota nyekundu nyingine iliyo jirani yake inayoitwa Antares zinatengeneza umbo la pembe tatu linalobadilika siku hadi siku. Kuanzia Alhamisi tarehe 27, na tarehe 28, hadi Jumamosi tarehe 29 utaona nyota tatu hizi yaani Zuhura, Zohali na Antares zikiwa katika mstari mmoja na kutengeneza mandhari nzuri angani. Zuhura itakuwa inan’gaa kati ya Zohali ambyo itakuwa kulia juu kidogo na Antares itakuwa chini kushoto kidogo ya Zuhura.  Angalia picha ilioambatishwa ya mabadiliko ya mandhari hii.

 

Ukifuatilia kwa siku chache zaidi, Zuhura inaendelea kupanda juu hadi tarehe kufikia tarehe 1 Novemba Mwezi mwandamo utaunganika chini ya Zuhura na siku ya pili yake, yaani tarehe 2 Novemba Mwezi, Zuhura na Zohali zitengeneza mstari mmoja na kuleta mandhari ya kuvutia mno. Angalia picha iliyoambatishwa ya hali itakavyokuwa angani siku hizo.

 

Nenda nje kuanzia leo na fuatilia Zuhura, Zohali na Antares zikibadilisha umbo ya pembe tatu siku hadi siku, na wiki ijayo utaona Mwezi mwandamo mstari mmoja na Zuhura na Zohali.  Ukiangalia juu zaidi karibu na utosini pia tutaona sayari nyingine ambayo ni Mirihi (Mars) ambayo ina n’gaa kwa mwanga mwekundu. 

 

Ukitaka kutofautisha kati ya sayari na nyota uangali mn’garo wake.  Nyota humeremeta wakati sayari hun’gaa kwa utulivu.  Zuhura ni rahisi kutambua kwa vile inan’gaa mno, lakini kwa vile Zohali na Mirihi zinan’gaa kiasi utaweza kuzitambua kwa kulinganisha kama zinameremeta au zimetulia.

 

Ukiwa na darubini hata ndogo unaweza kuona pete inayozunguka sayari ya Zohali na ni sayari ambayo inapendeza mno kuliko zote.

 


Dr N T Jiwaji

 

https://sites.google.com/site/astronomyintanzania/zuhura-zohali-antares

 

https://sites.google.com/site/astronomyintanzania/mwezi-zuhura-zohali-antares

Comments