Kupatwa Kamilifu kwa Mwezi Alfajiri Jumatatu Septemba 28

Kupatwa Kamilifu kwa Mwezi Alfajiri Jumatatu Septemba 28


Baada ya kupatwa kwa Jua hivi karibuni tarehe 13 Septemba,tukio ambalo sisi hapa Taznania hatukubahatika kushuhudia, Mwezi sasa unasogea siku hadi siku na utakamilisha nusu mzunguko siku ya Jumatatu alfajiri ya Septemba 28 na kuwa mstari mmoja tena na Dunia na Jua katika umbo la Mwezi Mpevu.Siku hiyo ya Jumatatu alfajir, Dunia itakuwa kati ya Mwezi na Jua hivyo kivuli kikubwa cha Dunia kitapiga Mwezini na kusababisha Mwezi kupatwa kamilifu.  Kivuli cha Dunia ni kikubwa sana kuliko Mwezi kwa hiyo tukio la kupatwa Mwezi huonekana kwa muda mrefu zaidi ya saa moja.   Pia tukio hili huonwa na watu wote Duniani ambao wako upande wa usiku wakati tukio linaendelea angani.Kuanzia saa 10:07 alfajiri siku ya Jumatatu tarehe 28 Septemba, kivuli kizito cha Dunia kitaanza kupanda juu ya uso wa Mwezi Mpevu na kusogea pole pole kujaza hadi kufunika sura nzima ya Mwezi, saa 11:11.  Huu ndiyo mwanzo wa kupatwa kikamilifu kwa Mwezi na utaendelea kuwa hivyo hadi Mwezi utakapo zama chini ya upeo wa magharibi saa 12:20.   
Mwezi utakapoanza kupatwa saa 10:07 utakuwa juu kiasi cha kutosha, cha nyuzi 30 juu ya upeo wa magharibi, kwa hiyo utaonekana vizuri katika giza la alfajiri kabla ya Jua kuchomoza.  Kutakuwa na masaa mawili hivi ya kufaidi mandhari ya ajabu angani wakati Mwezi utageuka rangi na kuwa mwekundu baada ya kufunikwa kikamilifu na kivuli cha Dunia.  
Rangi hiyo nyekundu hutokana na mwanga wa Jua unaopenya katika hewa ya anga la Dunia.  Mwanga huo unakuwa mwekundu kwa vile mwanga wa bluu hupindwa mno na kubaki Duniani.  Kwa vile mwanaga mwekundu hutokea baada ya kupita katika hewa ya anga letu, rangi inaweza ikafifia kama hewa yetu imechafuliwa na moshi, vumbi au uchafu mwingine wa hewani.  Kwa hiyo angalia kama rangi ya Mwezi siku ya Jumatatu alfajiri inakuwa na wekudu au la.  Isipokuwa nyekundu, basi inaashiria uchafuzi wa mazingira ya anga letu la Dunia.

Zaidi ya hiyo siku ilie ya kupatwa, Mwezi pia utakuwa jirani zaidi na Dunia katika mzunguko wake na hivyo utaonekana mkubwa kuliko kawaida.  Usikose kuangalia tukio la maajabu haya ya angani.


==xxx==


Comments