MUONEKANO WA MWEZI MWANDAMO WA IDDI

MUONEKANO WA MWEZI MWANDAMO WA IDDI

 

Mwisho wa mwezi huu, watu watavutwa kuangalia angani jioni upande wa magharibi mara baada ya magharibi kutafuta Mwezi mwandamo ambao utakamilisha ibada ya kufunga mwezi mtukufu wa Ramadhani.  Wengine watavutiwa na sayari mbili ambazo pia zinang’aa angani mara baada ya giza kuingia.  Sayari hizo si zingine ila ni sayari maarufu za Mushtarii (Jupiter) na Zohali (Saturn).  Mushtarii inang’aa vikali karibu na utosi, na Zohali inaonekana upande wa mashariki karibu na upeo.  ingawa Zohali siyo kali sana, mwanga wake unavuta na ni wa kutulia, mbali na nyota ambazo humeremeta.

 

Wanaoamka mapema kwa ajili ya sala ya alfajiri na kwenda kazini wanashangazwa na sayari nyingie inayong’aa kwa ukali sana jirani na upeo wa mashariki kabla ya Jua kuchomoza. Syari hiyo ni Zuhura (Venus) ambayo kwa sasa ina jina la Nyota ya Alfajiri, na baada ya miezi kadhaa sayari hiyo hiyo itakuwa Nyota ya Jioni itapohama nafasi na kuingia katika anga ya Jioni

 

Kwa wakati huu Mwezi upo katika anga ya alfajiri jirani na upeo wa mashariki kabla ya Jua kuchomoza.  Kila mwezi, Mwezi husogea nyuzi 12 angani, kwa hiyo ifikapo tarehe 23 Juni, Mwezi utakuwa bado upo anga ya alfajiri upande wa mashariki  na hilali yake inatambulika ukiangalia vizuri.  Siku ya pili, yaani tarehe 24, Mwezi utakuwa umesogea kiasi cha kuhamia upande wa pili wa Jua na kuingia katika anga ya jioni. 

 

Wakati wa machweo jioni ya tarehe 24 Juni, Mwezi utakuwa mchanga sana, na hilali yake nyembamba kiasi cha asilimia 0.4% tu na nyuzi 7 jirani na upeo wa magharibi.  Pamoja na hiyo, kwa vile anga ya magharibi huwaka sana wakati wa machweo kwa hiyo hilali changa hufunikwa kabisa ndani ya uang’avu wa anga.  Kwa vile Mwezi unazidi kushuka upeoni muda unavyosogea ni vigumu sana kuuona Mwezi mwandamo siku hiyo.

 

Lakini jioni ya Jumapili tarehe 25 Mwezi utakuwa umesogea juu kwa nyuzi 12 zaidi, na kufikia nyuzi 20 juu ya upeo wa magharibi. Hilali ya Mwezi pia utatanuka kufikia asilimia 3.3% kwa hiyo kutakuwa na muda wa kutosha kabisa kuuona Mwezi hilali, mara giza litapoingia.

 

Kutafuta Mwezi mwandamo inabidi kuwa katika eneo lenye uwazi upande wa magharibi na kuanza kuangalia dakika kumi au kumi na tano baada ya magharibi ili kupata anga lenye giza ya kutosha.  Kwa Dar es Salaam muda mzuri ni kuanzia saa 12:30 jioni, na upande wa pili wa Tanzania, sehemu za Kigoma, itakuwa baada ya saa 1:15 jioni.

 

 

==xx==

Comments